Binadamu Anaifanya Dunia Nini?
MIAKA mia tatu iliyopita, binadamu aliishi kwa ukaribu mwingi zaidi na asili (maumbile). Sana-sana, yeye hakutishwa na mabadiliko ya kibinadamu kwa mazingira ya tufe hili jinsi atishwavyo leo. Ule mvuvumko wa viwanda haukuwa umeanza. Hakukuwa na vituo vya nguvu za umeme, viwanda, magari, au vyanzo vingine vya uchafuzi wenye kuenea kotekote. Huenda ikawa ilikuwa vigumu kwa binadamu kuwazia kwamba yeye angeiangamiza dunia nzima.
Ingawa hivyo, hata zamani hizo, onyo juu ya kuangamizwa kwa tufe hili lilikuwa likizungushwa kotekote. Onyo hilo lilipatikana katika kitabu cha mwisho cha Biblia, nalo lilitabiri wakati ambapo Mungu angeingilia mambo ya binadamu ili “kuwaangamiza wale wanaoangamiza dunia.”—Ufunuo 11:17, 18, HNWW.
Ni faraja kama nini kwa wote wanaohangaikia usimamizi mbaya wa binadamu wa ki-siku-hizi juu ya dunia kujua kwamba Muumba wa sayari yetu yenye uzuri mwingi ataiokoa isiangamizwe! ‘Lakini,’ huenda wewe ukauliza kwa mshangao, ‘kweli sisi tumefikia hali mbaya sana hivi kwamba Mungu ahitaji kuingilia mambo?’ Basi, fikiria baadhi ya mambo ya uhakika na ujiamulie mwenyewe.
Misitu
Misitu hurembesha dunia na kuandaa chakula na makao kwa mamilioni ya jamii za vitu tofauti-tofauti. Miti ikuapo na kufanyiza chakula, hufanya huduma nyingine zilizo muhimu, kama kutwaa kaboni dayoksaidi na kutoa oksijeni yenye thamani kubwa. Hivyo, National Geographic husema kwamba, “huwa ina kipingamizi kimoja cha kuzuia tufe lisizidiwe na joto lenye kutisha uhai juu ya dunia kama tuujuavyo.”
Lakini binadamu anaangamiza urithi wake wa misitu. Misitu ya Amerika ya Kaskazini na Ulaya inauawa na uchafuzi. Na uagizaji mkubwa wa mataifa yenye viwanda unaua misitu ya kitropiki. Gazeti moja la Kiafrika lilieleza kwamba katika 1989, “meta za kyubiki milioni 66 [za miti ya kitropiki zili-]tarajiwa kusafirishwa nje—asilimia 48 kwenda Japani, asilimia 40 kwenda Ulaya.”
Pia, katika mabara fulani, wakulima huteketeza misitu ili wapate ardhi ya kulima. Muda si muda udongo huo dhaifu wa msituni humalizika nguvu, na wakulima hulazimika kuteketeza msitu zaidi. Yakadiriwa kwamba katika karne hii pekee, karibu nusu ya misitu ya ulimwengu imetoweka.
Bahari Kuu
Pia bahari kuu za dunia zina ushiriki muhimu katika kusafisha halianga, na utendaji mbalimbali wa binadamu unaziangamiza. Kadiri kubwa sana za kaboni dayoksaidi hutwaliwa na hizo bahari kuu. Halafu, mimea-bahari hutwaa kaboni dayoksaidi na kutoa oksijeni. Dakt. George Small aeleza umaana wa kawaida hii ya uhai: “Asilimia 70 ya oksijeni ambayo huongezwa kwenye halianga kila mwaka hutokana na mimea baharini.” Hata hivyo, wanasayansi fulani waonya kwamba mimea-bahari ingeweza kupunguzwa sana kwa sababu ya kupungua kwa gesi ya ozoni katika halianga, jambo ambalo laaminiwa husababishwa na binadamu.
Pia, binadamu hujaza vitu vichafu, mafuta, na hata takataka zenye sumu ndani ya bahari kuu. Ingawa nchi fulani-fulani huafikiana kuweka mpaka juu ya kadiri ya takataka watakazoruhusu zitupwe baharini, nyingine hukataa. Taifa moja la Magharibi hata huhifadhi haki yalo ya kumwaga-mwaga takataka za nyukilia baharini. Mpelelezi maarufu wa bahari kuu Jacques Cousteau aonya hivi: “Ni lazima tuziokoe bahari kuu ikiwa twataka kuokoa ainabinadamu.”
Maji ya Kunywa
Binadamu aangamiza hata maji yake ya kunywa! Katika mabara maskini, mamilioni ya watu hufa kila mwaka kwa sababu ya maji yaliyochafuliwa. Katika mataifa matajiri zaidi, miongoni mwa vitu ambavyo huchafua vyanzo vya maji mna dawa za mbolea na za kuua wadudu ambazo huchukuliwa na maji na kuingia katika mito na kupenya-penya katika maji ya chini ardhini. Katika 1986 dawa za kuua wadudu zilizotengenezwa na ulimwengu zilikuwa tani milioni 2.3, na kadiri ya kuongezeka kwazo yaripotiwa kuwa asilimia 12 kwa mwaka.
Chanzo kingine cha uchafuzi ni kemikali zinazomwagwa-mwagwa. ‘Mapipa yenye kemikali hizo,” yaeleza Scientific American, “ni sawa tu na makombora yaliyotegewa saa ambayo yatalipuka yaishapo kuchakaa.” Jarida hilo laongeza kwamba namna hii ya uchafuzi inatukia “ulimwenguni pote katika maelfu ya mimwago ya takataka za kemikali.”
Tokeo ni nini? Kotekote duniani, mito iliyokuwa safi sana wakati mmoja inageuzwa kuwa mitaro ya utakataka wa viwandani. Yakadiriwa kwamba Wanaulaya milioni 20 hunywa maji kutokana na Mto Rhine, hali mto huo umechafuliwa sana hivi kwamba utopetope ambao huzolewa kutokana na sakafu yao ni hatari mno kuutumia kwa kujazia mashimo ya ardhi!
Mazoea ya Ukulima
La kugutusha ni kwamba, binadamu anaangamiza hata ardhi yake ya ukulima. Katika United States pekee, asilimia 20 ya ardhi iliyowekwa kando iwe ya unyunyiziaji imeharibiwa, kulingana na Scientific American. Kwa nini? Kwa sababu unyunyiziaji wa kupita kiasi huongeza chumvi nyingi mno udongoni. Kwa njia hiyo nchi nyingi zimeharibu ardhi yenye thamani nyingi. “Ukubwa wa ardhi ambayo sasa inakuwa isiyozaa kwa sababu ya kutiliwa chumvi unalingana na ile inayotumiwa kwa mazao kupitia miradi mipya ya unyunyiziaji,” yataarifu The Earth Report. Tatizo jingine lililoenea kotekote ni kuweka mifugo mingi mno ya kulishwa, jambo ambalo huenda likawa linachangia mweneo wa majangwa.
Magari Mengi Mno
Sasa tuache hayo ya ardhi na maji ya sayari yetu. Lakini namna gani juu ya hewa yayo? Hiyo pia inaangamizwa, na wakosaji ni wengi. Kumtaja mmoja tu, lifikirie gari. Yanayofuata ni maonyo kutoka majarida matatu maarufu ya kisayansi: “Magari hutokeza uchafuzi mwingi wa hewa kuliko utendaji mwinginewo mmoja wa kibinadamu.” (New Scientist) “Sasa hivi kuna magari milioni 500 yaliyosajiliwa katika sayari hii . . . Kujaza tangi zayo humeza karibu theluthi moja ya mafuta yanayofanyizwa ulimwenguni. . . . Hesabu ya magari inaongezeka haraka kuliko idadi ya watu.” (Scientific American) “Petroli katika hatua zote za utengenezaji, utumizi na utupaji ni chanzo kikubwa cha uharibifu wa mazingira na cha magonjwa.”—The Ecologist.
Ndiyo, sayari yetu inatumiwa vibaya, inaangamizwa. Bahari zayo, maji ya kunywa, mashamba, na hata halianga yayo vinachafuliwa kwa kadiri kubwa mno. Kwa uhakika, hiyo pekee ingedokeza kwamba wakati uko karibu wa Mungu kuingilia mambo na “kuwaangamiza wale wanaoangamiza dunia.” (Ufunuo 11:18, HNWW) Hata hivyo, kuna njia nyinginezo, hata mbaya kuliko hizo, ambavyo dunia inaangamizwa. Acheni tuone hizo ni nini hasa.
[Blabu katika ukurasa wa 4]
“Ni lazima tuziokoe bahari kuu ikiwa twataka kuokoa ainabinadamu.”—Jacques Cousteau