La Kwanza Katika Mali
MUME wangu hutumikia akiwa mwangalizi asafiriye wa Mashahidi wa Yehova katika Mali, nchi iliyo na idadi ndogo ya watu magharibi mwa Afrika. Sehemu yayo ya kaskazini imefunikwa na Jangwa la Sahara, na sehemu kubwa iliyobaki ya nchi ni bara lenye nyasi na miinuko na mabonde. Mali ni kubwa kuliko Uingereza, Ufaransa, na Hispania zikiunganishwa. Ingawa nchi hizi zina wakazi zaidi ya 140 milioni, Mali ina idadi ya watu milioni kumi tu—ambao kati yao 150 ni Mashahidi.
Makao yetu ambayo kutoka kwayo tulianzia shughuli ni Ziguinchor, jiji dogo linalopakana na Senegal. Mnamo Novemba 1994 tulikwenda kwa ndege kutoka hapo hadi Dakar, kisha tukaendelea hadi jiji kuu la Mali, Bamako, jiji kubwa lenye wakazi zaidi ya nusu milioni. Kutoka Bamako tulisafiri ama kwa teksi ya jangwa, basi, au gari-moshi hadi kwa majiji madogo zaidi, kama vile Ségou, San, na jiji la kale la Mopti. Tulikaa katika kila mahali hapo kwa juma moja hivi ili kushiriki katika huduma ya Kikristo pamoja na Mashahidi wachache huko.
Katika Desemba tulirudi Bamako kufurahia mkusanyiko wa wilaya, ambao ulikuwa na kilele cha hudhurio la watu 273. Jinsi tulivyofurahi kuona wapya 14 wakibatizwa! Siku baada ya mkusanyiko, tuliondoka kwa basi kuelekea jiji la Sikasso, ambapo Jumba la Ufalme la kwanza katika Mali lililojengwa na Mashahidi wa Yehova lilipangiwa kuwekwa wakfu mwisho-juma uliofuata.
Tatizo Kweli
Kutaniko katika Sikasso lina Mashahidi 13 tu, 5 wao ambao ni mapainia, au wahudumu wa wakati wote. Tunapofika Jumatatu, tuna hamu ya kujua mipango yao ni nini kwa ajili ya uwekaji wakfu. Wanatuambia kwamba wanamtegemea mume wangu Mike, ili kuupangia! Kwa hiyo baada ya kufungua mizigo yetu, tunakwenda kutazama hilo Jumba la Ufalme. Tunapoliona, tunafurahi sana kwamba jengo kama hilo lingeweza kujengwa na Mashahidi hawa wachache. Hata hivyo, bado kuna mengi ya kufanywa. Hakuna pazia, sehemu ya nje haijapakwa rangi, na hakuna kibao cha ishara “Jumba la Ufalme la Mashahidi wa Yehova.”
Twagundua kwamba kwa muda wa siku chache, angalau wageni 50 wanakuja kutoka Bamako ili kuhudhuria uwekaji wakfu. Watu wenyeji pia wamealikwa. Hilo kutaniko lina mzee mmoja tu, Pierre Sadio. Tunapomuuliza anatarajia vipi kumaliza jumba kabla ya Jumamosi, siku ya uwekaji wakfu, marafiki wanasonga karibu ili kusikia jibu lake. “Nafikiri Yehova atatusaidia kulimaliza kwa wakati,” yeye ajibu.
Kuna mengi yanayohitajiwa kufanywa katika kipindi hicho kidogo cha wakati! Ninauliza kwa kusita ikiwa naweza kusaidia kutoa pazia. Tabasamu kubwa la kitulizo laonekana katika nyuso zilizo karibu nami. Kisha Mike adokeza kwamba tutengeneze kibao cha ishara kwa ajili ya sehemu ya mbele ya jumba. Mara sote twaongea kwa wakati mmoja. Kila mtu amesisimka sana. Litakuwa tatizo kweli kumalizia sehemu ndogo-ndogo zilizobaki za jumba kwa wakati!
