Utafutaji wa Elimu Nzuri
ELIMU nzuri hutayarisha watoto kukabili maisha kwa mafanikio katika jamii ya leo. Huwapa stadi za kielimu, kutia ndani uwezo wa kusoma na kuandika vizuri na kufanya hesabu. Isitoshe, huathiri kushughulika kwao na wengine na huimarisha viwango vifaavyo vya maadili.
Hata hivyo, kwa sababu ya nyakati hizi hatari, ni vigumu sana kuandaa elimu kama hiyo. Mwalimu mmoja mzoefu wa Australia alilalamika hivi: “Madarasa yamefanyizwa na watoto waelekeao kufanya jeuri, wanaotumia lugha chafu na ya matusi; watoto waliochoka kutokana na kukosa usingizi kama tokeo la utazamaji wa televisheni; watoto wenye kukosa lishe bora au wenye njaa; na watoto waliolelewa bila nidhamu.” Na walimu watakwambia kwamba: “Watoto watukutu ni vigumu kuwafundisha.”
Albert Shanker, mkuu wa Shirika la Walimu la Marekani, alifafanua tashwishi ya walimu hivi: “Inawabidi kufunza kuhusu dawa za kulevya na alkoholi, kufunza kuhusu ngono, . . . kufunza ujistahi wa mwanafunzi, kuchungua silaha kikundini, . . . na mambo mengine mengi. Kila kitu isipokuwa kufundisha kwenyewe. . . . Kile ambacho kwa kweli wameombwa wafanye ni kuwa wafanyakazi wa kijamii, akina mama, akina baba, matabibu, polisi, wanalishe, wafanyakazi wa afya wa umma, wastadi wa kitiba.”
Kwa nini jambo hili lahitajika kwa walimu? Muhtasari wa mfanyizo wa darasa moja katika jiji moja kubwa katika kaskazini-mashariki mwa Marekani waonyesha sababu. The New York Times liliripoti taarifa za mtaalamu mmoja kuhusu wastani wa darasa la wanafunzi 23. Yeye alisema kwamba “watoto 8 hadi 15 yaelekea waishi katika umaskini; 3 yaelekea wamezaliwa na akina mama wenye kutumia dawa za kulevya; 15 waishi na wazazi wasio na wenzi.”
Kwa wazi, familia yaelekea kuvunjika. Katika Marekani, karibu 1 wa kila watoto 3 wazaliwao ni haramu, na ndoa 1 katika kila 2 huishia katika talaka. Hata hivyo, asilimia ya kuzaa watoto nje ya ndoa katika Denmark, Ufaransa, Uingereza, na Sweden ni ya juu zaidi. Ni jitihada zipi zinazofanywa ili kukabiliana na matatizo ambayo hali hii yasababisha shuleni?
Kutafuta Masuluhisho
Shule za jaribio na za badala mbalimbali zimeanzishwa. Hizi kwa kawaida huwa ndogo—zikiwezesha usimamizi wa ukaribu zaidi—na nyingi hubuni mfumo wazo wa kielimu ili kutimiza mahitaji ya watoto kwa njia bora zaidi. Katika New York City, shule ndogo kama hizo 48 zimefunguliwa tangu 1993, na 50 zaidi zanuiwa kufunguliwa. “Ni jeuri [ya shuleni] ambayo imefanya jaribio hilo lifanywe,” likaonelea The New York Times. Kufikia 1992 shule za badala zaidi ya 500 zilikuwa zimeanzishwa katika Urusi, zikiwa na zaidi ya wanafunzi 333,000.
Kwa upande ule mwingine, The Toronto Star liliripoti: “Maelfu wawapeleka watoto wao kwenye shule za kibinafsi za kipekee.” Katika mkoa wa Kanada wa Ontario peke yao, karibu watoto 75,000 huhudhuria shule za kibinafsi. Sasa zapatikana pia kotekote katika Urusi, na gazeti China Today lasema kwamba zimetokea katika China “kama vioto vya mianzi baada ya mvua ya masika.” The Handbook of Private Schools huandaa orodha isiyolipiwa ya shule zipatazo 1,700 kama hizo katika Marekani, ambapo malipo ya kila mwaka yaweza kuwa dola 20,000 au zaidi.
