Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g96 9/22 kur. 11-13
  • Tumia Dawa kwa Hekima

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Tumia Dawa kwa Hekima
  • Amkeni!—1996
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Manufaa Dhidi ya Hatari
  • Viuavijasumu—Nguvu na Udhaifu
  • Je, Sindano Ni Bora Kuliko Tembe?
  • Dawa Bandia
  • Tatizo la Umaskini
  • Je, Wahitaji Dawa Kweli?
  • Je, Vita Dhidi ya Dawa za Kulevya Itashinda?
    Amkeni!—1999
  • Je! Dawa za Kulevya Zinaleta Maisha Bora?
    Kupata Faida Zote za Ujana Wako
  • Matumizi Mazuri na Mabaya ya Dawa za Kitiba
    Amkeni!—2009
  • Ni Nani Wanaotumia Dawa za Kulevya?
    Amkeni!—2001
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1996
g96 9/22 kur. 11-13

Tumia Dawa kwa Hekima

NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA NIGERIA

MWANAMKE huyo alilalamika kwamba alikuwa na maumivu ya kichwa na tumbo. Huyo daktari akasema naye kifupi. Kisha akamwandikia sindano za malaria za siku tatu, dawa aina ya paracetamol (acetaminophen) ya kukomesha kuumwa kichwa, dawa mbili za kutuliza kile ambacho huenda kilikuwa kidonda cha tumbo, dawa za kutuliza hangaiko lake, na mwishowe, kwa kuongezea zote hizo, vitamini za aina nyingi. Gharama ilikuwa kubwa, lakini mwanamke huyo hakupinga. Aliondoka akiwa na furaha kwamba dawa hizo zitatatua matatizo yake.

Mashauriano ya aina hiyo na daktari ni jambo la kawaida katika Afrika Magharibi. Uchunguzi mmoja uliofanywa katika taifa moja kubwa huko ulionyesha kwamba wafanyakazi wa utunzaji wa afya katika vitovu vya afya vya umma huandikia mgonjwa wastani wa dawa tofauti 3.8 kwa kila ziara. Kwa hakika, kwa watu wengi, daktari mzuri ni yule ambaye humwandikia mgonjwa dawa nyingi.

Labda uhakika wa watu wa Afrika Magharibi katika dawa unaeleweka unapofikiria jinsi hali ya afya ilivyokuwa. Zaidi ya miaka 40 iliyopita, mtungaji John Gunther aliandika kuhusu nyakati za mapema: “Pwani hii ya Watumwa . . . haikuua Waafrika tu; iliua Wazungu pia, nayo ndiyo sehemu ya Afrika ijulikanayo katika hadithi kuwa ‘Kaburi la Mzungu.’ Mfalme asiyepingwa wa Pwani ya Guinea kwa karne nyingi, alikuwa mbu. Homa ya kimanjano, homa aina ya blackwater, malaria, yalikuwa silaha zilizochaguliwa zenye kuumiza za mfalme huyo. Hali yenye kufisha ya tabia-nchi ya Pwani ya Magharibi si jambo la rekodi ya kitambo mno, lakini ni kumbukumbu lililopo. Kisa chenye kufurahisha kipendwacho sana hufafanua balozi ambaye, muda mrefu haukupita, alijipata amepewa mgawo wa kwenda Nigeria naye akauliza kuhusu malipo yake ya uzeeni. ‘Malipo ya uzeeni?’ mkuu wake katika Ofisi ya Koloni akajibu. ‘Mwenzangu mpendwa, hakuna mtu aendaye Nigeria ambaye hupata kuishi vya kutosha kuweza kustaafu.’”

Hali zimebadilika. Leo, kuna dawa za kupambana na si maradhi yaenezwayo na mbu tu bali maradhi mengineyo vilevile. Chanjo pekee zimepunguza kwa kutazamisha kiwango cha kifo kuanzia na surua, kifaduro, pepo punda, na ugonjwa wa koo. Kwa sababu ya chanjo, ndui imemalizwa. Polio pia yaweza karibuni kuwa maradhi ya wakati uliopita.

Si ajabu kwamba Waafrika wengi leo wana imani ya kina kwa thamani ya dawa. Bila shaka, imani hiyo haiko tu katika Afrika Magharibi. Katika Marekani, madaktari huandikia wagonjwa maagizo ya dawa bilioni 55 kila mwaka. Katika Ufaransa watu hununua wastani wa visanduku 50 vya tembe kila mwaka. Katika Japani mtu wa kawaida hutumia zaidi ya dola 400 (za Marekani) kwa mwaka katika dawa.

Manufaa Dhidi ya Hatari

Dawa za kisasa zimefanya mengi kusaidia wanadamu. Zinapotumiwa ifaavyo, hizo hutokeza afya nzuri, lakini zikitumiwa isivyofaa, hizo zaweza kuumiza na hata kuua. Kwa kielelezo, katika Marekani, watu 300,000 hivi hulazwa hospitalini kila mwaka kwa sababu ya athari mbaya za dawa, na 18,000 hufa.

Ili kutumia dawa kwa hekima, ni jambo la maana kutambua kwamba sikuzote kuna hatari. Dawa yoyote, hata aspirin, yaweza kutokeza athari za baadaye zenye kudhuru. Uwezekano wa athari za baadaye ni mkubwa ikiwa unameza dawa kadhaa kwa wakati uleule. Chakula na vinywaji pia huathiri jinsi dawa ifanyavyo kazi mwilini mwako na vyaweza kuongeza au kufanya kusiwe na athari.

Kuna hatari nyinginezo. Huenda ukawa na mzio kwa dawa fulani. Usipomeza dawa kama ulivyoagizwa—kiwango kifaacho kwa kipindi kifaacho cha wakati—huenda hazitakusaidia na zaweza kukudhuru. Tokeo lilo hilo laweza kukupata ikiwa daktari akuandikia dawa isiyo sahihi au dawa zisizohitajiwa. Waweza kudhuriwa pia ukimeza dawa zilizokwisha tarehe, zisizofikia kiwango kifaacho, au dawa bandia.

Ili kupunguza hatari, wapaswa kujua mambo mengi kadiri uwezavyo kuhusu dawa yoyote unayomeza. Waweza kunufaika sana kwa kujua mambo ya hakika.

Viuavijasumu—Nguvu na Udhaifu

Tangu kuanzishwa kwavyo miaka 50 hivi iliyopita, viuavijasumu vimeokoa maisha ya mamilioni ya watu. Vimeshinda maradhi yenye kufisha, kama vile, ukoma, kifua kikuu, nimonia, scarlet fever, na kaswende. Hivyo pia huchangia fungu la maana katika kuponya maambukizo mengineyo.

Dakt. Stuart Levy, profesa wa elimu ya dawa kwenye Shule ya Kitiba ya Chuo Kikuu cha Tufts katika Marekani, alisema: “[Viuavijasumu] vimebadili tiba kabisa. Ndicho kitu pekee ambacho kimebadili sana historia ya dawa.” Mtaalamu mwingine wa kitiba asema: “Hivyo ndivyo jiwe la msingi ambalo juu yalo tiba ya kisasa imejengwa.”

Hata hivyo, kabla ya kukimbia kwa daktari wako na kuomba ugavi, fikiria sehemu hasi. Viuavijasumu, vitumiwapo isivyofaa, vyaweza kudhuru sana. Hii ni kwa sababu viuavijasumu hufanya kazi kwa kushambulia na kuharibu bakteria mwilini. Lakini haviharibu bakteria zote zenye kudhuru sikuzote; aina fulani za bakteria hustahimili shambulizi hilo. Aina hizi zenye kukinza hazinusuriki tu bali huzaana na kupitishwa kutoka mtu mmoja hadi mwingine.

Kwa kielelezo, penicillin, ilikuwa yenye matokeo sana wakati mmoja katika kutibu maambukizo. Sasa, sababu moja ikiwa kwamba kuna ongezeko la bakteria zenye kukinza, makampuni ya dawa huuza mamia kadhaa ya aina za penicillin.

Waweza kufanya nini ili kuepuka matatizo? Ikiwa wahitaji viuavijasumu kikweli, hakikisha kwamba vinaagizwa na daktari aliye na sifa za ustahili na vyapatikana kutoka chanzo halali. Usimshurutishe daktari wako akuandikie viuavijasumu haraka—huenda yeye akataka ufanyiwe upimaji wa maabara ili kuhakikisha kwamba kiuavijasumu ulichoandikiwa chafaa ugonjwa wako.

Ni jambo la maana pia umeze kiwango kifaacho kwa kipindi kifaacho cha wakati. Unapaswa kumeza mfulizo wote wa viuavijasumu, hata ikiwa wahisi nafuu kabla ya hivyo kwisha.

Je, Sindano Ni Bora Kuliko Tembe?

“Nataka sindano!” Maneno haya husikiwa na wafanyakazi wengi wa afya katika nchi zinazoendelea. Msingi wa ombi hilo ni itikadi ya kwamba dawa inadungwa moja kwa moja kwenye mkondo wa damu nayo yaandaa tiba yenye nguvu zaidi kuliko tembe au vibonge. Katika nchi fulani ni jambo la kawaida kuona ‘madaktari wa kudunga sindano’ wasio na leseni wakiwa kazini.

Sindano huwa na hatari ambazo hazipatikani katika vibonge na tembe. Ikiwa sindano si safi, mgonjwa anaweza kuambukizwa mchochota wa ini, pepo punda, na hata UKIMWI. Sindano chafu yaweza pia kusababisha jipu lenye maumivu sana. Hatari zinaongezeka ikiwa sindano inadungwa na mtu asiye na ujuzi.

Ikiwa wahitaji sindano kikweli, hakikisha kwamba inadungwa na mtu ambaye anastahili kikitiba. Kwa ulinzi wako, sikuzote hakikisha kwamba sindano pamoja na sirinji hazina viini.

Dawa Bandia

Biashara ya dawa ya duniani pote ni yenye mapato sana, yenye kuleta faida ya dola bilioni 170 (za Marekani) hivi kila mwaka, kulingana na Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO). Wakiwa na hamu ya kutumia kwa faida hali hii, walaghai wametokeza dawa zilizoigizwa. Dawa za kuigizwa hufanana na dawa halisi—na ndivyo ilivyo pia na vibandiko na vifuko vyazo vya upakizi—lakini hizo ni bure.

Ingawa dawa bandia ziko kila mahali, hizo sanasana ziko katika nchi zinazoendelea, nazo huleta matokeo yenye kuhuzunisha. Katika Nigeria, watoto 109 walikufa kwa sababu ya figo kukosa kufanya kazi baada ya kumeza shira yenye kuondoa maumivu iliyokuwa na kiyeyusho cha kiwanda. Katika Mexico, wahasiriwa wa kuungua waliugua maambukizo ya ngozi yenye maumivu sana kutokana na zilizokuwa eti dawa ambazo zilikuwa na ungambao, kahawa, na vumbi. Katika Burma, wanakijiji wengi huenda waliuawa na malaria kwa sababu ya kumeza dawa ambazo hazikupambana na homa ya malaria. “Walio hatarini zaidi,” lataarifu WHO, “ni, kwa mara nyingine tena, walio maskini kabisa, ambao nyakati fulani hufikiri kwamba wamenunua kwa bei nzuri wanaponunua kile kionekanacho kuwa dawa nzuri iliyotokezwa na kampuni yenye sifa nzuri.”

Waweza kujilindaje na dawa bandia? Hakikisha kwamba unachonunua kinatoka katika chanzo chenye sifa nzuri, kama vile duka la dawa la hospitali. Usinunue kutoka kwa wauzaji wa barabarani. Muuza-dawa katika Benin City, Nigeria, aonya: “Kwa wauzaji wa barabarani, kuuza dawa ni biashara tu. Wao huuza dawa kama kwamba hizo ni peremende au biskuti. Dawa wanazouza mara nyingi zimekwisha tarehe au ni za bandia. Watu hawa hawajui chochote kuhusu dawa wanazouza.”

Tatizo la Umaskini

Matibabu ambayo mtu hupokea mara nyingi huamuliwa na kiasi cha fedha alizo nazo mtu. Ili kupunguza gharama na kuokoa wakati, watu katika nchi zinazoendelea huenda wakakosa kwenda kwa daktari na badala ya hivyo kwenda moja kwa moja katika duka la dawa kununua dawa ambazo kisheria huhitaji kuandikiwa na daktari. Kwa sababu wametumia dawa hiyo mbeleni au kwa sababu rafiki ameipendekeza, wanajua kile wanachotaka kwa ugonjwa wao. Lakini kile wanachotaka huenda kisiwe kile wanachohitaji.

Watu hujaribu kupunguza gharama kwa njia nyinginezo pia. Daktari anamfanyia mgonjwa upimaji wa maabara na kumwandikia dawa fulani. Mgonjwa huyo abeba maagizo hayo hadi kwenye duka la dawa lakini apata bei ikiwa juu. Kwa hiyo badala ya kutafuta fedha za ziada, watu mara nyingi hununua dawa ya bei ya chini au kununua baadhi tu ya dawa zilizoagizwa.

Je, Wahitaji Dawa Kweli?

Ikiwa wahitaji dawa kweli, pata kujua ile unayomeza. Usihisi aibu kumuuliza daktari au muuzaji wa dawa maswali kuhusu dawa uliyoandikiwa. Una haki ya kujua. Kwa vyovyote, ni mwili wako utakaoteseka.

Usipotumia dawa zako ifaavyo, huenda hutapata nafuu. Wahitaji kujua ni kiasi gani unachotumia, wakati wa kukitumia, na kwa muda gani. Wahitaji kujua pia ni vyakula, vinywaji, na dawa nyinginezo au utendaji gani uhitajio kuepuka unapotumia dawa. Na wahitaji kutambua athari za baadaye ziwezazo kutokea na unachopaswa kufanya zinapotokea.

Kumbuka pia kwamba dawa sizo suluhisho kwa kila tatizo la kitiba. Huenda huhitaji dawa kabisa. Gazeti World Health, kichapo cha WHO, lataarifu: “Tumia dawa wakati zihitajiwapo tu. Pumziko, chakula kizuri na kinywaji kingi mara nyingi vyatosha kumsaidia mtu kuhisi vyema.”

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 12]

“Magonjwa elfu huhitaji tiba elfu,” akaandika mshairi Mroma miaka ipatayo 2,000 iliyopita. Leo, mshairi huyo huenda angeliandika, ‘A thousand ills require a thousand pills’! Kwa kweli, yaonekana kuna kibonge kwa kila ugonjwa, halisi au wa kuwaziwa. Kulingana na Benki ya Ulimwengu, kuna aina za dawa 100,000 hivi ulimwenguni pote, zitengenezwazo kutokana na dutu amilifu zaidi ya 5,000.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 13]

Utumizi Wenye Busara wa Dawa

1. Usitumie dawa zilizokwisha tarehe.

2. Nunua kutoka chanzo chenye sifa nzuri. Usinunue kutoka kwa wauzaji wa barabarani.

3. Hakikisha unafahamu na kufuata maagizo.

4. Usitumie dawa alizoandikiwa mtu mwingine.

5. Usisisitize kudungwa sindano. Dawa za kumezwa mara nyingi hufanya kazi sawa na sindano.

6. Weka dawa mahali pasipo na joto, mbali na wawezapo kuzifikia watoto.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki