Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g96 7/22 kur. 28-29
  • Kuutazama Ulimwengu

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Kuutazama Ulimwengu
  • Amkeni!—1996
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Wanawake “Wanaokosekana”
  • Silaha au Maendeleo?
  • Hatari ya Moose Wenye Kuvuka Barabara
  • Janga la Nauru
  • Maradhi ya Guinea Worm Yashindwa
  • Saa ya Siku ya Uharibifu Yasonga Mbele
  • Watoto Wanaotoka Kuzaliwa Watupwa
  • Kunywa Maji kwa Ajili ya Kiu tu Hakutoshi
  • Kaburi Maarufu la Misri Lafunguliwa
  • Moose—Kongoni Mkubwa Aliye na Sura ya Ajabu
    Amkeni!—2013
  • Ni Nani Wanaosababisha Tisho la Vita vya Nyuklia?
    Amkeni!—2004
  • Je, Tisho la Nyuklia Limekwisha?
    Amkeni!—1999
  • Kuutazama Ulimwengu
    Amkeni!—1991
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1996
g96 7/22 kur. 28-29

Kuutazama Ulimwengu

Wanawake “Wanaokosekana”

“Katika zile jamii ambazo hutendea wanawake vizuri kwa habari ya afya, kuna wanawake 106 kwa kila wanaume 100. Huo ni ukweli wa kibiolojia,” lasema The Courier, gazeti ambalo huchapishwa na Jumuiya ya Ulaya. Lakini uchunguzi mbalimbali wa UM pia wataja jambo jingine: Katika nchi za Asia kama vile China, India, Jamhuri ya Korea, na Pakistan, kwa wastani kuna wanawake 94 pekee kwa kila wanaume 100. Kwa nini? “Maendeleo ya kisayansi yamefanya iwezekane kujua jinsia ya kijusu mapema sana” nayo yamezidisha “uwiano huo usio wa kawaida ya kuzaliwa kwa wanawake na wanaume,” laeleza The Courier. Kwa kielelezo, katika Jamhuri ya Korea, katika 1982, wasichana 94 walizaliwa kwa kila wavulana 100, lakini katika 1989, uwiano huo ulipunguka hadi wasichana 88 kwa kila wavulana 100. Kichapo cha UM Our Planet chaongeza hivi: “Takwimu zashtua sana: wanawake milioni 100 wa Asia ‘wanakosekana’ kwa sababu ya kuua vitoto vya kike na kutolewa mimba kwa vijusu vya kike.”

Silaha au Maendeleo?

Dola 100 za Marekani zaweza kununua ama bunduki moja aina ya AK-47 au tembe za vitamini-A zinazotosha kuzuia upofu kwa watoto 3,000 wenye umri wa mwaka mmoja. Dola milioni 100 zaweza kununua ama baruti za kutegwa ardhini milioni kumi au dawa za chanjo za kutosha kulinda watoto milioni 7.7 dhidi ya magonjwa sita yaliyo hatari zaidi wakati wa utoto. Dola milioni 800 zaweza kununua ama ndege za kijeshi 23 aina za F-16 au chumvi ya iodini ya kudumu kwa miaka 10, ya kulinda watu bilioni 1.6 dhidi ya matatizo yatokanayo na ukosefu wa iodini mwilini, kama vile kuwa punguani. Karibu dola bilioni 2.4 zaweza kununua nyambizi moja ya nyuklia ama maji na vifaa vya afya kwa watu milioni 48. Ulimwengu unatanguliza nini? Kulingana na The State of the World’s Children 1996, mauzo ya silaha kwenye nchi zenye kuendelea katika 1994 pekee zilijumlika kuwa dola bilioni 25.4, pesa ambazo zingetumiwa kwa miradi ya maendeleo.

Hatari ya Moose Wenye Kuvuka Barabara

Kwa nini moose huvuka barabara? Swali hilo si mchezo kwa wanabiolojia wa Newfoundland wa wanyama wa pori au kwa madereva wa huko na yale maelfu ya watalii ambayo hutumia barabara kuu za mkoa huo. “Kuna aksidenti zipatazo 300 zenye kuhusu moose na magari kila mwaka kwenye barabara kuu za Newfoundland, ambazo kati yazo kadhaa zimetokeza vifo vya madereva,” lasema gazeti la habari The Globe and Mail. “Uzito ufikao kilo 450 wa moose waweza kuponda sehemu ya juu ya gari kama tu mwamba, ukiua au kulemaza.” Kupunguza tu idadi ya moose 150,000 walio katika kisiwa hicho huenda kusiwe na matokeo, asema Shane Mahoney wa Idara ya Mali za Asili, kwa sababu katika maeneo kadhaa ambapo hakuna moose wengi, kuna aksidenti nyingi mno. Kwa kuchunguza miendo ya makundi hayo, wanasayansi wanatumaini watajifunza ni kwa nini moose, ambao kwa kawaida huogopa magari, huamua kuvuka barabara.

Janga la Nauru

Nauru, ambayo ni jamhuri iliyo ndogo zaidi na iliyojitenga zaidi ulimwenguni, pindi moja ilijulikana kwa ajili ya umaridadi wayo wa kitropiki. Mabaharia wa Ulaya walioona kwa mara ya kwanza kisiwa hicho chenye kilometa 20 za mraba katika karne ya 18 walikiita Kisiwa Chenye Kupendeza. Hata hivyo, sasa ni ukanda mwembamba tu pwani ndio uwezao kukaliwa, na Nauru imekuwa “taifa lililoharibiwa zaidi kimazingira duniani,” lasema The New York Times. Kwa nini? Machimbo ya juu-juu. Kwa miaka 90 fosfati, ambayo ni tokeo la kinyesi cha ndege kwa maelfu ya miaka na vijiumbe vya maji, zimechimbwa, “zikiacha michongoko ya chokaa ya kijivu yenye hali mbaya sana, mingine ikifikia kimo cha meta 22.” Joto linalotokana na asilimia 80 ya kisiwa hicho kilichochimbwa limeathiri hali ya hewa pia, likipeleka mbali mawingu ya mvua na kutokeza ukame. Akiba za mwisho za fosfati zatarajiwa kuchimbwa kwa muda wa miaka mitano ijayo. Wanauru wengi wanahisi kwamba hakuna namna ila tu kuacha kisiwa hicho na kutumia mali zao kununua kisiwa kipya cha makao ambacho wao waweza kuhamia.

Maradhi ya Guinea Worm Yashindwa

“Baada ya ndui, guinea worm yaonekana kuwa maradhi ya pili ya kibinadamu yatakayoondolewa kabisa,” lasema The Economist. “Idadi ya visa vilivyoripotiwa, ambayo ilikuwa karibu 900,000 ulimwenguni pote juzi katika 1989, ilipunguka hadi 163,000 mwaka jana na katika nchi nyingi inapunguka kwa nusu kila mwaka.” Tofauti tu ni Sudan, “linalothibitisha kwamba vita na maradhi huandamana pamoja.” Guinea worm ni kimelea kinachoishi majini ambacho huanza kikiwa buu dogo lisiloweza kuonekana kwa macho, na tayari ameangamizwa katika Asia ya Kati, Pakistan, na nchi kadhaa za Kiafrika. Mashirika ya afya yameyadhibiti maradhi hayo kwa kutumia kemikali ya kuchuja maji, yakifundisha watu wachuje maji ya kunywa kupitia kitambaa, na kuzuia wale walioambukizwa wasioge au kutembea katika maji ya kunywewa. Mara aingiapo mwilini, guinea worm wa kiume hufa baada ya kujamiiana, nao wa kike waweza kufikia urefu wa meta moja kabla ya kuanza kutoka polepole kwa majuma kadhaa kwenye malengelenge yenye uchungu sana mguuni mwa mgonjwa, nyakati nyingi akilemeza au kuharibu misuli.

Saa ya Siku ya Uharibifu Yasonga Mbele

Ile saa maarufu ya uharibifu iliyo kwenye jalada la The Bulletin of the Atomic Scientists hivi karibuni imesogezwa mkono kwa dakika tatu kukaribia zaidi usiku-kati. Kitamathali saa hiyo huonyesha jinsi ulimwengu ulivyo karibu zaidi na vita ya nyuklia. Tangu kuanzishwa kwayo katika 1947, saa hiyo imerekebishwa mara 16 kwa mujibu wa hali za ulimwengu zinazobadilika. Wakati ambapo saa hiyo imepata kuwa karibu zaidi na usiku-kati—dakika mbili—ulikuwa 1953 baada ya mlipuko wa kwanza wa bomu la hidrojeni kufanywa na Marekani. Rekebisho la mwisho lilitokea 1991 wakati ambapo ilirudishwa nyuma hadi dakika 17 kufikia usiku-kati kwa sababu ya matumaini mazuri yaliyokuwapo baada ya Vita Baridi kwisha. Kusogeza mbele saa hiyo hadi dakika 14 kufikia usiku-kati kwaonyesha hangaiko lenye kuongezeka kuhusu uvutano wa ulimwengu, ukosefu wa usalama wa ulimwengu, na tisho la uharamia wa kinyuklia. “Ulimwengu ungali mahali hatari sana,” asema Leonard Rieser, msimamizi wa The Bulletin.

Watoto Wanaotoka Kuzaliwa Watupwa

Katika Italia mama aweza kukataa kisheria mtoto wake aliyetoka kumzaa, akiwaachia wenye mamlaka wa watoto kutafuta wenzi wa ndoa walio tayari kumwasilisha. Na katika 1995 watoto wapatao 600 walitupwa baada tu ya kuzaliwa, “wengi katika mapipa ya taka, wengine karibu na makanisa au vituo vya utumishi wa afya,” lasema gazeti la habari la Italia La Repubblica. Hali hiyo hutukia katika maeneo yenye viwanda zaidi na yenye utajiri zaidi katika nchi hiyo na vilevile katika maeneo yenye umaskini zaidi na yasiyositawi zaidi. Kulingana na Vera Slepoj, msimamizi wa Italian Society of Psychology, hilo ni “ishara ya onyo ya hisia ya kifo” ambayo imeenea katika jamii.

Kunywa Maji kwa Ajili ya Kiu tu Hakutoshi

“Mtu akitegemea kiu ndipo anywe maji, hatakunywa maji ya kutosha,” asema Dakt. Mark Davis, profesa wa fisiolojia ya mazoezi. Watu wengi wamepungukiwa maji kidogo, kwa kuwa hisia ya kiu hutokea baada ya umajimaji wa mwili kupunguka. Na kadiri watu wazidivyo kuzeeka, ndivyo wanavyozidi kutohisi kiu. Kama ilivyoripotiwa katika The New York Times, twahitaji maji zaidi wakati kuna joto au baridi sana na ukavu, tunapofanya mazoezi au tunapodhibiti ulaji wetu, na tunapokuwa na ugonjwa wowote unaoandamana na kuhara, homa, na kutapika, ambao hupoteza maji mengi mwilini. Wale wanaokula vyakula vyenye makapi mengi pia huhitaji maji mengi ili kuendelea kupeleka makapi kupitia tumbo. Ingawa matunda na mboga huwa na maji mengi, mahitaji yetu mengi zaidi hutoshelezwa kwa kunywa maji. Maji ndiyo bora zaidi kwa kuvunja kiu, kwa kuwa hayo huyeyushwa upesi mwilini. Kadiri maji yawavyo na sukari, ndivyo yachelewavyo kufyonzwa. Soda hasa yaweza kukufanya uwe mwenye kiu hata zaidi, kwa vile umaji-maji unahitajika kuyeyusha sukari. Kwa kuwa kafeini na alkoholi huelekea kutokeza mikojo mingi, kwa kutegemea vinywaji vinavyozibeba, hizo zaweza kufanya mwili upoteze maji. “Watu wazima wapaswa kunywa angalau maji gilasi nane zenye ukubwa wa desilita 2.4 kwa siku,” lasema Times.

Kaburi Maarufu la Misri Lafunguliwa

Kaburi la Nefertari katika Bonde la Malkia la Luxor, ambalo lilifungwa kwa miaka mingi, limefunguliwa kwa umma. “‘Kaburi hili ndilo lenye kuvutia sana katika ukingo wa magharibi wa Luxor, au hata katika Misri nzima,” akasema Mohammed el-Soghayer, mkuu wa idara ya Luxor ya Baraza Kuu la Vitu vya Kale. ‘Kwa wazi lilifanyizwa na wasanii hodari zaidi wakati huo wa Ramses 2 aliyejenga kaburi hilo la kifalme kwa sababu ya upendo wake mkuu kwa Nefertari. Alitaka awe na kaburi nzuri zaidi iwezekanavyo.’” Hata hivyo, hizo meta 430 za mraba zenye michoro mizuri sana karibu ziharibiwe na mafuriko, matope, na chumvi zenye kupenya. Katika 1986, baada ya miaka mingi ya kushauriana, kikundi cha kimataifa kilianza kazi ngumu ya kuunganisha vipande vya picha kwa kutumia picha zilizopigwa na mtaalamu wa vitu vya Misri ambaye ni Mwitalia Ernesto Schiaparelli, aliyegundua kaburi hilo. Hata hivyo idadi ya wageni imepunguzwa kwa sababu ya hangaiko juu ya unyevu. Nefertari pia aliheshimiwa na Ramses 2 alipoweka wakfu mojayapo mahekalu yake lililoko Abu Simbel kwake.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki