Brolga, Kasowari, Emu, na Jabiru—Baadhi ya Ndege Wenye Kutazamisha wa Australia
Na mleta-habari wa Amkeni! katika Australia
AKIWA na kucha zenye kutisha, kasowari asiyeweza kupuruka, mwenye kufafanuliwa kuwa ndege hatari kuliko wote ulimwenguni, aweza kuruka, kupiga teke, na kurarua, kwa nguvu zenye kushangaza. Akiwa na sifa kama hizo, na mwenye kujihami vivyohivyo, binamu yake emu hahitaji mabawa—yeye hukimbia kama upepo. Katika dansi, brolga hutangaza akili nyingi za Muumba na Mpangaji-Dansi wake. Na mwenye kupita hapo karibu, mrefu na mwembamba, jabiru ni kielelezo cha adhama na usawaziko wa kindege. Tai mwenye mkia wenye umbo la kabari, awe anapuruka au analinda windo aliloua, huonyesha ishara za mwindaji kamili wa hewani. Ndiyo, kila mmoja wa ndege hawa wenye fahari kwa kweli ni ajabu ya uumbaji. Basi, kwa furaha twawajulisha . . .
Kasowari Mwenye Rangi Nyingi —Mfadhili wa Msitu wa Mvua
Akiwa na uzani wa kilogramu kati ya 30 na 60, kasowari wa kusini, au mwenye dehedehe mbili, wa misitu ya mvua yenye kusitawi sana ya kaskazini-mashariki mwa Australia na wa New Guinea ni ndege mwenye kuvutia lakini mpweke. Akiwa mwenye kimo cha meta mbili hivi, wa kike ni mkubwa kuliko wa kiume na—jambo lisilo kawaida kwa ndege—ni mwenye rangi nyingi kidogo kuliko wa kiume, ambaye mbali na msimu wa kujamiiana kwa hekima hukaa mbali naye. Baada ya kujamiiana, jike hutaga kikundi cha mayai yenye rangi ya kijani chenye kung’aa, lakini kisha huenda zake, akimwacha dume kuyaatamia na kutunza makinda. Kisha ajamiiana na madume wengine na kuacha kila mmoja wao akiwa na kikundi cha mayai ya kutunza!
Hata hivyo, kukatwa kwa misitu kunawadhuru kasowari. Katika jaribio la kuongeza idadi yao, Hifadhi ya Billabong karibu na Townsville, Queensland, imeanzisha programu ya uzalishaji wa utekwani inayonuia kuwaachilia ndege warudi porini wanapokuwa wenye umri wa kutosha. Ingawa hula wanyama na mimea, kasowari hasa hula matunda, ambayo huyameza yakiwa mazima. Hivyo, mbegu za zaidi ya spishi mia za mimea husafiri bila kumeng’enywa kupitia utumbo na kusambazwa sana kotekote msituni katika mbolea yenye lishe. Hilo, wasema wataalamu wa hifadhi hiyo, laweza kumfanya kasowari awe spishi yenye kutegemewa, katika maana ya kwamba akitoweka spishi nyingi za mimea zitatoweka. Lakini je, ndege huyu ni hatari kwa wanadamu?
Ni hatari kwa watu wapumbavu tu ambao hukaribia sana. Kihalisi, wanadamu ndio tisho kubwa zaidi kwa kasowari kuliko vile yeye amepata kuwa tisho kwao. Katika vivuli vyenye giza-giza vya msitu wa mvua, ndege huyo atanguruma kwa kina kutoka kooni ili kukuonya kwamba yuko karibu. Kubali onyo; usiende karibu zaidi. Yaelekea sana, atatoka kwa kishindo kupitia kichaka, akitumia dirii yake ngumu ili kulinda kichwa chake. Lakini anapozuiwa kwenye pembe fulani, au kuumizwa au anapolinda mtoto wake, aweza kushambulia ukisonga karibu sana.
Emu—Mhamaji na Mfano wa Kitaifa
Akiwa na uhusiano wa karibu zaidi na mrefu kidogo kuliko kasowari, emu apatikana katika sehemu nyingi za mashambani za Australia. Kati ya ndege wote, ni mbuni tu aliye mkubwa kuliko emu. Emu mwenye kushtuliwa kwa urahisi ana miguu mirefu iwezayo kutokeza mbio za ghafula za kasi ya kilometa 50 hivi kwa saa, na kama kasowari, kila mguu una kucha tatu zenye kufisha. Hata hivyo, tofauti na binamu yake mwenye kuzingatia mipaka, emu ni mzururaji mwenye kuhama-hama na ni nadra sana yeye kuwa mkali. Yeye hula karibu kila kitu—tokonyasi, kabeji, hata buti za zamani! Baada ya emu jike kutaga mayai yake yenye rangi ya kijani kilichokolea—kwa kawaida yakiwa 7 hadi 10, lakini nyakati fulani yakifikia hadi 20—yeye, kama vile kasowari, hupatia dume kazi ya kuyaatamia na kutunza makinda.
