Jilinde na Umeme!
NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA SWEDEN
MMWEKO wa wastani wa umeme waweza kuwa na makumi ya mamilioni ya volti za umeme zenye makumi ya maelfu ya ampea za umeme. Kwa kulinganisha, mzunguko wa kawaida wa umeme wa nyumba kwa kawaida huwa wa kiwango cha ampea 15.a Waweza kufanya nini ili kupunguza hatari ya kupigwa na umeme? Ona madokezo yafuatayo.
• Ikiwezekana, ingia kwenye nyumba. Hata gari laweza kutoa ulinzi mzuri. Namna gani kuwa ndani ya jengo ndefu? Jengo ndefu lenye vipitisha umeme laweza kuwa mahali salama. Kwa kielelezo, Empire State Building katika New York City huokoka kupigwa na umeme karibu mara 25 kila mwaka. Hata hivyo, ni vizuri kuepuka majengo yasiyo na vipitisha umeme na vyenye paa za vyuma pamoja na kuwa karibu na erieli na nyua za chuma.
• Ondoka kwenye maeneo yaliyo wazi, kama vile bahari, viwanja, na wanja za mchezo wa gofu. Miti mirefu, inayosimama peke yayo yaweza pia kuwa hatari. Ikiwa uko kwenye eneo lenye miti mingi, jikinge mvua karibu na ile mifupi kabisa. Ikiwa dhoruba inakaribia sana nawe huwezi kuondoka kwenye eneo lililo wazi, chuchumaa chini kwenye ardhi na kukumbatia magoti yako. Usilale chini, kwa kuwa ni muhimu kubakiza sehemu ndogo iwezekanavyo iwezayo kupigwa.
• Hata unapokuwa ndani ya nyumba, unaweza kujihadhari. Yafuatayo ni madokezo machache: Jaribu kuepuka kugusa vipitisha umeme, kama vile meko na mabomba ya maji. Lingekuwa jambo la hekima kuepuka kuoga, na pia jaribu kutotumia simu. Toa kompyuta, televisheni, na vyombo vingine kwenye plagi, kwa kuwa vingeweza kuharibiwa iwapo nyumba inapigwa na umeme.
• Mtu akipigwa na umeme, ni muhimu kumhuisha apumue tena (CPR) upesi. Profesa Victor Scuka anayefanya kazi kwenye Idara ya Utafiti wa Umeme Mwingi ya Chuo Kikuu cha Uppsala, Sweden, anasema kwamba katika visa vingi majeruhi wengi wamesaidiwa na CPR, hata wakati ambapo walionekana kana kwamba wamekufa. “Lakini matibabu,” yeye aonya, “lazima yatolewe mara moja ili kuepuka madhara kwenye ubongo.”
Unapokumbwa na dhoruba yenye umeme, tumia tahadhari ambazo zimetoka kutajwa. Nawe yaelekea utaepuka kuwa jeruhi wa wonyesho huu wenye kuhofisha.
[Maelezo ya Chini]
a Ampea ni kizio cha mtiririko-umeme, kiwango cha mkondo-umeme kinachotumika. Volti huonyesha nguvu za mkondo-umeme. Ona Amkeni! la Februari 22, 1985, kurasa 26-27, Kiingereza.