Kemikali—Je, Ni Rafiki na Adui?
TUNAFANYA maamuzi mengi maishani kwa kulinganisha faida na hasara. Kwa kielelezo, watu wengi hununua gari kwa sababu ya manufaa yake. Lakini wanapaswa kulinganisha mafaa hayo na gharama za gari—bima, kusajiliwa, kupunguka kwa thamani—na kudumisha gari katika hali inayofaa listahili kuwa barabarani. Pia wanapaswa kufikiria hatari ya kujeruhiwa au kifo kwa sababu ya aksidenti. Hali inafanana na hiyo kwa njia fulani kuhusu kemikali-sanisia—faida zake zapaswa kulinganishwa na hasara zake. Chukua mfano wa kemikali inayoitwa MTBE (methyl tertiary buty lether), ikiwa nyongeza ya fueli inayozidisha kuchomeka kwa mafuta na kupunguza moshi wa gari.
Kwa sehemu, kwa sababu ya MTBE, hewa katika majiji mengi ya Marekani ni safi zaidi ya ilivyokuwa kwa miaka kadhaa. Lakini hewa safi “imeleta athari,” laripoti New Scientist. Hii ni kwa sababu MTBE ni kemikali inayoweza kusababisha kansa, na imevuja kutoka kwenye makumi ya maelfu ya matangi yaliyo chini ya ardhi ya kuhifadhi petroli, mara nyingi ikichafua maji ya ardhini. Tokeo ni kwamba, sasa mji mmoja unahitaji kuleta asilimia 82 ya maji yake kutoka nje, kwa gharama ya dola milioni 3.5 kwa mwaka! Gazeti New Scientist lasema kwamba msiba huu “ungeweza kuwa mojawapo ya matatizo makubwa zaidi ya uchafuzi wa maji ya ardhini nchini Marekani kwa miaka mingi.”
Kemikali fulani zimepigwa marufuku na kuondolewa kwenye masoko kabisa kwa sababu ya madhara ambazo zinasababisha kwenye mazingira na kwa afya. Lakini huenda ukajiuliza, ‘kwa nini hili linatokea? Je, kemikali zote hazichunguzwi kikamili kujua ikiwa zina sumu kabla hazijaanza kuuzwa?’
Matatizo ya Kuchunguza Sumu
Kwa kweli, kuchunguza kemikali ikiwa zina sumu ni mchanganyiko wa sayansi na kukisia. “Wakadiriaji wa sumu hawajui kubainisha waziwazi kati ya kemikali ‘salama’ na ‘zisizo salama’ kushughulika nazo,” asema Joseph. V. Rodricks katika kitabu chake Calculated Risks. Hiyo ni kweli hata kuhusu dawa, ambazo nyingi hutengenezwa kisanisia. “Hata uchunguzi uliofanywa kwa makini sana,” yasema The World Book Encyclopedia, “sikuzote hauwezi kufunua uwezekano wa kwamba dawa hiyo ingeweza kutokeza athari zisizotazamiwa.”
Maabara yana dosari fulani za kiasili. Kwa kielelezo, maabara hayawezi kuigiza kikamili utendaji wa kemikali ikiwa nje ambako kuna vitu vya namna mbalimbali na vilivyo tata. Nje ya maabara kuna mamia, hata maelfu ya kemikali-sanisia zilizo tofauti, nyingi ambazo zaweza kuingiliana na nyingine na vilevile na vitu vilivyo hai. Baadhi ya kemikali hizi hazina madhara zikiwa peke yake, lakini zinapoungana, zikiwa ndani au nje ya miili yetu, zinaweza kutokeza sumu mpya. Kemikali nyingine huwa sumu, hata husababisha kansa, baada tu ya kuyeyushwa na mwili.
Wakadiriaji wa hatari wanaweza kuamuaje usalama wa kemikali ingawa kuna magumu ya namna hiyo? Kiwango ambacho kinatumiwa kimekuwa kuwapa wanyama wa maabara kemikali iliyopimwa na kisha kutumia matokeo hayo kwa binadamu. Je, njia hii hutegemeka sikuzote?
Je, Uchunguzi wa Wanyama Wategemeka?
Mbali na kuzusha maswali ya kiadili kuhusu kutenda wanyama kikatili, kuchunguza sumu kwa kutumia wanyama huzusha maswali mengine. Mathalani, mara nyingi wanyama mbalimbali huathiriwa na kemikali kwa njia tofauti. Kiasi kidogo cha dioksini yenye sumu kali kitaua nungubandia, lakini kiasi hicho kitahitaji kuongezwa mara 5,000 ili kuua buku! Hata wanyama wenye uhusiano wa karibu kama panya na buku huathiriwa na kemikali nyingi kwa njia tofauti.
Kwa hiyo ikiwa jinsi aina moja ya mnyama anavyoathiriwa haiwezi kuonyesha kwa uhakika jinsi aina nyingine itakavyoathirika, watafiti wanaweza kuwa na uhakika gani kwamba kemikali fulani itakuwa salama kwa binadamu? Ukweli ni kwamba, hawawezi kuwa na uhakika.
Hapana shaka wanakemia wana kazi ngumu. Wanahitaji kuwafurahisha wateja wao, kuwafurahisha wale wanaohangaikia hali njema ya wanyama, na kubaki wakiwa na dhamiri safi kwamba bidhaa wanazotokeza ni salama. Kwa sababu hizi, maabara fulani sasa yanachunguza kemikali kwa kutumia chembe zilizotolewa kwa binadamu. Hata hivyo, itakuwa wakati fulani ujao kabla hatujajua kama uhakikisho wa usalama waweza kupatikana.
Uchunguzi wa Maabara Ukosapo Kufaulu
Dawa ya kuua wadudu iitwayo DDT, ambayo bado inapatikana kwenye mazingira, ni mfano mmoja wa kemikali iliyotangazwa kimakosa kuwa salama ilipotolewa mara ya kwanza. Baadaye wanasayansi walitambua kwamba DDT hubaki kwa muda mrefu ndani ya viumbehai, jambo linalofanana na sumu nyingine zilizo hatari. Matokeo hatari ya hili ni gani? Naam, mfuatano wa mlishano, ambao umefanyizwa kwa mamilioni ya viumbe duni, kisha samaki, na hatimaye ndege, dubu, fisimaji, na kuendelea, huwa faneli hai, ikitokeza sumu nyingi kwa walaji wa mwisho. Katika kisa kimoja, kibisi, aina ya ndege wa majini, walishindwa kuangua hata kifaranga mmoja kwa zaidi ya miaka kumi!
Faneli hizi zilizo hai hutenda kazi kwa njia nzuri sana hivi kwamba kemikali fulani, ingawa hazigunduliwi kwa urahisi ndani ya maji, huwa zenye nguvu kwa kiwango kikubwa kwa walaji wa mwisho. Kielelezo kizuri ni nyangumi waitwao Beluga wa Mto St. Lawrence, Amerika Kaskazini. Wana sumu kali sana hivi kwamba wanachukuliwa kuwa takataka yenye sumu hatari wanapokufa!
Kemikali fulani zilizo katika wanyama wengi zimepatikana zikijifanya kuwa homoni. Na ni hivi majuzi tu kwamba wanasayansi wameanza kugundua athari zisizo wazi ambazo kemikali hizi zaweza kusababisha.
Kemikali Zinazoigiza Homoni
Homoni ni wajumbe wa kemikali wenye maana mwilini. Hizo husafiri kupitia mishipa ya damu hadi kwenye sehemu nyingine za mwili, ambapo ama zinachochea ama kukandamiza utendaji fulani, kama vile ukuzi wa mwili au vipindi vya kuzaa. Kwa kupendeza, habari mpya za hivi majuzi za Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) zilisema kwamba “uthibitisho mwingi wa kisayansi unaozidi kuongezeka” waonyesha kwamba kemikali-sanisia fulani, zinapotumiwa, huvuruga homoni ama kwa kuziiga kwa njia inayoleta madhara ama kwa kuzizuia.
Kemikali hizo zatia ndani PCB,a dioksini, furan, na dawa fulani za kuua wadudu, kutia ndani mabaki ya DDT. Kemikali hizi zinazoitwa vivuruga homoni, zina uwezo wa kuvuruga utaratibu wa kawaida wa mwili wa mfumo wa kutokeza homoni.
Homoni moja ambayo kemikali hizi huigiza ni homoni ya kike iitwayo estrojeni. Uchunguzi uliochapishwa katika jarida la kitiba Pediatrics wadokeza kwamba ongezeko la kubalehe mapema miongoni mwa wasichana wengi lingeweza kuhusianishwa na mafuta ya nywele yaliyo na estrojeni na vilevile kemikali zilizo kwenye mazingira zinazoigiza estrojeni.
Mwanamume akiathiriwa na kemikali fulani katika wakati fulani wenye maana sana wa ukuzi wake, aweza kupatwa na madhara makali. “Majaribio yameonyesha kwamba,” yasema ripoti katika gazeti Discover, “PCB zinapotumiwa wakati fulani hususa wakati wa ukuzi zaweza kubadili kasa na mamba wa kiume kuwa wa kike au ‘wawe kati ya jinsia zote.’”
Kwa kuongezea, sumu za kemikali hudhoofisha mifumo ya kinga, zikiwafanya wanyama wapatwe na maambukizo ya virusi kwa urahisi. Kwa kweli, maambukizo ya virusi yanazidi kuenea haraka zaidi kuliko wakati wowote, hasa miongoni mwa wanyama walio katika kiwango cha juu cha mlishano wa chakula, kama vile dolfini na ndege wa baharini.
Miongoni mwa wanadamu, watoto ndio huathiriwa zaidi na kemikali zinazoigiza homoni. Watoto waliozaliwa na wanawake waliomeza mafuta ya makapi ya mchele yaliyokuwa na PCB katika Japani miaka kadhaa iliyopita, “walipatwa na ukuzi wa polepole wa kimwili na wa kiakili, matatizo ya tabia kutia ndani kutotenda sana na kutenda kupita kiasi, uume ulio mdogo kupita kiasi, na kiwango cha akili kilichopungua pointi tano chini ya wastani,” laripoti gazeti Discover. Uchunguzi uliofanyiwa watoto walioishi katika maeneo yaliyo na PCB ya kiwango cha juu katika Uholanzi na Amerika Kaskazini ulifunua madhara makali yaliyo na matokeo sawa na haya kwa ukuzi wao wa kimwili na wa kiakili.
Pia linalohusianishwa na kemikali hizi, laripoti shirika la WHO, yawezekana ni ongezeko katika kansa “zinazohisiwa na homoni” miongoni mwa wanaume na wanawake, kama vile kansa ya matiti, kansa ya pumbu, na kansa ya kibofu. Kwa kuongezea, katika nchi nyingi, bila shaka upungufu unaoendelea katika wastani wa idadi ya shahawa katika wanaume, vilevile ubora wa shahawa, waweza kuhusianishwa na ongezeko la matumizi ya kemikali. Katika mabara fulani, wastani wa idadi ya shahawa umepungua kwa asilimia 50 katika miaka 50!
Katika makala iliyotangulia, daktari mmoja alinukuliwa akisema kwamba sisi ni “kizazi cha kufanyiwa uchunguzi.” Yaonekana yuko sahihi. Kweli, kemikali nyingi ambazo tumevumbua zimetufaidi, lakini nyingine hazijafanya hivyo. Kwa hiyo, tutakuwa wenye hekima tukiepuka kushughulika isivyo lazima na kemikali zinazoweza kutudhuru. Kwa kushangaza, nyingi za kemikali hizi zaweza kupatikana nyumbani mwetu. Makala yetu itakayofuata itazungumzia jambo tunaloweza kufanya ili kujilinda kutokana na kemikali zinazoweza kuwa hatari.
[Maelezo ya Chini]
a Kemikali zinazoitwa PCB (polychlorinated biphenyls), ambazo zimetumika ulimwenguni pote tangu miaka ya 1930, ni elementi za misombo zaidi ya 200 yenye mafuta-mafuta inayotumiwa katika mafuta ya kulainisha, plastiki, mipira ya nyaya za umeme, dawa za kuua wadudu, sabuni za kuoshea, na bidhaa nyinginezo. Ingawa sasa utengenezaji wa PCB umepigwa marufuku katika nchi nyingi, kati ya tani milioni moja na milioni mbili zimetengenezwa. Madhara ya sumu yametokana na PCB zilizotupwa ambazo sasa ziko kwenye mazingira.
[Picha katika ukurasa wa 7]
Nyangumi hawa wana sumu nyingi sana hivi kwamba wanaonwa kuwa takataka yenye sumu hatari wanapokufa
[Hisani]
©George Holton, The National Audubon Society Collection/PR