Visiwa vya Canary—Tabia-Anga Tulivu, Mandhari Yenye Ushawishi
NA MLETA-HABARI ZA AMKENI! KATIKA HISPANIA
ILISEMWA kwamba ng’ambo ya bahari, kupita zile Nguzo za Hercules, kulikuwa na visiwa fulani vya kupendeza sana. Udongo ulikuwa na rutuba sana, tabia-anga ilikuwa tulivu sana, hivi kwamba chochote kile kingekua huko. Hivi vilikuwa vile Visiwa vya Fortunate. Sasa twavijua kuwa Visiwa vya Canary, “Canary” likitolewa kutokana na canis la Kilatini, linalorejezea mbwa wakubwa, wakali waliokuwa tele huko.
Mchanganyiko huu wa kuwazia mambo ya kweli na yasiyo ya kweli, uliofuatwa kikamilifu na waandikaji wa Kiroma na Kigiriki, ulitegemea hadithi zilizotungwa na mabaharia wachache wajasiri walioabiri katika Atlantiki kabla ya wakati wa Kristo. Leo, mtalii ndiye afuataye mapito ya wanamaji hao wa kale. Visiwa hivyo ni halisi vya kutosha, ingawa kiasi fulani cha ule uvutio na kadiri kubwa ya ule upendezi wa kushangaza umekwisha. Tabia-anga yazo ni tulivu kwelikweli, yenye ushawishi wa kutosha kuvutia mamilioni ya wageni watafutao utulizo wa kuyaepuka kidogo majira ya baridi kali ya Ulaya Kaskazini.
Ile tabia-anga anana sio uvutio wa pekee. Visiwa hivyo vina unamnamna usio na kifani wa mandhari na mimea ionyeshayo sana kwamba ilikuwa vizuri mbuga za kitaifa zikafanyizwa katika vinne kati ya vile visiwa vikuu saba.
Tenerife—Bustani ya Mwamba Juu ya Mawingu
Kisiwa kilicho kikubwa zaidi, Tenerife, kimemilikiwa na Pico de Teide, volkeno isiyolipuka yenye kuinuka juu ya mawingu yaingiayo kwa mfululizo kutoka Atlantiki. Kuzunguka ile kuba ya volkeno kuna uwanja-duara mkubwa sana chini ya vilima-vilima, ambao ukiwa pamoja na ile volkeno yenye fahari hufanyiza ile Mbuga ya Kitaifa ya Teide. Mbuga hiyo ina maua ya pekee yavuvumukayo mwishoni mwa masika na kiangazi cha mapema wakati ile mimea ijifaidipo na unyevunyevu uliorundikana kutokana na theluji za wakati wa baridi. Kwa ghafula ile nchi kame ya volkeno hugeuzwa kuwa bustani ya miamba ing’arayo kwa urangirangi mwingi.
Mawili kati ya maua ya mbuga hiyo yaliyo ya pekee zaidi isivyo kawaida hayapatikani kwingineko kote ulimwenguni. Hayo ni lile tajinaste jekundu na lile ua Teide la urujuani. Lile tajinaste jekundu ndio mmea ambao labda ndio wa kuvutia zaidi wa ile jamii-visiwa—maelfu ya vikundi vya maua mekundu yanayokua yakiviringana kwa kushikana kuzunguka shina pweke lifikialo kimo cha karibu meta mbili au zaidi. Yale machanuo marefu yafanana na vibomba-moshi vya kimaua vilivyoinua mkono kusalimu lile anga la samawati-nzito.Lile ua Teide la urujuani, lipambalo koo la volkeno kwa mjazano wa kizambarau, ni la kusifika kwa uthabiti walo. Hilo hukua meta chache tu kutoka kwenye kile kilele cha meta 3,700, ambako hakuna mimea mingine yoyote hubaki hai.
