Sura 7
Yesu na Wanajimu
HESABU fulani ya wanaume waja kutoka Mashariki. Wao ni wanajimu—watu wanaodai kuwa wanatoa fasiri kuonyesha mahali nyota zilipo. Walipokuwa nyumbani Mashariki, waliona nyota mpya, nao wakaifuata kwa mamia ya kilometa mpaka Yerusalemu.
Wanajimu hao wafikapo Yerusalemu, wauliza: “Yuko wapi yeye aliyezaliwa mfalme wa Wayahudi? Kwa maana tuliiona nyota yake mashariki, nasi tumekuja kumsujudia.”
Mfalme Herode katika Yerusalemu asikiapo hilo, audhika sana. Kwa hiyo awaita makuhani wakuu na kuuliza ni wapi Kristo angezaliwa. Wakitegemeza jibu lao kwenye Maandiko, wajibu hivi: “Katika Bethlehemu.” Kusikia hivyo, Herode aamuru wale wanajimu waletwe kwake naye awaambia: “Shikeni njia, mkaulize sana mambo ya mtoto; na mkiisha kumwona, nileteeni habari, ili mimi nami niende nimsujudie.” Lakini, kwa kweli, Herode ataka kumpata mtoto huyo ili amuue!
Baada ya wao kuondoka, jambo la ajabu latukia. Nyota waliyoiona walipokuwa Mashariki yasafiri mbele yao. Kwa wazi, hiyo si nyota ya kawaida, lakini imetolewa kusudi iwaelekeze. Wanajimu hao waifuata mpaka inaposimama pale pale juu ya nyumba ambamo Yusufu na Mariamu wanaishi.
Wanajimu hao waingiapo ndani ya nyumba hiyo, wamkuta Mariamu na mtoto wake mchanga, Yesu. Ndipo wote wamsujudia. Kisha watoa mifuko yao ya zawadi za dhahabu, uvumba na manemane. Baadaye, wakaribiapo kurudi wakamwambie Herode mahali alipo mtoto, waonywa na Mungu katika ndoto wasifanye hivyo. Kwa hiyo waondoka kwenda kwenye nchi yao kupitia njia nyingine.
Wewe wafikiri ni nani aliyetoa nyota hiyo iliyoenda angani iwaongoze wanajimu hao? Kumbuka, nyota hiyo haikuwaongoza moja kwa moja kwa Yesu katika Bethlehemu. Badala ya hivyo, waliongozwa mpaka Yerusalemu ambako walikutana na Mfalme Herode, aliyetaka kumuua Yesu. Naye angalifanya hivyo kama Mungu hangejiingiza na kuwaonya wanajimu hao wasimwambie Herode alipokuwa Yesu. Adui ya Mungu, Shetani Ibilisi, ndiye aliyetaka kumuua Yesu, naye alitumia nyota hiyo ajaribu kutimiza kusudi lake. Mathayo 2:1-12; Mika 5:2.
▪ Ni nini kinachoonyesha kwamba nyota ambayo wanajimu waliona haikuwa nyota ya kawaida?
▪ Yesu yuko wapi wanajimu hao wanapompata?
▪ Tunajuaje kwamba Shetani alitoa nyota hiyo iwaongoze wanajimu hao?