Visiwa Vinavyojengwa
“HAWAII.” Visiwa vya Hawaii hutoa maono ya paradiso ya kitropiki, fuo zenye jua, na pepo zenye kuburudisha. Lakini je, ulifahamu kutenganishwa kuliko wazi kwa visiwa hivi? Ukiangalia kwenye ramani mahali Hawaii ilipo, utapata visiwa hivi vikiwa vimetulia katikati ya Bahari ya Pasifiki Kaskazini—karibu mbali sana na nchi kavu uwezavyo kufika! Hivyo, waweza kuwazia, ‘Visiwa hivi vilipataje kuwako mahali hapo? Je, wanasayansi wanaamini kuwa visiwa vingine vitafanyizwa wakati ujao? Visiwa hivi vyaweza kutuambia nini kuhusu dunia iliyo chini ya miguu yetu?’
Jamii-Visiwa vya Hawaii
Watu wengi wanaotembelea Hawaii hufahamu safu ya visiwa vinane ambavyo husambaa kutoka kaskazini-magharibi hadi kusini-mashariki, vikubwa zaidi vikiwa Kauai, Oahu, Molokai, Lanai, Maui, na Hawaii. Kisiwa kilicho kidogo zaidi cha Niihau kiko magharibi ya Kauai, na Kahoolawe kiko kusini-magharibi ya Maui. Kisiwa cha Hawaii, kiitwacho pia Kisiwa Kikubwa, kina zaidi ya kilometa za mraba 10,000, huku kisiwa kidogo cha Kahoolawe kina kilometa za mraba 117 tu. Kwa kuongezea, safu ya visiwa hutia ndani visiwa vingine 124 vidogo zaidi, ambavyo huenea zaidi kuelekea kaskazini-magharibi. Visiwa vingine ambavyo havitiwi ndani katika eneo la Hawaii, karibu na mwisho wa safu hiyo upande wa kaskazini-magharibi, viko umbali wa karibu kilometa 2,500 kutoka kwenye Kisiwa Kikubwa! Visiwa hivyo 124 vidogo zaidi, vikiwa hasa vimefanyizwa kwa matumbawe na mchanga, eneo lake hufanyiza jumla ya kilometa za mraba nane tu. Kwa kufaa, watu fulani hutumia jina Jamii-Visiwa vya Hawaii kurejezea kikundi kizima cha visiwa.
Tukifikiria kuwa visiwa hivi pamoja na visiwa hivyo vidogo hutegemezwa na vizingiti vya chini ambavyo huinuka, kwa wastani, zaidi ya meta 4,000 juu ya eneo linalovizunguka la bahari, twaanza kuelewa kwamba hivyo ni ncha na taji za milima mikubwa zilizofichuliwa. Kwa hakika, vikipimwa kutoka kwenye msingi kwenye sakafu ya bahari, Mauna Kea na Mauna Loa kwenye kisiwa cha Hawaii vina urefu wa meta 10,000. Hivyo, kwa njia fulani ndiyo milima mirefu zaidi ulimwenguni!
Kujenga Kisiwa
Hebu tuchunguze zaidi kisiwa cha Hawaii. Wanajiolojia wamehakikisha kwamba Kisiwa Kikubwa kimefanyizwa na volkano tano zenye makaa mawe. Wageni wengi wamejua zile tatu kubwa zaidi—Mauna Kea, ambayo yafikiriwa kuwa volkano bwete na hujivunia kilele kirefu zaidi katika Hawaii, meta 4,205 juu ya usawa wa bahari; Mauna Loa, ambayo iko na urefu wa meta 4,169 na ndiyo volkano kubwa zaidi katika Hawaii kwa ukubwa; na Kilauea, ambayo ndiyo volkano changa zaidi na iko upande wa kusini wa kisiwa hicho. Kwa kuongezea, volkano ya Kohala hufanyiza ncha ya kaskazini-magharibi ya kisiwa hicho, na Hualalai huinuka juu ya pwani ya Kona.
