Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g96 7/22 kur. 12-14
  • “Utaratibu wa Ulimwengu Mpya”—Waanza Kihafifu

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • “Utaratibu wa Ulimwengu Mpya”—Waanza Kihafifu
  • Amkeni!—1996
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Vita Vyadumu kwa Kuhuzunisha
  • Kukaribia Kufilisika
  • Dini, Je, Ni Kani Yenye Kuleta Uthabiti?
  • Sherehe Zenye Umaana Bila Mengi ya Kusherehekea
  • Utaratibu wa Ulimwengu Mpya Ulipokuwa Ukitatanika, Theokrasi ya Kweli Ilisitawi!
  • Mipango ya Mwanadamu kwa Ajili ya Usalama wa Kimataifa
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1992
  • Jitihada Inayoendelea ya Kutafuta Utengemano Mpya wa Ulimwengu
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1991
  • Siri—Katika Jina la Bwana
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1997
  • Warusi Wathamini Sana Uhuru wa Kuabudu
    Amkeni!—2000
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1996
g96 7/22 kur. 12-14

“Utaratibu wa Ulimwengu Mpya”—Waanza Kihafifu

NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA UJERUMANI

MWAKA 1991 ulipoanza, watu walikuwa na matumaini. Vita baridi ilikuwa imekwisha. Ni kweli kwamba kulikuwa na tatizo la Kuwait, ambayo ilikuwa imevamiwa na Iraki mwezi wa Agosti uliokuwa umepita. Lakini Umoja wa Mataifa ulikuwa umeonyesha uwezo wao na kuamuru Iraki iondoke kabla ya Januari 15. Amri hiyo ilikuwa ikitegemezwa na muungano wa kijeshi wa mataifa 28 wa UM ambao ulipangwa haraka na ambao ulikuwa tayari kulazimisha Iraki isalimu amri. Kulikuwa na matumaini makubwa kwamba msimamo thabiti uliochukuliwa na jumuiya ya ulimwengu ulikuwa ishara ya kuanza kwa enzi mpya.

George Bush, ambaye wakati huo alikuwa rais wa Marekani, alisema juu ya “uwezekano, kwetu na kwa vizazi vijavyo, wa kufanyiza utaratibu wa ulimwengu mpya, ulimwengu ambamo utawala wa sheria, wala si mashindano makali, ungeongoza mwenendo wa mataifa.”

Iraki nayo ikapuuza ile tarehe ya mwisho ya Januari 15, na mashambulio makubwa sana ya ndege na makombora yakafanywa dhidi ya vituo vya kijeshi vya Iraki. Kwa wazi, jumuiya ya ulimwengu ilikuwa imeazimia kutekeleza amri hiyo. Muda usiozidi miezi mitatu baadaye, mnamo Aprili 11, UM ulitangaza kwamba Vita ya Ghuba imekwisha. Ahadi ya utaratibu wa ulimwengu mpya ulio thabiti kiuchumi na kisiasa ilionekana ikielekea kuwa halisi.

Vita Vyadumu kwa Kuhuzunisha

Katikati ya 1991 jamhuri mbili, Slovenia na Kroatia, zilitangaza uhuru kutoka kwa Yugoslavia ya wakati huo, jambo lililoanzisha vita ya wenyewe kwa wenyewe ambayo hatimaye ilisababisha kufanyizwa kwa mataifa kadhaa yaliyojitenga. Muda usiozidi mwaka mmoja baadaye, mchanganuzi wa kisiasa Mfaransa Pierre Hassner alisema: “Kama Ulaya ya kabla ya 1914, utaratibu wa ulimwengu mpya wa George Bush uliishia Sarajevo.” Hata hivyo, mtazamo wa amani ukawa na tumaini mazungumzo yalipoanza katika Dayton, Ohio, Marekani, mnamo Novemba 1995 na mkataba wa amani ulitiwa sahihi katika Paris mnamo Desemba 14. Huku 1995 ukielekea kwisha, kukawa na matumaini mapya kwamba kumbe utaratibu wa ulimwengu mpya ungali uliwezekana.

