Angahewa Letu Linapoharibiwa
KATIKA 1971, akiwa njiani kuelekea mwezini ndani ya Apollo 14, Edgar Mitchell alipoona dunia alisema hivi: “Yaonekana kama kito cha samawati na cheupe kinachometameta.” Lakini leo mtu akiwa angani angeona nini?
Ikiwa miwani maalumu zingemruhusu kuona gesi zisizoonekana za angahewa la dunia, angeona picha tofauti kabisa. Katika gazeti India Today, Raj Chengappa aliandika hivi: “Angeona mitoboko mikubwa katika ngao-linzi ya ozoni juu ya Antarktika na Amerika ya Kaskazini. Badala ya umeremeti wa kito cha samawati na cheupe angeona dunia iliyofifia, iliyo chafu ikiwa imejaa, mawingu ya dayoksidi za kaboni na salfa yanayozunguka vuruvuru.”
Ni nini kimetoboa mashimo katika ngao linzi ya ozoni katika angahewa letu la juu? Je, ongezeko la vichafuzi vya angahewa kwa kweli ni hatari hivyo?
Jinsi Ozoni Inavyoharibiwa
Zaidi ya miaka 60 iliyopita, wanasayansi walitangaza uvumbuzi wa kijokofushaji kilicho salama ambacho kingechukua mahali pa vinginevyo vilivyokuwa na sumu na kutoa harufu mbaya. Hiyo kemikali mpya ilifanyizwa na molekuli zilizokuwa na kaboni moja, klorini mbili, na atomi za florini mbili (CCl2F2). Hiyo na kemikali zifananazo nayo zilizotengenezwa na mwanadamu huitwa klorofluorokaboni (CFCs).
Kufikia miaka ya mapema ya 1970, utengenezaji wa kemikali za CFC ulikuwa umekuwa biashara kubwa ulimwenguni pote. Zilikuwa zikitumiwa si katika friji tu bali pia katika mikebe ya kunyunyiza erosoli, katika vidhibiti-hewa, katika visafishio, na utengenezaji wa vibebeo vya chakula cha haraka na bidhaa nyingine za plastiki.
Hata hivyo, katika Septemba 1974, wanasayansi wawili, Sherwood Rowland na Mario Molina, walieleza kwamba kemikali za CFC polepole hupaa kwenye angatando ambapo hatimaye kemikali hizo hutoa klorini yazo. Kila atomi ya klorini, wanasayansi hao walipiga hesabu, ingeweza kuharibu maelfu ya molekuli za ozoni. Lakini badala ya ozoni kuharibiwa kwa usawia katika lile angahewa la juu, uharibifu umekuwa mwingi zaidi juu ya maeneo ya nchani.
Kila masika tangu 1979, kiasi kikubwa cha ozoni kimetoweka kisha hutokea katika Antarktiki. Huu upungufu wa kimsimu katika ozoni huitwa shimo la ozoni. Zaidi, katika miaka ya majuzi shimo hilo limeendelea kuwa nene na ladumu zaidi. Katika 1992, vipimo vya setalaiti vyalifunua shimo la ozoni lililo la saizi kubwa—kubwa kuliko Amerika Kaskazini. Na si ozoni nyingi iliyosalia katika hilo. Vipimo vya puto vyalifunua kushuka kwa zaidi ya asilimia 60—kiwango cha chini sana kilichopata kurekodiwa.
Kwa sasa, viwango vya ozoni vimekuwa vikishuka pia katika angahewa la juu katika sehemu nyingine za dunia. “Vipimo vya karibuni zaidi,” laripoti lile gazeti New Scientist, “vyaonyesha kwamba . . . kulikuwa na thamani zisizo za kawaida za chini sana za ukolezi wa ozoni katika 1992 katikati ya latitudo 50° Kaskazini na 60° Kaskazini, ikienea Ulaya Kaskazini, Urusi na Kanada. Kiwango cha ozoni kilikuwa asilimia 12 chini ya kawaida, chini kuliko wakati mwingine wowote katika miaka 35 ya uangalizi wenye kuendelea.”
“Hata yale matabiri yaliyo ya msiba zaidi,” lataarifu lile jarida la Scientific American, “sasa yaonyeshwa kuwa yalipunguza uzito wa kutoweka kwa ozoni kulikosababishwa na klorofluorokaboni. . . . Na ilhali katika wakati huo, sauti zenye nguvu katika serikali na viwanda zilipinga sana kanuni hizo, kwa msingi wa uthibitisho wa kisayansi usio kamili.”
Tani zikadiriwazo kuwa milioni 20 za kemikali za CFC tayari zimeachiliwa kuingia katika angahewa. Kwa sababu kemikali za CFC huchukua miaka kuabaa juu katika angatando, mamilioni ya tani bado hazijafikia angahewa la juu ambapo hufanya madhara yazo. Hata hivyo, si kemikali za CFC tu ambayo ni chanzo cha klorini yenye kuharibu ozoni. “NASA yakadiria kwamba yapata tani 75 za klorini huachwa katika tabaka la ozoni kila wakati basi la anga lirushwapo,” laripoti lile gazeti Popular Science.
Ni Madhara Yaliyoje?
Yale madhara ya ozoni inayopungua kwenye angahewa la juu hayajaeleweka kikamili. Hata hivyo, jambo moja linaloonekana kuwa hakika ni kwamba kiasi cha miali yenye madhara ya UV (kiukaurujuani) inayofikia dunia kinaongezeka, kikitokeza visa vingi vya kansa ya ngozi. “Wakati wa mwongo uliopita,” laripoti jarida la Earth, “kiwango cha miali ya UV yenye madhara kinachofikia kizio cha kaskazini kila mwaka kimepanda kufikia asilimia 5.”
Ongezeko la asilimia 1 katika kiukaurujuani lakadiriwa kusababisha ongezeko la asilimia 2 hadi 3 la kansa ya ngozi. Gazeti la Kiafrika Getaway lasema hivi: “Kuna visa vipya vya kansa zaidi ya 8 000 katika Afrika Kusini kila mwaka . . . Sisi tuna mojapo ya viwango vya chini zaidi vya ulinzi vya ozoni na mojapo visa vingi zaidi vya kansa ya ngozi (mahusiano hayo hayakupatana kwa sadfa tu).”
Jambo la kwamba kule kuharibiwa kwa ozoni katika angahewa la juu kungesababisha ongezeko la kansa ya ngozi lilikuwa limetabiriwa na wanasayansi Rowland na Molina miaka mingi iliyopita. Walipendekeza kupiga marufuku mara moja matumizi ya kemikali za CFC kwenye erosoli katika Marekani. Kwa kutambua hatari hiyo, nchi nyingi zimekubali kuacha kufanyiza kemikali za CFC kufikia Januari 1996. Hata hivyo, kwa wakati huu matumizi ya kemikali CFC yaendelea kutokeza hatari kwa uhai duniani.
Kule kushuka kwa ozoni kote Antarktika, laripoti Our Living World, “kumeruhusu unururishi wa kiukaurujuani kupenya ndani zaidi kwenye bahari kuu kuliko ilivyodhaniwa mbeleni. . . . Hili limesababisha kupungua kwa kiasi kikubwa katika ule ufanyizwaji wa viumbe vyenye seli moja vifanyizavyo msingi wa ule mfuatano wa chakula cha baharini.” Machunguzo huonyesha pia kwamba ongezeko katika miali UV hupunguza zao la mimea mingi, ikitokeza hatari kwa ugawaji wa chakula tufeni.
Hakika, ule utumiaji wa kemikali za CFC waweza kutokeza msiba mkubwa. Hata hivyo angahewa letu linapigwa na vichafuzi vingine vingi. Kimojapo ni gesi ya kiangahewa ambayo ni muhimu kwa uhai duniani iwapo ya kiasi katiti.
Matokeo ya Uchafuzi
Miaka ya katikati ya karne ya 19, wanadamu walianza kuchoma kiasi kikubwa cha makaa-mawe, gesi, na mafuta, ikiongeza kiasi kikubwa cha kaboni dayoksidi kwenye angahewa. Kwa wakati huo kiasi cha hii gesi-katiti ya kiangahewa kilikuwa karibu sehemu 285 kwa milioni. Lakini, kama tokeo la matumizi yaliyoongezeka ya mwanadamu ya fueli za visukuku, kiwango cha kaboni dayoksidi kimefikia zaidi ya sehemu 350 kwa milioni. Gesi hii yenye kunasa joto iliyo katika angahewa imekuwa na matokeo gani?
Wengi huamini kwamba lile ongezeko la viwango vya kaboni dayoksidi ndilo limesababisha kupanda kwa halijoto ya dunia. Hata hivyo, wachunguzi wengine husema kwamba ujoto wa tufeni hususa ni kwa sababu ya kubadilikana kwa jua letu—kwamba jua limekuwa likitoa nishati nyingi katika nyakati za majuzi.
Hata iweje, ule mwongo wa 1980 ulikuwa ndio wenye joto zaidi tangu rekodi zianze kuwekwa katikati ya karne ya 19. “Mwelekeo huo uliendelea hadi mwongo huu,” laripoti gazeti la Afrika Kusini The Star, “huku 1990 ukiwa ndio mwaka wenye joto zaidi katika rekodi, 1991 wa tatu kwa joto, na 1992 . . . wa kumi kwa joto kwenye rekodi ya miaka 140.” Yale mapunguo madogo kwa muda wa miaka miwili iliyopita yasemwa yalisababishwa kwa vumbi lililotupwa katika angahewa Mlima Pinatubo ulipolipuka katika 1991.
Matokeo ya wakati ujao ya ongezeko la halijoto duniani yajadiliwa sana. Lakini kwa wazi jambo moja ambalo ongezeko la joto tufeni limefanya ni kutatanisha lile jukumu gumu tayari la kutabiri halihewa. New Scientist lataarifu kwamba utabiri mbaya “huenda ukaongezeka kadiri hali ya kuongezeka kwa joto tufeni kubadilipo tabia-anga.”
Kampuni nyingi za bima zahofia kwamba kuongezeka kwa joto tufeni kutafanya sera zao zisiwe na faida. “Wakikabiliwa na mfuriko [fulani] wa masaibu,” lakiri The Economist, “wanabima fulani wamepunguza uandalizi wa kinga ya misiba ya asili. Wengine wanazungumzia kuacha soko hilo kabisa. . . . Wanatishwa na kukosa hakika.”
Kwa kiasi kikubwa, katika 1990, mwaka wenye joto zaidi katika rekodi, sehemu iliyo kubwa ya ule utando wa barafu ya Arktiki imepungua kwa digrii kubwa. Hili lilitokeza mamia ya dubu wa nchani kuachwa kwenye shida kwa zaidi ya mwezi mmoja katika Kisiwa cha Wrangell. “Kwa kuongezeka kwa joto la tufeni,” laonya lile gazeti la BBC Wildlife, “hali hizi . . . huenda ziwe tukio la kawaida.”
“Wastadi wa halihewa,” ikaripoti karatasi habari moja ya Afrika katika 1992, “wanalaumu ongezeko la joto tufeni kuwa ndilo linalosababisha ongezeko lenye kutazamisha la idadi ya vilima-barafu vinavyopeperushwa kaskazini kutoka Antarktika na kutokeza hatari kwa meli katika Atlantiki ya kusini.” Kulingana na ile makala ya Januari 1993 ya Earth, kule kupanda kwa kiwango cha bahari katika ufuo kusini mwa California ni kwa sababu ya ongezeko la ujoto wa maji, kwa sehemu.
Kwa kusikitisha, wanadamu huendelea kujaza kiasi kingi cha gesi zenye sumu katika angahewa. “Katika Marekani,” chaarifu kile kitabu The Earth Report 3, “ripoti ya 1989 na Shirika la Ulinzi wa Kimazingira yakadiria kwamba zaidi ya tani 900,000 za kemikali zenye sumu hujazwa kwenye hewa kila mwaka.” Tarakimu hizi zafikiriwa kuwa kadirio la chini kwa sababu hazitii ndani mioshi itokayo katika mamilioni ya magari.
Ripoti zenye kugutusha za uchafuzi wa hewa zaja kutoka mataifa yale mengine yenye viwanda pia. Yenye kuogofya hasa yamekuwa ni yale mafunuo ya majuzi ya uchafuzi wa hewa usiodhibitiwa katika mabara ya Ulaya ya Mashariki katika wakati wa miongo ya utawala wa Kikomunisti.
Miti ya dunia, inayovuta kaboni dayoksidi na kutoa oksijeni, imekuwa miongoni mwa majeruhi yaliyodhuriwa na hewa yenye sumu. New Scientist liliripoti: “Miti ya Ujerumani kwa kuongezeka inakua bila afya, kulingana na . . . waziri wa kilimo [aliyesema] kwamba uchafuzi wa hewa waendelea kuwa mojapo sababu kuu za kudhoofika kwa afya ya misitu.”
Hali ni hiyohiyo kwenye Mbuga ya Juu ya Transvaal ya Afrika Kusini. “Ishara za kwanza za madhara ya mvua ya asidi sasa zatokea kwenye Transvaal ya Mashariki ambapo sindano za msonobari zabadilika kutoka njano nzito yenye afya hadi njano yenye vidoadoa,” aripoti James Clarke katika kitabu chake Back to Earth.
Ripoti kama hizo huja kutoka ulimwenguni pote. Hakuna nchi isiyoweza kupatwa na madhara hayo. Zikiwa na mabohari yanayofika juu kwenye anga, nchi zenye viwanda hutapanya uchafuzi wazo kwenye mabara jirani. Rekodi ya mwanadamu ya maendeleo yenye pupa kiviwanda haipi tumaini.
Hata hivyo, kuna msingi wa kuwa na tazamio zuri. Tunaweza kuwa na uhakika kwamba angahewa letu lenye thamani litaokolewa kutoka kwa maangamizi. Jifunze katika makala inayofuata jinsi hilo litatimizwa.
[Picha katika ukurasa wa 7]
Kuharibiwa kwa ozoni kwenye angahewa la juu kumeongoza kwenye ongezeko la kansa ya ngozi
[Picha katika ukurasa wa 9]
Ni nini madhara ya uchafuzi kama huo?