Bado wazazi wengine wamechagua kuwafundisha watoto wao nyumbani. Katika Marekani peke yake, yakadiriwa kwamba idadi ya shule za nyumbani imepanda kutoka karibu 15,000 katika 1970 hadi wengi kufikia milioni moja katika 1995.
Matokeo Tofauti
Si mifumo yote ya shule ulimwenguni kote ambayo inapata matokeo sawa. Katika Julai 1993, Shanker alikiambia kikundi cha waelimishaji wa Marekani hivi: “Nchi nyinginezo zinaendeleza shule na zinapata matokeo ambayo kwa msingi ni bora zaidi kuliko yetu.” Kutolea kielezi, alieleza kuhusu kutano moja na mume na mke fulani kutoka Urusi waliohamia Marekani. Yeye alisimulia hivi: “Walisema kwamba hata ingawa mtoto wao yuko katika shule ya kibinafsi nzuri sana, kijana wao wa darasa la nane alikuwa akijifunza yale ambayo alikuwa amejifunza katika darasa la tatu huko Urusi.”
Ule uliokuwa Muungano wa Sovieti ulisitawisha mfumo wa shule ambao ulifunza karibu watu wao wote kusoma na kuandika. Kwa upande ule mwingine, kulingana na kadirio la Idara ya Elimu ya Marekani, Wamarekani milioni 27 hawawezi kutambulisha ishara ya barabara au nambari kwenye basi. Canberra Times la Australia liliripoti kwamba “asilimia ya juu kufikia 25 ya watoto wa shule za msingi walikuwa katika shule za sekondari bila kuweza kusoma na kuandika.”
Kwa kiwango fulani matatizo shuleni sasa yako karibu kila mahali. Katika kitabu Education and Society in the New Russia cha 1994 chasema kwamba “asilimia 72.6 ya walimu wa Sovieti waliohojiwa walikubali kwamba mfumo wa elimu ulikuwa katika matatizo makali.” Kulingana na Tanya, mwalimu mzoefu katika Moscow, kisababishi kikuu cha matatizo ni kwamba “wazazi na wanafunzi wenyewe hawaheshimu elimu kamwe.” Kwa kielelezo, yeye alionelea kwamba “mwalimu hupata mshahara ambao ni nusu ya ule wa kawaida wa dereva wa basi—au hata chini ya huo.”
Elimu Nzuri Ni Muhimu
Kadiri jamii ya kibinadamu izidivyo kuwa tata, ndivyo elimu nzuri inavyokuwa na umuhimu mkubwa. Katika mahali pengi kiasi cha elimu kinachotakwa ili kumwezesha kijana kupata kazi ambayo itamtegemeza na familia ya wakati ujao kimekuwa cha juu zaidi. Hivyo basi, wale ambao wamepata stadi za msingi za elimu watakuwa na nafasi bora zaidi za kupata kazi. Mahususi waajiri wanahangaikia lile jambo la msingi—mwomba kazi aweza kufanya kazi vizuri kadiri gani.
Msimamizi wa ofisi ya kuhudumia kazi alionelea hivi kuhusu wahitimu wengi wa shule za sekondari: “Hawajafunzwa kufanya kazi.” Yeye aliongezea hivi: “Katika kushughulika na vijana tatizo ambalo daima waajiri hunielezea ni kwamba hawawezi kusoma au kuandika vizuri. Hawawezi kujaza fomu ya kuomba kazi.”
Wazazi kwa hakika watataka elimu nzuri kwa ajili ya watoto wao, na walio wachanga kwa hekima watataka elimu kwa ajili yao. Lakini ni muhimu kwamba watumie funguo zinazofaa. Funguo hizi ni zipi, na zaweza kutumiwaje?
[Blurb katika ukurasa wa 6]
Katika Urusi, “mwalimu hupata mshahara ambao ni nusu ya ule wa kawaida wa dereva wa basi”