Kutazama Ubuni wa Sayansi wa Leo
MAGARI, simu, kompyuta—zaidi ya miaka 130, je, yaelekea yeyote angeweza kuona kimbele uvumbuzi wavyo? Mwandikaji wa ubuni wa sayansi (SF) Jules Verne aliviona! Ufahamu huu wa kina wenye kushangaza wa kisayansi ulipatikana katika hati fulani iliyogunduliwa hivi majuzi ya riwaya ya Jules Verne yenye kichwa Paris in the Twentieth Century. Katika riwaya hii ambayo awali haikuchapishwa, Verne hata alifafanua mashini ambayo kwa kushangaza ilifanana na mashini ya kisasa ya faksi!a
Hata hivyo, hata waandikaji ambao ni werevu wa ubuni wa sayansi, hawawezi kufikia kuwa manabii wa kweli. Kwa kielelezo, riwaya ya Jules Verne Journey to the Center of the Earth yapendeza kuisoma, lakini wanasayansi sasa wajua kwamba haiwezekani kufanya safari kama hiyo. Wala haielekei kuwezekana kwamba mwaka wa 2001 utaona ama visafari vya angani hadi Sumbula vya vyombo vyenye watu au sayari nyinginezo, kama wengine walivyodokeza mapema.
Waandikaji wa ubuni wa sayansi pia wameshindwa kutabiri mengi ya maendeleo yenye kutazamisha ya kisayansi ambayo yametimia. Katika makala fulani iliyotokea katika The Atlantic Monthly, mwandikaji wa ubuni wa sayansi Thomas M. Disch akubali: “Ebu fikiria kushindwa kwote kwa SF kuwazia muhula wa kompyuta . . . , madhara ya ongezeko la joto tufeni au kuharibiwa kwa tabaka la ozoni au UKIMWI. Ebu fikiria ukosefu wa usawaziko wa muungano wa kisiasa wa serikali. Fikiria mambo yote haya, na kisha uulize kile ambacho SF iliweza kusema kimbele kuyahusu. Yaelekea haikusema chochote.”
Ubuni wa Sayansi—Biashara Kubwa
Bila shaka, kwa mashabiki ubuni wa sayansi si sayansi halisi bali ni utumbuizo. Walakini, kuna wale ambao hushuku thamani yayo katika upande huo pia. Sifa ya ubuni wa sayansi kuwa fasihi hafifu ilianza mapema katika karne hii kwa kuchapishwa kwa magazeti ya hali ya chini ambayo hususa yalikazia ubuni wa sayansi. Ya kwanza kati ya hizi, lile gazeti Amazing Stories, lilianza kuuzwa katika 1926. Mwanzilishi walo, Hugo Gernsback, maarufu kwa kubuni neno lililokuja kuitwa “ubuni wa sayansi.” Wengi walihisi kwamba masimulizi haya ya kiushupavu kwa hakika, yalikuwa na manufaa madogo, ikiwa kulikuwa na yoyote.
Ubuni wa sayansi ulianza kuchukuliwa kwa uzito zaidi baada ya Vita ya Ulimwengu 2. Fungu muhimu ambalo sayansi ilichangia katika vita hiyo lilipatia sayansi hadhi mpya. Matabiri ya waandikaji wa ubuni wa sayansi yakaanza kuonekana yenye kuaminika mno. Basi vijitabu vya ucheshi, magazeti na vitabu vyenye jalada jepesi vya kusoma vya ubuni wa sayansi vikaanza kuwa vingi. Vitabu vya ubuni wa sayansi vyenye jalada gumu vikawa vitabu vyenye kuuzwa sana. Lakini kadiri ubuni wa sayansi ulivyong’ang’ana kutimiza mahitaji ya soko kubwa, ndivyo ubora wa uandishi—na usahihi wa kisayansi—mara nyingi ilivyopuuzwa. Mwandikaji wa ubuni wa sayansi Robert A. Heinlein alalamika kwamba “chochote chenye kusomeka na hata chenye kutumbuiza kwa kiasi” sasa chachapishwa, kutia ndani “idadi kubwa ya riwaya za hali ya chini za kukisia.” Mwandikaji Ursula K. Le Guin aongeza kwamba hata “habari ya hali ya chini” huchapishwa.
Licha ya uchambuzi kama huo, ubuni wa sayansi umefikia vipeo vipya vya umaarufu, ukiwa umepata motisha kuu, si kutokana na wanasayansi, bali kwa biashara ya sinema.
Ubuni wa Sayansi Watokea Sinemani
Filamu za ubuni wa sayansi zimekuwako tangu 1902 wakati Georges Méliès alibuni ile filamu A Trip to the Moon. Kizazi cha baadaye cha vijana waenda-sinema kilisisimuliwa na Flash Gordon. Lakini katika 1968, mwaka mmoja kabla ya mwanadamu kutua mwezini, ile filamu 2001: A Space Odyssey ilitambuliwa kisanaa na ikawa fanikio la kibiashara pia. Hollywood sasa ilianza kutenga pesa nyingi kwa ajili ya filamu za ubuni wa sayansi.
Kufikia mwishoni mwa miaka ya 1970 na mapema miaka ya 1980, filamu kama vile Alien, Star Wars, Blade Runner, na ET: The Extraterrestrial zilichangia nusu ya mapato yote ya kulipia kiingilio ili kutazama sinema katika Marekani. Kwa hakika, ubuni wa sayansi uliandaa moja ya filamu zenye kufanikiwa sana za wakati wote, Jurassic Park. Pamoja na hiyo filamu kukaja kuwa vuvumko la bidhaa za aina 1,000 za Jurassic Park. Si ajabu, televisheni pia imefuata mkondo wa upepo. Yale maonyesho maarufu Star Trek yalitokeza programu kadhaa kuhusu anga za nje.
Walakini, wengi wahisi kwamba ili kutimiza mahitaji mengi kwa sababu ya umaarufu, waandikaji wengine wa ubuni wa sayansi wameridhia sifa ambazo ziliupa ubuni wa sayansi kiwango fulani cha ubora. Mtungaji vitabu Mjerumani Karl Michael Armer adai kwamba ‘ubuni wa sayansi sasa ni biashara maarufu inayotokezwa si na ubora wayo bali na ufundi wa kuuza.’ Wengine hulalamika kwamba wahusika wakuu wa ubuni wa sayansi wa leo, si watu, bali ni miigizo maalum ya kitamasha. Mhakiki mmoja hata asema kwamba ubuni wa sayansi “wakirihisha na ni hafifu katika mengi ya maonyesho yao.”
Kwa kielelezo, nyingi za zile eti huitwa filamu za ubuni wa sayansi kwa hakika hazihusu sayansi wala wakati ujao kamwe. Mipangilio ya wakati ujao nyakati nyingine hutumiwa tu kama mandhari-nyuma ya maonyesho ya waziwazi ya jeuri. Mwandikaji Norman Spinrad aonelea kwamba katika mengi ya masimulizi ya leo ya ubuni wa sayansi, mtu fulani “apigwa risasi, adungwa kisu, avukika, ayeyeyushwa, araruliwa, anyafuliwa, au alipuliwa.” Katika filamu nyingi uhalifu huu huonyeshwa kwa kina chenye kuogofya!
Eneo jingine la kufikiria ni ile nyanja ionyeshwayo uwezo usio wa kawaida ambayo huonyeshwa katika vitabu na filamu kadhaa za fantasia ya sayansi. Ingawa watu wengine huenda waone masimulizi kama hayo kuwa mapambano ya kiistiara tu kati ya wema na uovu, baadhi ya uandishi huu huonekana kuvuka istiara na kukuza mazoea ya uwasiliani-roho.
Uhitaji wa Usawaziko
Bila shaka, Biblia haikatazi utumbuizo wa kimawazo kama vile huenda ikafikiriwa. Katika kielezi cha Yothamu cha miti, mimea isiyoweza kusema yaonyeshwa ikizungumza—hata ikifanya mipango na njama. (Waamuzi 9:7-15) Nabii Isaya vivyo hivyo alitumia mbinu ya mawazio alipoonyesha watawala wa kitaifa waliokufa zamani za kale wakifanya maongezi kaburini. (Isaya 14:9-11) Hata baadhi ya vielezi vya Yesu vilikuwa na sehemu ambayo haingeweza kutukia kihalisi. (Luka 16:23-31) Mbinu za kuwazia kama hizo zilitumika si katika kutumbuiza tu bali katika kushauri na kufundisha.
Waandikaji wengine leo huenda kihalali watumie mipangilio ya wakati ujao kushauri na kutumbuiza. Hata hivyo, wasomaji ambao ni Wakristo wenye kudhamiria wapaswa kukumbuka, kwamba Biblia hutuhimiza kutolea uangalifu mambo ambayo ni safi na yenye kujenga. (Wafilipi 4:8) Pia hutukumbusha: “Dunia yote pia hukaa katika yule mwovu.” (1 Yohana 5:19) Baadhi ya filamu na vitabu vya ubuni wa sayansi hutumika kama njia ya kutoa maoni na falsafa ambazo hazipatani na Biblia, kama vile mageuzi, kutokufa kwa nafsi ya binadamu, na uhai unaourudi kuzaliwa tena. Biblia hutuonya tusiwe windo la “falsafa na uwongo mtupu.” (Wakolosai 2:8, New World Translation) Kwa hivyo tahadhari yahitajika inapohusu ubuni wa sayansi, kama ilivyo na aina zote za vitumbuizo. Twapaswa kuwa wateuzi kuhusu kile ambacho tunasoma au kutazama.—Waefeso 5:10.
Kama ilivyotajwa mapema, filamu nyingi maarufu ni zenye jeuri. Je, kula kwetu lishe la umwagaji-damu wa bure kungempendeza Yehova, ambaye kumhusu husemwa: “Yeyote anayependa jeuri nafsi Yake kwa hakika humchukia”? (Zaburi 11:5, NW) Na kwa kuwa uwasiliani-roho hushutumiwa katika Maandiko, Wakristo wahitaji kuamua vizuri inapohusu vitabu au filamu ambazo huonyesha kiinimacho au ulozi. (Kumbukumbu la Torati 18:10) Ng’amua pia kwamba iwapo mtu mzima anaweza kutofautisha fantasia na uhalisi bila tatizo kubwa, watoto wote hawawezi. Ili kukazia jambo kuu, wazazi wahitaji kuwa macho kuhusu jinsi watoto wao wanavyoathiriwa na kile wanachosoma au kutazama.b
Wengine huenda wakaamua kwamba wanapendelea aina nyingine za usomaji na utumbuizo. Lakini hakuna uhitaji wa watu kama hao kuwa wenye kuhukumu wengine kwa upande huu au kutokeza ubishi juu ya mambo ambayo ni uchaguzi wa kibinafsi.—Warumi 14:4.
Kwa upande mwingine, Wakristo wanaochagua kufurahia aina mbalimbali za ubuni kama kitumbuizo cha mara kwa mara wafanya vema kukumbuka onyo la Sulemani: “Hakuna mwisho wo wote wa kutunga vitabu vingi; na kusoma sana huuchosha mwili.” (Mhubiri 12:12) Wengi katika ulimwengu wa leo kwa wazi wamevuka mipaka katika ujitoaji wao kwa vitabu na filamu za ubuni wa sayansi. Makundi na mikutano ya ubuni wa sayansi vimevuvumka. Kulingana na gazeti la Time, mashabiki wa Star Trek katika kontinenti tano wamejitolea mhanga kujifunza lugha ya kiubuni iitwayo Klingon, ambayo ilionyeshwa katika maonyesho ya Star Trek katika televisheni na filamu. Tabia ya kupita kiasi kama hiyo haipatani na shauri la Biblia kwenye 1 Petro 1:13: ‘Kuwa na usawaziko.’
Hata katika hali yao bora zaidi, ubuni wa sayansi hauwezi kuridhisha udadisi wa wanadamu kuhusu yatakayotokea wakati ujao. Wale ambao kwa hakika wanataka kujua wakati ujao ni lazima wageukie chanzo ambacho ni hakika. Tutazungumzia jambo hili katika makala yetu inayofuata.
[Maelezo ya Chini]
a Kwa maneno ya Verne “simu ya picha [ambayo] yapeleka mbali ishara zozote za mwandiko, sahihi au muundo.”—Newsweek, Oktoba 10, 1994.
b Ona makala “Mtoto Wako Anapaswa Kusoma Nini?” katika toleo la Amkeni! la Machi 22, 1978, (Kiingereza).
[Picha katika ukurasa wa 7]
Wazazi wapaswa kusimamia utumbuizo wa watoto wao
[Picha katika ukurasa wa 7]
Wakristo ni lazima wawe wateuzi inapohusu ubuni wa sayansi