Kigezo cha Jinsi ya Kuwatendea Wakimbizi
KATIKA ile Sheria ambayo Yehova Mungu alipatia taifa la Israeli, Waisraeli walikumbushwa juu ya hali yao wakiwa wakimbizi katika Misri. (Kutoka 22:21; 23:9; Kumbukumbu la Torati 10:19) Kwa hiyo waliagizwa wawatendee kwa fadhili wakazi wa kigeni waliokuwa miongoni mwao, kwa hakika kama ndugu.
Sheria ya Mungu ilitaarifu hivi: “Na mgeni [ambaye mara nyingi alikuwa mkimbizi] akikaa pamoja nawe katika nchi yako, usimdhulumu. Mgeni akaaye pamoja nawe atakuwa kama mzalia kwenu; mpende kama nafsi yako; kwa maana ninyi mlikuwa wageni katika nchi ya Misri.”—Mambo ya Walawi 19:33, 34.
Akitambua kwamba wakazi wa kigeni mara nyingi wangeweza kupatwa kwa urahisi na hatari na kwamba hawakuhisi usalama, Yehova alitoa sheria hususa kwa hali-njema yao na ulinzi. Fikiria haki zifuatazo walizopewa.
HAKI YA KUFANYIWA KESI KWA HAKI: “Mtakuwa na sheria moja tu, kwa huyo aliye mgeni, na kwa mzalia.” “Usipotoshe hukumu ya mgeni.”—Mambo ya Walawi 24:22; Kumbukumbu la Torati 24:17.
HAKI YA KUSHIRIKI SEHEMU YA KUMI: “Kila mwaka wa tatu, mwisho wake, toa fungu la kumi lote la maongeo yako ya mwaka huo, uliweke ndani ya malango yako; na Mlawi kwa kuwa hana fungu wala urithi pamoja nawe, na mgeni, na yatima, na mjane aliyefiliwa na mumewe, walio ndani ya malango yako, na waje wale na kushiba.”—Kumbukumbu la Torati 14:28, 29.
HAKI YA KUPATA MSHAHARA UFAAO: “Usimwonee mtumishi mwenye ujira aliye maskini na uhitaji, kama ni wa nduguzo, au kama ni wageni wako mmojawapo walio katika nchi yako, ndani ya malango yako.”—Kumbukumbu la Torati 24:14.
HAKI YA MUUAJI ASIYEKUSUDIA KUPATA KIMBILIO: “Miji hiyo sita itakuwa miji ya makimbilio kwa ajili ya wana wa Israeli, na kwa ajili ya mgeni, na kwa ajili ya huyo aketiye kati yao hali ya ugeni; ili kila amwuaye mtu, naye hakukusudia kumwua, apate kukimbilia huko.”—Hesabu 35:15.
HAKI YA KUSAZA: “Na mtakapovuna mavuno ya nchi yenu, usivune kabisa kabisa pembe za shamba lako, wala usiyakusanye masazo ya mavuno yako; wala usiyakusanye masazo ya mizabibu yako, wala usiyaokote matunda ya mizabibu yako yaliyopukutika; uyaache kwa ajili ya maskini na mgeni. Mimi ndimi BWANA, Mungu wenu.”—Mambo ya Walawi 19:9, 10.
Kwa hakika, Muumba wetu, Yehova Mungu, ana huruma kwa wakimbizi, naye ni lazima anafurahi tunapokuwa na huruma pia. “Mfuateni [“Iweni waigaji wa,” NW] Mungu,” akaandika mtume Mkristo Paulo, “mkaenende katika upendo.”—Waefeso 5:1, 2.
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 9]
Mvulana aliye kushoto: UN PHOTO 159243/J. Isaac