Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g95 11/22 kur. 4-7
  • Mataifa Maskini Yawa Mahali pa Mataifa Tajiri pa Kutupia Takataka

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Mataifa Maskini Yawa Mahali pa Mataifa Tajiri pa Kutupia Takataka
  • Amkeni!—1995
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Kuregesha Ambako Ni Hatari
  • Si Visumbufu Peke Yavyo Vinavyokufa
  • Kurudi Nyuma Kiunafiki
  • Siku ya Kutozwa Hesabu ya Wenye Pupa
  • Je, Hilo Pigano Linafanikiwa?
    Amkeni!—1996
  • Kemikali Chungu Nzima Zilizotengenezwa na Watu
    Amkeni!—1998
  • Tumefanikiwa Kadiri Gani Kuokoa Mazingira Yetu?
    Amkeni!—2003
  • Kwa Nini Tutunze Mazingira?
    Amkeni!—2007
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1995
g95 11/22 kur. 4-7

Mataifa Maskini Yawa Mahali pa Mataifa Tajiri pa Kutupia Takataka

KAMA yatima asiyehitajiwa, shehena lenye sumu lilikuwa limetanga-tanga kutoka meli hadi meli na bandari hadi bandari likitafuta mahali pa kulitupa. Mapipa 11,000 yakiwa yamejaa resini zenye sumu, viuavisumbufu, na kemikali nyinginezo hatari yalisafirishwa kutoka Jibuti, Afrika, hadi Venezuela hadi Siria hadi Ugiriki. Hatimaye mapipa yenye kuvuja yalianza kumdhuru mmoja wa wanameli wenye kuyasafirisha. Mtu mmoja alikufa, na wengi wa wale wengine walishikwa na ugonjwa wa ngozi, figo, na wa kupumua kutokana na kemikali zenye sumu kutoka kwa hayo mapipa melini.

Meli, malori, magari-moshi zikiwa zimeshehenezwa taka zenye kufisha kama hizo hupitana-pitana sayarini zikitafuta mahali pa kuzitupa. Mara nyingi sana nchi ambazo tayari zinatafunwa na umaskini, njaa kuu, na maradhi huwa jaa la tani nyingi za takataka zenye sumu na zilizo chafu. Wanamazingira wahofia kutokea kwa msiba wa kimazingira hivi karibuni.

Rangi kuu-kuu, vimumunyishaji, magurudumu, betri, taka zenye unururishi, na masao yaliyojaa risasi na kemikali za aina ya PCB, huenda zisikuvutie wewe, lakini zavutia biashara yenye kuvuma ya taka za kiviwanda. Kwa kinyume, kadiri serikali inavyochukua msimamo mkali kimazingira, ndivyo viwanda vyayo hutupa taka nyingi mno zenye sumu katika nchi za ng’ambo. “Karibu tani milioni 20 za kemikali zenye sumu husafirishwa kila mwaka ili kutupwa katika Nchi Zinazositawi na [kampuni] laghai” za mataifa yenye viwanda vingi, likataarifu gazeti The Observer la kila juma la London. Vipenyo vya kuepea vya kisheria na ufikilizaji usio thabiti humaanisha kwamba maelfu ya tani za taka zenye sumu humwagwa katika nchi za Kiafrika, Kiasia, na Amerika ya Kilatini.

Si ajabu basi kwamba makampuni haya hushawishika kumwaga taka huko! Ile gharama yaweza kupunguzwa sana ikiwa mahali pafaapo patumiwa. Kielelezo cha hili ni meli United States, ambayo wakati mmoja ilikuwa meli yenye fahari ya Marekani. Ilinunuliwa katika 1992 ili kurekebishwa upya kwa ajili ya uvinjari wa kitalii. Yaelekea ilikuwa na asbesto nyingi mno kuliko meli nyingineyo iliyoelea baharini. Kubambuliwa kwa asbesto kungegharimu dola milioni 100 katika Marekani. Hiyo meli ilisafirishwa hadi Uturuki, ambako ingeweza kubambuliwa kwa dola milioni 2. Lakini serikali ya Uturuki ilikataa—ilikuwa hatari mno kuruhusu nyuzi za asbesto zenye kuenea zaidi ya meta 46,000 mraba zisababishazo kansa kubambuliwa nchini mwao. Hiyo meli hatimaye iligugurushwa kwenye bandari ya nchi nyingine, mahali ambapo kanuni za kimazingira si kali mno.

Kuregesha Ambako Ni Hatari

Biashara za magharibi katika mabara yanayositawi huenda zikajifikiria kuwa wafadhili wa mataifa maskini. Harvey Alter wa Kikoa cha Biashara cha Marekani adai kwamba “biashara ya kupeleka taka nchi za nje na kuregesha huinua viwango vya kuishi katika nchi hizi.” Lakini pitio la baadhi ya tabia za makampuni yaliyo ng’ambo lilipata kwamba katika visa vilivyo vingi, badala ya kuinua viwango vya kuishi, makampuni haya “yaelekea hayalipi zaidi ya mishahara ya chini ya huko, yakichafua mazingira na kuuza bidhaa ambazo katika visa vingine ni hatari na zauzwa kwa ulaghai.”

Papa John Paul 2 alionyesha hangaiko lake katika warsha ya hivi majuzi juu ya uchafuzi katika nchi zinazositawi. Papa alisema hivi: “Ni makosa makubwa sana mataifa tajiri yanapojifaidi kutokana na uchumi na katiba dhaifu za nchi zilizo maskini kwa kuzipelekea tekinolojia zenye kuchafua na taka ambazo huharibu mazingira na afya ya watu.”

Kielelezo halisi chapatikana kusini mwa Afrika, makao ya kiwanda cha kuregesha taka za hidrajiri kilicho kikubwa kupita vyote ulimwenguni. Katika ile iliyoitwa “moja ya kashfa za uchafuzi wa kontinenti iliyo mbaya kupita zote,” hizo taka zenye sumu ziliua mfanyakazi mmoja, mwingine alipoteza fahamu kwa muda, na thuluthi moja ya wafanyakazi wanaugua kutokana na sumu ya aina fulani ya hidrajiri. Serikali mbalimbali katika mataifa fulani yenye viwanda hukataza ama huweka sheria kali dhidi ya kutupa taka fulani za hidrajiri. Meli za mashirika katika angalau mojapo ya nchi hizi husafirisha shehena hatari kwenye fuo za Afrika. Kikoa fulani cha wakaguzi kilipata mapipa 10,000 ya taka za hidrajiri kutoka makampuni matatu ya kigeni yakiwa yamewekwa kwenye hicho kiwanda.

Kupelekea mataifa yanayositawi taka ili kuziregesha kwaonekana kuwa afadhali zaidi kuliko kuyamwagia taka. Kwaweza kutokeza bidhaa nzuri, kuandaa kazi, na kuchochea uchumi. Lakini kama ripoti iliyopo juu kutoka kusini mwa Afrika inavyoonyesha matokeo yenye msiba pia yaweza kutokea. Kupata upya bidhaa zenye thamani kutokana na dutu hizi kwaweza kutoa kemikali hatari ambazo husababisha uchafuzi na ugonjwa na hata nyakati nyingine kifo kwa wafanyakazi. Gazeti la New Scientist laonelea hivi: “Hakuna shaka kwamba kuregesha nyakati nyingine hutumiwa kama kisingizio cha kutupa takataka.”

Mbinu hiyo yafafanuliwa na U.S.News & World Report hivi: “Kuweka vibandiko bandia, vipenyo vya kisheria vya kuepea na ukosefu wa ustadi huyafanya mataifa yanayositawi kuwa shabaha rahisi kwa wafanyabiashara wa taka wajanja ambao huchuuza uchafu wenye sumu kwa jina ‘mbolea ya kikaboni’ ama viuavisumbufu vilivyopita muda wa kutumia kuwa ‘msaada wa kilimo.’”

Maquiladoras, ama viwanda vinavyomilikiwa na wageni, vimevuvumka katika Mexico. Kusudi la msingi la makampuni ya kigeni ni kuepa sheria kali za uchafuzi na kupata faida ya wafanyakazi wengi wa malipo ya chini. Makumi ya maelfu ya Wamexico huishi katika vibanda vizungukwavyo na mitaro yenye maji meusi kwa uchafu. “Hata mbuzi hawayanywi,” akasema mwanamke mmoja. Ripoti fulani ya Shirika la Kitiba la Marekani iliita eneo la mpakani “mtaro mchafu na mahali pazuri pa kuenezea maradhi yenye kuambukiza.”

Si Visumbufu Peke Yavyo Vinavyokufa

“Nchi yaweza kukatazaje sumu fulani nyumbani na bado kuitengeneza na kuiuzia nchi nyingine? Umaadili wa jambo hili u wapi?” akauliza Arif Jamal, mtaalamu wa kilimo na visumbufu kutoka Khartoum. Yeye alionyesha picha za mapipa yaliyokuwa na alama: “Hazipaswi kutumiwa”—yaliyotoka katika nchi yenye viwanda. Yalipatikana katika hifadhi ya wanyama wa pori ya Sudan. Karibu-karibu kulikuwa na marundo ya wanyama waliokufa.

Nchi moja tajiri “kila mwaka hupeleka katika nchi za nje kilo zipatazo milioni 227 za viuavisumbufu vilivyopigwa marufuku, vilivyowekewa masharti ama visivyofaa kwa matumizi ya nyumbani,” laripoti The New York Times. Heptaklori aina fulani ya DDT, isababishayo kansa ilipigwa marufuku kutumiwa kwenye mimea ya kula katika 1978. Lakini kampuni ya kemikali iliyoibuni yaendelea kuitengeneza.

Uchunguzi wa UM ulivumbua ugavi mwingi wa “viuavisumbufu vyenye sumu sana” katika mataifa yanayositawi yapatayo 85. Karibu watu milioni moja husumishwa vibaya kila mwaka, na labda 20,000 hufa kutokana na kemikali.

Biashara ya tumbaku huenda iitwe upeo wa pupa hatari. Makala fulani katika Scientific American yenye kichwa “Kipuku cha Tumbaku Tufeni” yataarifu hivi: “Kiasi cha maradhi yanayohusiana na tumbaku na vifo ulimwenguni ni kikubwa mno.” Umri wa wastani wa mvutaji sigareti anayeanza waendelea kupungua mno, na idadi ya wanawake wavutaji sigareti yaongezeka haraka mno. Makampuni ya tumbaku yenye nguvu kwa kuungana na watangazaji wenye hila yanafanikiwa kushinda soko kubwa la nchi ambazo hazijasitawi sana. Maiti na miili yenye maradhi yatapakaa katika barabara yao kuelekea utajirini.a

Hata hivyo, ni lazima isemwe kwamba si makampuni yote ambayo hayajali hali-njema ya mataifa yanayositawi. Kuna makampuni mengine ambayo hujitahidi kuendeleza biashara ifaayo na yenye kuaminika katika nchi zinazositawi. Mathalani, kampuni moja huandaa marupurupu ya kustaafu na ya afya na hulipa wafanyakazi wayo mara tatu ya mshahara utakikanao. Kampuni nyingine imechukua msimamo thabiti juu ya haki za binadamu nayo imevunjilia mbali mikataba mingi kwa sababu ya kupuuzwa kwa haki za binadamu.

Kurudi Nyuma Kiunafiki

Katika 1989 mwafaka wa mkutano wa UM ulitiwa sahihi katika Basel, Uswisi, ili kusimamia usafirishaji wa taka hatari miongoni mwa mataifa. Huo ulishindwa kusuluhisha hilo tatizo, nalo New Scientist likaripoti hivi kwenye mkutano wa baadaye wa mataifa hayohayo, uliofanywa katika Machi 1994:

“Katika kuitikia hasira yenye kueleweka ya mataifa yenye kusitawi, nchi 65 zilizoshiriki katika Mkutano wa Basel zilipiga hatua kubwa mbele zilipoamua kuongeza mambo mengine katika mkutano huo kwa kupiga marufuku kupeleka taka hatari nje ya nchi za OECD [Shirika la Muungano wa Kiuchumi na Usitawi] hadi nchi ambazo si wanachama wa OECD.”

Lakini uamuzi huu wa baadaye zaidi ulionekana usiopendelewa na nchi zilizositawi. New Scientist lilitoa hangaiko layo hivi: “Hivyo, habari ya kwamba Marekani, Uingereza, Ujerumani na Australia sasa zinajaribu kuharibu huo uamuzi inahangaisha. Hati fulani kutoka serikali ya Marekani zilisaliti juhudi ‘za ukimya’ zayo za kiungwana za ‘kurekebisha’ hayo marufuku kabla ya kuukubali huo mkutano.”

Siku ya Kutozwa Hesabu ya Wenye Pupa

“Sasa, nyinyi wanaume wenye vingi, ni wakati wenu wa kulia na kupiga mayowe kwa sababu ya misiba inayowangojea!” yaonya Biblia kwenye Yakobo 5:1. (The New Testament in Modern English, ya J. B. Phillips) Kutozwa hesabu kutakuja mkononi mwa mmoja anayeweza kunyoosha mambo: “BWANA ndiye afanyaye mambo ya haki, na hukumu kwa wote wanaoonewa.”—Zaburi 103:6.

Wale wanaoishi sasa katika umaskini wenye uonevu wanaweza kupata faraja, kwa kujua kwamba karibuni maneno ya Zaburi 72:12, 13 yatatimizwa: “Kwa maana atamkomboa mhitaji aliapo, na mtu aliyeonewa iwapo hana msaidizi. Atamhurumia aliye dhaifu na maskini, na nafsi za wahitaji ataziokoa.”

[Maelezo ya Chini]

a Ona Amkeni! la Mei 22, 1995, “Kuua Mamilioni ili Kufanya Mamilioni.”

[Sanduku katika ukurasa wa 6]

Takataka Hatari Ambazo Zakataa Kutoweka

“Taka za Nyukilia Hatari Zajazana Bila Suluhisho la Hivi Karibuni.” Ndivyo kilivyosema kichwa kikuu katika safu ya sayansi ya The New York Times Machi uliopita. “Jambo sahili,” hiyo makala ikasema, “ni kuzizika. Lakini sasa hilo linashutumiwa huku wanasayansi wakijadiliana, na mashirika ya Kiserikali yakichunguza, ikiwa jaa la chini lililopendekezwa katika Nevada huenda hatimaye lilipuke katika mlipuko wa nyukilia uliochochewa na taka za plutonimu.”

Wanasayansi wamependekeza mipango mingi ya kuweza kuondolea ulimwengu plutonimu ya ziada, lakini gharama, mabishano, na hofu zimefanya hiyo miradi kutupiliwa mbali. Wazo moja ambalo ni lenye kuudhi wengi ni kuzizika baharini. Wazo jingine liwazikalo ni kuzilipulia juani. Suluhisho jingine, ni kutumia vitendanishio ili kuzichoma. Lakini hayo yalitupiliwa mbali, kwani kutimiza hilo ‘kungechukua mamia ama maelfu ya miaka.’

Dakt. Makhijani wa Taasisi ya Utafiti wa Nishati na Mazingira alisema hivi: “Kila suluhisho ambalo ni zuri kiufundi lina sehemu za kisiasa ambazo hazifai, na kila suluhisho zuri kisiasa huelekea kuwa lisilofaa kiufundi. Hakuna yeyote mwenye masuluhisho ya ujumla yaliyo mazuri kwa tashwishi hii, kutia ndani sisi.”

Ili kuandaa umeme kwa nyumba milioni 60—asilimia 20 ya nguvu za nchi—vitendanishio 107 katika kiwanda cha nguvu za nyukilia katika Marekani hutokeza tani 2,000 za fueli iliyotumika kila mwaka, na tangu 1957 ile fueli iliyotumika imehifadhiwa kwa muda kwenye viwanda vyao vya nyukilia. Kwa miongo watu wamengojea bila kufaulu ili serikali itafute njia ya kuitupa. Marais 9 wamekuwa katika utawala, na Bunge 18 zimetoa mipango na kuweka siku ya mwisho ya uwekaji salama wa taka zenye unururishi katika majengo ya chini ya ardhi, lakini utupaji wa mwisho wa taka zenye kufisha ambazo lazima zilindwe kwa maelfu ya miaka bado wangoja suluhisho.

Kwa kinyume, trilioni za tanuru za mfanyikotendani ambazo Yehova Mungu huendeleza katika nyota za mbali za ulimwengu wote mzima hazitishi, na moja anayoiendeleza katika jua letu huwezesha kuwako kwa uhai duniani.

[Hisani]

UNITED NATIONS/IAEA

[Picha katika ukurasa wa 7]

Kemikali zenye sumu huchafua maji ya kunywa na kuosha

[Picha katika ukurasa wa 7]

Watoto wacheza katikati ya taka hatari ama zenye kufisha

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki