Vizuizi Vinavyozuia Mawasiliano
ROBERT ni mishonari wa Watch Tower aishiye Sierra Leone, Afrika Magharibi. Siku moja muda mfupi baada ya kuwasili nchi hiyo, alipokuwa akitembea barabarani, aliona kwamba watoto wa huko walikuwa wakiimba: “Mzungu!” Mzungu!” Robert, ambaye ni Mmarekani mweusi, alitazama huku na huku aone mzungu, lakini hapakuwa na mtu yeyote hapo. Ndipo akang’amua kwamba watoto walikuwa wakipiga kelele kumhusu!
Hakukuwa na ubaya wowote katika kuimba huko. Hao watoto walikuwa tu wanaonyesha kwamba Robert ni wa utamaduni ulio tofauti na wao. Kumwita Robert mzungu kulikuwa ndiko njia bora zaidi ya kutaja tofauti iliyokuwako kati yao.
Jinsi Utamaduni Huathiri Jinsi Tulivyo
Utamaduni umefafanuliwa kwa mapana kuwa “mawazo yanayoshirikiwa yenye kufanana, . . . desturi, itikadi, na ujuzi unaotambulisha njia fulani ya maisha.” Sisi hujifunza maadili mengi ya kitamaduni kupitia kufundishwa kwa njia ya moja kwa moja, lakini sisi hujifunza mengi bila hata kujua. Mtafiti mmoja alisema hivi: “Tangu wakati wa kuzaliwa kwa [mtoto] desturi zinazofuatwa na wazazi wake hufanyiza maono na tabia yake. Kufikia wakati awezapo kuzungumza, yeye ni tokeo la utamaduni wake, na kufikia wakati ambapo yeye ni mtu mzima na kuweza kushiriki katika utendaji wa utamaduni, tabia za [utamaduni] huwa zake, itikadi za [utamaduni] huwa zake, na mambo yasiyowezekana kwa [utamaduni] hayawezekani kwake.”
Kwa njia nyingi utamaduni hufanya maisha yawe rahisi kwetu. Tukiwa watoto sisi hujifunza upesi jinsi ya kuwapendeza wazazi wetu. Kujua mambo yakubaliwayo na yasiyokubaliwa na jamii yetu hutuongoza katika kufanya maamuzi juu ya jinsi ya kutenda, mavazi, na jinsi ya kushughulika na wengine.
Bila shaka, kile tulicho tukiwa watu mmoja-mmoja hakitegemei malezi yetu ya kitamaduni pekee. Katika kila utamaduni kuna tofauti miongoni mwa watu. Jinsi tulivyo huamuliwa pia na tabia ya urithi, maono yetu maishani, na mambo mengine mengi. Hata hivyo, utamaduni ndio njia ambayo sisi hutumia kuona ulimwengu.
Kwa kielelezo, utamaduni wetu huamua si lugha tusemayo tu bali pia jinsi tuisemavyo. Katika sehemu fulani za Mashariki ya Kati, watu huthamini uwezo wa kujieleza kwa ustadi kwa kutumia maneno mengi, ya kujirudia-rudia pamoja na misemo. Kwa kutofautisha, watu wa nchi fulani za Mashariki ya Mbali huzungumza kidogo sana. Mithali moja ya Kijapani yaonyesha wazo hilo: “Kwa kinywa chako, utaangamia.”
Utamaduni wetu huamua jinsi tuonavyo wakati. Katika Uswisi, ukichelewa kwa dakika kumi kwa miadi fulani, unatarajiwa uombe radhi. Katika nchi nyinginezo unaweza kuchelewa kwa muda wa saa moja au mbili na usitarajiwe kuomba radhi.
Utamaduni wetu pia hutufundisha maadili. Fikiria jinsi ambavyo ungehisi mtu akikuambia: “Unaongeza uzito sana. Unanenepa kwelikweli!” Ikiwa ulilelewa katika utamaduni wa Kiafrika ambako ukubwa wa mwili huthaminiwa, yaelekea ungefurahia hayo maneno. Lakini ikiwa ulilelewa katika utamaduni wa Magharibi ambako wembamba huthaminiwa sana, yaelekea maneno hayo ya unyoofu yangekuudhi.
‘Njia Yetu Ndiyo Bora!’
Kile ambacho mara nyingi huzuia mawasiliano kati ya watu wa tamaduni tofauti ni kwamba kila mahali watu hufikiria kwamba utamaduni wao ndio bora. Wengi wetu hufikiri kwamba itikadi zetu, maadili, mapokeo, na namna ya kuvaa, na mawazo juu ya urembo ni sawa, yafaa, na bora kuliko mengine yote. Pia sisi huelekea kuhukumu tamaduni nyinginezo kwa kuzilinganisha na maadili ya kikundi chetu. Kufikiri hivyo ni kuona utamaduni wetu kuwa bora kuliko nyinginezo. The New Encyclopædia Britannica huonelea: “Kuona utamaduni wetu kuwa bora . . . ni jambo linalopata karibu ulimwengu mzima. Washiriki wa karibu tamaduni zote za ulimwengu huona njia zao wenyewe za maisha kuwa bora kuliko hata zile za majirani wao wa karibu.”
Miaka 200 iliyopita, Mwingereza mmoja mwenye cheo alieleza jambo hilo waziwazi, akisema: “[Kwa] maoni yangu, wageni ni wapumbavu.” Mhariri wa kitabu chenye manukuu hayo aliandika: “Ni lazima [hiyo] iwe hisia ya karibu ulimwengu wote.”
Vielelezo vya kutovumilia wale wa tamaduni nyinginezo vimejaa. Ingawa liliandikwa awali na mwandikaji wa vitabu Mjerumani katika miaka ya 1930, nukuu lifuatalo mara nyingi husemwa kuwa lilitajwa na kiongozi wa Nazi Hermann Göring: “Nisikiapo neno utamaduni, mimi hutwaa bastola yangu.”
Maoni ya kishupavu ya kuona utamaduni wako kuwa bora yaweza kutokeza ubaguzi, ambao nao unaweza kutokeza chuki na pambano. Richard Goldstone ni kiongozi wa mashtaka wa Mahakama ya Uhalifu ya Kimataifa inayochunguza uhalifu wa vita katika Rwanda na ile iliyokuwa Yugoslavia. Kuhusu matendo makatili katika mapambano hayo yote mawili, yeye alisema: “Jambo hili laweza kutokea mahali popote. Hapa pana nchi mbili tofauti, zikiwa na tamaduni na historia tofauti, lakini ukatili unaofanana [una]fanywa na jirani dhidi ya jirani mwenzake. Aina hii ya vita vikatili vya kikabila au kidini ni ubaguzi tu ulioongezeka ukawa wenye jeuri. Kile kikundi cha watu kinachohasiriwa ni lazima kishushiwe hadhi kabisa au kuonwa kuwa cha kishetani. Mara hilo lifanywapo, hilo huondolea watu wa kawaida vizuizi vya kiadili ambavyo kwa kawaida vingewazuia wasitende matendo ya kuogofya kama hayo.”
Kupanua Mtazamo Wetu
Mara nyingi watu tuwachaguao kuwa marafiki wetu ni wale walio kama sisi, watu wenye kushiriki mitazamo yetu na maadili yetu. Sisi huwatumaini na kuwaelewa. Sisi hustarehe tukiwa pamoja nao. Tukiona tabia ya mtu mwingine kuwa isiyo ya kawaida au isiyo nzuri, yaelekea marafiki wetu watakubaliana nasi kwa sababu wao wana ubaguzi uleule kama sisi.
Basi, twaweza kupata manufaa gani katika kuwasiliana na wengine wanaotofautiana na sisi kwa sababu ya malezi ya kitamaduni? Kwanza, mawasiliano mazuri yatatusaidia kuelewa sababu zinazofanya wengine wafikiri na kutenda jinsi wafanyavyo. Kunle, kutoka Afrika Magharibi, asema: “Watoto wengi katika Afrika hukatazwa sana wasiongee wanapokula chakula. Lakini, katika baadhi ya nchi za Ulaya, kuongea wakati wa kula kunapendekezwa. Basi ni nini hutukia wakati Mzungu anapokula pamoja na Mwafrika? Yule mzungu anashangaa kwa nini huyu Mwafrika anakula chakula kwa mawazo mazito na kwa ukimya. Wakati uo huo, yule Mwafrika anashangaa ni kwa nini huyo Mzungu anaongea kama kasuku!” Kwa wazi katika hali kama hizo, kuelewa malezi ya kitamaduni ya kila mmoja kwaweza kuondoa ubaguzi wa kijamii.
Tupatapo kuwajua watu wa tamaduni nyinginezo, hatuboreshi tu jinsi tunavyowaelewa wengine bali pia sisi wenyewe hujielewa vizuri zaidi. Mstadi mmoja wa mambo ya kibinadamu aliandika: “Kitu ambacho yule mkazi wa ndani ya bahari hawezi kugundua ni maji. Yeye angefahamu maji yapo ikiwa tu aksidenti fulani ingemleta juu na kumwonyesha hewa. . . . Uwezo wa kuona utamaduni wa jamii yetu kwa ujumla . . . hutaka kiasi fulani cha uwezo wa kushughulikia mambo bila ubaguzi ambao mara nyingi haupo kamwe.” Hata hivyo, kwa kufahamu tamaduni nyinginezo, sisi ni kama yule mkazi wa bahari anayeonyeshwa hewa; twatambua “maji” ya kitamaduni tunamoishi. Mwandikaji Thomas Abercrombie alieleza jambo hilo vizuri: “Mtu ambaye hajavutiwa na utamaduni wa kigeni hawezi kamwe kujua vizuizi vya utamaduni wake.”
Kwa ufupi, kuthamini tamaduni nyinginezo kwaweza kuboresha maisha zetu kwa kupanua mtazamo wetu, ili tuweze kujielewa na kuelewa wengine vizuri zaidi. Ingawa urithi wa kitamaduni na mawazo ya kwamba utamaduni wako ndio bora yaweza kuwa vizuizi vinavyozuia mawasiliano, lakini si lazima yawe hivyo. Vizuizi hivyo vyaweza kushindwa.
[Blabu katika ukurasa wa 6]
“Washiriki wa karibu tamaduni zote za ulimwengu huona njia zao wenyewe za maisha kuwa bora kuliko hata zile za majirani wao wa karibu.”—The New Encyclopædia Britannica
[Picha katika ukurasa wa 7]
Twaweza kujifunza kufurahia vitu vizuri vya tamaduni nyinginezo
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 6]
Dunia: Mountain High Maps® Copyright © 1995 Digital Wisdom, Inc.