Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g96 1/8 kur. 3-5
  • Lile Pigano la Kuokoa Sayari Yetu

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Lile Pigano la Kuokoa Sayari Yetu
  • Amkeni!—1996
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Tisho Lenye Kukua
  • Lile Pigano Ili Kulinda Sayari
  • Angahewa Letu Linapoharibiwa
    Amkeni!—1994
  • Je, Hilo Pigano Linafanikiwa?
    Amkeni!—1996
  • Sayari Yetu Dhaifu—Vipi Kuhusu Wakati Ujao?
    Amkeni!—1996
  • Jinsi Angahewa Letu Litakavyookolewa
    Amkeni!—1994
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1996
g96 1/8 kur. 3-5

Lile Pigano la Kuokoa Sayari Yetu

NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA HISPANIA

YURY, anayeishi katika jiji la Urusi la Karabash, ana watoto wawili, na wote wawili ni wagonjwa. Yeye ana wasiwasi lakini hashangai. “Huku hakuna watoto wenye afya,” yeye aeleza. Watu wa Karabash wanasumishwa. Kila mwaka kiwanda cha hapo hutupa hewani tani 162,000 za vichafuzi—tani tisa kwa kila mwanamume, mwanamke, na mtoto anayeishi huko. Katika Nikel na Monchegorsk kwenye Kola Peninsula, kaskazini mwa Mzingo Aktiki, “miwili ya mitambo ya kuyeyusha nikeli iliyo mikubwa kupita yote ulimwenguni na ya kale mno . . . hutupa hewani metali nzito zaidi na salfa dioksidi kila mwaka kuliko viwanda vinginevyo vyote vya jinsi hiyo katika Urusi.”—The New York Times.

Hewa si afadhali kamwe katika Jiji la Mexico. Uchunguzi uliofanywa na Dakt. Margarita Castillejos ulipata kwamba hata katika eneo la jiji wanalokaa matajiri, watoto walikuwa wagonjwa siku nne kwa kila siku tano. “Kuwa kwao wagonjwa kumekuwa jambo la kawaida,” mwanamke huyo akaonelea. Kimojapo visababishi vikuu, asema ni kungugu lenye kuenea linalotokezwa na maelfu ya magari ambayo husongamana katika barabara za jiji. Ukolevu wa ozoni ni mara nne zaidi ya kima cha juu cha mwongozo wa Shirika la Afya Ulimwenguni.

Katika Australia hiyo hatari haionekani—lakini ni hatari vilevile. Ni lazima sasa watoto wavae kofia wanaporukaruka katika uwanja wa kuchezea shuleni. Kufyekwa kwa kilinzi cha ozoni katika Kizio-Nusu cha Kusini kumefanya Waaustralia kuanza kuliona jua kuwa adui badala ya rafiki. Tayari wameona ongezeko la mara tatu katika kansa ya ngozi.

Katika sehemu nyinginezo za ulimwengu, kupata maji ya kutosha ni mng’ang’ano wa kila siku. Wakati Amalia alikuwa na umri wa miaka 13, ukame ulikumba Msumbiji. Kwa mwaka wa kwanza kulikuwa uhaba wa maji na mwaka uliofuata hakukuwa na yoyote. Mimea ilinyauka na kufa. Amalia na familia yake walilazimika kula matunda ya mwituni na kuchimba kwenye lalio la mto ili kupata angalau tone la maji yenye thamani.

Katika jimbo la India la Rajasthan, ni ardhi ya kulisha mifugo ambayo yayoyomea kwa kasi mno. Phagu, mzee mmoja wa mbari ya wafugaji, mara kwa mara huteta na wakulima wa hapo. Yeye hawezi kupata malisho kwa ajili ya kundi lake la kondoo na mbuzi. Kwa sababu ya uhaba mkubwa wa ardhi yenye rutuba, karne nyingi za kukaa pamoja kwa amani baina ya wakulima wa wafugaji zimefikia kikomo.

Hali ni mbaya hata zaidi katika Sahel, ukanda mpana wa ardhi wenye unyaufu wa kadiri kwenye ukingo wa kusini wa Sahara katika Afrika. Kama tokeo la ufyekaji misitu kisha tokeo la ukame, makundi mazima ya mifugo yamefyekwa na mashamba madogo yasiyohesabika yamemezwa na jangwa lenye kusogelea. “Sitapanda tena,” akaapa mkulima mmoja wa kabila la Fulani kutoka Niger baada ya kuona mtama wake ukikosa kufaulu kwa mara ya saba. Tayari ng’ombe wake walikuwa wamekufa kutokana na ukosefu wa malisho.

Tisho Lenye Kukua

Kuna kigezo chenye kutisha kifuatacho ukame wa hivi majuzi, mavuno yaliyofeli, na hewa iliyochafuliwa ambayo husonga pumzi jiji baada ya jiji. Hizi ni dalili za sayari yenye maradhi, sayari ambayo haiwezi tena kumudu mahitaji yote ambayo mwanadamu anairundikia.

Hakuna kitu kilicho muhimu zaidi duniani kwa uokokaji wetu kuliko hewa tunayopumua, chakula tunachokula, na maji tunayokunywa. Kuzidisha mambo, vitu hivi vya lazima katika kutegemeza uhai ama vinachafuliwa ama kutoweshwa—na mwanadamu mwenyewe. Katika nchi nyingine hali ya mazingira tayari yatisha uhai. Kama vile aliyekuwa rais wa Muungano wa Sovieti Mikhail Gorbachev alivyosema waziwazi, “ikolojia imetukaba kooni.”

Hilo si tisho la kuchukuliwa vivi hivi tu. Idadi ya watu ulimwenguni inaongezeka kwa haraka sana, na matakwa juu ya rasilimali ambazo ni zenye mipaka yanarudufika. Lester Brown, msimamizi wa Taasisi ya Worldwatch, hivi majuzi alitaarifu kwamba “tisho kubwa mno kwa wakati ujao wetu si uvamizi wa kijeshi bali ni kudhoofika kwa mazingira ya sayari.” Je, hatua za kutosha zinachukuliwa ili kuepushia mbali msiba?

Lile Pigano Ili Kulinda Sayari

Ni vigumu kumsaidia mraibu wa alkoholi ambaye amesadiki kwamba hana tatizo la kileo. Vivyo hivyo, hatua ya kwanza katika kuboresha afya ya sayari ni kufahamu mweneo wa maradhi. Huenda elimu ni fanikio la mazingira lenye kutokeza sana katika miaka ya hivi majuzi. Watu wengi leo wanafahamu kabisa kwamba dunia yetu inadhoofishwa na kuchafuliwa—na kwamba jambo fulani lazima lifanywe kuihusu. Tisho la kudhoofika kwa mazingira lanyemelea zaidi kuliko tisho la vita ya nyukilia.

Viongozi wa ulimwengu hawachukui vivi hivi hayo matatizo. Viongozi wa serikali wapatao 118 walihudhuria mkutano wa Earth Summit katika 1992, wakati ambapo hatua chache zilichukuliwa kuelekea kulinda angahewa na rasilimali za dunia zinazodidimia. Nchi nyingi zilitia sahihi mkataba kuhusu tabia ya nchi ambao katika huo zilikubaliana kuweka mfumo wa kuripoti mabadiliko katika mitoko ya kaboni, zikiwa na nia ya kumaliza jumla ya mitoko hiyo yote katika wakati ujao wa karibuni. Pia zilifikiria njia ya kulinda salama unamna mwingi wa viumbe vya sayari yetu, jumla ya idadi ya spishi za mimea na wanyama. Mkataba haukuweza kufikiwa juu ya kulinda misitu ya ulimwengu, lakini huo mkutano ulitokeza hati mbili—“Julisho-Wazi la Rio” na “Ajenda 21,” ambazo zilikuwa na mwongozo kuhusu jinsi nchi mbalimbali zingeweza kufikia “maendeleo ya kuvumilika.”

Kama vile mtaalamu wa mazingira Allen Hammond aonyeshavyo, “mtihani mkuu utakuwa kama mkataba uliofanywa katika Rio utatiliwa maanani—kama maneno ya ujasiri yataongoza kwenye hatua fulani katika miezi na miaka ya usoni.”

Hata hivyo, kupiga hatua mbele kwenye kutokeza kulitukia mnamo 1987, katika Mkataba wa Montreal, uliohusisha mwafaka wa kimataifa wa kuondoshea mbali klorofluorokaboni (CFC) katika kipindi fulani cha wakati kilichowekwa.a Kwa nini wahangaike hivyo? Kwa sababu CFC zasemekana kuwa zachangia upungufu wa haraka wa tabaka la ozoni lenye kukinga la dunia. Ozoni katika angahewa la juu la dunia huchangia fungu muhimu katika kuchuja miali ya jua ya kiukaurujuani, ambayo yaweza kusababisha kansa ya ngozi na uvimbe jichoni. Hili si tatizo katika Australia tu. Hivi majuzi, wanasayansi wamechungua upungufu wa asilimia 8 katika ukolevu wa ozoni wa wakati wa kipupwe juu ya baadhi ya maeneo yenye hali-hewa ya kadiri ya Kizio-Nusu cha Kaskazini. Tayari tani milioni 20 za CFC zimepaa kuelekea tabakastrato.

Yakikabiliwa na uchafuzi huu wa angahewa wenye kuleta msiba, mataifa ya ulimwengu yaliweka kando tofauti zayo yakachukua hatua ya kuazimia. Hatua nyinginezo za kimataifa pia zimekuwa zimetokea katika kulinda spishi zilizohatarishwa, kuhifadhi Antaktika, na kudhibiti usafirishaji wa taka zenye sumu.

Nchi nyingi zinachukua hatua za kusafisha mito yazo (salmoni sasa wamerudi Mto Thames wa Uingereza), kudhibiti uchafuzi wa hewa (umepungua asilimia kumi katika majiji ya Marekani yenye kungugu mbaya mno), kutumia vyanzo vya nishati visivyoharibu mazingira (asilimia 80 ya nyumba katika Iceland zinapashwa joto kwa nishati za asili), na kuhifadhi urithi wao wa kiasili (Kosta Rika na Namibia zimegeuza asilimia 12 hivi ya jumla ya eneo la ardhi zao kuwa mbuga za kitaifa).

Je, ishara hizi chanya zatoa ithibati ya kwamba wanadamu wanachukua kwa uzito hizo hatari? Je, ni muda mfupi tu kabla ya sayari yetu kuwa katika afya nzuri mara nyingine tena? Makala zinazofuata zitajaribu kujibu maswali hayo.

[Maelezo ya Chini]

a CFC zimetumiwa kwa mapana katika mikebe ya kunyunyiza erosoli, friji, vidhibiti-hewa, visafishio, na utengenezaji wa vihami vya povu. Ona Amkeni! la Desemba 22, 1994, “Angahewa Letu Linapoharibiwa.”

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki