Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g96 6/8 kur. 3-5
  • Ulimwengu Usio na Magari?

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Ulimwengu Usio na Magari?
  • Amkeni!—1996
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Msongamano wa Magari wa Ulimwenguni Pote
  • Lile Tisho la Uchafuzi
  • Kutafuta Masuluhisho Yanayokubalika
    Amkeni!—1996
  • Binadamu Anaifanya Dunia Nini?
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1990
  • Kaboni Monoksaidi—Mwuaji Asiyeonekana
    Amkeni!—2000
  • Halihewa Yenye Mchafuko
    Amkeni!—1998
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1996
g96 6/8 kur. 3-5

Ulimwengu Usio na Magari?

JE, WAWEZA kuwazia ulimwengu usio na magari? Au waweza kutaja uvumbuzi ambao kwa karne iliyopita umebadili mitindo-maisha na mwenendo wa watu kwa njia kuu kama ambavyo magari yamefanya? Bila magari, hakungekuwa na moteli, hakungekuwa mikahawa ambapo watu hushughulikiwa wakiwa magarini mwao, hakungekuwa mahali pa maonyesho ambapo watu huketi magarini mwao. La maana zaidi, bila basi, teksi, magari, au magari ya kubeba mizigo, ungefikaje kazini? shuleni? Wakulima na watengenezaji-vitu wangefikishaje bidhaa zao sokoni?

“Biashara moja kati ya kila biashara sita za Marekani hutegemea kutengenezwa, kusambazwa, kurekebishwa, au kutumiwa kwa magari,” yataja The New Encyclopædia Britannica, ikiongeza hivi: “Mauzo na risiti za makampuni ya magari huwakilisha zaidi humusi ya biashara ya mauzo-jumla ya Marekani na zaidi ya robo ya biashara ya rejareja. Kwa nchi nyinginezo milinganisho hii ni midogo kidogo, lakini Japani na nchi za Ulaya magharibi zimekaribia kwa haraka sana kiwango cha Marekani.”

Hata hivyo, watu fulani husema kwamba ulimwengu usio na magari ungekuwa mahali bora zaidi. Wanasema hilo kwa sababu mbili hasa.

Msongamano wa Magari wa Ulimwenguni Pote

Ikiwa umepata kuendesha gari kuzunguka barabara kwa kipindi kirefu ukitafuta nafasi ya kuegesha, unatambua vema sana kwamba hata ingawa magari yana faida, kuwa na magari mengi katika eneo lililosongamana hakuna faida. Au ikiwa umepata kunaswa katika msongamano mkubwa wa magari, unajua jinsi inavyofedhehesha kuzuiwa katika gari ambalo liliundwa kusonga lakini limelazimishwa kusimama tuli.

Katika 1950, Marekani ndiyo ilikuwa nchi pekee iliyokuwa na gari 1 kwa kila watu 4. Kufikia 1974, Italia, Sweden, Ubelgiji, Ufaransa, Uholanzi, Uingereza, na Ujerumani zilifikia kiwango hicho. Lakini kufikia wakati huo tarakimu ya Marekani ilikuwa imepanda hadi karibu gari 1 kwa kila watu 2. Sasa Ujerumani na Luxembourg zina gari 1 hivi kwa kila wakazi 2. Italia, Ubelgiji, Ufaransa, Uholanzi, na Uingereza hazijaachwa nyuma sana.

Majiji mengi makubwa—haidhuru yako wapi ulimwenguni—yamesongamana magari hivi kwamba yafanana na maegesho makubwa sana ya magari. Kwa kielelezo, katika India wakati wa uhuru katika 1947, New Delhi, jiji layo kuu, lilikuwa na magari ya kawaida na magari ya kubebea mizigo 11,000. Kufikia 1993 tarakimu hiyo ilipita 2,200,000! Ongezeko kubwa mno—lakini “idadi ambayo yatarajiwa kurudufika kufikia mwishoni mwa karne hii,” kulingana na gazeti Time.

Wakati huohuo, katika Ulaya Mashariki, yenye robo tu ya idadi ya magari kwa kila mtu kwa kulinganisha na Ulaya Magharibi, kuna wale wawezao kuwa wateja milioni 400. Kwa miaka michache, hali katika China, inayojulikana hadi sasa kwa baiskeli zayo milioni 400, itakuwa imebadilika. Kama ilivyoripotiwa katika 1994, “serikali inapanga ongezeko la haraka katika utokezaji wa magari,” kuanzia kiwango cha kila mwaka cha magari milioni 1.3 hadi milioni 3 kufikia mwishoni mwa karne hii.

Lile Tisho la Uchafuzi

“Uingereza imeishiwa na hewa safi,” likasema gazeti The Daily Telegraph la Oktoba 28, 1994. Labda hilo limetiwa chumvi lakini hata hivyo ni la kweli vya kutosha kusababisha hangaiko. Profesa Stuart Penkett, wa Chuo Kikuu cha East Anglia, alionya hivi: “Magari yanabadili muundo wa hali ya kiasili ya angahewa.”

Kiwango cha juu cha uchafuzi wa kaboni monoksidi, chasema kitabu 5000 Days to Save the Planet, “huunyima mwili oksijeni, hulemaza ufahamu na kufikiri, hupunguza mwendo wa sihiari na kusababisha usinziaji.” Na Shirika la Afya Ulimwenguni lasema: “Yapata nusu ya wakazi wa jijini katika Ulaya na Amerika Kaskazini wanapatwa na viwango vya juu isivyokubalika vya kaboni monoksidi.”

Yakadiriwa kwamba katika sehemu fulani mitokezo ya magari huua watu wengi kila mwaka—kuongezea kusababisha uharibifu wa kimazingira wenye kugharimu mabilioni ya dola. Katika Julai 1995 ripoti ya habari ya televisheni ilisema kwamba Waingereza wapatao 11,000 hufa kila mwaka kutokana na uchafuzi wa hewa wenye kusababishwa na magari.

Katika 1995 Kongamano la Umoja wa Mataifa la Tabia-Nchi lilikutana katika Berlin. Wawakilishi kutoka nchi 116 walikubali kwamba jambo fulani lapasa kufanywa. Lakini kwa fadhaiko la wengi, jukumu la kuweka miradi hususa na kuanzisha kanuni hususa au kuorodhesha programu mahususi liliahirishwa.

Kulingana na kile ambacho kitabu 5000 Days to Save the Planet kilisema katika 1990, ukosefu huu wa maendeleo labda ulitarajiwa. “Jinsi uwezo wa kisiasa na kiuchumi unavyoongoza jamii ya kisasa ya viwanda,” hicho kikataja, “huamua kwamba hatua za kukabiliana na uharibifu wa mazingira zakubalika tu ikiwa haziingilii uendeshaji wa kiuchumi.”

Hivyo, majuzi Time lilionya juu ya “uwezekano wa kwamba kuongezeka kwa kaboni dioksidi na gesi nyinginezo za kuongeza joto katika angahewa kutaongeza joto polepole tufeni. Tokeo, kulingana na wanasayansi wengi, laweza kuwa ukame, kuyeyuka kwa barafu duniani, kupanda kwa usawa wa bahari, mafuriko ya pwani, dhoruba mbaya zaidi na misiba mingine ya tabia-nchi.”

Uzito wa tatizo la uchafuzi wataka kwamba jambo fulani lifanywe. Lakini ni jambo gani?

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki