Dunia Yetu Iliyoharibiwa-Mashambulizi Yapiga Maeneo Mengi
JUNI mwaka jana, Mkutano wa Dunia juu ya mazingira ulifanywa katika Rio de Janeiro, Brazili. Ili itokee wakati mmoja na mkutano huo, mwezi huohuo, gazeti India Today lilichapisha tahariri ya Raj Chengappa, mhariri msaidizi walo. Ilikuwa na kichwa “Dunia Iliyojeruhiwa.” Mafungu yayo ya kufungua yalitoa picha yenye kuchochea sana mawazo:
“Katika 1971 Edgar Mitchell aliporuka kwenda mwezini akiwa ndani ya Apollo 14, yale aliyoona alipotazama dunia kwa mara ya kwanza kutoka angani yalimchochea aeleze kishairi uzuri wayo. ‘Inaonekana kama kito cha buluu na nyeupe yenye kumeremeta . . . Iliyopambwa kwa vitambaa vyeupe vyenye kuzunguka-zunguka polepole . . . Kama lulu ndogo ikiwa katika bahari nyeusi ya fumbo,’ akaeleza hisia zake katika ujumbe aliopeleka kwa redio kwenye kituo cha anga za juu cha Houston.
“Miaka ishirini na mmoja baadaye, kama Mitchell angerudishwa kwenye anga za juu, wakati huu akiwa na miwani yenye kumruhusu kuona zile gesi zisizoonekana za angahewa ya dunia, angeona picha tofauti sana. Angeona matundu makubwa mno katika ozoni yenye kukinga dunia yaliyo juu ya Antaktika na Amerika Kaskazini. Badala ya kito cha buluu na cheupe chenye kumeremeta angeona dunia isiyovutia, iliyo chafu, yenye kujaa mawingu meusi yenye kuzunguka-zunguka ya dioksaidi za kaboni na sulfuri.
Kama Mitchell angetwaa kamera yake na kupiga picha misitu yenye kufunika dunia na kuilinganisha na zile alizopiga katika 1971, angeshtushwa sana na kiasi ambacho imepungua. Na kama angefungua darubini yake ya pekee ili kumsaidia kuchunguza ile takataka iliyomo ndani ya maji ya dunia, angeona mistari ya sumu yenye kupitana-pitana juu ya matungamano ya ardhi na vidonge vyeusi vya lami vyenye kufunika sehemu kubwa ya sakafu ya bahari. ‘Houston,’ angalipeleka ujumbe kwa redio, ‘jamani tumefanya nini?’
“Kwa kweli, sisi hatuhitaji kwenda kilometa 36,000, ndani ya anga za juu ili tujue jambo ambalo tumefanya. Leo, twaweza kunywa, kupumua, kunusa na kuona uchafuzi. Katika muda wa miaka 100, na zaidi sana katika miaka 30 iliyopita, wanadamu wameileta dunia ukingoni mwa msiba. Kwa kurusha katika angahewa kiasi kikubwa mno cha gesi zenye kunasa joto tunaanzisha mabadiliko yenye kudhoofisha halihewa. Gesi zinazotumiwa na friji zetu na visawazisha-halihewa vyetu ndivyo vinavyopunguza sasa tabaka ya ozoni, na kutuweka katika hatari ya kupatwa na kansa ya ngozi na kugeuza muundo vichukua-tabia katika wanyama wadogo. Wakati huohuo, tumeharibu sehemu kubwa za ardhi, tumeharibu misitu kwa mwendo wa kasi sana, tumetupa tani nyingi za sumu ndani ya mito ovyoovyo na kumwaga kemikali zenye sumu ndani ya bahari zetu.
“Sasa zaidi ya chochote kinginecho tisho kwa wanadamu huja kutoka uharibifu wa mazingira ya dunia. Na inahitaji shirika lenye kutenda duniani pote ili kuzuia maangamizi.”
Baada ya kuhesabu matatizo mengi yanayohusu mazingira ambayo lazima mataifa yakazie fikira kuyatatua yahusuyo mazingira, Raj Chengappa amalizia tahariri yake kwa maneno haya: “Yote hayo lazima yafanywe bila kukawia. Kwa maana tisho si kwa wakati ujao wa watoto wako tena. Ni la sasa hivi.”
Hivyo madaktari wa dunia wakusanyika. Mashauriano hufanywa, maponyo hudokezwa, lakini madaktari hao hawawezi kuafikiana. Wao hubishana tu. ‘Si yenye ugonjwa kwa kweli,’ baadhi yao wasema. ‘Ni mahututi!’ wengine walia. Majadiliano yazidi, maponyo yazidi kupendekezwa, madaktari wakawia-kawia kuchukua hatua, huku mgonjwa akizidiwa. Hakuna lifanywalo. Wahitaji kufanya uchunguzi zaidi. Wamwandikia mgonjwa dawa lakini dawa hazitolewi. Ole, yote hayo ni mbinu za kukawiza ili kuruhusu uchafuzi uendelee nazo faida zirundamane. Mgonjwa hapati dawa, taabu zake zaongezeka, hatari yazidi, na kuharibiwa kwa dunia kwaendelea.
Dunia na uhai ulioko juu yayo ni tata sana, umefumishwa kwa njia inayotatanisha. Mamilioni ya viumbe hai vyenye kuhusiana yamerejezewa kuwa utando wa uhai. Kata uzi mmoja, nao utando huenda ukaanza kufumuka. Angusha domino moja, na nyingi zaanguka. Kufyekwa kwa msitu wa mvua hutoa kielezi cha jambo hilo.
Kwa usanidimwanga (fotosinthesi) misitu ya mvua hutwaa kaboni dioksaidi kutoka hewani na kuirudishia oksijeni. Hunywa kiasi kikubwa mno cha maji ya mvua lakini hutumia kidogo sana katika kufanyiza chakula chayo. Kiasi kikubwa sana cha maji hayo hurudishwa katika angahewa kikiwa mvuke. Huko mvuke huo hufanyiza mawingu mapya ya mvua kwa ajili ya mvua nyingine ihitajiwayo kwa ajili ya misitu ya mvua na mamilioni ya mimea na wanyama walio hai ilishayo chini ya uvuli wa matawi yayo mabichi.
Halafu misitu ya mvua yafyekwa. Kaboni dioksaidi inabaki juu ikiwa kama blanketi yenye kunasa joto la jua. Oksijeni kidogo sana inaongezwa kwenye angahewa kwa faida ya wanyama. Mvua kidogo sana inarudishwa katika angahewa ikiwa mvuke kwa ajili ya mvua zaidi. Badala ya hivyo, mvua yoyote iangukayo hukimbia kasi juu ya ardhi kuingia ndani ya vijito, ikichukua udongo wenye rutuba unaohitajiwa kwa ukuzi wa mimea. Vijito na maziwa huchafuliwa, samaki hufa. Udongo huchukuliwa na kupelekwa baharini na kufunika matumbawe ya tropiki, nayo matumbawe hayo hufa. Mamilioni ya mimea na wanyama ambao wakati mmoja walisitawi chini ya uvuli wa matawi mabichi watoweka, mvua kubwa ambayo wakati mmoja ilinyeshea ardhi yapungua, nao ule utaratibu wa polepole unaochukua muda mrefu wa ardhi kuwa jangwa waanza. Kumbuka, lile Jangwa kubwa la Sahara la Afrika lilikuwa kijani wakati mmoja, lakini sasa eneo hilo la mchanga lililo kubwa zaidi ya yote duniani linaingia katika sehemu za Ulaya.
Kwenye Mkutano wa Dunia, United States na nchi nyinginezo matajiri zilitumia msongo kujaribu kufanya Brazili na nchi nyingine zinazositawi ziache kufyeka misitu yao ya mvua. “United States hutoa hoja,” kulingana na ripoti ya New York Times, “kwamba misitu, hasa misitu ya kitropiki, inaharibiwa kwa kadiri yenye kushtusha katika ulimwengu unaositawi na kwamba dunia kwa ujumla itakuwa katika hali mbaya kama tokeo. Misitu, [United States] yatoa hoja, ni kitu chenye thamani ambacho husaidia kurekebisha halihewa kwa kufyonza kaboni dioksaidi yenye kunasa joto na ni makao ya sehemu kubwa ya spishi [jamii ya viumbe] zilizo hai.”
Shtaka la unafiki lilikuja haraka kutoka kwa mataifa yenye kuendelea. Kulingana na The New York Times, “wanachukizwa na yale wanayoona kuwa jitihada ya kuingiliwa kwa enzi kuu zao na nchi ambazo zilifyeka misitu yao muda mrefu uliopita kwa ajili ya faida lakini sasa zataka kuweka mzigo wenye kulemea wa kuhifadhi misitu ya tufe juu ya nchi zinazong’ang’ana ili ziendelee kujimudu kiuchumi.” Mjumbe wa Malesia alilisema jambo hilo waziwazi: “Hakika sisi hatutahifadhi misitu yetu kwa ajili ya wale ambao waliharibu misitu yao wenyewe na sasa wanajaribu kudai yetu kuwa sehemu ya urithi wa ainabinadamu.” Katika Pasifiki Kaskazini-magharibi, United States ina asilimia 10 tu inayobaki ya misitu ya mvua iliyokua zamani za kale, nayo ingali inafyekwa, na bado United States inataka Brazili, ambayo ingali ina asilimia 90 ya misitu yayo ya Amazoni, ikome kabisa kufyeka miti.
Wale ambao huhubiria wengine, ‘Msiharibu misitu yenu,’ huku wakiharibu yao wenyewe, hukumbusha wale ambao huelezwa kwenye Warumi 2:21-23: “Basi wewe umfundishaye mwingine, je! hujifundishi mwenyewe? Wewe uhubiriye kwamba mtu asiibe, waiba mwenyewe? Wewe usemaye kwamba mtu asizini, wazini mwenyewe? Wewe uchukiaye sanamu, wateka mahekalu? Wewe ujisifuye katika torati, wamvunjia Mungu heshima kwa kuiasi torati?” Au ikisemwa kwa lugha ya kimazingira, ‘wewe, uhubiriye, “Hifadhini misitu yenu,” wafyeka yako mwenyewe?’
Mahangaikio ya joto linalozidi kuongezeka tufeni kote, yanafungamanishwa karibukaribu na uharibifu wa misitu. Mambo ya kemikali na vitokeza-joto ni magumu, lakini hangaikio linalenga sana-sana juu ya kemikali moja katika angahewa, kaboni dioksaidi. Hiyo ni sababu kubwa katika kuongezeka kwa joto kwa dunia. Watafiti wa Kituo cha Utafiti cha Byrd Polar waliripoti mwaka jana kwamba “mito ya barafu ya milima yenye kimo cha katikati na cha chini inayeyuka sasa na kupungua—baadhi yayo kwa kasi sana—na kwamba rekodi ya barafu iliyomo katika mito hiyo ya barafu huonyesha kwamba miaka 50 iliyopita imekuwa yenye joto zaidi kuliko pindi nyingine yoyote ya miaka 50” iliyorekodiwa. Kaboni dioksaidi ndogo mno ingemaanisha kuwa na baridi zaidi; kaboni dioksaidi nyingi zaidi ingemaanisha kuyeyuka kwa vilimabarafu na mito ya barafu kwenye ncha za dunia na kufurikisha majiji ya pwani.
Kuhusu kaboni dioksaidi India Today lilisema hivi:
“Huenda ikafanyiza kisehemu tu cha gesi za angahewa: Asilimia 0.03 ya jumla yote. Lakini bila kaboni dioksaidi, sayari yetu ingekuwa baridi kama mwezi. Kwa kunasa joto linaloenezwa kutoka uso wa dunia, hurekebisha joto tufeni kote kuwa digrii 15 za selsio zenye kuendeleza uhai. Lakini kiasi hicho kikiongezeka, dunia ingegeuka kuwa bafu kubwa la mvuke wenye joto.
“Kama vituo vya kukagua halijoto ya kitufe vinatoa habari yenye kutegemeka, mkazo unaongezeka kwamba jambo fulani lifanywe. Miaka ya 1980 ilikuwa na sita kati ya miezi saba ya kiangazi yenye joto kupita yote tangu halihewa ilipoanza kurekodiwa yapata miaka 150 iliyopita. Kwa wazi mhalifu ni: ongezeko la asilimia 26 la kaboni dioksaidi katika angahewa kupita kiwango cha kabla ya wakati wa ukuzi wa viwanda.”
Chanzo chadhaniwa kuwa tani bilioni 1.8 za kaboni dioksaidi zinazotokezwa kila mwaka kwa kuchoma mafuta ya visukuku. Mapatano yaliyotumainiwa ya kutumia udhibiti zaidi juu ya kutokezwa kwa kaboni dioksaidi yalipuuzwa sana kwenye Mkutano wa Dunia wa hivi karibuni hivi kwamba iliripotiwa kwamba “yalipandisha halijoto” huko ya wataalam wa tabia ya dunia. Mmoja wao alipandwa sana na hasira hivi kwamba alisema hivi: “Hatuwezi kuendelea kana kwamba hakuna lolote lililotukia. Ni uhakika usioweza kukanushwa kwamba akaunti ya benki ya gesi ya tufe lote imepoteza usawaziko wayo. Lazima jambo fulani lifanywe au sivyo karibuni tutakuwa na mamilioni ya wakimbizi wa kimazingira.” Alikuwa akirejezea wale ambao wangekimbia nchi zao zilizofurikishwa.
Suala jingine lenye kuhangaisha lahusu yale yaitwayo eti mashimo yaonekanayo katika tabaka la ozoni linalokinga dunia kutokana na miale ya kiukaurujuani yenye kusababisha kansa. Mhalifu mkuu ni ile gesi CFC (gesi ya methani yenye mchanganyiko wa florini na klorini). Zinatumiwa katika kutengeneza friji, virekebisha-joto, na sabuni na kuwa vitu vya kupuliziwa katika kufanyiza yavuyavu ya plastiki. Katika nchi nyingi zingali zinarushwa angani na minyunyizo ya erosoli. Zifikapo eneo la tabakastrato, miali ya jua ua kiukaurujuani huivunjavunja, nayo klorini huru huachiliwa, kila atomi yayo yaweza kuharibu angalau molekyuli 100,000 za ozoni. Mashimo, maeneo yaliyo na viwango vya ozoni vilivyopungua sana, huachwa katika tabaka la ozoni, katika Antaktika na katika latitudo za Kaskazini za dunia, jambo ambalo humaanisha kwamba miali mingi zaidi ya kiukaurujuani hufikia dunia.
Miali hii huua mimea planktoni na krili (chakula cha nyangumi), zilizo sehemu ya msingi ya mfululizo wa vyakula vya baharini. Mabadiliko hufanyizwa katika molekyuli za DNA (chembe za urithi) zilizo na fungu la sheria za vichukuatabia vya uhai. Mimea huathiriwa. Miali hii husababisha mtotojicho na kansa ya ngozi katika wanadamu. Watafiti wa NASA walipopata kiasi kikubwa cha klorini monoksaidi juu ya maeneo ya kaskazini mwa United States, Kanada, Ulaya, na Urusi, mmojapo watafiti hao alisema hivi: “Kila mtu apaswa kushtushwa na hilo. [Hali] ni mbaya zaidi ya vile tulivyodhani.” Lester Brown, msimamizi wa Worldwatch Institute, aliripoti hivi: “Wanasayansi wakadiria kwamba punguo linaloongezeka la tabaka la ozoni katika kizio cha kaskazini litasababisha vifo 200,000 zaidi katika U[nited] S[tates] pekee kutokana na kansa ya ngozi wakati wa miaka 50 inayofuata. Ulimwenguni pote, mamilioni ya maisha yatakuwa hatarini.”
Unamna-namna wa biolojia, kule kuendeleza mimea na wanyama wengi kadiri iwezekanavyo wakifanya kazi zao katika makazi yao ya asili, ni hangaikio jingine la wakati huu. Gazeti Discover lilichapisha habari kutoka kitabu cha karibuni cha mwanabiolojia Edward O. Wilson The Diversity of Life, ambamo aliorodhesha kuangamia kwa maelfu ya spishi za ndege, samaki, na wadudu, pamoja na spishi zisizoonwa kuwa za maana: “Nyingi za spishi zilizotoweka ni spishi za kuvu zenye kufaana na mizizi ya mimea yenye mbegu, hizo husaidia ufyonzaji wa vilishaji kwa mifumo ya mizizi ya mimea. Wanaekolojia wametaka kujua kwa muda mrefu ni jambo gani lingetukia kwa mifumo ya ekolojia ya ardhi ikiwa kuvu hizo zingeondolewa, nasi tutajua karibuni.”
Katika kitabu hicho Wilson aliuliza pia na kisha akajibu swali hili kuhusu umaana wa kuokoa spishi:
“Inafanyiza tofauti gani ikiwa baadhi ya spishi zamalizika, ikiwa hata nusu ya spishi zote za Dunia zatoweka? Acha nihesabu njia hizo. Vyanzo vipya vya habari ya kisayansi vitapotezwa. Uwezekano wa kuwa utajiri mkubwa mno wa kibiolojia utaharibiwa. Vitu ambavyo havijagunduliwa kama vile dawa, mazao, madawa ya tiba, mbao, utembo, mseto kutoka mimea, mimea yenye kurudisha udongo, vitu vinavyotumiwa badala ya petroli, na vitu vingine ambavyo hutengenezwa na vingine vizuri bado havitavumbuliwa. Watu wengine hupenda kudharau vitu vidogo-vidogo na visivyojulikana sana, wadudu na magugu, wakisahau kwamba nondo wasiojulikana sana kutoka Latini Amerika aliokoa ardhi ya malisho ya Australia isiharibiwe na ukuzi wenye kuenea sana wa mpungate, kwamba ua liitwalo waridi periwinkili liliandaa ponyo kwa ajili ya ugonjwa wa Hodgkini na lukemia ya limfu wa utotoni, kwamba ganda la mvinje wa Pasifiki hutoa tumaini kwa wanaopatwa na kansa ya matiti na ya ovari, kwamba kemikali fulani kutoka mate ya ruba huyeyusha damu iliyogandamana wakati wa upasuaji, na orodha ambayo tayari ni ndefu na yenye kutokeza yaendelea ijapokuwa ni utafiti mdogo ambao umefanywa ili kuvumbua maponyo kutoka kwa mimea na wanyama.
“Katika ndoto za kujisahaulisha ni rahisi pia kusahau utumishi mbalimbali unaoandaliwa wanadamu na mifumo ya ekolojia. Inatajirisha udongo na kufanyiza hewa hasa tupumuayo. Bila usaidizi huo muda ubakio wa kukaa duniani wa jamii ya kibinadamu ungekuwa wenye taabu sana na mfupi.”
Habari hiyo imepoteza ladha kwa kurudiwa-rudiwa, lakini ni kisehemu kidogo tu kinachowakilisha sehemu kubwa zaidi iliyofichika. Kuharibiwa kwa dunia kutakoma wakati gani? Na ni nani atakayekukomesha? Makala inayofuata itatoa majibu.
[Blabu katika ukurasa wa 4]
Lile jangwa kubwa la Sahara la Afrika lilikuwa kijani wakati mmoja
[Blabu katika ukurasa wa 5]
‘Wewe uhubiriye, “Hifadhini misitu yenu,” wafyeka yako mwenyewe?’
[Blabu katika ukurasa wa 5]
Kaboni dioksaidi kidogo mno—halihewa baridi zaidi
Nyingi mno yayo—mito ya barafu yenye kuyeyuka
[Blabu katika ukurasa wa 6]
“Inafanyiza tofauti gani ikiwa baadhi ya spishi zamalizika?”
[Blabu katika ukurasa wa 6]
Bila vijiumbe, muda wa kukaa duniani wa jamii ya kibinadamu ungekuwa mfupi na wenye taabu
[Picha katika ukurasa wa 7]
Msitu wa mvua wa Amazoni, ukiwa na uzuri wao wote wa asili
Misitu zaidi ya mvua, baada ya kuharibiwa na mwanadamu
[Hisani]
Abril Imagens/João Ramid
F4/R. Azoury/Sipa
[Picha katika ukurasa wa 8]
Kemikali za sumu zinazotupwa ovyoovyo zikichafua hewa, maji, na udongo
Feig/Sipa