Sababu Iliyofanya Abadili Vipaumbele Vyake
NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA UINGEREZA
Mwanguo mzuri sana wa wimbo ulijaa hewani kwa ghafula. Melodia zenye kusikika wazi sana zikamiminika, yaonekana bila kikomo. Nilisimama nikiwa nimeduwaa. “Ni ‘nightingale!’” akanong’ona Jeremy. Polepole tukasonga hatua kwa hatua kuzunguka hicho kichaka, tukijitahidi kukaza macho mahali ilipokuwa ikitoka sauti hiyo nzuri ajabu. Kisha, tukamwona ndege mwenye haya aliye na rangi ya hudhurungi-nyangavu ndani sana ya hicho kichaka. “Ilikuwa vyema kumwona,” akasema Jeremy tulipokuwa tukiondoka hatimaye. “Ni watu wachache sana ambao hupata kumwona.”
NILIKUWA nimekuja kutumia siku hiyo pamoja na Jeremy, mlinzi wa hifadhi ya asili ya hektari 800 ya Minsmere ya Royal Society for the Protection of Birds (RSPB), iliyoko kwenye moja ya maeneo ya mashariki zaidi ya Uingereza. Wakati wa vita ya ulimwengu ya pili, sehemu hii ya pwani ya Bahari ya Kaskazini ilifurikishwa ili kukinza shambulizi lililoelekea kutokea la Ujerumani. Likiwa tokeo, mashamba ya matete yakasitawi nao ndege wa mabwawa wakaanza kumiliki malisho hayo yaliyofurikishwa. Msisimuko uliongezeka katika 1947 wakati jozi nne za domo-juu zilipojenga viota, kwa kuwa spishi hii haikupata kuzaana katika Uingereza kwa zaidi ya miaka 100.
Muda si muda RSPB ikachukua usimamizi wa mahali hapo, na sasa ni eneo la hifadhi lenye umaana wa kimataifa. Kwa kuongezea mashamba ya matete, makao hayo ya ndege hutia ndani nyangwa zenye chumvi-chumvi na za maji matamu—ulio mkubwa zaidi ukiitwa Scrape—changarawe, vilima vya mchanga, mabwawa, makonde ya majani, nyika, na misitu ya miti yenye kupukutisha na vilevile misunobari. Zaidi ya spishi 330 za ndege zimewekwa katika rekodi, 100 hivi zikizaana kwenye hifadhi hiyo. Unamna-namna huu mkubwa wa ndege hasa ni kwa sababu ya njia za uhamaji zilizo kandokando ya mwambao wa mashariki, lakini usimamizi wenye ustadi pia umechangia.
“Nilikuja hapa katika 1975,” akaniambia Jeremy, “kwa sababu Minsmere ilitoa mwito wa ushindani usio wa kawaida. Tangu 1966 domo-juu alikuwa ishara, na hatimaye utambulisho, wa RSPB. Sasa Minsmere huonwa na watu wengi kuwa hifadhi bora zaidi ya RSPB, ikipata wageni kufikia 80,000 kila mwaka.”
Magumu ya Mwanzoni
“Upendezi wangu ulichochewa shuleni,” Jeremy aliendelea kusema tulipokuwa tukiendelea kutembea. “Nilijifunza kutia ndege pete (ili kuwatambulisha kwa urahisi na kuchunguza miendo yao), nikajifunza uhamaji. Kufikia miaka ya mwisho-mwisho ya 1960, nilikuwa nikipenda kutia pete kati ya ndege 12,000 na 20,000 kwa mwaka. Kisha, Chris Mead wa British Trust for Ornithology alinialika kujiunga na safari ya kwenda Hispania ili kutia pete ndege wahamaji wa ng’ambo ya Sahara. Wavu uliotumiwa ulikuwa mweusi na wenye nyuzi ndogo-ndogo sana, wenye urefu wa kuanzia meta 6 hadi 18, ambao unaning’inizwa, na kuwekwa kwa uangalifu mbele ya miti ili ndege wasiuone. Ndege hawadhuriwi, na wanapotolewa ndani ya wavu, pete ndogo ya utambulishaji, ambayo kwa kawaida hutengenezwa kwa Monel Metal, hushikizwa kuzunguka mguu.a Kuwaachilia ndege hao huhitaji ustadi pia. Mweka ndege pete harushi ndege hewani kamwe, kama uonavyo kwenye televisheni nyakati fulani. Yeye huwaacha waende watakapotaka. Kwa kielelezo, mbayuwayu hukwamia mavazi ya sufu ya mtu na kupuruka wakati tu wanapokuwa tayari.
“Hilo lilikuwa ono lenye kuvutia ambalo ilinilazimu nichukue likizo ya majuma sita—nalo lilifanya nipoteze kazi yangu! Likiwa tokeo, niliamua kufanya badiliko la ghafula na kufuatia kazi niliyoipenda—kuhifadhi maumbile ya asili, hasa ndege. Nilifurahi wakati RSPB waliponialika kujiunga nao katika 1967.”
Thamani ya Nyimbo na Miito ya Ndege
Waweza kutambulishaje ndege? Nyakati fulani kwa kuona, lakini kufanya hivyo kwa nyimbo, au mwito wa ndege, kunategemeka zaidi. Ustadi wa Jeremy kwa habari hii unajulikana sana. Mtaalamu wa mambo ya asili David Tomlinson kwa kushangazwa aliandika kwamba Jeremy “hawatambulishi ndege kwa wimbo wao tu, bali nasema kwa uthabiti yeye aweza kuwatofautisha kwa namna wanavyovuta hewa ndani kati ya miito yao!”
“Ndege huzungumza,” akaeleza Jeremy. “Kila mwito humaanisha kitu tofauti. Kwa kielelezo, wakati kuna mnyama-mwindaji karibu, domo-juu, ndoero, shakwe, na viguuhina wote wana miito yao hususa, lakini kila mwito humaanisha kitu kilekile: ‘Kuna mbweha karibu!’ Naweza kuamka kutoka usingizi mzito na kujua mara moja kutokana na spishi ya ndege anayeita, mahali alipo mbweha. Lakini usisahau kwamba mbweha pia wana uwezo bora sana wa kusikia. Tulishangaa kwa nini membe hawakuwa wakizaana kwa matokeo mwaka mmoja, tukatambua kwamba mbweha fulani alikuwa akisikiliza makinda yakiita kutoka ndani ya mayai kabla tu ya kuanguliwa. Mara tu alipowapata, aliwala!”
Usanii wa Utazamaji-Ndege
Mtazamaji-ndege mzuri katika Uingereza aweza kurekodi kufikia spishi tofauti-tofauti 220 kwa mwaka. Wachunguzaji wa ndege walio nadra, ambao ni watazamaji-ndege wenye bidii wanaojaribu kurekodi kuonekana kwa ndege walio nadra, waweza kutambulisha hadi 320.b Habari za kuonekana kwa ndege huwafanya wasafiri kotekote nchini wakajionee wenyewe. Jeremy ameridhika zaidi. “Siwezi kuendesha gari kwa zaidi ya kilometa 16 ili kuona spishi iliyo nadra,” akasema waziwazi. “Kwa hakika, nimepata kusafiri ili kuona tatu tu: nutcracker, chamchanga mwenye kifua-manjano, na tandawala mkuu, wote katika eneo la kilometa 16. Hata ingawa najua spishi 500 vyema sana, natambua kwamba najua asilimia ndogo ya spishi zote za ndege zilizopo. Wajua, kuna spishi 9,000 za ndege ulimwenguni pote!”
Tulipokuwa tukielekeza darubini zetu kwenye mabwawa, Jeremy akaongeza, kwa hamu hivi: “Siwezi kutamani maisha yenye furaha zaidi au yenye matokeo zaidi, hasa kwa miaka yangu 16 katika Minsmere!” Nilimtazama nikakumbuka makala iliyokuwa imetokea tu kwenye The Times, gazeti la habari la Uingereza. Ilisema: “Minsmere palikuwa matokeo ya upeo [ya Jeremy], kazi ya maisha yake.” Jeremy alikuwa akiondoka Minsmere. Kwa nini?
Mbegu na Ukuzi
Mapema katika siku hiyo, tulikuwa tumeshuhudia wonyesho wa kujamiiana usio wa kawaida wa domo-juu. “Uzuri wa wonyesho huo,” Jeremy akataja, “hauwezi kuelekezwa kwa kusalimika fulani kwa kimageuzi. Lakini nakumbuka nikikiri miaka michache iliyopita, wakati nilipoulizwa ikiwa niliamini kuna Mungu: ‘Sijui hata kidogo—na sijui njia ya kutambua!’ Kwa hiyo nilipotiwa moyo kuchunguza Biblia, nilikubali kwa utayari. Sikujua mengi kuihusu na nilifikiri kwamba hakukuwa na chochote cha kupoteza—na labda lingekuwa jambo lenye manufaa. Sasa, likiwa tokeo la kile nilichojifunza, naondoka Minsmere ili kuwa mhudumu wa wakati wote.”
Kwa miaka kumi Michael, ambaye ni ndugu ya Jeremy alikuwa amekuwa “painia,” neno litumiwalo na Mashahidi wa Yehova kufafanua waeneza-evanjeli wao wa wakati wote. Tulipoketi tukinywa chai yetu, Jeremy alianza kufafanua mipango yake ya kujiunga na ndugu yake. “Wenzangu wote wanastahi uamuzi niliofanya,” akaeleza Jeremy. “RSPB wanapendezwa na ni wenye kujali. Wamenipa utegemezo wao kamili na hata kunipendekeza nipate tuzo la sifa la kitaifa.”
Hata hivyo, nilijua kwamba kulikuwa na uchambuzi.
Uhitaji wa Usawaziko
“Watu wengi wamekuwa wenye kutegemeza, lakini kwa kuhuzunisha, wengine yaonekana wana maoni mabaya kuhusu kazi yangu hapa,” akaeleza Jeremy. “Wanahisi kwamba ulinzi mkubwa zaidi wa hali ya kiroho ni kuwa karibu na maumbile ya asili, kutunza wanyama wa porini—kufanya kazi ya uhifadhi. Wananiambia kwamba hapa ni karibu zaidi uwezavyo kufikia paradiso, kwa hiyo kwa nini uondoke?
“Kwa wazi, kazi hiyo ina upande wa kiroho, lakini hilo halitoshani na hali ya kiroho. Hali ya kiroho ni mali ya kibinafsi, sifa ambayo huchukua wakati ili kuisitawisha. Huhusisha uhitaji wa kushirikiana na kutunza kutaniko la Kikristo, kujenga na kujengwa. Nyakati fulani nimehisi nikiwa najaribu kufanya kile Yesu alisema hatuwezi kufanya—kutumikia mabwana wawili. Sasa natambua kwamba mazingira yaliyo salama zaidi ni katikati ya kutaniko la Kikristo, na njia ya kufika huko ni kufanya upainia!”
Vipaumbele vya Utunzaji
“Usinielewe vibaya. Kutunza nikiwa mlinzi ni ono lenye kuvutia na lenye kuthawabisha, hata ingawa ni lenye kufadhaisha nyakati fulani. Kwa kielelezo, uchafuzi wa PCB na zebaki katika makao haya ni wa viwango vyenye kutia wasiwasi—na hatujui hasa ni kwa nini, ingawa twashuku ni mikunga inayouleta.c Lakini siwezi kufanya mengi ili kurekebisha usawaziko. Hakuna mtu kama mwanaikolojia stadi. Sote twapapasa-papasa, tukijifunza kadiri tuwezavyo. Twahitaji mwongozo. Ni Muumba wetu tu ajuaye jinsi tupaswavyo kuishi na kutunza dunia na unamna-namna wayo mwingi wa uhai.”
Kwa utulivu, Jeremy alitaja kifupi hisia zake: “Sikuweka maisha yangu wakfu kwa Yehova kuokoa wanyama wa pori; yeye aweza kwa ukamilifu kushughulikia hilo mwenyewe. Kupitia Ufalme wake, atahakikisha kwamba wanyama wa pori wanashughulikiwa nasi kwa wakati wote katika njia ambayo ataka. Kuhubiri habari njema za Ufalme ni lazima kuwe kipaumbele sasa ikiwa nitajiondolea mzigo wa daraka la kutunza mwanadamu mwenzangu.”
Nilikutana na Jeremy tena hivi majuzi. Ilikuwa miaka mitatu tangu tuwe na siku hiyo yenye furaha pamoja kwenye hifadhi hiyo. Sasa aishi kilometa nane kutoka Minsmere aipendayo, akipainia kwa furaha na ndugu yake. Lakini aliniambia kwamba watu fulani wanasema kwamba wangali wanaona ikiwa vigumu kumwelewa. Je, unaona hivyo? Kwa Jeremy, lilikuwa tu ni suala la vipaumbele.
[Maelezo ya Chini]
a Monel Metal ni muungano wa nikeli na shaba yenye nguvu ya mkazano wa hali ya juu, yenye kukinza ulikaji.
b Katika Marekani wachunguzaji wa ndege walio nadra hujulikana vizuri kuwa waorodheshaji.
c PCB ni polychlorinated biphenyl, taka ya viwanda.
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 17]
Hisia Nyingi Mno za Furaha
Ni mtu 1 tu kati ya watu 10 atakayeweza kumwona nightingale wanayemsikia, lakini mara mtu anapousikia, wimbo huo hauwezi kusahaulika. “Ni muziki safi, kitu kamili kilichomalizwa,” akaandika Simon Jenkins katika The Times la London. Ndege huyo mara nyingi huimba kwa kuendelea—mmoja amerekodiwa kuimba kwa muda wa saa tano na dakika 25. Ni nini kifanyacho wimbo huo uwe wa kipekee? Zoloto la nightingale laweza kutokeza aina nne tofauti za muziki kwa wakati mmoja, kutia ndani sauti kamilifu zinazolingana. Na aweza kufanya hili akiwa amefunika mdomo wake au kinywa chake kikiwa kimejaa chakula kwa ajili ya makinda yake machanga. Kwa nini huimba sana? Kwa shangwe tu, watazamaji fulani wasema. “Je, maumbile yote ya asili yana uumbaji wenye kushangaza zaidi kuliko zoloto la nightingale?” amalizia Jenkins.
[Hisani]
Roger Wilmshurst/RSPB
[Picha katika ukurasa wa 15]
Scrape
[Hisani]
Kwa hisani ya Geoff Welch
[Picha katika ukurasa wa 16]
Shakwe mwenye kichwa cheusi
[Hisani]
Kwa hisani ya Hilary na Geoff Welch
[Picha katika ukurasa wa 16]
Domo-juu
[Picha katika ukurasa wa 18]
Membe sandwichi
[Picha katika ukurasa wa 18]
Kiguuhina