Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g96 6/8 kur. 5-8
  • Kutafuta Masuluhisho Yanayokubalika

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Kutafuta Masuluhisho Yanayokubalika
  • Amkeni!—1996
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Kupunguza Vichafuzi
  • Kupunguza Mwendo
  • Kutumia Baiskeli
  • Kufanyiza Muundo Mpya
  • Sehemu Tu ya Tatizo
  • Kupata Suluhisho Lifaalo
    Amkeni!—1996
  • Ulimwengu Usio na Magari?
    Amkeni!—1996
  • Ah, Angalau Hewa Safi!
    Amkeni!—1996
  • Jinsi ya Kukabiliana na Msongamano wa Magari
    Amkeni!—2007
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1996
g96 6/8 kur. 5-8

Kutafuta Masuluhisho Yanayokubalika

SI MAGARI peke yayo yatokezayo uchafuzi. Makao ya kibinafsi, viwanda, na vituo vya nguvu za umeme lazima pia vishiriki lawama. Hata hivyo, fungu la magari katika uchafuzi wa duniani pote ni kubwa.

Kwa hakika, kitabu 5000 Days to Save the Planet huthubutu kusema hivi: “Ikiwa sababu ya hasara hizi zote ingeelezwa—hasa hasara kwa tabia-nchi yetu kwa kutokezwa kwa kaboni monoksidi—basi yaelekea magari hayangetengenezwa kamwe.” Hata hivyo, hicho chakubali hivi: “Lakini hilo ni chaguo ambalo wala watengeneza-magari, wala wajenzi wa barabara, wala mashirika ya serikali, wala watu wote kwa ujumla, ambao maisha yao huzidi kutegemea usafiri wa kibinafsi, hawako tayari kulitafakari.”

Je, tekinolojia iliyompeleka mwanadamu mwezini haiwezi kutokeza gari lisiloleta uchafuzi? Kufanya si rahisi kamwe kama kusema, hivyo hadi vizuizi vya kufanyiza gari lisilotokeza uchafuzi viwezapo kushindwa, utafutaji wa masuluhisho mengineyo yanayokubalika waendelea.

Kupunguza Vichafuzi

Katika miaka ya 1960 Marekani ilipitisha sheria iliyoamrisha kuwekwa kwa vithibiti kwenye magari ili kuzuia mitokezo ya vichafuzi. Nchi na serikali nyinginezo zimefanya vivyohivyo.

Vifaa vigeuzavyo michemuo ya magari ili isidhuru, ambavyo huhitaji kutumia petroli isiyo na madini ya risasi, sasa vyatumiwa sana ili kuchuja vichafuzi vyenye kudhuru. Kati ya 1976 na 1980, baada ya idadi kubwa ya waendesha-magari kuanza kutumia petroli isiyo na madini ya risasi, kiwango cha madini ya risasi katika damu ya Wamarekani kilipungua kwa thuluthi. Na kilifanya vyema kupungua, kwa kuwa madini ya risasi yenye kupita kiasi yaweza kuathiri mfumo wa neva na kuzuia uwezo wa kujifunza. Hata hivyo, kwa kuhuzunisha, ingawa viwango vya madini ya risasi vimepungua katika nchi nyingi za ulimwengu uliositawi, hilo halijatukia katika nchi ambazo hazijasitawi sana.

Mafanikio ya vifaa vya kugeuza michemuo ili isidhuru yanatosheleza, lakini utumizi wavyo bado wabishaniwa. Kwa sababu ya kupungua kwa uwezo wakati ambapo risasi haikuongezwa tena, mfanyizo wa hidrokaboni wa petroli ulibadilishwa. Hilo limetokeza ongezeko katika mitoko ya vichochezi vinginevyo vya kansa, kama vile benzeni na tolini, ambavyo mitokezo yavyo haiwezi kupunguzwa na vifaa vya kugeuza michemuo ili isidhuru.

Isitoshe, vifaa vya kugeuza michemuo ili isidhuru huhitaji utumizi wa platini. Kulingana na Profesa Iain Thornton, wa Chuo cha Imperial katika Uingereza, moja ya athari zayo mbaya imekuwa ongezeko la platini iliyotanda katika vumbi lililo kando ya barabara. Yeye alionya juu ya uwezekano kwamba “namna ziwezazo kuyeyuka za platini zaweza kuingia katika mtungo wa chakula.”

Licha ya mafanikio yoyote ya “vifaa vya kugeuza michemuo ili isidhuru katika Amerika Kaskazini, Japani, Korea Kusini na nchi kadhaa za Ulaya,” 5000 Days to Save the Planet chakiri hivi kihalisi, “ongezeko kubwa mno la idadi za magari ulimwenguni pote limeharibu manufaa kwa ubora wa hewa.”

Kupunguza Mwendo

Njia nyingine ya kupunguza mitoko ya magari ni kuendesha gari polepole. Lakini katika Marekani, majimbo fulani hivi majuzi yameongeza kiwango cha mwendo. Katika Ujerumani kuweka vizuizi hakupendwi na wengi. Watengenezaji magari wanaokazia uwezo wao wa kutengeneza magari yenye nguvu ambayo huruhusu kwa urahisi mwendo wa kasi upitao kilometa 150 kwa saa kwa wazi wanapinga kupunguzwa kwa viwango vya mwendo, sawa na idadi kubwa ya madereva. Hata hivyo, yaonekana sasa kwamba Wajerumani zaidi na zaidi wako tayari kukubali vizuizi vya mwendo si kwa sababu za kimazingira tu bali pia kwa sababu ya usalama.

Katika nchi fulani madereva wanatakwa kupunguza mwendo wakati uchafuzi ufikapo viwango visivyokubalika—au labda kuacha kuendesha kabisa. Uchunguzi wa 1995 ulifunua kwamba asilimia 80 ya Wajerumani ingekubali kuanzishwa kwa viwango vya mwendo ikiwa viwango vya ozoni vyawa juu sana. Majiji kadhaa kotekote ulimwenguni, kutia ndani Athens na Rome, tayari yamechukua hatua za kupunguza uendeshaji chini ya hali fulani. Mengineyo yanafikiria kufanya vivyo hivyo.

Kutumia Baiskeli

Ili kupunguza msongamano wa magari, majiji fulani yameanzisha bei zilizopunguzwa kwa usafiri wa basi. Mengine huandaa usafiri usio na malipo kwa madereva ambao hulipa ada ndogo kuegesha magari yao katika maegesho yapatikanayo. Majiji mengine yana barabara zilizotengwa kwa ajili ya mabasi na teksi tu ili kuharakisha aina hizi za usafiri.

Njia mpya ya kukabiliana na tatizo hilo ilitajwa hivi majuzi katika gazeti The European: “Wakichochewa na kampeni katika Uholanzi katika miaka ya mwisho-mwisho ya 1960, watu wa Denmark wenye maarifa wamefanya mpango wa kupunguza uchafuzi wa hewa na msongamano wa magari kwa kushurutisha watu watumie magurudumu mawili badala ya manne.” Baiskeli huwekwa katika mahali kadhaa kotekote katika barabara za Copenhagen. Kutumbukiza kisarafu ndani ya kifaa fulani hutoa baiskeli ya kutumiwa. Arbuni yaweza kudaiwa baiskeli irudishwapo baadaye katika mahali pafaapo. Kupita kwa wakati kutaonyesha ikiwa mradi huu utathibitika kuwa wenye kutumika na kupendwa na wengi.

Ili kutia moyo utumizi wa baiskeli badala ya magari, majiji fulani ya Ujerumani huruhusu waendesha-baiskeli kupitia barabara iendayo upande mmoja tu iliyo kinyume cha magari! Kwa kuwa thuluthi hivi ya safari zote jijini na zaidi ya thuluthi ya zile za mashambani ni fupi zaidi kuliko kilometa tatu, wananchi wengi wanaweza kwa urahisi kuenda safari hizo kwa kutembea au kwa kuendesha baiskeli. Hilo laweza kusaidia kupunguza uchafuzi; kwa wakati huohuo, waendesha-baiskeli watakuwa wakipata mazoezi ya mwili yahitajikayo.

Kufanyiza Muundo Mpya

Kazi inaendelea ya kuunda magari yasiyotoa uchafuzi. Magari ya umeme yawezayo kuenda kwa betri yametokezwa, lakini yana mapungukio kuhusiana na mwendo na muda wa uendeshaji. Na ndivyo ilivyo na magari yatumiayo nguvu za jua.

Uwezekano mwingine unaochunguzwa ni kutumia hidrojeni kuwa fueli. Hidrojeni huungua karibu bila mitokezo yoyote ya vichafuzi, lakini ni ghali sana.

Akitambua uhitaji wa kuvumbua upya magari rais Clinton wa Marekani alitangaza katika 1993 kwamba serikali na viwanda vya magari vya Marekani zingeshirikiana katika kuunda gari la wakati ujao. Alisema hivi: “Tutajaribu kuanzisha jambo la ujasiri la kitekinolojia la kiwango kikubwa sawa na lolote ambalo taifa letu limepata kujaribu.” Ikiwa itawezekana “kufanyiza gari lenye matokeo mno na lifaalo kimazingira kwa ajili ya karne ya 21,” ambalo alilizungumzia, ni jambo linalobaki kuonwa. Mipango ina lengo la kutokeza kiolezo cha kwanza mnamo mwongo mmoja—hata hivyo, kwa gharama kubwa mno.

Watengeneza-magari fulani wanafanyia kazi violezo ambavyo hutumia mchanganyiko wa petroli na umeme. Linalopatikana tayari katika Ujerumani—kwa gharama kubwa mno—ni gari la michezo linalotumia umeme liwezalo kuchapua mwendo mnamo sekunde tisa kuanzia kikao cha kusimama hadi kilometa 100 kwa saa, likizidi hadi mwendo wa kilometa 180 kwa saa. Lakini baada ya kilometa 200, betri hupungua nguvu na husimama hadi betri zichajiwe tena kwa angalau muda wa saa tatu. Utafiti unaendela, na maendeleo zaidi yatarajiwa.

Sehemu Tu ya Tatizo

Jinsi ya kuondosha mitoko yenye sumu ni sehemu tu ya tatizo. Magari pia husababisha uchafuzi wa kelele, jambo ajualo yeyote anayeishi karibu na barabara yenye magari mengi. Kwa kuwa kelele ya magari isiyokwisha yaweza kuathiri afya vibaya, hiyo pia ni sehemu ya msingi ya tatizo linalohitaji kutatuliwa.

Wapendao maumbile ya asili watataja pia kwamba mandhari nyingi za mashambani za urembo wa asili huharibiwa na kilometa nyingi za barabara kuu zenye sura mbaya, pamoja na mahali pa biashara penye sura isiyofurahisha na mabango ya matangazo ambayo huenda yakapakana na barabara hizo. Lakini huku idadi ya magari iongezekapo, ndivyo na uhitaji wa barabara zaidi.

Magari fulani, baada ya miaka mingi ya kuchafua hewa katika kutumikia wenyewe, huendelea na uchafuzi wayo hata “baada ya kifo.” Magari yaliyotupwa, yakiwa tu yenye kuudhi macho, yamekuwa tatizo sana hivi kwamba imebidi sheria ipitishwe katika mahali fulani kuepuka kurundikana kwayo ovyoovyo sehemu za mashambani. Je, gari lifaalo, ambalo limetengenezwa kwa maunzi yaliyo rahisi kutengenezwa upya, litapata kuundwa? Gari kama hilo halitapatikana karibuni.

“Wajerumani wengi wanahangaikia sana mazingira,” lataja gazeti la habari la majuzi, likiongeza, “lakini ni wachache tu wanaochukua hatua ifaayo.” Ofisa wa serikali alinukuliwa kusema hivi: “Hakuna anayejifikiria kuwa mkosaji, wala hakuna aliye tayari kulaumiwa.” Ndiyo, matatizo ni magumu kutatua katika ulimwengu uliojaa watu ambao ni “wenye kujipenda wenyewe,” na “wasiotaka kufanya suluhu.”—2 Timotheo 3:1-3.

Hata hivyo, utafutaji wa suluhisho linalokubalika waendelea. Je, suluhisho lifaalo kwa uchafuzi na magari laweza kupatikana?

[Picha katika ukurasa wa 7]

Je, uchafuzi waweza kupunguzwa kwa utumizi wetu wa usafiri wa umma, mpango wa kusafiri kwa kikundi cha wenye magari katika gari moja, au kuendesha baiskeli?

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki