Je, Hilo Pigano Linafanikiwa?
“ITUNZENI sayari hii, ndiyo tuliyo nayo tu.” Huu ulikuwa wito wenye kutazamisha wa Mwana-Mfalme Philip wa Uingereza, msimamizi wa World Wide Fund for Nature.
Maelfu ya miaka mapema, mtunga-zaburi aliandika: “Mbingu ni mbingu za BWANA, bali nchi amewapa wanadamu.” (Zaburi 115:16) Mungu ametupatia dunia kuwa maskani yetu, nasi ni lazima tuitunze. Hiyo ndiyo maana ya ikolojia.
Kihalisi neno “ikolojia” humaanisha “kujifunza kuhusu maskani.”a Ufafanuzi mmoja uliotolewa na The American Heritage Dictionary ni “kujifunza kuhusu matokeo yenye madhara ya ustaarabu wa kisasa kwenye mazingira, kwa kusudi la kuyazuia au kuyapindua kwa kuhifadhi.” Kwa ufupi, ikolojia humaanisha kuvumbua uharibifu ambao mwanadamu ametokeza na kisha kutafuta njia za kurekebisha hali. Wala hiyo si kazi rahisi.
Kweli Tatu za Ikolojia Kuhusu Maskani
Barry Commoner, mwanabiolojia, katika kitabu chake Making Peace With the Planet, adokeza sheria tatu sahili za ikolojia ambazo husaidia kueleza kwa nini dunia inaelekea sana kuathiriwa na utumizi mbaya.
Kila kitu kimeunganishwa na kila kitu kinginecho. Kama vile tu jino lililoharibika liwezavyo kuathiri mwili wetu wote, ndivyo uharibifu kwa kiingizwa fulani kiwezacho kuanzisha msururu mzima wa matatizo ya mazingira.
Kwa kielelezo, wakati wa miaka 40 iliyopita, asilimia 50 ya misitu ya Himalaya ya Nepal imekatwa ama kwa ajili ya kuni ama bidhaa za mbao. Mara miti ilipofyekwa, udongo ulio kwenye miinamo ya mlima ulimomonyolewa mara mvua za msimu zilipowasili. Bila udongo wa juu, miti yenye kuota haingeweza kutia mizizi kwa urahisi, na milima mingi ikawa jangwa. Kwa sababu ya kufyeka misitu, Nepal sasa inapoteza mamilioni ya tani za udongo wa juu kila mwaka. Na hayo matatizo hayako katika Nepal peke yake.
Katika Bangladesh mvua nzito, ambazo wakati mmoja zilifyonzwa na miti, huteremka kwa kasi bila kuzuilika kwenye milima yenye kufunuliwa kisha huelekea pwani, mahali ambapo husababisha mafuriko yenye kuleta misiba. Katika nyakati zilizopita, Bangladesh ilikuwa na mafuriko makubwa mara moja kila miaka 50; sasa ni kila miaka 4 ama chini ya hiyo.
Katika sehemu nyinginezo za ulimwengu, kufyekwa kwa misitu kumeongoza kwenye ueneaji wa jangwa na mabadiliko katika tabia ya nchi ya mahali. Misitu ni moja tu ya maliasili ambazo mwanadamu anatumia vibaya. Kwa kuwa wanaikolojia bado wajua kwa kiasi fulani mambo machache kuhusu sehemu zihusianazo za mfumo wetu mkubwa mno wa mazingira, tatizo huenda lisigunduliwe hadi madhara makubwa yawe yamefanyika tayari. Hili ni kweli katika kisa cha utupaji-taka, ambacho huonyesha ifaavyo sheria ya pili ya ikolojia.
Kila kitu lazima kiende mahali fulani. Ebu wazia vile maskani ya kawaida yangefanana ikiwa hakungekuwa na kuzoa takataka. Sayari yetu ni mfumo wa jinsi hiyo uliojifunganya—taka zetu zote lazima zitupwe mahali fulani katika maskani yetu ya kidunia. Ule uharibifu wa kadiri wa tabaka la ozoni huonyesha kwamba hata gesi zionekanazo kutodhuru, kama vile klorofluorokaboni (CFC), hazipotelei tu angani bila kutokeza madhara. CFC ni moja tu ya mamia ya dutu ziwezazo kudhuru zinazoachiliwa kwenye anga, mito, na bahari-kuu.
Ni kweli, bidhaa nyingine—ziitwazo “ziwezazo kuozeshwa”—baada ya muda fulani zaweza kuvunjwa na kufyonzwa na taratibu za kiasili, lakini nyingine haziwezi. Bichi za ulimwengu zimetapakaa mikebe ya plastiki ambayo itakuwako kwa miongo ya miaka ijayo. Zisizoonekana sana ni taka za viwanda zenye sumu, ambazo mara nyingi huzikwa mahali fulani. Ingawa hazionekani, hakuna uhakikisho kwamba sikuzote zitasahauliwa. Bado zaweza kupenyeza kwenye ugavi wa maji ulioko chini ya ardhi na kutokeza hatari za kiafya mbaya zaidi kwa mwanadamu na wanyama. “Hatujui la kufanya na kemikali zote zinazotokezwa na viwanda vya kisasa,” akakubali mwanasayansi wa Hungaria kwenye Taasisi ya Hidrolojia ya Budapest. “Hata hatuwezi kuzifuatilia.”
Takataka yenye kutisha kuliko zote ni taka za unururishi, matokezo ya vituo vya nguvu za nyukilia. Maelfu ya tani za taka za nyukilia zimewekwa katika mahali pa muda, ingawa nyingine tayari zimetupwa katika bahari-kuu. Ijapokuwa miaka mingi ya utafiti wa kisayansi, bado suluhisho halijapatikana la kuhifadhi kwa njia salama yenye kudumu, na hakuna lolote litapatikana karibuni. Hakuna ajuaye ni lini unururishi huenda ukatokeza madhara. Hatari hii ya kimazingira kwa hakika haitatoweka—hizo taka zitakuwa zenye unururishi kwa karne nyingi ama mileani zijazo, au mpaka Mungu atakapochukua hatua. (Ufunuo 11:18) Kupuuza kwa mwanadamu habari kuhusu kutupa taka ni kikumbusha pia cha sheria ya tatu ya ikolojia.
Acha mifumo ya asili ifuate mwendo wayo. Yaani, mwanadamu ahitaji kushirikiana na mifumo ya asili badala ya kujaribu kuichenga kwa kutumia jambo fulani alifikirialo kuwa afadhali zaidi. Viuavisumbufu fulani ni kielelezo kifaacho. Vilipoanza kutumiwa kwa mara ya kwanza, viliwezesha wakulima kudhibiti magugu na kihalisi kuondosha visumbufu viharibifu. Mazao mengi yalionekana kuwa uhakika. Lakini mambo yakaenda mrama. Magugu na wadudu walithibitika kuwa sugu kwa kiuavisumbufu kimoja baada ya kingine, na ikawa wazi kwamba viuavisumbufu vilisumisha wawindaji wa asili wa wadudu, wanyama wa porini, na hata mwanadamu mwenyewe. Labda umeathiriwa na usumishaji wa kiuavisumbufu. Basi wewe ni mmoja wa majeruhi angalau milioni moja ulimwenguni pote.
