Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g96 10/8 kur. 15-18
  • Msafiri Dhaifu Lakini Hodari

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Msafiri Dhaifu Lakini Hodari
  • Amkeni!—1996
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Kito Kirembo cha Uumbaji
  • Safari Zenye Kuvutia
  • Kuhama Wakiwa Wengi
  • Sehemu Ambazo Wao Huenda
  • Safari ya Kipepeo Anayeitwa “Monarch”
    Je, Ni Kazi ya Ubuni?
  • Mfumo Unaoongoza Safari ya Kipepeo
    Amkeni!—2008
  • Hifadhi ya Asili Yageuzwa Kuwa Mahali pa Mauaji ya Kiholela ya Vipepeo-Maliki
    Amkeni!—1996
  • Siku Moja Katika Maisha ya Kipepeo
    Amkeni!—1993
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1996
g96 10/8 kur. 15-18

Msafiri Dhaifu Lakini Hodari

NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA KANADA

WACHORAJI huwachora na watunga mashairi huandika kuwahusu. Aina nyingi huishi katika misitu ya mvua ya kitropiki. Wengi huishi kwenye misitu, mashambani, na katika nyanda. Wengine hustahimili baridi za vilele vya milima; wengine, hustahimili joto la majangwa. Wamefafanuliwa kuwa mojawapo wadudu maridadi zaidi.

BILA shaka unafahamu kiumbe hiki maridadi chenye madaha—kipepeo. Hata hivyo, aina moja ya kipepeo, imepata umashuhuri ulimwenguni pote kwa sababu ya uwezo wayo wa kusafiri. Msafiri huyu dhaifu lakini hodari ni kipepeo-maliki. Ebu tuone kwa ukaribu zaidi kito hiki cha uumbaji na safari zake za uhamaji zenye kushangaza sana.

Kito Kirembo cha Uumbaji

Jiwazie ukiwa katika konde katika siku ya jua yenye joto-joto. Kazia macho vipepeo hao wa ajabu wakiruka hapa na pale miongoni mwa maua ya mwituni, daima wakitafuta chakula na kinywaji. Simama tuli ukiwa umenyoosha mikono yako. Mmoja yuaja karibu. Aha, yuataka kutua kwenye mkono wako! Tazama jinsi anavyotua kwa uanana.

Sasa mchunguze kwa ukaribu zaidi. Tazama jozi mbili za mabawa yake mepesi yenye poda-poda yaliyo na rangi ya machungwa, na ambayo yana mishipa myeusi na kingo nyeusi na madoa-doa meupe. Imesemwa kwamba kipepeo-maliki alipata jina layo kutokana na masetla Wazungu katika Amerika ambao walimhusianisha na maliki wao, William of Orange. Hakika, kipepeo huyu ni “maliki.” Lakini mrembo huyu dhaifu, mwenye uzani wa nusu gramu tu na mabawa yanayoenea kwa sentimeta nane hadi kumi, aweza kusafiri safari ndefu zenye magumu.

Safari Zenye Kuvutia

Ingawa baadhi ya vipepeo husemwa kwamba huhamia mbali zaidi kipupwe kianzapo, ni kipepeo-maliki pekee ambaye hufunga safari ndefu wakijua kihususa wanakoenda na kusafiri kwa wingi sana. Uhamaji wa kipepeo-maliki kwa kweli ni ajabu ya kipepeo. Ebu fikiria baadhi ya matimizo yenye kuvutia ya wasafiri hawa hodari.

Safari zao za kutoka Kanada wakati wa vuli na kwenda makao yao ya kipupwe katika California au Mexico ni zaidi ya kilometa 3,200. Wao huvuka maziwa makubwa, mito, nyanda, na milima. Mamilioni kati yao humaliza kwa mafanikio uhamaji wao wa kwenda juu katika milima ya Sierra Madre katika Mexico ya kati.

Safari kama hizo hushangaza hata zaidi unapokumbuka kwamba vipepeo hao wachanga hawajapata kamwe kufunga safari hizo wala hawajapata kuona makao yao ya kipupwe. Lakini bila kukosea wao huhisi njia wanayopaswa kwenda na kujua wakati ambapo wamefika kwenye makao yao ya kipupwe. Wanafauluje?

Gazeti Canadian Geographic lataarifu: “Kwa wazi, kuna programu fulani ya kijeni yenye kutatanisha sana katika bongo zao ndogo za hali ya chini, labda njia fulani za kusoma mkao wa miale ya jua, kama ambavyo nyuki hufanya, au kusoma uga sumaku wa dunia, ambao yaonekana huongoza ndege. Uwezo wa kutambua halijoto na unyevu hususa waweza kuwasaidia wafikapo mwisho wa safari yao. Lakini kufikia sasa sayansi imeshindwa kupata majibu.” Kama ilivyo na viumbe vilivyotajwa katika kitabu cha Biblia cha Mithali, “vina akili nyingi.”—Mithali 30:24.

Vipepeo-maliki ni warukaji stadi. Wao huenda kwa karibu kilometa 12 kwa saa, kupaa kwa karibu kilometa 18 kwa saa, na—kama ambavyo kila mtu ambaye amejaribu kuwashika ajuavyo—wao huruka ghafula kwa kasi zaidi, kwa karibu kilometa 35 kwa saa. Wao wanajua sana kutumia pepo—hata wakiruka dhidi ya pepo za kawaida zinazoelekea mashariki zenye kuwakabili ili waendelee kuelekea kusini-magharibi wanakoenda. Wakitumia njia zenye kutatanisha za kuruka, wao hukabiliana na mabadiliko-badiliko ya mwendo wa upepo na njia unaoelekea. Kama ambavyo tu waendesha ndege zisizo na injini na mwewe hufanya, wao hupaa kwenye hewa yenye joto inayotoka chini. Kulingana na chanzo kimoja cha habari, kipepeo-maliki husafiri umbali ufikao kilometa 200 kwa siku. Wao huruka wakati wa mchana tu. Usiku wao hupumzika, mara nyingi mahali palepale kila mwaka.

Mwanasayansi wa Chuo Kikuu cha Toronto David Gibo amegundua kwamba kipepeo-maliki hufanya zaidi ya kupaa na kwenda tu hewani. Yeye aripoti hivi: “Ni lazima vipepeo hawa watumie upepo katika njia ninayofikiri ni zenye werevu zaidi kuliko wanavyofanya bata bukini wanaohama.” Kule kupiga-piga kwa mabawa, kupaa, na kujilisha huruhusu vipepeo-maliki kufika Mexico wakiwa na mafuta ya kuwatosha kupitisha kipupwe na kuanza safari yao ya kurudi kaskazini katika masika. Profesa Gibo asema pia: “Ni kwa kuenda na upepo kunakofanya watimize safari yao ndefu na kufika wakiwa wenye nguvu na wenye afya nzuri.”

Kuhama Wakiwa Wengi

Imejulikana kwa muda mrefu kwamba vipepeo-maliki walio magharibi ya Milima ya Rocky huhama kusini na kupitisha kipupwe katika California. Wao waweza kuonekana wakiwa wamening’inia makundi-makundi katika misunobari na miti ya eucalyptus katika sehemu fulani kando-kando za pwani ya kusini ya California. Lakini mahali idadi kubwa za kipepeo-maliki walio kaskazini mwa Kanada zilipokuwa zikienda hapakujulikana kwa muda fulani.

Fumbo hilo lilifumbuliwa 1976. Makao yao ya kipupwe yaligunduliwa hatimaye—kilele chenye msitu katika milima Sierra Madre ya Mexico. Mamilioni na mamilioni ya vipepeo yalipatikana yakiwa yamejaza kabisa matawi na mashina ya miti fir yenye rangi ya kijani-kijivu. Mwono huo wenye kuvutia huendelea kuwa kivutio chenye kupendeza wageni.

Mojayapo mahali pazuri zaidi katika Kanada pa kuona kipepeo-maliki kwa wingi ni katika Hifadhi ya Kitaifa ya Point Pelee, Ontario, ambako wao hujikusanya kwa wingi katika matayarisho ya kuhama kusini. Katika mwisho-mwisho wa kiangazi wao hujikusanya katika mahali pa kusini zaidi pa Kanada, wakingoja kwenye ukingo wa kaskazini wa Ziwa Erie mpaka pepo na halijoto ziwafae kabla ya kuanza safari yao ya kusini kuelekea makao yao ya kipupwe katika Mexico.

Sehemu Ambazo Wao Huenda

Wakianza safari Point Pelee, wao husafiri kisiwa hadi kisiwa wakivuka Ziwa Erie ili kuanza safari ndefu kuvuka bara la Marekani. Wakiwa njiani, vikundi vingine vya kipepeo-maliki hujiunga nao katika uhamaji. Juu sana kwenye milima katika kaskazini-magharibi mwa Mexico City, vipepeo wakadiriwao kuwa milioni mia moja hujikusanya ili kupitisha kipupwe.

Uhamaji mwingine hupitia Florida na kuvuka Karibea, nao huenda mahali ambapo hapajajulikana katika Peninsula ya Yucatán au katika Guatemala. Wawe katika Mexico au katika himaya nyinginezo za kipupwe, kipepeo-maliki hujikusanya katika vikundi vidogo-vidogo zaidi katika misitu ya milima.

Mtu aweza kufikiri kwamba safari yao ndefu ya kwenda kwenye makao yao ya kipupwe ingewapeleka kwenye nchi ya likizo yenye nyanda zenye joto-joto na jua. Lakini sivyo. Katika milima ya Transvolcanic Range ya Mexico, ambako wao huenda, kuna baridi. Hata hivyo, tabia ya nchi iliyoko kwenye vilele vya milima inawafaa kabisa wakati wa kipupwe. Ni baridi vya kutosha kuwafanya kutumia wakati katika hali ya karibu kutotenda—hivyo wakirefusha maisha zao kwa miezi minane hadi kumi, jambo linalowaruhusu kwenda Mexico, kupitisha kipupwe huko, na kuanza tena safari. Unaweza kusema ni likizo ya aina fulani.

Masika hufika, na kipepeo-maliki huwa watendaji tena. Siku ziwavyo ndefu zaidi, hao vipepeo huruka-ruka kwenye jua, wao huanza kujamiiana, na kuanza safari yao ya kurudi kaskazini. Inafikiriwa kwamba wengine waweza kumaliza safari yote ya kurudi, lakini kwa kawaida ni wazao ndio hufika katika milima ya Kanada na kaskazini mwa Marekani wakati wa kiangazi. Vizazi vitatu au vinne vya mayai, mabuu, pupa, na vipepeo hurudi polepole kuvuka kontinenti. Kipepeo wa kike—akiwa amejaza mayai mia moja au zaidi yaliyotungishwa—huruka-ruka kwenye maua ya mwituni na kutaga mayai moja-moja katika upande wa chini wa majani machanga ya milkweed. Na hivyo duru hiyo huendelea na kuendelea, na safari ya kipepeo-maliki ya kurudi makao ya kiangazi huendelea.

Kwa kweli kipepeo-maliki ni kiumbe chenye kushangaza. Ni pendeleo kama nini kwa wanadamu kuweza kuchunguza na kusoma utendaji wake. Hata hivyo, si ajabu kwamba makao ya kipepeo-maliki ya wakati wa kipupwe ambayo yalikuwa siri kwa muda mrefu katika Mexico, na vilevile makao mengine katika California yanatishwa na utendaji wa binadamu. Kudhani kwamba warembo hawa dhaifu wana mahali pengine pa kwenda kwaweza kufanya watokomee. Ni jambo la kupongezwa kwamba, jitihada zinafanywa za kuwalinda wasitokomee. Litakuwa jambo tukufu kama nini wakati ambapo katika dunia iliyo Paradiso iliyoahidiwa na Muumba ambayo sasa iko karibu, wasafiri hao dhaifu lakini hodari watahakikishiwa mahali salama!

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 15]

Kipepeo: Parks Canada/J. N. Flynn

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 17]

Ukurasa 16 juu na chini: Parks Canada/J. N. Flynn; katikati: Parks Canada/D. A. Wilkes; ukurasa 17 juu: Parks Canada/J. N. Flynn; katikati na chini: Parks Canada/J. R. Graham

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki