Kemikali Chungu Nzima Zilizotengenezwa na Watu
KARNE hii ingeweza kuitwa kwa kufaa karne ya kizazi cha kemia. Kemikali zilizotengenezwa na watu zimebadili maisha yetu. Nyumba zetu, ofisi zetu na viwanda vimejaa vipulizaji, vikolezo bandia, vipodozi, rangi za nguo, wino, rangi, dawa za kuua wadudu, dawa, plastiki, vituliza-joto, vitambaa sanisia—idadi ya kemikali zinazotumiwa ni kubwa sana.
Ili kutimiza mahitaji ya ulimwengu ya bidhaa hizi, kulingana na Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO), gharama za kutengeneza kemikali tufeni pote zinakaribia kufikia dola trilioni 1.5. Shirika la WHO linaripoti kwamba kemikali zipatazo 100,000 tayari zinauzwa na kwamba nyingine mpya 1,000 hadi 2,000 zinaongezwa kila mwaka.
Hata hivyo, kemikali hizi chungu nzima hutokeza maswali kuhusu namna zinavyoathiri mazingira na vilevile afya yetu. Kwa wazi tuko katika hali ambayo haijapata kuonekana tena. “Sisi sote ni sehemu ya kizazi kinachofanyiwa uchunguzi, na matokeo kamili hayatajulikana kwa miongo kadhaa ijayo,” akasema daktari mmoja.
Je, Kemikali Zaidi Huzidisha Hatari?
Mara nyingi zaidi watu wanaoathiriwa na vichafuzi vya kemikali, lasema shirika la WHO, ni “maskini, watu wasiojua kusoma na kuandika, wenye ujuzi kidogo au wasiokuwa na ujuzi wowote au maarifa ya msingi juu ya hatari zinazoletwa na kemikali wanazoshughulika nazo kwa njia ya moja kwa moja au kwa njia isiyo ya moja kwa moja kila siku.” Jambo hili ni kweli hasa kuhusu dawa za kuua wadudu. Lakini sote tunaathiriwa na kemikali.
Asilimia 20 hivi ya visima vya maji vya California, chasema kitabu A Green History of the World, vina viwango vya uchafu wa kemikali, kutia ndani dawa za kuua wadudu, vinavyozidi mipaka rasmi ya usalama. “Katika Florida,” kitabu hicho chaongezea, “visima 1,000 vimefungwa kwa sababu ya uchafuzi; katika Hungaria miji na vijiji 773 vina maji yasiyofaa kutumiwa, nchini Uingereza asilimia kumi ya maji yaliyo chini ya ardhi yamechafuliwa kupita mipaka ya usalama ya Shirika la Afya Ulimwenguni na katika sehemu fulani za Uingereza na Marekani watoto wachanga hawawezi kupewa maji ya mfereji kwa sababu yana nitrati nyingi.”
Kemikali-sumu nyingine yenye faida lakini iliyo hatari ni zebaki. Hiyo huingia kwenye mazingira kupitia vyanzo kama vile bomba la moshi wa viwanda na mabilioni ya taa zenye kuakisi mwanga. Vivyo hivyo, risasi yaweza kupatikana katika bidhaa nyingi, kutoka kwa fueli hadi rangi. Lakini kama vile zebaki, risasi yaweza kuwa sumu, hasa kwa watoto. Ripoti moja kutoka Cairo, nchini Misri, yasema kwamba mtoto wa kawaida akiishi mahali palipo na uchafuzi wa risasi, “kiwango chake cha kufikiri chaweza kupunguzwa kwa pointi nne.”
Kulingana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Mazingira, kila mwaka tani zipatazo 100 za zebaki, tani 3,800 za risasi, tani 3,600 za fosfati, na tani 60,000 za dawa za kusafisha huingia katika Bahari ya Mediterania likiwa tokeo la utendaji wa kibinadamu. Kwa kueleweka, bahari hiyo ina matatizo. Lakini si bahari hiyo pekee. Kwa kweli, Umoja wa Mataifa ulitangaza mwaka wa 1998 kuwa Mwaka wa Kimataifa wa Bahari. Ulimwenguni pote, bahari zote ziko taabani, hasa kwa sababu ya uchafuzi.
Ingawa tekinolojia ya kemikali imetutokezea bidhaa nyingi zenye faida, tunatumia na kutupa nyingi zazo kwa kudhuru sana mazingira. Je, tumejifanya kuwa “mateka wa maendeleo,” kama alivyosema mwandishi mmoja wa habari katika gazeti la habari hivi majuzi?
[Sanduku katika ukurasa wa 4]
Kemikali na Utendanaji wa Kemikali
Neno “kemikali” hurejezea vitu vyote vinavyofanyiza ulimwengu unaotuzunguka, kutia ndani zaidi ya elementi za msingi mia moja, kama vile chuma, risasi, zebaki, kaboni, oksijeni, nitrojeni. Misombo ya kemikali, au miunganisho ya elementi mbalimbali, hutia ndani vitu kama vile maji, asidi, chumvi, na vileo. Nyingi ya misombo hii hutokea kiasili.
“Utendanaji wa kemikali” umefasiliwa kuwa “hatua ambayo kitu kimoja kinabadilishwa kwa njia ya kemia kuwa kitu kingine.” Moto ni utendanaji wa kemikali; hugeuza kitu kiwezacho kuchomeka—karatasi, petroli, hidrojeni, na kadhalika—kuwa kitu au vitu tofauti kabisa. Utendanaji mwingi wa kemikali hutukia bila kukoma, kutuzunguka na ndani yetu.
[Picha katika ukurasa wa 3]
Maskini huteseka zaidi kutokana na vichafuzi vya kemikali