Dunia—Zawadi ya Mungu Kwetu
“HAPO mwanzo Mungu aliziumba mbingu na nchi.” Pia alitangaza dunia kuwa ‘njema sana.’ (Mwanzo 1:1, 31) Hakukuwa na marundo ya takataka yaliyoiharibu; hakuna uchafu ulioichafua. Zawadi maridadi ilikabidhiwa wanadamu: “Mbingu ni mbingu za BWANA, bali nchi amewapa wanadamu.”—Zaburi 115:16.
Kwenye Isaya 45:18, yeye aeleza kusudi lake kwa dunia: “Maana BWANA, aliyeziumba mbingu, asema hivi; Yeye ni Mungu; ndiye aliyeiumba dunia na kuifanya; ndiye aliyeifanya imara; hakuiumba ukiwa, aliiumba ili ikaliwe na watu; Mimi ni BWANA, wala hapana mwingine.”
Yeye aonyesha kihususa ni nini daraka la mwanadamu kuelekea dunia—“ailime na kuitunza.”—Mwanzo 2:15.
Yehova aweka kielelezo. Yeye hutunza dunia. Njia moja ni kwa kufanyiza upya maandalizi muhimu ya dunia, mambo ambayo uhai wote duniani hutegemea. Toleo maalumu la Scientific American lilikuwa na makala kuhusu baadhi ya mizunguko, ambayo ilitia ndani mzunguko wa nishati za dunia, mzunguko wa nishati za viumbe-hai, mzunguko wa maji, mzunguko wa oksijeni, mzunguko wa kaboni, mzunguko wa nitrojeni, na mzunguko wa madini.
Dunia—Yastaajabisha na Maridadi Pia
Mwanabiolojia maarufu sana Lewis Thomas, katika gazeti la sayansi Discover, aliandika sifa hii iliyo kamili juu ya dunia:
“Staajabu isiyo na kifani, muundo usiolinganika tuujuao kufikia sasa katika ulimwengu wote mzima, fumbo la sayansi la kianga lililo kubwa kupita yote, yenye kutamausha jitihada zetu zote ili kuifahamu, ni dunia. Ndipo tunapoanza tu kufahamu jinsi ilivyo ya ajabu na yenye kupendeza, jinsi inavyosisimua, kitu chenye kupendeza mno kieleacho kuzunguka jua, kikijifunga katika angahewa lacho la samawati, kikijitengenezea na kupumua oksijeni, kikijitengenezea nitrojeni kutoka kwa hewa hadi kwenye udongo wacho, kikijifanyizia halihewa kutokana na misitu ya mvua, kikijitengenezea kinga kutokana na vitu vilivyo hai: magenge ya chokaa, matumbawe, visukuku vitokanavyo na aina ya uhai wa kale uliofunikwa na tabaka za uhai wa hivi karibuni zikiwa zimeingiliana kuzunguka tufe.”
Haya ni machache tu ya maandalizi ambayo Yehova ameyaweka ili kuendeleza dunia ikiwa zawadi maridadi kwa wanadamu, makao yaliyoumbwa yadumu milele kwa ajili ya watu na mamilioni yasiyohesabika ya viumbe-hai vingine. Zaburi 104:5 husema hivi: “Uliiweka nchi juu ya misingi yake, isitikisike milele.” Shahidi mwingine aliyepuliziwa alishuhudia hivi udumifu huuhuu wa dunia: “Kizazi huenda, kizazi huja; nayo dunia hudumu daima.”—Mhubiri 1:4.
Wanaanga wanaozunguka dunia wamesema kwa uvutio kuhusu duara hii maridadi na dhaifu ikiabiri katika mzunguko wayo kuzunguka jua na wameeleza umuhimu wa jamii ya kibinadamu kuthamini urembo wayo na kuitunza. Mwanaanga Edgar Mitchell, mara ya kwanza alipoiona dunia kutoka angani, aliwasilisha habari hii kwenye kituo cha Houston: “Yaonekana kama kito cheupe na samawati yenye kumetameta . . . chenye kuzungukwa na visetiri vyeupe vyenye kuvurura polepole . . . , kama lulu ndogo katika bahari nyeusi tititi ya kifumbo.” Maelezo ya mwanaanga Frank Borman yalikuwa haya: “Sisi twashiriki sayari maridadi sana. . . . Staajabu kubwa ndiyo sababu ulimwenguni hatuwezi kuthamini kile tulicho nacho.” Mmoja wa wanaanga wa mruko wa mwezini wa Apollo 8 alisema hivi: “Katika ulimwengu wote mzima, popote tulipotazama, mahali palipokuwa na rangi tu palikuwa kwenye dunia. Huko tungeweza kuona samawati maridadi ya bahari, ukahawia mbalimbali wa bara, na weupe-weupe wa mawingu. . . . Kilikuwa kitu kilicho maridadi zaidi cha kuona, katika mbingu zote. Watu chini hapa hawang’amui kile walicho nacho.”
Uhakika waonyesha kwamba taarifa hiyo kuwa kweli—watu hawang’amui hazina waliyo nayo. Badala ya kutunza zawadi hii kutoka kwa Mungu, jamii ya kibinadamu inaichafua na kuiharibu. Wanaanga pia wameona hili. Paul Weitz, mwelekezi wa mruko wa kwanza wa angani wa chombo Challenger, alisema kwamba uharibifu ambao mwanadamu ameufanya katika angahewa la dunia ni “mbaya sana” unapotazamwa kutoka angani. “Kwa kusikitisha, ulimwengu huu haraka waja kuwa sayari isiyofaa.” Aongezea zaidi hivi: “Ni ujumbe upi unatolewa kwetu? Tunachafua kiota chetu wenyewe.” Na uharibifu huu umezidi katika hizi “siku za mwisho” zilizo hatari sana. Yehova ametangaza hukumu yake dhidi ya wale wanaoharibu dunia, yaani, kwamba yeye ‘atawaharibu hao waiharibuo dunia.’—Ufunuo 11:18.
Jamii Isiyo na Shukrani Isiyostahili Zawadi ya Mungu
Jamii yenye kufuatilia vitu vya kimwili imetupilia mbali kanuni za kiroho kwa kushindwa kabisa na tamaa za kimwili. Miongozo yenye kutumika ambayo Yehova aliwapa wanadamu kwa ajili ya maisha yenye furaha na yenye kuridhisha imesukumwa kando na usitawi wa roho ya mimi kwanza ambayo hudhihirisha nyakati zetu.
Timotheo wa Pili 3:1-5 lafafanua hivi kikamilifu nyakati zenye hatari tunazoishi: “Lakini ufahamu neno hili, ya kuwa siku za mwisho kutakuwako nyakati za hatari. Maana watu watakuwa wenye kujipenda wenyewe, wenye kupenda fedha, wenye kujisifu, wenye kiburi, wenye kutukana, wasiotii wazazi wao, wasio na shukrani, wasio safi, wasiowapenda wa kwao, wasiotaka kufanya suluhu, wasingiziaji, wasiojizuia, wakali, wasiopenda mema, wasaliti, wakaidi, wenye kujivuna, wapendao anasa kuliko kumpenda Mungu; wenye mfano wa utauwa, lakini wakikana nguvu zake; hao nao ujiepushe nao.”
Roho ya biashara huchochea ununuaji, na utangazaji ndio kibaraka chayo. Utangazaji mwingi wa kibiashara wafaa; mwingi wao ukiwa haufai. Jambo hili la pili lafaana na ono la Eric Clark katika The Want Makers: “Si kwamba tu utangazaji husaidia kuuza vitu visivyofaa kwa watu ambao hawawezi kuzigharimia, bali hufanya hivyo kwa bei ambazo ni za juu kupita kiasi.” Asema Alan Durning wa World Watch: “Watangazaji wa kibiashara hawauzi bidhaa halisi bali mitindo-maisha, fashoni, na fantasia, wakiunganisha bidhaa zao na ile tamaa ya daima ya kindani.” Utangazaji wa kibiashara hunuia kutufanya tusiridhike na kile tulicho nacho na tutamani kile ambacho hatuhitaji. Hutokeza tamaa isiyoridhishwa; huongoza kwenye mdhoofiko utokanao na utumizi wenye kupita kiasi wa bidhaa; hutokeza usambaaji wa majaa ya taka ambayo huchafua dunia. Ushawishi wao wa kiujanja hupenyeza hata ndani ya mioyo dhaifu ya wale wanaoishi katika umaskini hohehahe. Watangazaji wengi wa kibiashra huuza kwa bidii bidhaa ambazo zajulikana kuwa huua ama hufanya watu wawe wagonjwa.
Jambo muhimu ni msimamo wetu pamoja na Mungu, kama vile Mhubiri 12:13 husema: “Hii ndiyo jumla ya maneno; yote yamekwisha sikiwa; Mche Mungu, nawe uzishike amri zake, maana kwa jumla ndiyo impasayo mtu.” Wale wanaofanya hivyo watastahili kuishi katika Paradiso ya Yehova iliyo safi! Yesu aliahidi: “Msistaajabie maneno hayo; kwa maana saa yaja, ambayo watu wote waliomo makaburini wataisikia sauti yake. Nao watatoka; wale waliofanya mema kwa ufufuo wa uzima, na wale waliotenda mabaya kwa ufufuo wa hukumu.”—Yohana 5:28, 29.
Wakati Zawadi ya Mungu Itakapothaminiwa
Hiyo itakuwa dunia ya ajabu kama nini! Yehova ametupa ufafanuzi huu wenye kutwesha pumzi: “[Mimi Yohana] nikaona mbingu mpya na nchi mpya; kwa maana mbingu za kwanza na nchi ya kwanza zimekwisha kupita, wala hapana bahari tena. Naye [Mungu] atafuta kila chozi katika macho yao, wala mauti haitakuwapo tena; wala maombolezo, wala kilio, wala maumivu hayatakuwapo tena, kwa kuwa mambo ya kwanza yamekwisha kupita.”—Ufunuo 21:1, 4.
Vitu vya kale vitakuwa vimetoweka pia kama vile majaa ya takataka, taka zenye sumu, na wale ambao husukumia wengine takataka zao. Kisha watu walio hai peke yao duniani watakuwa wale ambao wanawapenda majirani wao kama wao wenyewe, wanaomsifu Yehova kwa zawadi yake ya dunia, na wanaofurahia kuitunza na kuiweka katika hali ya kiparadiso.—Mathayo 22:37, 38; 2 Petro 3:13.
[Sanduku katika ukurasa wa 11]
Ubatili wa Ufuataji wa Vitu vya Kimwili
Yesu alisema ukweli mtupu wakati alipoonya hivi: “Angalieni, jilindeni na choyo, maana uzima wa mtu haumo katika wingi wa vitu vyake alivyo navyo.” (Luka 12:15) Jambo la maana si kile tulicho nacho: bali ni vile tulivyo. Ni rahisi sana kujihusisha na shamrashamra na msisimuko wa maisha—kuchuma pesa, kurundika mali, kuparamia anasa zote ambazo mwili unatamani—na kufikiri kwamba tunaishi maisha kwa utimilifu, bila kukosa chochote, wakati ambapo huenda tunakosa yaliyo bora ambayo maisha hutoa.
Ni kadiri maisha yanavyopita ndivyo tunavyong’amua kile tulichopoteza. Tunang’amua ukweli wa yale ambayo Biblia husema: Maisha ni mafupi mno—ukungu utokomeao, moshi, pumzi, kivuli kipitacho, nyasi ya kijani kibichi ambayo hunywea, ua ambalo hunyauka. Yameenda wapi? Tumefanya nini? Kwa nini tulikuwa hapa? Je, maisha ni hayahaya tu? Je, ni ubatili wa ubatili, na kukimbizana na upepo?—Ayubu 14:2; Zaburi 102:3, 11; 103:15, 16; 144:4; Isaya 40:7; Yakobo 4:14.
Mtu aliye hospitalini, anayekufa, akitazama nje, na kuona upande wa vilima ukiwa umeangazwa na mwanga wa jua wenye ujoto, mchanganyiko wa nyasi na magugu, viua vichache vyenye kunawiri, shomoro linayechakura udongo ili kupata nafaka chache—ni mandhari ambayo huenda isisisimue mno. Lakini kwa mtu anayekufa, ni maridadi. Tamaa yenye kusikitisha moyo humkumba, kufikiria shangwe sahili zilizoje alizozikosa, mambo madogo ambayo humaanisha mengi. Kwa muda mfupi sana yameenda!
Maandiko ya Kigiriki ya Biblia huitaja waziwazi hivi: “Kwa maana hatukuja na kitu duniani, tena hatuwezi kutoka na kitu; ila tukiwa na chakula na nguo tutaridhika na vitu hivyo.” (1 Timotheo 6:7, 8) Maandiko ya Kiebrania huitaja wazi zaidi hivi: “Alivyotoka tumboni mwa mamaye, atakwenda tena tupu-tupu kama alivyokuja; asichume kitu cho chote kwa ajili ya kazi yake, hata akichukue mkononi mwake.”—Mhubiri 5:15.
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 8]
Picha ya NASA