Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g99 4/8 kur. 13-16
  • Mvua ya Radi—Mfalme wa Kutisha wa Mawingu

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Mvua ya Radi—Mfalme wa Kutisha wa Mawingu
  • Amkeni!—1999
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Jinsi Mvua ya Radi Inavyotokea
  • Fataki Katika Anga
  • Faida Kubwa Zaidi ya Dhoruba
  • Namna Gani Mvua ya Mawe?
  • Chamchela na Mvua ya Radi
  • Jilinde na Umeme!
    Amkeni!—1996
  • Yaani Kunanyesha Tena?
    Amkeni!—2004
  • Maajabu ya Uumbaji Humtukuza Yehova
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2005
  • Zingatia Kazi za Mungu za Ajabu
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2001
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1999
g99 4/8 kur. 13-16

Mvua ya Radi—Mfalme wa Kutisha wa Mawingu

Na mleta-habari wa Amkeni! katika Australia

WATU wengi wamevutiwa sana na mawingu tangu walipokuwa watoto. Mtu mmoja mwenye umri wa miaka 80 asimulia jinsi ambavyo angelala kwenye nyasi mara nyingi alipokuwa mtoto na kutazama mawingu “yakijipanga kwenye anga,” kama asemavyo. Yeye akumbuka akiwazia mara nyingi kinachoyafanyiza mawingu. Je, yalikuwa pamba? Ni kwa nini kila wingu lilionekana tofauti sana? Wingu lile lilifanana na meli yenye matanga, lile nalo lafanana na farasi anayerukaruka. Kisha likatokea wingu jingine linalofanana na jumba kubwa linalopanuka. Mawingu hayo yaliendelea kufurahisha fikira zake za kitoto yalipokuwa yakielea katika anga yakiwa na ukubwa na maumbo yenye kubadilika-badilika. Yeye asema kwamba, hadi leo, bado yeye hufurahia kutazama mawingu yanapoonekana kana kwamba “yanacheza mchezo wa kuigiza bubu” katika anga. Labda hata wewe unapendezwa na jambo hili.

Hata hivyo, huenda ikawa mawingu yenye kuvutia zaidi na yenye kutisha zaidi ni yale yanayoweza “kuzungumza.” Yanaitwa cumulonimbus, au mawingu ya mvua ya ngurumo na radi. Mawingu haya meusi na yenye kutisha yanaweza kufikia kimo cha kilometa 16 au zaidi kwenda juu angani, nayo ndiyo husababisha mvua ya radi. Mawingu ya dhoruba yakusanyikapo katika anga yanaweza kuangaza kwa mpigo wa radi na kutoa ngurumo za radi. Wakati wa usiku ngurumo na radi zaweza kutokeza wonyesho wenye kustaajabisha wa sauti na mwangaza wa ajabu, jambo ambalo lapita maonyesho yoyote ya fataki ya mwanadamu. Hunyesha mvua ya mawe na kisha huelekea sehemu nyingine, mara nyingi ikitokeza harufu safi ya mvua kwenye ardhi iliyokuwa imekauka.

Jinsi Mvua ya Radi Inavyotokea

Katika nyakati za juzi mwanadamu amefaulu kuiona Dunia-Sayari kutoka angani. Anapotazama anaona utando wa mawingu ukifunika sehemu kubwa ya uso wa dunia. Mwandishi Fred Hapgood anatufahamisha kwamba “kwa wakati wowote ule, nusu ya uso wa tufe, eneo la kilometa za mraba milioni 250, huwa limefunikwa kwa [mawingu]—mengine yakiwa membamba, yenye mviringo, yamelaliana, yamechomoza, yamefanana na kamba, na pamba, na yote yakiwa na mng’ao mbalimbali na weusi mbalimbali, yakienea, kupaa na kutoweka ulimwenguni kote.” Mvua za radi huwa sehemu ya mawingu haya makubwa—kwa kweli, kila mwaka duniani kuna visa vipatavyo 15,000,000 vya mvua ya radi, na visa 2,000 huwapo wakati wowote ule.

Mvua ya radi hutokea wakati ambapo hewa baridi iliyo nzito inapolalia hewa yenye unyevunyevu iliyo nyepesi. Hali yoyote kama vile, joto la jua, mpaka baina ya halihewa zilizo tofauti, au mwinuko wa ardhi, huifanya hewa yenye unyevunyevu na joto ipande kupitia hewa baridi. Hiyo hutokeza mkondo wa hewa, na nishati ya joto iliyo ndani ya hewa hiyo na katika mvuke hubadilishwa na kuwa upepo na nishati ya umeme.

Kwa kawaida hali za hewa zinazohitajiwa ili kutokeza mvua ya radi hupatikana katika maeneo yaliyo karibu na Ikweta. Hili huonyesha kwa nini Amerika Kusini na Afrika ndiyo mabara yenye kupatwa na mvua ya radi zaidi ya mengine yote na kwa nini kwa muda mrefu Afrika ya Kati na Indonesia zimeonwa kuwa na visa vingi zaidi vya mvua ya radi ulimwenguni. Rekodi inayokubaliwa ni ile ya mji wa Kampala, Uganda, ya kuwa na mvua ya radi kwa siku 242 kila mwaka. Hata hivyo, mvua ya radi hunyesha pia katika sehemu nyingine nyingi za dunia.

Fataki Katika Anga

Sifa mbili za mvua ya radi zinazotambuliwa na wote ni ngurumo na radi. Lakini ni nini husababisha tukio hili la kustaajabisha, na ambalo mara nyingi hutisha? Radi ni mtiririko wa elektroni unaotokea wakati ambapo tofauti katika chaji ya umeme kati ya sehemu mbili inapozidi uwezo wa hewa. Hili laweza kutokea ndani ya wingu, kati ya mawingu, au kati ya mawingu na ardhi. Wakati radi inapotokeza mtiririko wa chaji, hiyo huifanya hewa iwe na kipimo cha juu sana cha halijoto kwa muda mfupi—joto hilo laweza kufikia digrii Selsiasi 30,000.

Radi yaweza kuwa ya aina ya mchirizi, ama yenye kugawanyika, ama radi ya wingu. Ikiwa mtiririko wa elektroni unaonekana ukiwa mstari mmoja dhahiri, unaitwa radi ya mchirizi. Ikiwa mstari huo waonekana ukiwa umegawanyika, basi huitwa radi iliyogawanyika. Ikiwa mwale wa radi unatukia katika wingu, au kati ya wingu na wingu, radi ya aina hii huitwa radi ya wingu. Wataalamu wanasema kwamba radi nyingi ambazo sisi huona hutokana na mawingu yakielekea chini.

Radi hudhuru viumbe vilivyo hai—na hata hujeruhi na kuua wanadamu na wanyama. Watu walio kwenye fuo na katika viwanja vya gofu na nje katika sehemu za mashambani wako katika hatari kubwa ya kupigwa na radi kwa sababu hawana kinga dhidi ya chaji ya umeme.— Angalia sanduku katika ukurasa wa 15.

Ni asilimia 30 pekee ya watu wanaopigwa na radi ambao hufa, na kiwango cha visa vya wale wanaopatwa na majeraha ya muda mrefu hupungua wakati huduma ya kwanza inapotolewa bila kukawia. Hata hivyo, kinyume na hadithi zinazopendwa, radi inaweza na mara nyingi hupiga zaidi ya mara moja eneo lilelile!

Mipigo ya radi husababisha visa vingi vya moto. Mioto hiyo yaweza kuangamiza maeneo makubwa ya nchi. Kwa wastani asilimia 10 ya visa vya mioto ya msitu katika Marekani husababishwa na radi. Hii hutokeza kuchomeka kwa zaidi ya asilimia 35 ya jumla ya misitu yote na vichaka katika nchi hiyo.

Lakini mipigo ya radi ina manufaa pia. Kwa kielelezo, misitu hunufaika kwa njia kadha wa kadha. Moto unaoanzishwa na radi hupunguza vichaka ikiwa moto huo si mkali. Jambo ambalo laweza kupunguza hatari ya kuwako kwa visa vya moto mkali uwezao kufikia matawi ya miti. Radi huleta pia mabadiliko yenye faida kwa gesi ya nitrojeni, ambayo haiwezi kutumiwa na mimea ikiwa katika hali ya gesi. Radi huigeuza gesi hii kuwa katika misombo ya nitrojeni, ambayo ni muhimu katika ufanyizaji wa tishu za mimea na katika ukuzi wa mbegu, ambazo huandaa protini zilizo muhimu katika maisha ya wanyama. Inakadiriwa kwamba asilimia 30 hadi 50 za oksaidi za nitrojeni zilizo katika mvua huletwa na radi na kwamba tufeni pote tani milioni 30 za nitrojeni iliyogeuzwa kuwa misombo ya kemikali hufanyizwa kwa njia hii kila mwaka.

Faida Kubwa Zaidi ya Dhoruba

Mvua ya radi yaweza kutokeza kiasi kikubwa sana cha maji. Sababu kuu ya kunyesha kwa mvua kubwa sana kwa wakati mfupi ni ya kwamba kuinuliwa juu kwa mvuke mwingi wa dhoruba kubwa hubeba kiasi kikubwa cha maji na kisha kuyaachilia kwa ghafula. Kipimo cha mvua kama hiyo kimefikia kiasi cha inchi nane kwa saa moja. Bila shaka, kwaweza kukawa pia na athari ya mvua kubwa kama hiyo.

Dhoruba isongapo polepole, ni maeneo machache ya ardhi kwa kulinganishwa yanayopokea mvua nyingi, na hili laweza kutokeza mafuriko ya ghafula. Wakati wa dhoruba ya namna hiyo, maji yanayotiririka juu ya ardhi hufanya mito na vijito kufurika. Inakadiriwa kwamba karibu thuluthi moja ya uharibifu wote unaosababishwa na mafuriko katika Marekani huletwa na mafuriko ya ghafula yanayoletwa na mvua ya radi.

Hata hivyo, mvua ya dhoruba huleta manufaa mengi. Udongo, matangi ya maji na mabwawa hupata maji mengi sana. Utafiti umeonyesha kwamba asilimia 50 hadi 70 ya mvua inayonyesha katika maeneo fulani-fulani hutokana na mvua ya radi, na kwa hiyo katika maeneo haya mvua ya dhoruba ni muhimu kwa uhai.

Namna Gani Mvua ya Mawe?

Jambo moja lenye kuleta hasara sana la mvua ya radi ni kwamba mara nyingi huandamana na mawe mengi. Mawe hutokezwa wakati matone ya mvua yanapoganda na kisha kuongezeka kwa ukubwa yanapozungushwa katika duru ya kupanda na kushuka kwa hewa. Kumekuwapo na visa fulani vya kustaajabisha sana kuhusu mawe ya mvua yaliyo makubwa na mazito sana. Yaripotiwa kwamba jiwe moja la mvua lililokuwa na urefu wa sentimeta 26 na upana wa sentimeta 14 na kimo cha sentimeta 12 lilianguka huko Ujerumani mnamo mwaka wa 1925. Uzito wake ulikadiriwa kuwa zaidi ya kilogramu mbili. Moja kati ya mawe makubwa zaidi ya mvua lililowahi kurekodiwa katika nchi ya Marekani lilianguka katika jimbo la Kansas mnamo mwaka wa 1970. Jiwe hilo lilikuwa na kipimo cha sentimeta 44 katika mzingo wake ulio mkubwa zaidi na lilikuwa na uzito wa gramu 776. Jiwe la mvua lenye ukubwa wa jinsi hiyo linapoanguka kutoka juu kwenye mawingu laweza kumwua mtu.

Kwa uzuri, mawe ya mvua huwa madogo zaidi ya hayo na huelekea kuwa yenye kusumbua badala ya kuuwa. Na pia kwa sababu ya hali ya mvua ya radi inayotokeza mawe, maeneo yanayoathiriwa na mvua ya mawe yenye kuharibu ni machache. Hata hivyo, hasara inayosababishwa na mvua ya mawe kwa mazao ya kilimo ulimwenguni inakadiriwa kuwa mamia ya mamilioni ya dola kila mwaka.

Chamchela na Mvua ya Radi

Tokeo lenye hatari zaidi la mvua ya radi huenda liwe ni chamchela. Karibu chamchela zote huandamana na mvua ya radi, lakini si mvua yote ya radi huandamana na chamchela. Inapotokea, chamchela huwa bomba jebamba la upepo unaozunguka kwa nguvu, ukiwa na kipenyo cha wastani wa mamia kadhaa ya meta, na ambao hufika chini kutoka kwenye wingu zito la mvua ya radi. Mwendo wa pepo katika chamchela zenye nguvu sana waweza kuwa wa zaidi ya kilometa 400 au 500 kwa saa. Utendaji wa pamoja wa pepo zenye kuzunguka kwa nguvu na kuinuka juu katikati kwa pepo hizo kwaweza kuporomosha majengo na kuvurumisha hewani vifusi vinavyoweza kuua. Chamchela hutukia katika nchi nyingi ulimwenguni.

Pepo zinazovuma kuelekea upande mmoja tu na ambazo huandamana na hewa zinazoshuka na pepo ndogo-ndogo hata ingawaje hazisababishi maafa sana, huwa na uwezo mkubwa wa kusababisha uharibifu. Hewa zinazoshuka zaweza kusababisha pepo zenye uharibifu kwenye ardhi au karibu na ardhi zinazoweza kufikia mwendo wa kilometa 150 kwa saa. Pepo ndogo-ndogo huwa kali sana nazo zaweza kufikia mwendo wa kilometa 200 kwa saa.

Ni wazi kwamba mvua ya radi yapasa kuhofiwa na kwamba tunapaswa kutambua hatari zake. Hizo ni mojawapo tu ya sehemu nyingi za uumbaji ambazo tungali tuna mengi ya kujifunza kuzihusu.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 15]

Hadhari za Radi

Shirika la Mambo ya Dharura la Australia ladokeza hadhari zifuatazo wakati wa mvua ya radi.

Kujikinga Ukiwa Nje

◼ Jikinge ndani ya gari ambalo si wazi au ndani ya jengo; epuka vibanda vidogo-vidogo, mahema yaliyotengenezwa kwa kitambaa, na miti iliyojitenga au vikundi vidogo-vidogo vya miti.

◼ Ukiwa mahali pa wazi mbali na mahali pa kujisetiri, chuchumaa (Peke yako), ni afadhali zaidi kuchuchumaa ndani ya bonde, miguu ikiwa pamoja, na uondoe vitu vilivyotengenezwa kwa chuma kichwani na mwilini. Usilale chini, lakini epuka kuwa kitu kirefu zaidi kwenye sehemu hiyo.

◼ Nywele zako zikisimama kwa kuendelea au ukisikia kelele za mvumo kutoka kwa vitu vilivyo karibu, kama vile miamba na nyua, nenda kwenye sehemu nyingine mara moja.

◼ Usipeperushe tiara au mifano ya ndege iliyofungiwa nyaya za kuiongoza.

◼ Usitumie vitu virefu au vilivyotengenezwa kwa chuma katika sehemu zilizo wazi kama vile vifaa vya kuvulia samaki, miavuli, au vigoe vya kuchezea gofu.

◼ Usiguse au kusogelea vitu vilivyoundwa kwa chuma, nyua zilizotengenezwa kwa waya, au nyaya za kuanikia nguo.

◼ Usipande farasi au baiskeli au magari yaliyo wazi.

◼ Ikiwa unaendesha gari, punguza mwendo au uegeshe gari mbali na vitu virefu kama vile miti na nyaya za umeme. Kaa ndani ya magari yasiyo wazi au ndani ya trela, lakini usiguse au kuegemea vifaa vilivyotengenezwa kwa chuma.

◼ Ikiwa unaogelea au kuteleza kwenye mawimbi, ondoka majini mara moja na utafute mahali pa kujisetiri.

◼ Ikiwa unasafiri kwa mashua, nenda ufuoni haraka iwezekanavyo. Ikiwa si salama kufanya hivyo, jikinge chini ya kitu kirefu kilichojengwa, kama vile daraja au katika gati. Hakikisha kwamba mlingoti na kamba za mashua zimeunganishwa vema na waya ya ardhini iliyo majini.

Kujikinga Ukiwa Ndani ya Nyumba

◼ Kaa mbali na madirisha, vifaa vya umeme, mifereji, na vitu vingine vya chuma vilivyoko kwenye nyumba.

◼ Epuka kutumia simu. Na ikiwa unataka kupiga simu ya dharura, fanya hivyo kwa ufupi iwezekanavyo.

◼ Kabla ya dhoruba kufika, tenganisha antena zote na nyaya za umeme za radio na televisheni. Tenganisha vifaa vya kompyuta kutoka kwa vyanzo vya nguvu za umeme. Kisha ukae mbali na vifaa vinavyotumia nguvu za umeme.

[Hisani]

From the publication Severe Storms: Facts, Warnings and Protection.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki