Matokeo ya Msiba
HALI huwaje unapokuwa mkimbizi? Jaribu kuwazia unaishi kwa amani, lakini kwa ghafula ulimwengu wako wabadilika. Kwa ghafula, majirani wako wawa maadui. Wanajeshi waja ambao watapora na kuchoma makao yako. Una dakika kumi kufunganya na kutoroka ili kuokoa uhai wako. Unaweza kuchukua mfuko mmoja mdogo tu, kwa kuwa utahitajika kuubeba kwa kilometa nyingi. Utaweka nini ndani yao?
Waondoka katikati ya sauti za milipuko ya risasi na mizinga. Unajiunga na wengine ambao wanatoroka pia. Siku nyingi zapita; waburuta miguu ukiwa na njaa, kiu, na ukiwa umechoka mno. Ili kusalimika, ni lazima uulazimishe mwili wako kuendelea hata ingawa umechoka. Walala chini. Watafuta chakula mashambani.
Wakaribia nchi salama, lakini walinzi wa mpakani hawakuruhusu kuvuka. Wanapekua-pekua mfuko wako na kuchukua kila kitu chenye thamani. Wapata kizuizi kingine na wavuka mpaka. Wawekwa katika kambi chafu ya wakimbizi, iliyo na ua wa seng’enge. Ingawa umezungukwa na wengine ambao wako katika hali kama yako, wahisi ukiwa peke yako na ukiwa umevurugika.
Wakosa uandamani wa familia yako na marafiki. Wajipata ukitegemea kabisa msaada kutoka nje. Hakuna kazi ya kufanya wala chochote cha kufanya. Wapigana na hisia za kuwa bure, kukata tumaini, na hasira. Wahangaika juu ya wakati wako ujao, ukijua kwamba kukaa kwako katika kambi hiyo yaelekea kutakuwa kwa muda tu. Kwa vyovyote, kambi hiyo si nyumbani—ni kama chumba cha kungojea au bohari la watu ambao hawatakikani na mtu yeyote. Wajiuliza ikiwa utarudishwa kwa lazima kule ulikotoka.
Hii ndiyo hali ya mamilioni leo. Kulingana na Tume ya Umoja wa Mataifa Inayoshughulikia Wakimbizi (UNHCR), watu milioni 27 ulimwenguni pote wamekimbia vita au mnyanyaso. Watu wengine milioni 23 wamehamishwa katika nchi zao wenyewe. Yote yakiwa yamefikiriwa, mtu 1 kati ya watu 115 duniani amelazimishwa kukimbia. Walio wengi ni wanawake na watoto. Wakiwa matokeo ya vita na taabu, wakimbizi huachwa wahurumiwe na hali katika ulimwengu huu usiowataka, ulimwengu ambao huwakataa, si kwa sababu wao ni nani, bali kwa sababu ya kile walicho.
Kuwapo kwao ni ishara ya vurugu kubwa mno ulimwenguni pote. Lataarifu UNHCR: “Wakimbizi ni dalili ya hatimaye ya mvunjiko wa kijamii. Wao ni kiunganishi cha mwisho, cha wazi zaidi, katika visababishi vingi na athari zifafanuazo kiwango cha mvunjiko wa kijamii na wa kisiasa wa nchi fulani. Wakitazamwa na watu duniani kote, wao ni ishara ya hali ya wakati huu ya ustaarabu wa kibinadamu.”
Wataalamu husema kwamba kiwango cha tatizo hilo hakina kifani na kinaongozeka bila dalili ya kwamba kitakoma. Ni nini ambacho kimeongoza kwa hali hiyo? Je, kuna suluhisho lolote? Makala zifuatazo zitachunguza maswali haya.
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 3]
Mvulana aliye kushoto: UN PHOTO 159243/J. Isaac
Picha ya U.S. Navy