Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g03 12/22 kur. 26-27
  • Misitu Ni Muhimu Kadiri Gani?

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Misitu Ni Muhimu Kadiri Gani?
  • Amkeni!—2003
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Haifai Kukata Miti
  • Sababu ya Kuhifadhi Misitu
  • Watu Wanahitaji Kubadili Tabia
  • Misitu
    Amkeni!—2023
  • Ni Nani Atakayeokoa Misitu ya Mvua?
    Amkeni!—2003
  • Manufaa za Misitu ya Mvua
    Amkeni!—1998
  • Dunia Yetu Iliyoharibiwa-Mashambulizi Yapiga Maeneo Mengi
    Amkeni!—1993
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—2003
g03 12/22 kur. 26-27

Misitu Ni Muhimu Kadiri Gani?

INGAWA thuluthi moja ya dunia ina misitu, idadi hiyo inaendelea kupungua. Katika mwaka wa 1998, gazeti Choices—The Human Development Magazine, lililochapishwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo, lilisema kwamba katika nchi zinazoendelea pekee, “misitu yenye ukubwa wa hekta milioni 4 [ekari milioni 10]—sawa na ukubwa wa Uswisi—hukatwa kila mwaka.”

Haifai Kukata Miti

Wataalamu fulani wanasema kwamba si jambo la akili kukata miti ili kupata pesa. Ripoti moja inasema kwamba misitu “ina faida nyingi zaidi inapohifadhiwa kuliko inapokatwa au kuharibiwa.” Kwa nini?

Dakt. Philip M. Fearnside na Dakt. Flávio J. Luizão, ambao ni watafiti katika Taasisi ya Kitaifa ya Utafiti wa Amazon, huko Manaus, Brazili, waliambia Amkeni! kwamba misitu ya mvua “hufaidi dunia.” Faida hizo zinatia ndani kufyonza na kuhifadhi kaboni-dioksidi (gesi inayoongeza joto la dunia), kuzuia mmomonyoko wa udongo na mafuriko, kurutubisha udongo, kudhibiti mvua, na kuandaa makao kwa ajili ya wanyama walio katika hatari ya kuangamia na kulinda mimea ya msituni. Misitu pia hufanyiza mandhari yenye kupendeza na mahali pa kustarehe. Watafiti hao wanasema kwamba manufaa hizo zote zina faida za kiuchumi.

Kwa mfano, fikiria faida ya kuhifadhi kaboni. Misitu inapokatwa, miti hutoa kaboni ambayo hufanyiza kaboni-dioksidi na kuingia hewani hivyo kusababisha ongezeko la joto duniani. Kwa hiyo, tunaweza kukadiria faida ya kiuchumi ambayo misitu huleta inapohifadhi kaboni kwa kuhesabu gharama ya kupunguza kaboni inayotokezwa na shughuli za wanadamu.

Kulingana na Marc J. Dourojeanni, mshauri wa mazingira katika ofisi ya Brazili ya Benki ya Maendeleo ya Amerika, makadirio hayo yanaonyesha kwamba “misitu ina thamani kubwa zaidi inapohifadhi kaboni kuliko inapokatwa na watu ili wapate mashamba au mbao.” Hata hivyo, bado misitu mingi zaidi inakatwa. Kwa nini?

Sababu ya Kuhifadhi Misitu

Fikiria mfano huu: Watu kadhaa wanamiliki mtambo wa kutokeza nguvu za umeme. Mtambo huo unasambaza nguvu za umeme kwenye miji ya karibu, lakini watu hawalipii huduma hiyo. Baada ya muda, wamilikaji wa mtambo huo wanaona, ‘Ni afadhali kuufunga mtambo, kuubomoa na kuuza vifaa vyote ili kupata pesa kuliko kuwa na mtambo ambao hauleti faida yoyote.’ Maafisa fulani katika nchi zenye misitu mingi wana maoni kama hayo pia. Hivyo wanaona kwa kuwa watu ulimwenguni hawalipii huduma za misitu, ni afadhali kukata misitu (ni kama kubomoa mtambo) na kuuza miti (kuuza vifaa) ili kupata faida yote mara moja.

Dourojeanni anasema kwamba jambo hilo linaweza kuepukwa kwa kuwaonyesha watu faida za kifedha za kuhifadhi misitu. Profesa Dakt. José Goldemberg, mwanafizikia wa nyuklia Mbrazili, aliyekuwa msimamizi wa Chuo Kikuu cha São Paulo, anapendekeza watu wanaotumia nishati ya mafuta na makaa ya mawe watozwe “kodi ya kaboni ya ulimwenguni pote.”

Kwa maoni ya watetezi wa nadharia hiyo, kodi hiyo itatozwa kulingana na kiasi cha nishati kilichotumiwa na nchi fulani na vilevile kiasi cha gesi zinazoongeza joto la dunia ambazo zilitokezwa. Kwa mfano, Marekani ambayo ina asilimia 5 hivi ya watu duniani hutoa asilimia 24 hivi ya gesi hizo. Wapangaji fulani wa mikakati wanasema kwamba nchi ambazo hazikati misitu ili zijitajirishe haraka ndizo zitakazolipwa kodi hiyo. Basi ni kana kwamba watu wanaotumia nguvu za umeme wanalipia huduma za umeme, na wamilikaji watachochewa kudumisha ‘mtambo huo wa umeme’ kwa sababu wanapata faida.

Hata hivyo, ni nani atakayeamua bei ya huduma za mazingira? Kisha ni nani atakayekusanya na kulipa pesa hizo?

Watu Wanahitaji Kubadili Tabia

Dourojeanni anapendekeza kwamba “kongamano la misitu la ulimwenguni pote lianzishwe ili masuala hayo yajadiliwe vizuri zaidi.” Kongamano hilo litaamua bei za huduma za misitu. Kisha “shirika la misitu ulimwenguni lianzishwe kusimamia harakati hizo za kimataifa.”

Ijapokuwa inaonekana ni jambo la busara kuwa na shirika la kimataifa la kushughulikia tatizo la kimataifa, Dourojeanni anakiri hivi: “Taasisi na tume nyingi zilizoanzishwa kushughulikia masuala ya misitu hazijasaidia.” Anasema kwamba kinachohitajiwa hasa ni “mabadiliko makubwa ya kijamii na kiuchumi.” Ama kweli, kuhifadhi misitu kunahitaji badiliko la moyoni si badiliko la sheria tu.

Je, matatizo kama hayo yatasuluhishwa wakati wowote? Muumba wa dunia, Yehova Mungu anaahidi kwamba yatasuluhishwa. Biblia inasema kwamba ameanzisha serikali ambayo itatawala dunia nzima na kusuluhisha matatizo yote. Serikali hiyo ‘haitaharibiwa kamwe.’ (Danieli 2:44) Isitoshe, itahakikisha rasilimali za dunia zinatumiwa vizuri, huku wakazi wa dunia wakiendelea kujifunza kumhusu Muumba wao, ambaye Biblia inamwita Yehova. (Isaya 54:13) Wanadamu wote watakaoishi wakati huo wataithamini dunia kabisa, kutia ndani misitu.

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 26]

Ricardo Beliel / SocialPhotos

© Michael Harvey/Panos Pictures

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki