Wengi Sana Huishi na Kufa Katika Umaskini Wenye Kuumiza Sana!
YATI aondoka mtaa wake mchafu katika nchi fulani iliyo kusini-mashariki mwa Asia akielekea kiwandani ambako yeye hushona vipande vya ngozi na kamba za viatu. Kwa kazi ya mwezi mmoja—majuma ya muda wa saa 40 kuongezea kazi ya ziada ya muda wa saa 90—hupata mapato yapunguayo dola 80. Kampuni ya viatu ambayo imemwajiri hujishaua kuwa mwendelezaji mwenye kudhamiria wa haki za binadamu katika mabara ambayo hayajasitawi sana. Katika ulimwengu wa Magharibi, kampuni hii huuza hivyo viatu kwa zaidi ya dola 60 kwa jozi. Labda mishahara hujumlika kuwa dola 1.40 ya hizo.
Yati ‘anapokiacha kiwanda safi, chenye mwangaza wa umeme,’ yasema ripoti ya Boston Globe, “ana fedha za kutosha tu kukodisha kibanda cha meta 3 kwa 3.6, chenye kuta chafu zilizojaa mijusi. Hakina fanicha, hivyo Yati pamoja na wanachumba wawili hulala katika hali ya kujikunja kwenye sakafu ya matope na vigae.” Kwa kusikitisha hali yake ni ya kawaida.
“Je, watu hawa wako afadhali kimaisha wakiwa na mimi ama bila mimi?” ateta mkuu mmoja wa shirika la biashara. “Huo mshahara mdogo huwapa uwezo wa kufurahia maisha mastahifu. Huenda wakawa hawaishi katika maisha ya anasa, lakini hawalali njaa.” Hata hivyo, mara nyingi wana utapiamlo, na watoto wao mara nyingi hulala njaa. Wao hukabili hatari za kila siku katika mahali pa kazi hatari. Na wengi wanakufa kifo cha polepole kwa kushughulika na taka zenye sumu. Je, hayo yaweza kuitwa “maisha mastahifu”?
Hari, mfanyakazi wa shamba kusini mwa Asia, aliona mambo kwa njia tofauti. Alieleza hali kwa maneno na ufasaha wa kishairi ule mzunguko wa uhai na kifo wenye kutamausha uliomzunguka. “Katikati ya kinu na mchi,” yeye akasema, “pilipili haiwezi kudumu. Sisi maskini ni kama pilipili—kila mwaka sisi hutwangwa, na hivi karibuni hakuna chochote ambacho kitakuwa kimebaki.” Hari hakuyaona kamwe “maisha mastahifu” hayo, wala hakupata mwonjo wowote wa maisha ya anasa ambayo waajiri wake yaelekea waliyaishi. Siku chache baadaye, Hari alikuwa amekufa—jeruhi jingine la umaskini hohehahe.
Halaiki huishi na kufa kama Hari. Wao hunywea katika taabu, wakiwa dhaifu sana kukinza, kwani nishati zao huwa zimekamuliwa. Na akina nani? Ni watu wa aina gani wangefanya hili? Wao huonekana kuwa wafadhili wazuri. Wao husema wanataka kulisha kitoto chako, kusaidia mimea yako ikue, kuboresha maisha yako, kukufanya tajiri. Kwa uhalisi, wanuia kujitajirisha. Kuna fursa za kuuza, faida za kuchumwa. Ikiwa matokeo ya pupa yao ni watoto wenye utapiamlo, wafanyakazi wenye kusumishwa, na mazingira yaliyochafuliwa, haidhuru. Ni gharama ambayo makampuni yako tayari kulipia kwa ajili ya pupa yao. Kwa hiyo kadiri faida zinavyozidi, ndivyo na idadi zenye kushtua za majeruhi.
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 3]
Picha ya U.N. 156200/John Isaac