Zile jamhuri za Muungano wa Jamhuri za Kisoshalisti za Sovieti zilikuwa zinatengana polepole. Katika 1991, Lithuania, Estonia, na Latvia zilikuwa za kwanza kutangaza uhuru wazo, zikifuatwa upesi na jamhuri nyinginezo. Jumuiya hafifu iliyoitwa Jumuiya ya Mataifa Huru ilianzishwa Desemba, ingawa baadhi ya washiriki wa zamani wa Muungano wa Sovieti walikataa kujiunga nayo. Kisha, mnamo Desemba 25, Gorbachev akajiuzulu urais wa Sovieti.

Lakini, hata jamhuri moja-moja zikaanza kuasi. Kwa kielelezo, Chechnya, ambayo ni eneo dogo la Waislamu katika eneo la kaskazini mwa Caucasus la Urusi, ilikuwa iking’ang’ania uhuru. Majaribio yayo ya kupata uhuru mwishoni mwa 1994 yalisababisha shambulio lililobishaniwa la majeshi ya Urusi. Hata ingawa watu wapatao 30,000 wamepoteza uhai tangu tatizo hilo lianze mapema katika miaka ya 1990, vita hiyo imeendelea hadi mwaka huu.

Kufikia Oktoba 1995, mapambano kati ya 27 na 46—kulingana na jinsi yalivyoainishwa—yalikuwa yakiendelea ulimwenguni kote.

Kukaribia Kufilisika

Mwanzoni mwa miaka ya 1990, utaratibu wa ulimwengu mpya ulikuwa ukithibitika kuwa si hafifu tu kisiasa bali hafifu kiuchumi vilevile.

Katika 1991, Nikaragua ilipunguza thamani ya fedha yayo, na hata baada ya kufanya hivyo cordoba milioni 25 zilitoshana na dola moja tu ya Marekani. Wakati uo huo, Zaire ilikuwa inapitia infleshoni yenye kiwango cha asilimia 850, jambo lililolazimisha wananchi wayo wavumilie mojayapo viwango vya chini zaidi vya kuishi ulimwenguni. Uchumi wa Urusi ulikuwa na matatizo pia. Infleshoni ikifikia asilimia 2,200 kwa mwaka katika 1992, jambo lililofanya pesa ikose thamani. Ingawa mambo yaliboreka baadaye, katika 1995 matatizo ya kiuchumi hayakuwa yamemalizika kamwe.

Kashfa kubwa zaidi ya kifedha katika karne hii ilitokea katika 1991, wakati Bank of Credit & Commerce International ilipoanguka, ikiangushwa na upunjaji na matendo ya uhalifu. Wenye akiba katika nchi 62 walipata hasara zifikazo mabilioni ya dola za Marekani.

Si mataifa yenye uchumi dhaifu pekee yaliyoathiriwa; Ujerumani yenye nguvu iliathiriwa na matokeo ya muungano wayo. Hali ya ukosefu wa kazi ikapanda huku wafanya kazi wakidai wapate likizo ndefu zaidi na utunzi bora zaidi wa afya. Hali ya wafanyakazi wengi kukosa kufika kazini kwa ukawaida pamoja na kutumiwa vibaya kwa mfumo wa msaada kuliongeza mkazo zaidi kwa uchumi.

Katika Marekani, mfululizo wa misiba mibaya sana ulisababisha hasara kubwa miongoni mwa makampuni ya bima, ambayo yalijikuta yakilazimika kulipa madai ya bima. Na katika 1993 kitabu Bankruptcy 1995: The Coming Collapse of America and How to Stop It kilionya dhidi ya hatari za madeni ya mataifa yenye kuongezeka sana na upungufu wa bajeti. Hata uthabiti wa kampuni ya bima ya Lloyd ya London ulitiliwa shaka. Ikiwa imepata hasara nyingi, ilikuwa ikilazimika kufikiria jambo lisilowezekana—uwezekano wa kufilisika.

Dini, Je, Ni Kani Yenye Kuleta Uthabiti?

Katika 1991 gazeti la kila siku la Ujerumani Frankfurter Allgemeine Zeitung lilisema hivi: “Wazo hili la utaratibu wa ulimwengu mpya lategemea desturi ya muda mrefu ya maoni ya Marekani juu ya ulimwengu, ambayo yote yamekuwa na msingi wa kidini na ambayo yamefanyizwa kwa njia za Kikristo.”

Mtu angefikiri kwamba msingi huo wa kidini ungeongeza uthabiti kwa utaratibu wa ulimwengu mpya. Lakini kwa hakika kukosa uvumilivu wa kidini na zogo zilisababisha ukosefu wa uthabiti wenye kuenea sana. Algeria na Misri zilikuwa nchi mbili kati ya serikali nyingi zilizokuwa zikitofautiana na Waislamu wenye siasa kali. Uharamia mwingi uliochochewa kidini ukakumba hizo nchi mbili. Ghasia za kidini katika India zilitia ndani muda wa siku tisa za jeuri za kidini katika Bombay mwaka wa 1993 zilizosababisha vifo vya zaidi ya watu 550.

Mgawanyiko wa kidini ulipunguza maendeleo ya muungano wa Kikristo wa ulimwenguni pote katika 1994 wakati Kanisa la Kianglikana lilipowatawaza wanawake 32 kuwa makasisi. Papa John Paul 2 aliliita hilo “kikwazo kikubwa sana kwa tumaini lolote la kuungana kwa Kanisa Katoliki na dini za Kianglikana.”

Mnamo Aprili 19, 1993, uvutano kati ya serikali ya Marekani na washiriki wa madhehebu ya kidini, Branch Davidians—ambao tayari ulikuwa umetokeza pambano katika ua wa madhehebu hiyo katika Waco, Texas, na kuuawa kwa maofisa wanne wa usalama—ulisababisha vifo vya angalau washiriki 75 wa madhehebu hiyo. Miaka miwili baadaye uchunguzi ulikuwa ukifanywa juu ya uwezekano wa kwamba bomu la haramia lililoua watu 168 katika jengo la serikali katika Oklahoma City laweza kuwa lilikuwa kulipiza kisasi shambulio la Waco.

Ulimwengu ulishtuka sana mapema katika 1995 kusikia juu ya shambulio la haramia aliyetumia gesi yenye sumu katika mfumo wa reli ya chini ya ardhi ya Tokyo. Watu kumi walikufa, na maelfu wengine zaidi wakawa wagonjwa. Ulimwengu ulishtuka hata zaidi wakati lawama ilipowekwa juu ya madhehebu ya apokalipsi iitwayo Aum Shinrikyo, au Aum Kweli Kuu Zaidi.

Sherehe Zenye Umaana Bila Mengi ya Kusherehekea

Katika 1492, Columbus alifika Kizio cha Magharibi bila kutarajia. Ile sherehe ya 1992 ya miaka 500 ya tukio hilo ilijaa ubishi. Wazao wapatao milioni 40 wa Wahindi Wamarekani waliudhikia jambo la kwamba Mzungu fulani “aligundua” nchi ambazo wazazi wao wa kale walikuwa wameishi na kusitawi muda mrefu hata kabla ya huyo mzungu kuzaliwa. Wengine walimwita mvumbuzi huyo “mtangulizi wa kutumiwa kwao vibaya na kushindwa.” Na kwa hakika, kufika kwa Columbus katika Kizio cha Magharibi kulikuwa msiba kuliko baraka kwa wakazi wacho wenyeji. Wale walioitwa eti washindi Wakristo waliwanyang’anya ardhi, utawala, hadhi na uhai zao.

Mnamo Septemba 1995, Israeli ilianza sherehe ya miezi 16 ya kuadhimisha ukumbusho wa mwaka wa 3,000 tangu Mfalme Daudi ashinde Yerusalemu. Lakini sherehe hiyo ilianza vibaya Waziri Mkuu Yitzhak Rabin alipopigwa risasi mnamo Novemba 4 dakika chache tu baada ya kuhutubia mkutano wa amani. Jambo hilo lilitilia shaka mwendo wa amani ya Mashariki ya Kati, na kuthibitisha kwamba kuna tofauti kubwa za kidini si kati ya Wayahudi na Wapalestina pekee bali hata miongoni mwa Wayahudi wenyewe.

Miadhimisho kadhaa ya miaka ya 50 ilisherehekewa kati ya 1991 na 1995 kuhusiana na Vita ya Ulimwengu 2—lile shambulio la Pearl Harbor lililofanya Marekani iingie vitani; kuvamiwa kwa Ulaya na majeshi ya Muungano; kukombolewa kwa kambi za mateso za Nazi; ushindi wa majeshi ya Muungano katika Ulaya; na kuangushwa kwa bomu la kwanza la atomu Japani. Kwa sababu ya damu na machozi yanayoshirikishwa na matukio hayo, watu fulani waliuliza ikiwa matukio hayo yalistahili kusherehekewa kweli.

Hilo lilitokeza mwadhimisho wa tukio jingine muhimu, kuanzishwa kwa shirika la Umoja wa Mataifa mnamo Oktoba 1945. Kukawa na matumaini mengi kwamba hatimaye njia ya kupata amani ilikuwa imepatikana.

Umoja wa Mataifa, kama Boutros Boutros-Ghali, katibu wao mkuu, alivyosema majuzi akiutetea, umepata ushindi mwingi. Lakini haujafanikiwa katika kutimiza kusudi lao kuu, yaani “kudumisha amani na usalama wa kimataifa.” Mara nyingi majeshi yao yamejaribu kudumisha amani katika sehemu ambazo hakukuwa na amani ya kudumishwa. Kufikia 1995, ulishindwa kuutegemeza utaratibu wa ulimwengu mpya ulio hafifu.

Utaratibu wa Ulimwengu Mpya Ulipokuwa Ukitatanika, Theokrasi ya Kweli Ilisitawi!

Kwa kutazama ukosefu wa uthabiti wa kisiasa, kiuchumi na kidini uliosababisha tumaini lao la utaratibu wa ulimwengu mpya liporomoke mbele yao, watu wengine walianza kusema juu ya mvurugo wa ulimwengu mpya. Kwa habari hiyo, Mashahidi wa Yehova waliona uthibitisho mwingine zaidi kwamba ni ulimwengu mpya unaofanyizwa tu na Mungu ndio utakaokuwa na uthabiti katika jamii ya kibinadamu.

Katika nchi fulani mwisho wa Vita Baridi ulimaanisha uhuru mkubwa zaidi kwa Mashahidi wa Yehova, ukiwaruhusu kufanya mikusanyiko ya kimataifa yenye kutokeza sana katika Budapest, Kiev, Moscow, Prague, St. Petersburg, Warsaw, na kwingineko. Hiyo iliimarisha mpango wa kikutaniko wa ulimwenguni pote wa Mashahidi wa Yehova na kuwasaidia kuharakisha kazi yao ya kuhubiri. Basi, haishangazi kwamba idadi ya Mashahidi watendaji katika moja tu ya maeneo hayo iliongezeka kutoka 49,171 katika 1991 hadi 153,361 katika 1995. Katika kipindi hichohicho cha miaka minne, idadi ya Mashahidi ulimwenguni pote ikaongezeka kutoka 4,278,820 hadi 5,199,895. Theokrasi ya kweli inasitawi kuliko wakati mwingine wowote!

Ndiyo, mamilioni ya watu sasa wanategemeza matumaini yao ya wakati ujao juu ya ahadi ya Yehova Mungu ya “mbingu mpya na nchi mpya” ambamo “haki yakaa.” (2 Petro 3:10, 13) Ni jambo la hekima kama nini kuliko kutumainia utaratibu wa ulimwengu mpya wa kibinadamu, ambao, baada ya kuanza kihafifu, karibuni utaangamizwa!—Danieli 2:44.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki