Volkeno—Je, Umo Hatarini?
VOLKENO zilipukazo, zikimwaga majivu yenye moto na mitiririko yenye kung’aa ya mawe yaliyoyeyuka, hutokeza baadhi ya maonyesho ya ajabu sana ya nguvu za asili duniani. Huenda wewe binafsi hujashuhudia tukio kama hilo, lakini huenda umefurahia kuoga kwenye chemchemi-moto ya kivolkeno au ukafurahia kula chakula kilichopandwa kwenye udongo wenye rutuba ulio na majivu ya volkeno. Wengine hata hufaidika nyumbani kwao na nishati zitokanazo na joto la dunia.
Hata hivyo, hivi majuzi wengi waishio karibu na volkeno-tendaji wameshuhudia vifo na uharibifu usababishwao na misiba ya volkeno. Tangu ule mlipuko mkubwa wa Mlima St. Helens katika kusini-magharibi mwa Jimbo la Washington, Marekani katika Mei 18, 1980, sehemu mbalimbali za ulimwengu zimekumbwa na milipuko mikubwa ya daima iliyo hatari. Idadi ya vifo katika kipindi hiki imepita jumla ya vifo iliyorekodiwa kwa miongo saba iliyopita, na uharibifu wa mali umejumlika kuwa mamia ya mamilioni ya dola. Ikaribiayo kuwa misiba imetokea mara nyingi wakati majivu ya volkeno yaliyo angani yasababishapo ndege kupoteza nguvu, ikizilazimisha kutua kwa dharura.
Yenye kusababisha uharibifu mkubwa zaidi ni ile milipuko na mibubujiko ya matope iliyofuata ya Mlima Pinatubo, katika Filipino, iliyofagilia mbali makumi ya maelfu ya nyumba, na Nevado del Ruiz, katika Kolombia, iliyoua zaidi ya watu 22,000. Misiba zaidi yaweza kutokea. Wataalamu wa volkeno Robert Tilling na Peter Lipman, wa Uchunguzi wa Jiolojia ya Dunia wa Marekani, husema kwamba “kufikia mwaka wa 2000, idadi ya watu iliyo hatarini mwa kupatwa na madhara ya volkeno yaelekea itaongezeka kufikia angalau milioni 500.”
Hivyo huenda ukaliona kuwa jambo la hekima kuuliza: ‘Je, mimi naishi karibu na volkeno-tendaji, au volkeno iwezayo kuwa tendaji wakati mmoja? Ni aina gani za milipuko zilizo hatari zaidi, na je, zaweza kutangulia milipuko yenye kufisha hata zaidi? Ikiwa naishi kwenye eneo hatari kivolkeno, naweza kufanya nini ili kupunguza hatari?’
Volkeno-Tendaji—Ziko Wapi?
Ungeweza kushangaa ukitambua kuwa waishi karibu na volkeno-zimwe na kwamba hungeweza kuepuka kuathiriwa ikiwa ingeanza kutenda tena. Wanasayansi wachunguzao volkeno wamefanikiwa katika miongo ya karibuni si katika kutambua volkeno-tendaji na zimwe tu bali pia katika kufahamu kwa nini volkeno huelekea kupatikana katika sehemu fulani.
Tazama ramani (ukurasa 17), ionyeshayo mahali pa baadhi ya zile volkeno zaidi ya 500 ambazo zimerekodiwa kuwa tendaji. Je, wewe waishi karibu na mojawapo? Kwingineko, chemchemi zenye kurusha maji moto, mashimo yenye kutoa hewa na gesi zenye joto, na chemchemi-moto, hudokeza kuwapo kwa volkeno-zimwe nyingine; hizi pia zaweza kuwa tendaji wakati ujao. Zaidi ya nusu ya volkeno-tendaji zote hufuatana kandokando ya ukingo wa Pasifiki, zikijumuika kuwa kile kiitwacho Mviringo wa Moto. Baadhi ya volkeno hizo hutokea kwenye kontinenti mbalimbali, kama vile kwenye Milima ya Kaskedi ya Amerika Kaskazini na Milima ya Andes ya Amerika Kusini, na nyingine hufanyiza mifuatano ya visiwa katika bahari-kuu, kama vile Visiwa vya Aleutian, Japani, Filipino, na kusini mwa Indonesia. Volkeno pia hupatikana kwa kawaida ndani na karibu na Mediterania.
Wanasayansi wametambua kuwa volkeno hizo hutokea kwenye mipaka ya vipande au mabamba makubwa yaliyo mwendoni, hasa mahali ambapo bamba la bahari-kuu huingia chini ya lile la nchi kavu. Utendaji huo huitwa subduction. Joto linalotokezwa na miendo hiyo huyeyusha mawe ambayo huinuka hadi kwenye uso wa dunia. Kwa kuongezea, miendo ya ghafula kati ya mabamba husababisha matetemeko ya dunia yenye nguvu katika sehemu nyingi za maeneo yakumbwayo na milipuko ya volkeno.
Pia volkeno hutokea sehemu ambapo mabamba ya bahari-kuu huachana. Mingi ya milipuko hiyo hutukia kwenye sakafu ya bahari-kuu nayo haionekani na mwanadamu. Hata hivyo, ikiwa waishi katika nchi ya kisiwa cha Iceland, uko juu ya Mwinuko wa Reykjanes, uunganao na Mwinuko wa Atlantiki ya Kati, ambapo mabamba yanayotia ndani Amerika Kaskazini na Kusini yanaachana na yale yanayotia ndani Ulaya na Afrika. Katika visa vingine vichache, sehemu moto zilizo peke yazo chini ya mabamba ya uso wa dunia zimetokeza volkeno kubwa katika Hawaii na kwenye kontinenti ya Afrika.
Hatari Ni Zipi?
Kiwango cha hatari cha volkeno huongozwa na historia ya karibuni ya utendaji wayo, kutia ndani na ukubwa wa milipuko ya volkeno na hatari zinazohusianishwa nayo. Ukubwa wa hatari hulingana na idadi ya watu wanaoishi katika kanda hatari na utayari wao wa kukabiliana na mlipuko. Kwanza acheni tuchunguze zile hatari.
Kwa ujumla, milipuko iliyo hatari zaidi hutokezwa na mawe yaliyoyeyushwa yenye silika nyingi. Aina hii ya mawe yaliyoyeyushwa ni nzito, na yaweza kwa muda fulani kuziba volkeno hadi kanieneo iwe ya kutosha kulipua volkeno. Mawe yaliyoyeyushwa yenye silika nyingi hukamatana na kuwa mawe yenye rangi-nyepesi nayo ni ya kawaida kwa volkeno kwenye mipaka ya mabamba. Milipuko pia yaweza kutokea wakati mawe yaliyoyeyushwa yakutanapo na maji na kuyafanya yawe mvuke. Majivu moto yatokezwayo na milipuko yaweza kufisha—volkeno tatu katika eneo la Karibea ya Kati ya Amerika ziliua zaidi ya watu 36,000 kwa kipindi cha miezi sita katika 1902.
Kwa upande mwingine, sehemu moto za bahari-kuu na volkeno zitokeazo mabamba yaachanapo, na nyingine nyingi, kwa sehemu kubwa hufanyizwa na mawe meusi mazito, ambayo yana silika kidogo lakini yenye chuma na magnesi kwa wingi. Mawe meusi yaliyoyeyushwa kwa kawaida huwa majimaji na hutokeza milipuko midogo au mibubujiko isiyolipuka na pia mtiririko wa mawe yaliyoyeyushwa wa polepole ulio rahisi kuepukwa na watu. Hata hivyo, milipuko hiyo yaweza kudumu—volkeno ya Kilauea katika kisiwa cha Hawaii imekuwa ikilipuka kwenye hicho kisiwa kwa mfululizo tangu Januari 1983. Ingawa uharibifu wa mali nyingi umetokana na mlipuko kama huo, hiyo huumiza au kuua watu mara chache sana.
Milipuko mingine huweka majivu mengi kandokando ya volkeno, ambayo yaweza kusababisha poromoko la ardhi au, yachanganyikapo na theluji, barafu, au maji, yaweza kusababisha matope mazito yawezayo kuteremka hadi kwenye mabonde. Mitiririko kama hiyo ya matope (ambayo huitwa pia kwa Kiingereza lahars kutokana na neno la Kiindonesia linalomaanisha mawe yaliyoyeyushwa) yaweza kufika kilometa nyingi kutoka kwenye volkeno, huenda hata muda mrefu baada ya volkeno kuacha kulipuka.
Iliyo hatari hata zaidi hasa, lakini yenye kutokea mara chache sana ni tsunami—mawimbi makubwa ya bahari-kuu yatokezwayo na mlipuko katika bahari-kuu au na poromoko la ardhi chini ya maji kandokando ya volkeno yenye kutokeza. Mawimbi haya yenye nguvu yaweza kusafiri kwa mwendo wa mamia ya kilometa kwa saa. Ingawa tsunami ziko chini sana kwenye bahari kuu, na hazihatarishi kamwe meli zipitazo, hizo hukua kwa kimo upesi zikiwa karibu na nchi kavu. Vilele vya mawimbi hayo huwa virefu kuliko nyumba na majengo mengi. Katika 1883 Krakatau ulipolipuka, watu 36,000 walipoteza uhai wao huku tsunami zikishambulia pwani za Java na Sumatra.
Madhara mengine ya volkeno yawezayo kuumiza au kutatiza uhai hutia ndani majivu na vipande vya volkeno viangukavyo, mshtuko wa mawimbi ya angani yatokezwayo na milipuko, moshi wenye sumu, mvua za asidi na matetemeko ya dunia. Kukiwa na volkeno hatari sana zilizogunduliwa ulimwenguni na hatari ziwezazo kutokea wakati fulani zisizo na hesabu, kufanya uchunguzi wa maana wa hatari za volkeno ni jukumu gumu sana.
Je, Waweza Kuipunguza Hatari?
Kadiri watu waongezekavyo ulimwenguni, wengi zaidi na zaidi huishi katika maeneo ya volkeno yawezayo kuwa hatari. Kwa sababu hiyo, pamoja na lile ongezeko la karibuni la utendaji wa volkeno ulimwenguni pote, wataalamu wa volkeno wameongeza jitihada zao ili kupunguza hatari za volkeno. Katika visa fulani, kutangazwa na kutabiriwa kwa milipuko kumefanikiwa, na uhai kuokolewa. Ni nini huwa msingi wa matabiri kama hayo?
Milipuko kwa kawaida hutanguliwa na matetemeko katika volkeno na muundo wake wa ndani, ikiashiria mwendo wa juu wa mawe yaliyoyeyushwa. Kadiri mawe yaliyoyeyushwa yaongezekapo katika volkeno, kanieneo huongezeka. Hewa huponyoka, nayo halijoto na asidi ya maji ya ardhini huongezeka. Milipuko midogo pia yaweza kutokea kabla ya ule mkubwa. Utendaji huu mbalimbali waweza kuchunguzwa.
Mapema vya kutosha kabla ya milipuko, wanajiolojia, waweza kukadiria hatari iwezayo kutokea kwa kuchunguza rekodi ya hayo mawe. Mara nyingi aina ya mitiririko ya volkeno na hatari za ziada hujirudia, au mitiririko huiga zile volkeno nyingine zilizochunguzwa. Kwa kutegemea habari hizo, ramani zenye kuonyesha maeneo yenye hatari kubwa zaidi zimechorwa kwa volkeno nyingi.
Njia za kuokoa uhai wa watu wengi kutokana na hatari za volkeno hutia ndani uchunguzi wa hatari na kuchunguzwa kwa volkeno na wataalamu wa volkeno na pia wenye mamlaka kutoa onyo la mapema la hatari iliyoko mbele. Tofauti na matetemeko ya ardhi, ambayo bado hayawezi kutabiriwa kwa usahihi, volkeno nyingi zilipukazo zaweza kuchunguzwa kwa ukaribu sana hivi kwamba watu wawezao kuathiriwa nayo waweza kuhamishwa kabla ya tukio hilo lenye uharibifu. Ni muhimu kuondoka kwenye eneo la hatari, kwa kuwa vitu vilivyotengenezwa na mwanadamu hutoa ulinzi mdogo sana dhidi ya hasira na joto la mtiririko na milipuko ya volkeno na nguvu zisababishazo uharibifu za maporomoko ya ardhi, mitiririko ya matope, na tsunami ya mawimbi.
Ingawa jitihada zistahilizo pongezi zinafanywa ili kupunguza majeraha, vifo na uharibifu usababishwao na milipuko ya volkeno na hatari zihusianazo nao, mwanadamu angali hawezi kutabiri milipuko na utendaji mwingine hatari kwa usahihi kabisa hivi kwamba aweza kuhakikisha usalama kamili kutokana na hatari za volkeno. Hata baadhi ya wale wachunguzao volkeno wamekufa kwa sababu ya kunaswa na milipuko isiyotazamiwa. Hata hivyo, ikiwa waishi karibu na volkeno iwezayo kutenda wakati mmoja, wapaswa kutii maonyo yatolewayo na wenye mamlaka. Kwa kufanya hivyo, uwezekano wako wa kuokoka msiba wa volkeno utaongezeka.—Imechangwa na mwastrojiolojia.
[Sanduku katika ukurasa wa18]
Kutabiri Milipuko ya Volkeno Kutoka Angani?
Wazia kupima miendo ya uso wa volkeno kwa usahihi wa hata sentimeta moja kutoka kwa sateliti zilizo kilometa 20,000 juu angani—zisafirizo kwa mwendo usiopungua kilometa tano kwa sekunde moja! Hilo limewezeshwa na ule Mfumo wa Vikao wa Tufeni (GPS), unaotia ndani sateliti kadhaa pamoja na redio vilivyo mahali pafaapo duniani. Kwa kila kipimo, vikao vya angalau sateliti nne hufuatiwa kwa usahihi. Wakati hupimwa kwa saa za kiatomu, zilizo sahihi sana. Vipimo hivyo, viwezavyo kuchukuliwa wakati wa halihewa yoyote, vina manufaa kadhaa kupita za uchunguzi ufanywao nchini. Vipimo vya GPS vyaweza kuboresha kwa kiwango kikubwa kutangazwa kwa milipuko ya volkeno, ambayo yaweza kutanguliwa na miaka mingi ya upanuzi wa volkeno. Tekinolojia hii tayari imetumiwa kwa ajili ya volkeno katika Iceland, Italia, Japani, na Marekani.
[Ramani katika ukurasa wa 17]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
Volkeno-tendaji na mabamba ya uso wa dunia
Volkeno-tendaji
Mipaka ya mabamba
Ziwakilishwazo juu ni baadhi ya zile volkeno-tendaji zaidi ya 500
[Hisani]
Mountain High Maps™ copyright © 1993 Digital Wisdom, Inc.
[Picha katika ukurasa wa 16]
Majivu kutoka volkeno ya Unzen, Japani, yakiteremkia eneo la makazi
[Hisani]
Orion Press-Sipa Press
[Picha katika ukurasa wa 16]
Mlima St. Helens ukilipuka
[Hisani]
USGS, David A. Johnston, Cascades Volcano Observatory
[Picha katika ukurasa wa 16]
Mlima Etna, Sicily, majuzi ulirusha mawe yaliyoyeyushwa kwa muda wa miezi 15
[Hisani]
Jacques Durieux/Sipa Press
[Picha katika ukurasa wa 17]
Mlima Kilauea, Hawaii, umeongeza hicho kisiwa karibu ekari 500
[Hisani]
©Soames Summerhays/Photo Researchers