Kila volkano ilikua kutokana na kumwagika kwa maelfu ya mitiririko ya lava. Milipuko huanza chini ya maji, ambapo lava hupoa kwa haraka, ikifanyiza ganda na mitiririko yenye umbo la ulimi ambayo ikiwekwa pamoja huonekana kama mito. Wakati volkano inayokua inapojitokeza juu ya maji, mitiririko ya lava hubadili umbo. Wataalamu wa volkano hutumia maneno ya Hawaii “pahoehoe” kwa mitiririko ya umajimaji ulio na uso laini, wenye mawimbi, na uonekanao kama kamba na “aa” kwa lava ambayo si laini, yenye uso usiosawazika, na ifananayo na vifusi. Volkano hutokeza mlima mpana wenye miteremko ambao kwa umbo hufanana na ngao walizobeba wanavita Waroma. Kreta kubwa hutokea juu ya volkano wakati magma, au miamba iliyoyeyuka, inapofoka au kujiondoa kwenye mianya karibu na uso. Pia, hifadhi ya magma ndani ya volkano hutokeza kanieneo. Kanieneo hii husukuma sehemu ya volkano kuelekea baharini, ikifungua vikundi vikubwa vya miatuko. Mwishowe, kama katika kisa cha Mauna Kea, milipuko ya volkano zenye umbo la ngao huwa zenye kulipuka zaidi, zikitokeza marundo ya volkano yenye umbo la pia ya vipande vya lava ambavyo hufunika volkano.
Mauna Loa na Kilauea zimethibitika kuwa kati ya volkano tendaji zaidi ulimwenguni. Rekodi za kihistoria kutoka kwa wenyeji wa Hawaii, wamishonari, wanasayansi, na wengine huonyesha kwamba milipuko 48 imetokea katika Mauna Loa tangu mwaka wa 1832 na zaidi ya milipuko 70 katika Kilauea tangu mwaka wa 1790. Milipuko hii imedumu kutoka muda wa saa kadhaa hadi miaka kadhaa. Uliokuwa mrefu zaidi uliorekodiwa ulikuwa ziwa la lava katika kreta ya Halemaumau katika Kilauea, ambao ulikuwa tendaji karibu kwa mfululizo tangu mapema mwa miaka ya 1800 hadi 1924. Kwa sasa, Kilauea imekuwa ikilipuka tangu Januari 1983, mara kwa mara ikitokeza mabubujiko ya moto yenye kutazamisha na mito ya lava ambayo imetiririka katika bahari.
Kwa sababu ya hali yake ya lava kuwa ya majimaji, mingi ya mifoko ya Hawaii imekuwa bila milipuko au milipuko ya kiasi. Hata hivyo, katika visa vichache, maji ya chini ya ardhi huchanganyika na magma, ikitokeza milipuko ya mvuke. Katika 1790, mlipuko kama huo uliwaua karibu watu 80 wakati kikosi cha wanavita wenyeji na familia zao walipofunikwa ndani ya gesi moto na vipande vya lava vilivyotupwa kutoka katika Kilauea.
Visiwa Vinavyosonga
Historia iliyorekodiwa kwa zaidi ya miaka 200 iliyopita yaonyesha kwamba ni volkano zilizo katika visiwa viwili tu vilivyo kusini-mashariki zaidi, Hawaii na Maui, ambazo zimekuwa zikitenda. Hali hii yenye kukoroweza iliwasukuma wanasayansi kuchunguza zaidi historia ya miamba ya safu ya kisiwa hicho. Ndani ya lava kuna kiasi kidogo sana cha potasiamu yenye nururishi pamoja na matokeo yake ya baada ya kuoza, agoni, ambazo wangeweza kupima katika maabara ili kukadiria umri wa miamba. Uchunguzi wa aina hiyo ulionyesha kusonga kuelekea kaskazini-magharibi kwa kuendelea kuzeeka kwa Jamii-Visiwa vya Hawaii kwa muda wa miaka milioni nyingi.
Kwa kuwa milipuko ya Hawaii imekuwa ikitokea sana katika sehemu ya kusini-mashariki ya safu ya kisiwa, je, hili lamaanisha kuwa chanzo cha magma chini yake kimekuwa kikisonga pia? Kwa kweli, wanajiolojia wamehakikisha kwamba chanzo cha magma, ambacho wao hukiita mahali moto, hakisongi. Badala ya hivyo, sakafu ya Bahari ya Pasifiki imekuwa ikisonga juu ya mahali hapo moto, ikiondoa volkano za kisiwa hicho kwenye mahali moto kama marundo ya miamba yaliyo juu ya mkanda wa kuchukulia unaosonga. Mwendo huuhuu husugua sakafu ya bahari ya Pasifiki kando ya matungamo ya mabara yanayopakana nayo na sehemu nyingine za sakafu ya bahari, ikisababisha mengi ya matetemeko ya dunia makubwa ambayo hutokea katika Ukingo wa Pasifiki. Ikiwa waishi Hawaii, nyumba yako imesonga sentimeta 7.5 kuelekea kaskazini-magharibi tangu mwaka jana!
Wanasayansi wanadokeza kwamba mahali moto pengine kama palipo chini ya Hawaii ndipo hutokeza volkano kote ulimwenguni, kwenye bara na baharini. Pengi pa mahali hapa moto huonyesha ithibati ya milipuko inayohama, ambalo lamaanisha kwamba huenda uso wa dunia umekuwa ukisonga mahali unapoishi pia.
Uumbikaji wa Visiwa Vipya . . .
Kwa kuwa mamia ya maelfu ya miaka imehitajika ili kujenga volkano kubwa kwenye Kisiwa Kikubwa, twaweza kutarajia kwamba kisiwa hicho kimekuwa kikisonga kutoka kwenye mahali moto katika wakati huo. Volkano mpya na visiwa vyapasa kutokea juu ya mahali hapo moto pia kwa kuwa panakabili sakafu ya bahari isiyovurugwa. Je, kuna uwezekano kwamba mwandamizi wa Kisiwa Kikubwa tayari amejidhihirisha?
Kwa kweli amejidhihirisha. Mlima wa chini ya maji unaotenda wa kivolkano, Loihi, unakua kusini mwa kisiwa cha Hawaii. Hata hivyo, usiutarajie ujitokeze kutoka baharini hivi karibuni. Ungali unahitaji kupaa meta 900 zaidi, ambazo zaweza kuchukua makumi ya maelfu ya miaka.
. . . Na Kuangamiza Visiwa vya Zamani
Ngao kubwa za kivolkano na mitiririko ya lava isiyo laini inayofanyiza Visiwa vya Hawaii huonekana kwa njia isiyo ya kweli kuwa salama kutokana na kuzamishwa tena ndani ya bahari. Lakini visiwa vidogo sana na milima ya baharini ya kaskazini-magharibi ya Hawaii haionyeshi hivyo. Kwa mfano, michanga na matumbawe ya visiwa visivyohusianishwa na Hawaii na visiwa vya Kure, vimejengwa juu ya milima mikubwa ya volkano ambayo vilele vyake sasa viko mamia ya meta chini ya usawa wa bahari. Kwa nini visiwa vya volkano hutoweka?
Visiwa hivi polepole humomonyolewa na maji ya mito, athari za mawimbi, na nguvu nyingine. Visiwa hivyo pia huzama kutokana na uzito wake vyenyewe vinaposukuma sakafu ya bahari. Majabali yenye miinamo yaliyo kando ya visiwa fulani huashiria utendaji mwingine ambao huozesha visiwa vya volkano—maporomoko ya ardhi. Vyombo vinavyotambua vitu vilivyozama baharini vinavyoonyesha vipande vya visiwa vilivyozama hufunua maporomoko makubwa ya ardhi ambayo huenea kwa makumi ya kilometa chini kwenye sakafu ya bahari.
Mahali Moto Katika Utendaji
Katika kisiwa cha Hawaii, wageni wanaotembelea Hifadhi ya Wanyama ya Volkano za Hawaii waweza kujionea wenyewe mandhari zinazobadilika kila wakati zinazotokezwa na utendaji wa kivolkano wa mahali moto. Wanasayansi wa Mahali pa Kuchunguzia Volkano Hawaii, palipo kwenye ukingo wa kreta ya Kilauea hufuatilia milipuko inayoendelea na ile inayotisha kutokea. Uchunguzi wao umeongoza kwenye uelewevu zaidi kuhusu jinsi volkano hufanya kazi na jinsi ambavyo uso wa dunia umekuwa ukihama. Kwa kicho, twaweza kuthamini kwamba nguvu zenye uweza za jiolojia zimefanyiza na kuunda Jamii-Visiwa vya Hawaii—safu hii yenye fahari ya visiwa katikati ya Bahari ya Pasifiki.
[Ramani katika ukurasa wa 25]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
Visiwa vya Hawaii
Mlipuko kwenye Kilauea
Niihau
Kauai
Oahu
Molokai
Lanai
Maui
Kahoolawe
Hawaii
[Hisani]
Mountain High Maps® Copyright © 1997 Digital Wisdom, Inc.
[Picha katika ukurasa wa 24]
Mstari wa mabubujiko katika ufa wa mashariki ya Kilauea
[Picha katika ukurasa wa 24, 25]
Mlipuko kwenye Kilauea
[Hisani]
Volkano: Dept. of Interior, National Park Service
[Picha katika ukurasa wa 25]
Mto wa lava juu ya Mauna Loa
[Picha katika ukurasa wa26]
Mlipuko juu ya Mauna Loa
[Hisani]
Juu kushoto na chini kulia: Dept. of Interior, National Park Service
[Picha katika ukurasa wa 26]
Mlipuko juu ya Kilauea
[Hisani]
U.S. Geological Survey
[Picha katika ukurasa wa 26]
Ziwa la lava juu ya Kilauea
[Hisani]
Juu kushoto na chini kulia: Dept. of Interior, National Park Service