Maoni ya Biblia
Jambo la Kufanya Unapoudhi Wengine
MAMBO si mazuri. Wewe wajua tu. Ndugu yako Mkristo anakuepuka kimakusudi. Yeye hajasema kile kinachomsumbua, lakini yeye hukusalimu kijuujuu tu—na ni wakati tu unapomsalimu kwanza! Je, umwendee ili upate kujua tatizo ni nini?
‘Hilo ni tatizo lake,’ huenda ukafikiri. ‘Ikiwa ana neno juu yangu, yeye apaswa aje aongee nami kulihusu.’ Kwa kweli, Biblia humtia moyo mtu anayeudhika achukue hatua ya kwanza na kufanya amani na ndugu yake. (Linganisha Mathayo 18:15-17.) Lakini namna gani mtu mwenye kuudhi? Yeye ana daraka jipi, ikiwa analo lolote?
Katika Mahubiri ya Mlimani yake, Yesu alisema hivi: “Basi ukileta sadaka [“zawadi,” NW] yako madhabahuni, na huku ukikumbuka ya kuwa ndugu yako ana neno juu yako, iache sadaka [“zawadi,” NW] yako mbele ya madhabahu, uende zako, upatane kwanza na ndugu yako, kisha urudi uitoe sadaka [“zawadi,” NW] yako.” (Mathayo 5:23, 24) Ona kwamba hapa maneno ya Yesu yanaelekezewa mtu mwenye kuudhi. Yeye ana daraka jipi ili kusuluhisha hilo jambo? Ili kujibu hilo, acheni tufikirie maana ya maneno ya Yesu kwa wasikilizaji wake Wayahudi wa karne ya kwanza.
‘Kuleta Zawadi Yako Madhabahuni’
Hapa Yesu atoa ufafanuzi wa wazi: Mwabudu Myahudi amekuja Yerusalemu kwa ajili ya mojawapo sikukuu za kila mwaka. Yeye ana zawadi—yaelekea ni mnyama—wa kudhabihu kwa Yehova.a Kutoa dhabihu hakukuwa kwa vyovyote desturi isiyo na maana. Kitabu Judaism—Practice and Belief chaeleza hivi: “Kuchagua makafara wanono, wasio na waa, kuwaona wakichunguzwa na wastadi, kutembea nao hadi yadi chache tu mbele ya madhabahu yenye kuwaka moto, kuwakabidhi, kuweka mikono kichwani [pa mnyama], kuungama uchafu au hatia fulani, au ama sivyo kumweka wakfu huyo mnyama, kumkata koo, au hata kumshika tu—hayo yalihakikisha umaana na hali yenye kicho ya wakati huo. . . . Hakuna mtu mwenye kuamini kwamba Mungu alikuwa ameamuru utaratibu huo wote . . . angeweza kuufanya bila kuhusika kihisiamoyo.”
Hivyo maneno ya Yesu kwenye Mathayo 5:23, 24 yawapeleka wasikilizaji wake hadi wakati uliojaa maana na kicho kwa mwabudu Myahudi. Msomi mmoja wa Biblia hufafanua mandhari hiyo hivi: “Mwabudu ameingia Hekaluni; yeye amepitia mfululizo walo wa nyua, Ua wa Wasio Wayahudi, Ua wa Wanawake, Ua wa Wanaume. Baada ya hapo kulikuwa na Ua wa Makuhani ambao katika huo watu wa kawaida wasingeweza kuingia. Mwabudu amesimama kwenye kitalu, akiwa tayari kumkabidhi kafara wake kwa kuhani; mikono yake iko juu ya [kichwa cha mnyama] ili kuungama.”
Kwenye wakati huo muhimu, mwabudu akumbuka kwamba ndugu yake ana neno juu yake. Huenda ikawa dhamiri yake mwenyewe yamwambia hilo, au huenda ikawa yeye amehisi kutokana na mtazamo wa ndugu yake kumwelekea, kwamba kuna hisia fulani ya kuudhika. Yeye afanye nini?
‘Iache Zawadi Yako Uende Zako’
“Iache sadaka [“zawadi,” NW] yako mbele ya madhabahu,” Yesu aeleza, “uende zako.” Kwa nini? Ni nini kingekuwa cha maana zaidi wakati huo kuliko kumtolea Yehova dhabihu? “Kwanza fanya amani yako na ndugu yako,” (NW) Yesu aendelea kueleza, “kisha urudi uitoe sadaka [“zawadi,” NW] yako.” Kwa hiyo huyo mwabudu aacha toleo lake likiwa hai kwenye madhabahu ya toleo la kuteketezwa naye aenda zake kumtafuta ndugu yake aliyeudhika.
Kwa kuwa ni sikukuu, ndugu yake aliyeudhika bila shaka yumo miongoni mwa wasafiri ambao wamemiminikia Yerusalemu. Kukiwa na barabara nyembamba na nyumba ambazo zimesongamana pamoja, Yerusalemu lina wakazi wengi. Lakini hii ni sikukuu, na jiji limejaa wageni.b
Hata ikiwa watu kutoka mji mmoja walisafiri na kupiga kambi pamoja, kupitia hilo jiji lililosongamana watu ili kumtafuta mtu fulani kungehitaji jitihada fulani. Kwa kielelezo, wakati wa Sikukuu ya Vibanda, wageni walijenga vibanda kotekote jijini na barabarani na bustanini kuzingira Yerusalemu. (Mambo ya Walawi 23:34, 42, 43) Hata hivyo, mwabudu Myahudi anapaswa amtafute ndugu yake aliyeudhika mpaka ampate. Kisha nini?
“Fanya amani yako na ndugu yako,” (NW) asema Yesu. Usemi uliofasiriwa “fanya amani yako” hutokana na kitenzi (di·al·lasʹso) kinachomaanisha “‘kuleta geuzo, kubadilishana,’ na kwa hiyo, ‘kupatanisha.’” Akiwa amejitahidi sana kumtafuta ndugu yake aliyeudhika, huyo mwabudu Myahudi anajaribu kufanya amani naye. Kisha, asema Yesu, yeye aweza kurudi hekaluni na kutoa zawadi yake, kwa maana sasa Mungu ataikubali.
Hivyo maneno ya Yesu kwenye Mathayo 5:23, 24 hufundisha somo muhimu: Upatanisho, au amani, huja kabla ya dhabihu. Njia ambayo sisi huwatendea waabudu wenzetu inahusiana moja kwa moja na uhusiano wetu na Mungu.—1 Yohana 4:20.
Jambo la Kufanya Unapoudhi Wengine
Namna gani basi, ukijipata mwenyewe katika hali iliyofafanuliwa mwanzoni mwa makala hii—unahisi kwamba umemuudhi mwabudu mwenzako? Wapaswa kufanya nini?
Ukitumia shauri la Yesu, chukua hatua ya kwanza ya kumwendea ndugu yako. Ukiwa na lengo jipi? Kumsadikisha kwamba yeye hana sababu ya kuudhika? La hasha! Huenda tatizo likawa kubwa zaidi ya kutoelewana kuliko sahili. “Fanya amani yako,” (NW) akasema Yesu. Ikiwezekana, ondoa uadui kutoka moyoni mwake. (Warumi 14:19) Ili kutimiza hilo, huenda ukahitaji kukiri, wala si kukanusha, hisia zake za kuudhika. Huenda ukahitaji pia kuuliza hivi, ‘Naweza kufanya nini ili kusahihisha mambo?’ Mara nyingi, kuomba radhi kwa moyo mweupe ndiko kunakohitajiwa tu. Hata hivyo, katika visa vingine mtu aliyeudhika huenda akahitaji wakati fulani ili kutuliza hisia zake.
Lakini, namna gani ikiwa zijapokuwa jitihada za mara kwa mara wewe huwezi kuleta upatanisho? Warumi 12:18 husema hivi: “Kama yamkini, kwa upande wenu, mkae katika amani na watu wote.” Hivyo waweza kuwa na uhakika kwamba maadamu umejitahidi sana kufanya amani, Yehova atapendezwa kukubali ibada yako.
[Maelezo ya Chini]
a Wakati wa kawaida wa kuleta matoleo ya kidhabihu ulikuwa wakati wa zile sikukuu tatu za kimsimu—Sikukuu ya Kupitwa, Sikukuu ya Pentekoste, na Sikukuu ya Vibanda.—Kumbukumbu la Torati 16:16, 17.
b Makadirio huwa tofauti-tofauti kwa habari ya idadi ya wasafiri waliomiminikia Yerusalemu la kale kwa ajili ya sikukuu mbalimbali. Mwanahistoria Myahudi wa karne ya kwanza Yosefu alikadiria kwamba Wayahudi wapatao milioni tatu walikuwapo kwa ajili ya Sikukuu ya Kupitwa.—The Jewish War, 2, 280 (14, 3); 6, 425 (9, 3).