Hekaheka za Utendaji
Sisi akina dada Wakristo twakimbia sokoni kutafuta kitambaa. Baadaye twamtafuta fundi wa kushona ili ashone pazia. “Una siku nne kuzimaliza,” twamwambia. Ili kutayarisha kitu chenye umaridadi, Mike ajitolea kutengeneza kining’inizi cha mmea cha macramé chenye kuvutia kwa ajili ya upande wa mbele wa jumba. Kwa hiyo tunaenda tena, wakati huu kutafuta kamba inayohitajika kwa ajili ya kining’inizi cha mmea na vilevile kutafuta chungu cha maua.
Mipango pia inafanywa ili mtu atengeneze kibao cha ishara cha Jumba la Ufalme. Ndani na nje ya jumba, kuna hekaheka za utendaji. Kikundi cha majirani kinakusanyika ili kutazama. Kuna mengi mno ya kufanya! Tutawalishaje wale wageni 50? Watalala wapi? Tunakwenda kasi juma lote kutayarisha, lakini hakuna chochote kinachoonekana kwenda sawa.
Tunarauka Ijumaa, siku moja kabla ya uwekaji wakfu. Wote wamejawa msisimko kwa sababu wageni kutoka Bamako watafika. Adhuhuri hivi kibao cha ishara ya Jumba la Ufalme chafika. Mike anapokifunua, akina ndugu watweta kwa kuvutiwa. Hata watazamaji wenye udadisi wanatazama kwa uthamini. Twangojea bila subira kinapowekwa kwenye ukuta wa mbele. Sasa ni dhahiri kwamba hili si jengo la kawaida tu. Ni “Jumba la Ufalme la Mashahidi wa Yehova.”
Karibu na hapo, kwenye nyumba ya painia, akina dada wana shughuli nyingi wakipika. Nyungu kubwa nyeusi yafurika ikichemka kwa chakula. Tunamaliza kuondoa ndoo za rangi na fagio kando ya jumba wakati makelele yanasikika: “Wamefika! Wamefika!” Mashahidi wanakuja wakikimbia kutoka kwenye jumba, wengine kutoka ndani ya nyumba. Majirani wanashangazwa kwa hayo yote. Akina ndugu wacheza-cheza kwa msisimko. Ni ukaribishaji ulioje wanaopokea hao Mashahidi wanapotoka katika basi! Najihisi nikiwa mwenye fahari sana kuwa mmoja wa Mashahidi wa Yehova.
Natazama wageni wote, mashahidi kutoka makabila ya wenyeji, na vilevile kutoka Burkina Faso na Togo. Wafaransa, Wajerumani, Wakanada, na Wamarekani wamekuja pia. Usiku huo tunakuwa na sherehe kubwa. Tunawasha moto mkubwa ili kuangaza uga. Nahisi kujifinya ili kuhakikisha kwamba nina pendeleo kweli la kuwa sehemu ya tukio hili. Usiku unapoendelea kupita, tunaanza kuondoka bila haraka kuelekea mahali petu pa kulala.
Watu wengi kufikia 20 wanakaa katika kao moja. Naweza kuona ni vigumu kwa wengine. Naona dada mwenyeji akimpeleka mgeni Mfaransa kwenye choo cha nje. Huyo mgeni ni mtu wa ukoo wa mmoja wa wamishonari, lakini mwenyewe si Shahidi. Wanaporudi, yeye asema: “Nyinyi watu ni maskini mno, lakini mna upendo na ni wenye fadhili kikweli.” Nahisi kusema: “La, si maskini. Watu wote wa Yehova ni matajiri!” Kwa kweli, ni wapi pengine uwezapo kuona kikundi cha watu kinachotofautiana kama hicho kikiishi kwa amani na upatano?
Uwekaji Wakfu Wenye Kugusa Moyo
Usiku ni mfupi, na siku ya uwekaji wakfu inafika haraka. Baada ya mkutano kwa ajili ya huduma ya shambani kwenye Jumba la Ufalme, Mashahidi wanaenda nje na kualika watu wa mjini kuja kwenye uwekaji wakfu. Nabaki ili kupanga maua na mimea. Akina dada wenyeji wana pilikapilika za kupika kwa ajili ya jioni.
Mwishowe, saa kumi kamili, wakati wa uwekaji wakfu wawadia. Kuna jumla ya watu 92, hata hivyo jumba halijasongamana. Nimesisimka sana hivi kwamba ni vigumu kuketi tuli. Pierre Sadio atoa historia ya kazi katika Sikasso. Alipopewa mgawo wa hapa, walikuwa yeye na mkeye na watoto wao wawili tu. Maisha yalikuwa magumu sana, lakini kwa wakati Yehova alibariki utumishi wao. Mtu wa kwanza kuwa Shahidi katika Sikasso sasa ni painia wa pekee. Kisha Pierre anaeleza jinsi Mashahidi wachache walivyoweza kujenga. Waliajiri mwashi, na kila Jumapili kutaniko lote lilifanya kazi siku nzima katika huo mradi.
Sasa Mike anahoji Mashahidi waliofanya kazi katika jumba hilo. Yeye auliza mmoja baada ya mwingine ikiwa walipata kufikiri kama siku hii ingefika na jinsi wanavyohisi wanapotazama Jumba la Ufalme lililojaa watu. Wengi wanazibwa kabisa kwa hisia hivi kwamba hawawezi kumaliza maelezo yao. Miongoni mwa Mashahidi waliopo, hakuna jicho lisilo na machozi.
Kisha hotuba ya uwekaji wakfu inatolewa na Ted Petras kutoka ofisi ya tawi ya Mashahidi wa Yehova katika Senegal. Sala ya uwekaji wakfu yatolewa, na akina ndugu wanapiga makofi kwa kipindi kirefu sana. Baadaye Mike anakaribisha kila mtu aliyesaidia kujenga hilo jumba aje mbele. Wanasimama hapo, nyuso zao ziking’aa, machozi ya shangwe yakitiririka mashavuni mwao. Tunapoimba wimbo wa kumalizia, ninahisi furaha sana. Kuwa mishonari kunaniwezesha kushiriki maono mengi mazuri ajabu. Tungekosa mengi mno kama tungebaki nyumbani Marekani.
Ushirika Zaidi Wenye Uchangamfu
Baada ya wakfu, viburudisho vyaandaliwa. Akina dada wanafuatana kwa mlolongo wakibeba sahani kubwa za matikiti vichwani mwao. Wanafuatwa na akina ndugu wawili, waliovalia kofia za mpishi kwa ajili ya pindi hii na wakiwa wamebeba sahani kubwa za keki. Keki hizo tambarare zimepambwa kwa njia nzuri na vipande vya machungwa na limau. Mazingira yote ni ya kisherehe sana.
Wageni wanaondoka baada ya kupewa chakula. Kisha Mashahidi wanakwenda kwa nyumba ya mapainia kwa ajili ya mlo wa jioni. Sote twakaa nje chini ya mwezi mpevu, moto wenye kuvuma ukiangaza uga. Nimesisimka na kuchoka sana kutokana na utendaji wa siku hivi kwamba siwezi kumaliza chakula changu. Nampa msichana mdogo mguu wa kuku ulioliwa nusu. Mapainia wenyeji wanatazama sahani zetu, na ikiwa kuna chochote kilichobaki, wanakimaliza. Hakuna cha masalio huku. Tumezoea vibaya sana katika Marekani.
Jioni yetu inapomalizika, ndugu mmoja anawakumbusha wale wanaotoka Bamako kwamba basi litawachukua 3:15 asubuhi. Asubuhi ifuatayo akina ndugu hao wanaketi kote ugani, wakingoja basi lifike. Halafu twaimba wimbo mmoja wa mwisho, “Asante, Yehova.” Machozi yaanza kutiririka, na tunapomaliza tu, basi laonekana. Akina ndugu na dada wote wanakumbatiana.
Tunasimama hapo tukipunga mikono huku basi likiondoka polepole. Wote katika basi wanapunga mikono hadi linapotoweka. Baada ya hilo, wote tuliobaki tunageuka na kutazamana. Ulikuwa uwekaji wakfu mzuri ajabu na juma zuri ajabu.—Imechangwa.
[Picha katika ukurasa wa 15]
Jumba la Ufalme la kwanza lililojengwa na Mashahidi wa Yehova katika Mali
[Picha katika ukurasa wa 16]
Kikundi hiki chenye furaha kilisafiri kwa basi