Hatimaye matokeo yaliyo kinyume ni uthibitisho unaokua wa kwamba viuavisumbufu huenda hata visiboreshe mazao. Katika Marekani, wadudu sasa hunyafua kiasi kikubwa zaidi cha mavuno kuliko vile walivyofanya kabla ya mageuzi makuu ya kiuavisumbufu. Vivyo hivyo, Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti wa Mpunga, yenye makao yayo katika Filipino, imepata kwamba viuavisumbufu haviboreshi tena mazao ya mpunga katika Kusini-Mashariki mwa Asia. Kwa hakika, programu fulani inayodhaminiwa na serikali ya Indonesia ambayo haitegemei sana viuavisumbufu imepata ongezeko la asilimia 15 katika utokezaji wa mchele tangu 1987 licha ya upungufu wa asilimia 65 katika utumizi wa viuavisumbufu. Hata hivyo, kila mwaka wakulima wa ulimwengu bado hutumia viuavisumbufu mno.
Zile sheria tatu za ikolojia zilizotolewa hapo juu husaidia kueleza kwa nini mambo yanaenda mrama. Maswali mengine muhimu ni, Ni uharibifu mkubwa kiasi gani ambao tayari umefanywa, na je, unaweza kurekebishwa?
Ni Uharibifu Mkubwa Kiasi Gani Ambao Umefanywa?
Ramani ya ulimwengu iliyoambatanishwa (ona kurasa 8-9.) huonyesha baadhi ya matatizo makuu ya kimazingira na mahali ambapo yamekumba sana. Kwa wazi, makao yanapotoweshwa au mambo mengine yanaposababisha utowesho wa mimea au spishi za wanyama, mwanadamu hawezi kurekebisha huo uharibifu. Uharibifu mwingine—kama vile kudhoofika kwa tabaka la ozoni—tayari umefanywa. Vipi kuhusu kudhoofika kwa mazingira kunakoendelea? Je, kuna lolote linalofanywa ili kukusimamisha au angalau katika kukupunguza?
Viwili vya vipimio vya uharibifu wa kiikolojia vilivyo muhimu zaidi ni kilimo na uvuvi. Kwa nini? Kwa sababu utokezaji wazo hutegemea mazingira mazuri na kwa sababu maisha yetu hutegemea ugavi wa chakula wenye kutegemeka.
Sekta zote mbili zinaonyesha dalili za kudhoofika. Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo limekadiria kwamba mashua za uvuvi za ulimwengu haziwezi kuvua zaidi ya tani milioni 100 za samaki bila kuhatarisha mno ugavi wa samaki. Jumla hiyo ilipitwa mnamo 1989, na kama ilivyotarajiwa, mwaka uliofuata uvuvi wa ulimwenguni pote ulishuka kwa tani milioni nne. Kupungua kwa baadhi ya vikundi-vikundi vya samaki kumekuwa kwa juu mno. Kwa kielelezo, katika kaskazini-mashariki mwa Atlantiki, uvuvi umepungua kwa asilimia 32 katika miaka 20 iliyopita. Matatizo makubwa ni kuvua mno, uchafuzi wa bahari-kuu, na kuharibiwa kwa maeneo ya kuzalishia.
Mwelekeo huu wenye kutazamisha unaonyeshwa katika utokezaji wa mazao. Wakati wa miaka ya 1960 na 1970, aina za mazao zilizoboreshwa pamoja na kilimo cha unyunyizaji na utumizi mwingi wa viuavisumbufu vya kemikali na mbolea bandia ziliongeza sana mavuno ya nafaka ulimwenguni. Sasa, viuavisumbufu na mbolea bandia zinapoteza uwezo wazo, na upungufu wa maji na uchafuzi pia huchangia mavuno madogo zaidi.
Ingawa kuna watu wapatao milioni 100 zaidi wa kulishwa kila mwaka, wakati wa mwongo wa miaka uliopita kumekuwa na upungufu katika jumla ya kiasi cha ardhi iliyolimwa. Na ardhi hii ilimikayo inapoteza urutuba wayo. Taasisi ya Worldwatch yakadiria kwamba kumomonyoka kwa udongo kumepokonya wakulima tani bilioni 500 za udongo wa juu wakati wa miaka 20 iliyopita. Jambo lisiloepukika, utokezaji wa chakula umeanza kushuka. Ripoti ya State of the World 1993 yaeleza kwamba “kule kushuka kwa asilimia 6 katika utokezaji wa nafaka wa kila mtu kati ya mwaka wa 1984 na 1992 labda [ndio] mwelekeo wa kiuchumi wenye kusumbua zaidi ulimwenguni leo.”
Kwa wazi, maisha ya mamilioni ya watu tayari yako hatarini kwa sababu ya kupuuza kwa mwanadamu mazingira.
Je, Mwanadamu Aweza Kushughulikia Hayo Matatizo?
Hata ingawa mwanadamu sasa aelewa jambo fulani kuhusu kile kinachoenda mrama, hicho si rahisi kurekebisha. Tatizo la kwanza ni kwamba fedha nyingi zingehitajiwa—angalau dola bilioni 600 kila mwaka—ili kutumia madokezo yote yaliyotolewa kwenye mkutano wa Earth Summit mnamo 1992. Kujifunga kisabuni pia kungehitajiwa—kujidhabihu kama vile kutupa kidogo zaidi na kuregesha mengi zaidi, kuhifadhi maji na nishati, kutumia usafiri wa umma badala ya usafiri wa kibinafsi, na lililo gumu zaidi kuliko yote, kufikiria kuhusu masilahi ya sayari badala ya mapendezi ya kibinafsi. John Cairns, Jr., mwenyekiti wa kamati ya Marekani ya kuregesha mifumo ya majini, aliliweka hilo tatizo katika taarifa fupi sana: “Nina mtazamo chanya kuhusu kile tuwezacho kufanya. Lakini nina mtazamo hasi kuhusu kile tutakachofanya.”
Gharama zenyewe za kufanya usafishaji kamili zinafanya nchi nyingi kuchagua kuahirisha siku ya kutozwa hesabu. Katika wakati wa matatizo ya kiuchumi, hatua za kutunza mazingira huonwa kuwa tisho kwa kazi za kuajiriwa au kipingamizi cha kiuchumi. Kusema si kazi, kazi ni kutenda. Kitabu Caring for the Earth hufafanua lile itikio kufikia sasa kuwa lafanana na “mvua ya ngurumo ikifuatwa na ukame wa kutotenda.” Lakini licha ya hali hii ya kutotenda, je, tekinolojia mpya haingeweza—ikipewa wakati—kupata ponyo lisiloumiza kwa maradhi ya sayari? Kwa wazi la.
Katika taarifa ya pamoja, U.S. National Academy of Sciences na Royal Society of London kwa wazi zilikiri hivi: “Ikiwa matabiri ya sasa ya ukuzi wa idadi ya watu yatathibitika kuwa sahihi na vigezo vya utendaji wa binadamu sayarini vyabaki bila kubadilika, sayansi na tekinolojia huenda zisiweze kuzuia ama kuzorota kwa mazingira kusikozuilika ama umaskini wenye kuendelea katika sehemu kubwa ya ulimwengu.”
Tatizo lenye kuogopesha la kukosa mahali pa kutupa taka za nyukilia ni kikumbusha cha kwamba sayansi si yenye uwezo wote. Kwa miaka 40 wanasayansi wamekuwa wakitafuta maeneo salama ya kudumu ya kuhifadhia taka zenye unururishi mwingi. Huo utafutaji unathibitika kuwa mgumu sana hivi kwamba nchi nyingine, kama vile Italia na Argentina, zimefikia mkataa kwamba hazitapata mahali kama hapo hadi kufikia mwaka wa 2040 ikiwa ni mapema mno. Ujerumani, nchi iliyo na mtazamo chanya zaidi katika nyanja hii, yatumaini kukamilisha mipango kufikia mwaka 2008.
Kwa nini taka za nyukilia ni tatizo hivyo? “Hakuna mwanasayansi ama mhandisi awezaye kutoa uhakikisho kamili kwamba taka zenye unururishi hazitavuja siku fulani kwa viwango hatari hata kutoka kwenye mabohari yaliyo bora zaidi,” aeleza mwanajiolojia Konrad Krauskopf. Lakini licha ya maonyo ya mapema kuhusu hilo tatizo la kutupa taka, serikali na viwanda vya nyukilia mbalimbali zilipiga hatua mbele bila uangalifu, zikidhania kwamba tekinolojia ya usoni ingetokeza suluhisho. Wakati huo wa usoni haukufika kamwe.
Ikiwa tekinolojia haina suluhisho la haraka kwa matatizo ya kimazingira, ni uchaguzi upi mwingine ambao umebaki? Je, hali ya uhitaji hatimaye italazimisha mataifa yafanye kazi pamoja ili kulinda sayari?
[Maelezo ya Chini]
a Kutoka kwa neno la Kigiriki oiʹkos (nyumba, maskani) na lo·giʹa (mtaala).
[Sanduku katika ukurasa wa7]
Utafutaji wa Vyanzo vya Nishati Vyenye Kujirekebisha
Wengi wetu huchukua nishati vivi hivi—mpaka wakati umeme unapokatika au kupanda kwa bei za mafuta [petroli]. Hata hivyo, utumizi wa nishati ni kimoja cha visababishi vikuu vya uchafuzi. Nishati nyingi zinazotumiwa hutokana na kuchoma kuni na fueli za visukuku, taratibu ambazo hutupa mamilioni ya tani za kaboni dioksidi kwenye angahewa na kuharibu misitu ya ulimwengu.
Nishati za nyukilia, ambazo ni uchaguzi mwingine, zinaendelea kutopendwa zaidi na zaidi kwa sababu ya hatari za aksidenti na ugumu wa kuhifadhi taka zenye unururishi. Vibadala vingine vyajulikana kuwa vyanzo vya nishati zenye kujirekebisha, kwa kuwa hutumia vyanzo vya nishati vinavyotukia kiasili ambavyo vyapatikana kila mahali. Kuna aina tano kuu.
Nishati za jua. Hizi zaweza kutumiwa kwa urahisi kwa ajili ya upashaji-joto, na katika nchi nyingine, kama Israeli, nyumba nyingi zina mabamba ya kunasa mwangaza wa jua ili kupasha maji joto. Kutumia jua ili kutokeza umeme ni vigumu zaidi, lakini seliumeme za jua za kisasa tayari zinaandaa umeme katika maeneo ya mashambani na yanakuwa nafuu zaidi kiuchumi.
Nguvu za upepo. Vipepeojembe vikubwa sasa vyatapakaa kwenye peo za macho katika sehemu kadhaa za ulimwengu zenye upepo mwingi. Umeme unaosambazwa na nishati hizi za kiupepo, kama ziitwavyo, umeendelea kuwa wenye gharama za chini na sasa wagharimu gharama za chini zaidi katika maeneo fulani kuliko ugavi wa nishati za kawaida.
Umeme unaotokezwa na maji. Tayari asilimia 20 ya umeme wa ulimwengu hutoka kwa mitambo ya umeme unaotokezwa na maji, lakini kwa kusikitisha mengi ya maeneo yenye uwezo katika nchi zilizositawi tayari yametumiwa. Mabwawa makubwa mno pia yaweza kutokeza madhara makubwa ya kimazingira. Matarajio ambayo ni bora, hasa katika nchi zinazositawi, yaonekana kuwa lile la kujenga mitambo mingi midogo ya umeme unaotokezwa na maji.
Nishati za ujoto wa ardhi. Nchi nyingine, hasa Iceland na New Zealand, zimeweza kuchovya ndani ya “mfumo wa maji-moto” ardhini. Utendaji wa kivolkeno chini ya ardhi hupasha maji joto, ambayo yaweza kutumiwa kupasha nyumba joto na kutokeza umeme. Italia, Japani, Mexico, Filipino, na Marekani pia zimesitawisha chanzo hiki cha nishati za kiasili kwa kadiri fulani.
Nguvu za Kupwa. Upwaji wa bahari-kuu unatumiwa katika nchi fulani, kama Uingereza, Ufaransa, na Urusi, ili kutokeza umeme. Hata hivyo, kuna maeneo machache ulimwenguni pote ambayo yangeweza kuwa rahisi na yenye kutumika kuandaa ugavi huu wa nishati kwa gharama za chini.
[Sanduku/Pichakatika ukurasa wa 8, 9]
Baadhi ya Matatizo Makuu ya Kimazingira ya Ulimwenguni
Kuharibiwa kwa misitu. Robo tatu za misitu ya eneo la halihewa ya kadiri na nusu ya misitu ya kitropiki ya ulimwengu tayari imepotezwa, na kiwango cha ufyekaji wa misitu kimeongezeka kwa kutazamisha wakati wa mwongo wa miaka uliopita. Makadirio ya hivi karibuni huonyesha kuharibiwa kwa misitu ya kitropiki kuwa kati ya kilometa za mraba 150,000 na 200,000 kila mwaka, karibu ukubwa wa Uruguai.
Taka zenye sumu. Nusu ya kemikali 70,000 zinazotengenezwa kwa sasa zaainishwa kuwa zenye sumu. Marekani peke yake hutokeza tani milioni 240 za taka zenye sumu kila mwaka. Ukosefu wa habari hufanya isiwezekane kuhesabu jumla ya ulimwenguni pote. Kwa kuongezea, kufikia mwaka 2000, kutakuwa na tani zipatazo 200,000 za taka zenye unururishi zilizohifadhiwa katika maeneo ya muda.
Kudhoofika kwa ardhi. Thuluthi moja ya eneo la uso wa ulimwengu inatishwa na kuenea kwa jangwa. Katika sehemu fulani za Afrika, Jangwa la Sahara limeenea kilometa 350 kwa miaka 20 tu. Tayari riziki ya mamilioni ya watu yatishwa.
Uhaba wa maji. Karibu watu bilioni mbili huishi katika maeneo ambapo kuna upungufu mkubwa sana wa maji. Jambo lenye kuzidisha huo upungufu ni kunyauka kwa maelfu ya visima vya kuchimbwa kwa sababu ya kushuka kwa viwango vya mawe yanayotokeza maji ambayo hivyo hutegemea.
Spishi zilizo katika hatari ya kutoweshwa. Ingawa takwimu zaweza kubishaniwa kwa kiasi, wanasayansi wakadiria kwamba kati ya spishi 500,000 na 1,000,000 za wanyama, mimea, na wadudu zitakuwa zimetoweshwa kufikia mwaka 2000.
Uchafuzi wa kiangahewa. Uchunguzi fulani wa UM katika miaka ya mapema ya 1980 ulipata kwamba watu bilioni moja huishi katika maeneo ya mji ambayo kila siku hupatwa na viwango vyenye kuhatarisha afya vya masizi au gesi zenye sumu, kama salfa dioksidi, nitrojeni dioksidi, na kaboni dioksidi. Ukuzi wa haraka wa majiji katika mwongo wa miaka uliopita kwa wazi umelizidisha tatizo hili. Isitoshe, tani bilioni 24 za kaboni monoksidi hutupwa kwenye angahewa kila mwaka, na inahofiwa kwamba “ongezeko [hili] la joto” huenda likatokeza kuzidi kwa joto tufeni.
[Ramani]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
Kufyeka misitu
Taka zenye sumu
Uchafuzi wa Kiangahewa
Uhaba wa maji
Spishi zilizohatarishwa
Kudhoofika kwa ardhi
[Hisani]
Mountain High Maps™ copyright© 1993 Digital Wisdom, Inc.
Picha: Hutchings, Godo-Foto
Picha: Mora, Godo-Foto