Kuutazama Ulimwengu
Je, “Kuishi Katika Dhambi” Si Dhambi?
Baraza la Daraka la Kijamii la Kanisa la Uingereza hivi majuzi lililishauri kanisa kwamba “kuishi katika dhambi” si dhambi tena, Guardian Weekly lilisema. Baraza hilo liliripotiwa kwamba pia lililishauri kanisa kuwa “kutaniko laweza kujifunza kutoka kwa wenzi wasiooana, kutia ndani wagoni-jinsia-moja wa kiume na wa kike, nao wapaswa kukinza kishawishi cha kutamani ‘kipindi cha maisha bora ya familia’ kilichopita.” Gazeti Guardian lamnukuu kasisi Philip Hacking akijibu: “Hili hulifanya Kanisa kuchekwa, nalo husababisha mkazo mwingi miongoni mwa Wakristo wengi waaminifu.”
Kupoteza Uwezo wa Kusoma na Kuandika
Watu wapatao milioni tatu katika Ujerumani wamepoteza uwezo wa kusoma na kuandika kwa sababu ya kukosa mazoezi. Johannes Ring, katibu wa Hazina ya Usomaji, alieleza kuwa maendeleo ambayo yamefanywa na vyombo vya habari vya kielektroni yameongezea tatizo hilo. Kwenye Mkutano wa Ulimwengu wa Kukabiliana na Kutojua Kusoma na Kuandika, Ring alisema kuwa hilo ongezeko katika aina hii ya kutojua kusoma na kuandika kwa sehemu ni tokeo la kuenea kwa matumizi ya televisheni, kompyuta, na michezo ya video, laripoti Frankfurter Allgemeine Zeitung.
Kunywa Maji Ili Ufikiri
Je, una tatizo la kukaza fikira? Huenda wahitaji kunywa maji zaidi, likadokeza Asiaweek. Gazeti hilo laripoti kwamba walimu na wazazi wa watoto fulani wa shule wa Hong Kong hivi majuzi walishauriwa kwamba kunywa maji mengi husaidia wanafunzi kukabiliana na ulegevu. Watoto wapaswa kunywa gilasi 8 hadi 15 za maji kwa siku, wazazi wakaambiwa. Ikinukuu kitabu The Learning Brain, ripoti hiyo yaonyesha uchunguzi mbalimbali unaoonyesha kuwa kukauka maji ya mwili kwaweza kutokeza uwezo mbaya wa kujifunza. Kunywa maji safi ni bora kuliko kunywa soda, kahawa, chai, au hata maji ya matunda, ambayo yaweza hata kuuchochea mwili kuondelea mbali umajimaji, likasema Asiaweek.
Onyo la Kiuavisumbufu
Wamarekani huathiriwa zaidi na viuavisumbufu kupitia bidhaa za nyumbani kuliko kupitia mboga na matunda yaliyonyunyiziwa viuavisumbufu, kulingana na watafiti katika Chuo Kikuu cha California kilichoko Berkeley. Dawa za kunyunyizia mende, tepe zinazoning’inia za kunasa nzi, dawa za viroboto, dawa za nondo, na bidhaa nyinginezo zinazofanana na hizo huwa na kemikali zenye sumu. Zaidi ya kusababisha usumishaji mwingi kila mwaka, nyingi za bidhaa hizo hutokeza madhara ya muda mrefu ya kiafya. Ile UC Berkeley Wellness Letter yapendekeza vibadala vilivyo salama zaidi: Rekebisha au uweke skrini na uzibe nyufa sakafuni na ukutani ili kuzuia visumbufu; funika kabisa vyakula na takataka kwa plastiki; tumia kinasa wadudu; fagia makombo; osha vitambara kwa mvuke wa maji moto; safisha nguo za sufu kwa ukawaida na kuziweka kwenye mifuko iliyofungwa. Mende wakiendelea kusumbua, jaribu kutumia mitego yenye gundi au kunyunyiza asidi-boriki nyuma ya makabati, lakini uwalinde watoto na wanyama-rafiki wasiguse vitu hivyo, ladokeza Wellness Letter.
Programu za Televisheni kwa Ajili ya Watoto—Ni Zenye Jeuri Kupita Kiasi
Uchunguzi fulani wa mfumo wa televisheni wa Marekani ulifikia mkataa wa kuwa kuna “mapigano maovu yenye jeuri” katika nyingi za programu zielekezwazo kwa watoto. Kulingana na The Wall Street Journal, ule uchunguzi uliofanywa katika Chuo Kikuu cha California, Los Angeles, ulichagua mfululizo wa katuni zipendwazo sana zilizokuwa na “jeuri ili tu kuonyesha jeuri.” Programu hizo huonyeshwa asubuhi za Jumamosi, wakati ambapo watoto hawako shuleni na huenda wazazi wao wasiwe wameamka. Ingawa aina hii ya programu si mpya, huo uchunguzi uligundua kwamba “yale mapigano maovu yasiyokoma katika maonyesho haya ni mwelekeo wa majuzi wa jeuri uonekanao kuongezeka.”
Mti wa Ajabu
Wanasayansi Waingereza wamegundua mbegu ziwezazo kuchuja maji bila matumizi ya kemikali za gharama kubwa. Mbegu zilizopondwa za mti wa Moringa oleifera wa kaskazini mwa India huvutia na kunata bakteria na virusi, ambazo baadaye zaweza kutolewa au kunaswa kwenye vichujio, laripoti gazeti The Times la London. Mbegu hizo zenye matumizi mengi zaweza pia kutumiwa kutengeneza mafuta ya kupika, sabuni, virembeshi, mafuta ya taa, na mafuta ya kutibu maambukizo ya ngozi. Huo mti ni rahisi kukuza, hustahimili kiangazi, waweza kuzuia upepo, na hata kuandaa kuni na sehemu ya ndani iwezayo kufanyizwa kuwa karatasi. Hivyo, watafiti hupendekeza upandaji wa miti hiyo ili kutokeza mbegu zitakazosaidia kuzuia mamilioni ya vifo kila mwaka vitokezwavyo na kunywa maji machafu.
Mwembamba Sana?
Katika jamii inayojali sana sura, wengi huona kwamba haiwezekani kamwe kwa mmoja kuwa mwembamba sana. Uchunguzi wa karibuni uliohakikisha hatari za kiafya za kunenepa kupita kiasi waweza kuonekana kuwa waunga mkono maoni haya ya watu wengi, lakini mwanzilishi wa uchunguzi huo, JoAnn Manson wa Chuo Kikuu cha Harvard, ataka ijulikane kwamba kuwa mwembamba sana ni hatari kwa afya pia. “Naamini kwamba waweza kuwa mwembamba sana kwa kukosa chakula kifaacho, mazoezi ya kupita kiasi, au kuvuta sigareti,” alinukuliwa akisema katika The Wall Street Journal. Likitaja madaktari kadhaa ambao hushutumu hatari za kuchunga ulaji kupita kiasi, Journal liliorodhesha hatari fulani za kuwa mwembamba isivyo kawaida—huenda chini ya asilimia 20 ya uzito wa wastani wa urefu wa mtu. Hizo ni kutokuwa na hamu ya chakula, mifupa kuwa myepesi, mabadiliko ya kihomoni, kuanguka-anguka, mivunjiko ya mifupa, na kukawia kupona.
Maumo ya Nyoka —Jambo Usilopaswa Kufanya
Kuhusu kutibu walioumwa na nyoka, wataalamu hawakubaliani sikuzote. Hata hivyo, kulingana na gazeti FDA Consumer, wataalamu wengi wa kitiba wa Marekani “karibu hukubaliana katika maoni yao ya mambo yasiyopaswa kufanywa.” Ukiwa umbali wa dakika 30 hadi 40 kutoka kwenye mahali pa kitiba, shauri ni: Usiweke barafu mahali pa kuumwa, usitumie vibano vya kuzuilia damu mishipani au mishtuko ya umeme, na usikikatekate kidonda. Mapendekezo yakubalikayo na wengi ni kwamba hata nyoka aonekane kuwa mwenye sumu au sivyo, maumo yote ya nyoka lazima yaonwe kuwa dharura za kitiba, naye aliyeumwa apaswa kupelekwa hospitalini mara moja. Njia ya kujizuia iliyo bora kabisa ni “kutowasumbua nyoka kamwe. Watu wengi huumwa kwa kujaribu kumwua au kumtazama nyoka kwa ukaribu,” lasema FDA Consumer.
Onyo kwa Wacheza Soka
Katika soka, mchezo upendwao sana ulimwenguni, wachezaji waweza kuupiga mpira kwa vichwa vyao. Hata hivyo, kufanya hivyo kwaweza kutokeza madhara kwenye ubongo kufanywapo mara nyingi, laripoti gazeti Jornal do Brasil. Kulingana na uchunguzi wa karibuni, wacheza soka waweza kuwa wasahaulifu, na kuwa na upungufu katika kiwango cha kufanya kazi cha ubongo wao kutokana na kuupiga mpira kwa kichwa. Ingawa si hatari sana, hayo madhara hufanana na yale wapatayo wanabondia wapigwao ngumi kichwani mara nyingi. Daktari wa Neva Paulo Niemeyer Filho adokeza kwamba wachezaji wapaswa kuepuka kutumia vichwa vyao kuupiga mpira uangukapo toka juu sana hewani kwa nguvu au ukiwa umelowa maji, jambo ambalo huufanya mpira kuwa mzito zaidi. Wataalamu kadhaa huamini kwamba kuupiga mpira kwa kichwa kupita kiasi kwaweza pia kuharibu uwezo wa mchezaji wa kuona.
Tabasamu Kutoka Moyoni Huambukiza
Kuna aina mbili za tabasamu, kulingana na watafiti wa Finland Dakt. Jari Hietanen wa Chuo Kikuu cha Tampere na Dakt. Veikko Surakka wa Taasisi ya Sayansi ya Kitiba kwenye Chuo Kikuu cha Helsinki. Aina moja ya tabasamu yajulikana na wataalamu kuwa tabasamu za kirafiki. Hizo huchochewa tu na hisia ya wajibu nazo huhusisha misuli ya mashavu tu. Kwa upande mwingine, tabasamu za kutoka moyoni huonyesha hisia halisi za furaha na huchochea si misuli ya mashavu tu bali pia misuli inayozunguka macho. Uchunguzi wa majuzi kutoka Finland wadokeza kwamba tabasamu za kutoka moyoni huambukiza. Kwa kugundua na kurekodi mwendo mdogo sana wa misuli, watafiti walitambua kwamba waliofanyiwa majaribio hayo walichochewa kutabasamu kwa kuona tu picha ya mtu aliyekuwa na tabasamu ya kutoka moyoni. Itikio hilo halikuonekana wakati wenye kufanyiwa majaribio walipotazama picha za watu wenye tabasamu za kirafiki.
Wanajimu Wakosea
Kulingana na gazeti la Kijerumani Die Zeit, wanajimu 44 katika Uholanzi majuzi walikubali kwa kujitolea kufanya mtihani uliotayarishwa na Dutch Society of Skeptics. Hao wanajimu walipewa orodha mbili. Moja ilikuwa na mahali na tarehe ya kuzaliwa kwa watu saba. Ile ya pili iliandaa habari nyingi za kibinafsi juu ya kila mmoja wa wale watu saba. Hao wanajimu waliombwa kuunganisha kila mtu kwenye orodha ya kwanza na maelezo yamhusuyo yaliyoko kwenye orodha ya pili kwa kutumia ujuzi wanaodaiwa kuwa nao wa kinajimu. Walifanikiwa kadiri gani? Nusu kati yao hawakupata hata jibu moja sahihi, na hakuna aliyeweza kuunganisha kwa usahihi zaidi ya watatu. Majaribio ya awali yalikuwa na matokeo kama hayo, lakini wanajimu walidai kuwa walipewa habari zisizofaa. Hata hivyo, katika kisa hiki, matakwa ya huo mtihani yalifanywa na wanajimu wenyewe.