La Palma—Nyungu Yenye Ujani Mwingi wa Kivolkeno
La Palma ina mojapo mashimo makubwa zaidi ulimwenguni. Uzingo wayo una kipenyo cha karibu kilometa 27 na ina kimo cha karibu meta 2,400. Uwazi mkubwa sana ulio chini, uchukuao sehemu ya kati ya kisiwa hicho, ni volkeno iliyoporomoka ambayo kwa muda wa miaka iliyopita imechongwa na upepo na mvua ikawa kama nyungu kubwa. Ndiyo sababu ilipata jina la Kihispania caldera (neno la Kihispania la kaldroni [nyungu]), ambalo ni neno litumikalo kwa mashimo kama hayo kotekote ulimwenguni.a
Nyungu hiyo, ambayo yote sasa ni mbuga ya kitaifa, karibu ifunikwe kikamili na msitu wa misonobari wenye uvutio mwingi. Msonobari wa Canary, ambao ndio mti upatikanao kwa wingi zaidi, wafunika miteremko yote isipokuwa ile iliyoinama sana, ukilinda kuta za ile nyungu dhidi ya mmomonyoko zaidi. Likiwa limekaribia kutengwa na ulimwengu wa nje na hali ya kutofikika kwalo, shimo kubwa hilo lisiloharibiwa ni maskani ya uzuri na amani kwa wapenda-asili wathubutuo kuingia ndani.
Gomera—Kikanyagio cha Kufika Amerika
Ilikuwa ni kutoka kisiwa hiki kilichojificha kwamba Columbus alitwesha matanga kuingia kusikojulikana. Kilikuwa kimetoka tu kushindwa na Wahispania, naye Columbus akatua katika kile kibandari cha San Sebastián ili kupakia maji na maandalizi.
Wakati wa Columbus, wakaaji wa kisiwa hicho, Waguanche, walikuwa bado wakiishi maisha ya kizamani, lakini walikuwa watu wenye kubadilikana. Kwa sababu ya hali ya vilima-vilima ya nchi, walikuwa wamesitawisha lugha ya pekee ya kupiga mbinja ikiwawezesha kusemezana kutoka kigongo-ardhi hadi kigongo-ardhi kwa umbali wa kilometa kadhaa au zaidi. Ingawa mbinu hii ya “uwasiliani-mbinja” imesahauliwa sana, ingali hutumiwa na wazee-wazee watakapo kupashana kihabari cha haraka. Mashahidi wa Yehova wakihubiri katika vijiji vilivyo peke yavyo wameusikia ujumbe “Wale Mashahidi ndio hawa!” ukipigiwa mbinja kutoka vilele vya vilima.
Katika miteremko ya juu zaidi ya kisiwa hicho kuna mbuga ya kitaifa iliyofanyizwa kulinda msitu fulani wa kale sana. Eneo lao la ndani-ndani, lililozungukwa na mvuke pande zote na kujaa matanzu yaliyopindika yakiwa yamefunikwa na kuvumwani, huamsha kumbukumbu za hadithi za kizimwi zilizosahauliwa zamani. Ingawa huenda ikaonekana ajabu, kwa kawaida mvua hunya hapa chinichini ya miti. Mawingu yarushwayo juu ya msitu na pepo zenye nguvu za kuelekea kaskazini ‘hukamwa’ maji yayo na ile miti. Hivyo, chini ya miti huwa kuna unyunyu wa daima, hali kule nje huenda kusiwe kunanyesha hata kidogo.
Mabaki ya visukuku yaonyesha kwamba msitu huu wa laureli (uitwao laurisilva) wakati mmoja ulikuwako kotekote katika mkoa wa Mediterania. Lakini badiliko la tabia-anga mileani nyingi zilizopita lilipunguza sana mweneo wao likawa vilele vichache tu vya vilima vya Visiwa vya Canary.
Lanzarote—Kisiwa cha Jangwa Chenye Tofauti
Lanzarote ni kisiwa cha jangwa ambacho, ingawa hakijaachwa, kwa hakika chafanana na jangwa. Mvua ni kama haipo kabisa. Maisha hapa yalikuwa yamekuwa magumu sikuzote kwa ile idadi ndogo, lakini karne mbili zilizopita mfululizo wa milipuko mikali ya kivolkeno ulibadili uso wa kisiwa hicho. Zile volkeno zilileta kifo na uhai. Kifo, katika maana ya kwamba kisiwa hicho kilizikwa na mitiririko ya umaji-volkeno utiririkao ukikomesha ghafula vijiji vingi na maboma ya nyumba. Uhai, katika maana ya kwamba wanakisiwa wamejiruzuku kutokana na majivu ya volkeno hizo.
Kwa sababu ya wingi mkubwa wa changarawe za kivolkeno zinyweazo maji, ambazo ni masalio kutoka kwa milipuko, wanakisiwa waweza kulima matunda na mboga hata ingawa huenda mvua isinye kwa miezi kadhaa. Mashamba hufunikwa na tabaka la milimeta kumi za changarawe ambazo zaidi ya kuhifadhi unyevunyevu wa ule udongo wa chini vilevile huteka hasa umajimaji kutoka kwenye hewa chepechepe ya usiku na kuupitishia udongo ulio chini. Mashamba ya mizabibu, mitini, minyanya, mihindi, na mazao mengine huchipuka bila kutarajiwa kutoka kwenye changarawe nyeusi hiyo.
Mbuga ya Kitaifa ya Timanfaya yatia ndani mashimo ya kutazamisha na eneo kubwa linalozunguka limezwalo na umaji-volkeno uliotapikwa na mashimo hayo. Ile tabia-anga iliyo kama ya jangwani imehifadhi umaji-volkeno kwa kugandamana ikiwa karibu na vile ilivyokuwa hapo awali, na mgeni azuruye mbuga hiyo huenda hata akawazia kwamba milipuko hiyo ilikoma jana tu. Ile mandhari ya volkeno ya kutazamisha, pamoja na vile vijiji vyeupe vya kupendeza, hukipa kisiwa uzuri wa pekee usio na kifani.
Bila shaka visiwa hivi vya kusisimua vya volkeno vyatoa sifa ya kubadilikana kwa wakaaji wavyo na mimea ikuayo huko. Juu ya yote, uzuri wavyo wa asili humsukuma mgeni mwenye kicho amhesabie sifa Muumba wa unamna-namna huo.
[Maelezo ya Chini]
a Ziwa Crater katika Oregon, Marekani, ni nyungu maarufu ambalo limekuja baadaye kujawa na maji.
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 18]
Wanyama na Maua ya Visiwa vya Canary
Canary. (1) Ndege hawa waliopewa jina la jamii ya visiwa hivyo wangali wengi, ingawa, wakiwa msituni, hawana urangirangi wa kuvutia kama wale ndege wa kufungiwa wapendwao na watu wengi ambao rangi zao dhahiri hutokana na uzalishani mteuzi wa zaidi ya karne nne.
Spishi Aeonium. (2) Namna zaidi ya dazani mbili hupatikana kotekote visiwani, nyingi zikikua katika miatuko ya miamba. Baadhi yazo, kama vile Aeonium lancerottensis, (3) hata hukua kutokana na umaji-volkeno uliogandamana.
Ua Teide la urujuani. (4) Machipuko haya yaliyo mepesi kuvunjika husitawi katika mazingira hasama ya kivolkeno karibu meta 3,700 juu ya usawa wa bahari.
Ndizi. (5) Ndizi zimelimwa katika Visiwa vya Canary kwa karne nyingi. Wakolonishi Wahispania walizipeleka Karibea muda mfupi baada ya kugunduliwa kwa Amerika.
Tajinaste nyekundu. (6) Vikundi vya maua madogo sana mekundu hukua kwa kuviringana kuzunguka shina pweke ambalo mara nyingi hufikia kimo cha zaidi ya meta mbili.
Mti drakoni. (7) Huu ukiwa ndio mti wa ajabu zaidi na wenye kupendwa zaidi katika visiwa hivi, kielelezo hiki chasemwa kuwa cha miaka elfu tatu. Vielezo vya kale kama hiki hutunzwa kwa uangalifu katika mbuga za manispaa.
[Ramani]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
La Palma
Tenerife
Gomera
Hierro
Lanzarote
Fuerteventura
Grand Canary
[Picha]
Tenerife humilikiwa na Pico de Teide, volkeno isiyotenda
1. The Canary.
2. Aeonium species.
3. Aeonium lancerottensis
4. The Teide violet.
5. The banana plant.
6. The red tajinaste.
7. The dragon tree.
[Picha katika ukurasa wa 16, 17]
1. Granadillo
2. Tabaiba Majorera
3. Verol dulce
4. Ercila
5. Hierba blanca
6. Teide violet