Shule Zina Shida Kubwa
Wazazi hupeleka watoto wao shuleni si kujifunza kusoma, kuandika, na kuhesabu tu. Wao hutarajia shule ziandae elimu kamili, ya kutayarisha vijana wawe watu wazima ambao wazazi waweza kujivunia. Lakini mara nyingi tarajio lao halitimizwi. Kwa nini? Kwa sababu shule ulimwenguni pote zina shida kubwa.
KATIKA nchi nyingi ukosefu wa fedha na walimu pia huhatarisha elimu ya watoto. Kwa kielelezo, kotekote Marekani, kuzorota kwa hali ya fedha miaka ya majuzi kulilazimisha shule fulani ‘zitie majalada mapya kwenye vitabu vya mafundisho badala ya kununua vipya, ziachilie rangi ya dari itoketoke, zikomeshe masomo ya sanaa na programu za michezo, au zisisomeshe siku nyingi mfululizo,’ lasema gazeti Time.[1]]
Katika Afrika, fedha za elimu ni kidogo sana. Kulingana na Daily Times la Lagos, nchi ya Nigeria ina mwalimu 1 kwa kila wanafunzi 70, “kukiwa na uelekeo thabiti kwamba mmoja kati ya kila walimu watatu hajahitimu.”[2] Katika Afrika Kusini—mbali na upungufu wa walimu—madarasa yaliyosongamana mno na msukosuko wa kisiasa huchangia kile ambacho South African Panorama hukiita “mchafuko katika shule za weusi.”[3]
Bila shaka, shule yenye utoshelevu wa wafanyakazi na vifaa haihakikishii mafanikio ya kielimu. Kwa kielelezo, katika Austria karibu theluthi ya vijana wa miaka 14 wasemekana hawawezi kufanya hesabu sahili wala kusoma ifaavyo.[4] Katika Uingereza, kadiri za kupita mitihani kwa wanafunzi katika hisabati, sayansi, na lugha ya taifa “iko nyuma sana ya zile zilizo Ujerumani, Ufaransa na Japani,” lasema The Times la London.[5]
Katika Marekani, walimu hulalamika kwamba ingawa wanafunzi hupata alama nyingi katika mitihani, wengi huwa bado hawawezi kuandika insha nzuri, kutatua matatizo ya hesabu, au kutayarisha muhtasari wa mambo muhimu ya masomo au hati mbalimbali.[6] Kwa hiyo, wakuu wa elimu ulimwenguni pote wanachunguza upya kisomo cha shule na njia zitumiwazo kukadiria maendeleo ya mwanafunzi.
Jeuri ya Shule
Ripoti zaonyesha jeuri ni nyingi kadiri ya kuogofya shuleni na inaongezeka. Katika Ujerumani, kongamano moja la walimu liliambiwa kwamba asilimia 15 ya watoto wa shule ‘wako tayari kwa vyovyote kugeukia jeuri—na asilimia 5 hawajiepushi hata na vitendo vya ukatili wa kupindukia, kwa kuwa wangeweza kupiga teke mtu hoi aliyelala sakafuni.’—Frankfurter Allgemeine Zeitung .[7]
Visa kimoja-kimoja vya ukatili wa kupindukia huamsha hangaiko kubwa. Kunajisiwa chooni kwa msichana wa miaka 15 na vijana wanne katika shule ya sekondari ya Paris kulifanya wanafunzi waandamane barabarani kudai usalama mkali zaidi shuleni.[8] Wazazi huhangaishwa na ongezeko la visa vya kutendwa vibaya kingono, kutendeshwa mambo ya hisani kwa kutishwa, na jeuri ya kihisia-moyo.[9] Visa hivyo havitukii Ulaya tu bali vinazidi kuongezeka ulimwenguni pote.
Wizara ya Elimu ya Japani yaripoti vuvumko la jeuri inayohusisha wanafunzi wa vidato vya chini na juu vya shule ya sekondari.[10] Gazeti The Star la Afrika Kusini, chini ya kichwa “Wanafunzi Wachukua-Bunduki Watawala Shule,” lilifananisha hali ya madarasa ya Soweto na enzi za “Uhayawani wa Magharibi” katika Marekani karne ya 19.[11] Hata sasa, kulingana na maneno ya The Guardian la London, sifa ya jeuri ya New York City imefikia “kilele kipya ilipotangazwa na shirika moja la usalama kwamba mavazi yasiyopenywa na risasi yanaagizwa upesi kwa wingi kwa ajili ya watoto wa shule.”[12]
Uingereza pia yasumbuliwa na pigo la jeuri shuleni. “Katika miaka 10 iliyopita,” asema ofisa mmoja wa chama cha walimu, “tumeona elekeo lenye kuongezeka la kugeukia silaha. Limefikia walio wachanga zaidi pia na visa vinaenea kati ya watu wa kike pia hali moja na wa kiume.”[13]
Basi, si ajabu kwamba wazazi kadhaa huamua kuondoa watoto wao shuleni na kuwafundishia nyumbani.a Mara nyingi wale waonao kwamba hilo halifai huhangaishwa na matokeo mabaya ya shule juu ya watoto wao, nao hushangaa walizuieje. Wazazi waweza kufanya nini wasaidie watoto wao washughulike na matatizo wakabiliyo shuleni? Na wazazi waweza kushirikianaje na walimu kuhakikisha kwamba watoto wafaidika kabisa na shule? Makala zinazofuata zatoa majibu kwa maswali hayo.
[Maelezo ya Chini]
a Makala “Kusomea Nyumbani—Je! Kunakufaa Wewe?” iliyochapishwa katika Amkeni! la Aprili 8, 1993, yapitia chaguo hili.