Kukutana na masetla Wanaulaya kulimsababishia emu magumu. Haraka masetla walimmaliza kabisa katika Tasmania. Na barani kupenda kwake ngano kulimfanya aonekane kuwa mnyama-msumbufu na kumfanya kuwa mhasiriwa wa wawindaji wa kulipwa. Hata hivyo, licha ya machinjo yasiyozuiwa, idadi ya emu ilizidi kupata nafuu kwa kutazamisha, ilifanya hivyo sana hivi kwamba katika Australia Magharibi tangazo la waziwazi la vita lilifanywa dhidi ya huyo ndege katika 1932. Serikali ilileta wanajeshi na bunduki ya kumimina risasi aina ya Lewis yenye kuwekelewa juu ya ndege! Hata ingawa hajulikani sana kwa kuwa na akili, emu alishinda pigano hilo. “Vita” hiyo ilikuwa dhihaka ya umma na aibu ya kisiasa; walitumia mifyatuo elfu kumi, lakini wakauwa mamia machache ya ndege. Lakini katika vita iliyofuata ya kudhoofisha daima—emu dhidi ya mashambulizi mawili ya wenye kuwinda ndege hao kwa kulipwa na risasi ambazo serikali ilipatia wakulima bila malipo—emu hawakuweza kustahimili zaidi ya hapo.
Hata hivyo, siku hizi, emu ni ishara ya kitaifa. Yeye husimama kwa fahari akielekeana na kangaruu kwenye kirauni cha Australia naye huzurura vichakani akiwa salama. Ukame ndio adui yake mbaya zaidi. Emu hata wanazalishwa na kutunzwa kimajaribio kwa ajili ya bidhaa nyingi: nyama isiyo na shahamu kabisa; ngozi imara, yenye kudumu; manyoya; na mafuta, ambayo hupatikana katika tishu teketeke ya shahamu iliyo kwenye kifua cha ndege huyo. Hifadhi hii iliyo mahali maalum ndiyo sababu mnofu wake hauna shahamu yoyote.
Je, Unapenda Kucheza Dansi?
Labda sivyo, lakini kwa hakika brolga wanataka. Kwenye “vyumba [vyao] vya kuchezea dansi” kandokando ya maji “idadi yoyote [ya korongo hawa wa kijivu], kuanzia jozi moja ya ndege hadi dazani hivi,” chasema kitabu The Waterbirds of Australia, “watajipanga wakikabiliana na kuanza kucheza dansi. Wataruka-ruka mbele na miguu yao iliyo kama milonjo mabawa yao yakiwa yamefunuliwa nusu na yakitikisika. Wakiinamisha na kuinua-inua vichwa vyao, wao husonga mbele na kurudi nyuma, wakilia kama kwamba wana maji kooni na kupiga filimbi kwa wanana. Pindi kwa pindi ndege mmoja atasimama na, akirusha kichwa chake nyuma, atapiga tarumbeta sana. Ndege hao waweza kuruka futi kadhaa hewani na kushuka ardhini wakiwa wametandaza mabawa yao meusi na kijivu. Vipande vya vitawi au nyasi hutupwa huku na huku na Brolga wanajaribu kuvishika vipande hivyo au kuvidunga kwa midomo yao vinapokuwa vikianguka.” Ni wonyesho wenye kuchochea, hasa ukifikiria ukubwa wa ndege hao, ambao wana kimo cha zaidi ya meta moja na walio na urefu wa mabawa wa meta mbili!
Ingawa spishi nyingi za ndege hufanya maonyesho yenye kuvutia sana ya kutafuta uchumba wakati wa msimu wa uzazi, brolga, mmojawapo korongo wakubwa zaidi, hupenda kucheza wakati wowote mwakani. Kwa hakika, jina lake latokana na kisakale cha Kiaborijini cha mcheza-dansi wa kike aliyejulikana sana aitwaye Buralga. Yeye alikataa uangalifu alioelekezewa na mchawi mwovu. Naye, kwa kuitikia, alimgeuza kuwa korongo mwenye madaha.
Jabiru—Koikoi Pekee wa Australia
Akiwa ndege wa mabwawa, jabiru, au koikoi mwenye shingo nyeusi, huzuru mara nyingi pwani zenye joto na unyevu za kaskazini na mashariki mwa Australia. (Jabiru wa Amerika Kusini ni spishi tofauti ya koikoi.) Akiwa mwembamba, mwenye kimo cha sentimeta 130, mwenye rangi yenye kupendeza, jabiru huonekana kwa urahisi miongoni mwa mamiriadi ya ndege wengineo wa mabwawa. Atembeapo katika maji yasiyo na kina kirefu, yeye atapiga kwa ghafula mdomo wake mrefu na wenye nguvu kuingia majini kwa nguvu nyingi sana hivi kwamba atahitaji kutikisa mabawa yake yafunguke kidogo ili kukabiliana na kani hiyo.
Na mabawa hayo ni yenye uweza kama nini! Akipanua mabawa yake kwa meta mbili kuanzia ncha moja hadi nyingine, akiwa na manyoya makuu yakiwa yameenea kama vidole, jabiru hupuruka kwa kuelea polepole kimviringo hadi aonekana akiwa kama kisalaba kidogo angani. Kwa kweli, jabiru akiwa hewani, akiwa na mabawa yake marefu, shingo ndefu na miguu mirefu akitokeza umbo jeusi dhidi ya jua kubwa jekundu la kiikweta lenye kutua, ni mfano unaothaminiwa sana wa mabwawa ya kaskazini mwa Australia.
Tai Mwenye Mkia Wenye Umbo la Kabari—Mfalme wa Anga
Umbali mfupi kutoka kilele chenye miamba cha mlima fulani katika Victoria, na kukabili upepo mwingi wenye nguvu ambao ulifukuza ndege wale wengine wote kutoka angani, tai mwenye mkia wenye umbo la kabari alikuwa akicheza hewani. Mwandikaji David Hollands alishuhudia wonyesho wa ustadi wa michezo ya hewani ambao huenda hangepata kuuona kamwe: “Tai huyo alijiangika juu kule,” yeye aandika, “bila kusonga na akiwa starehe kabisa katika mahali hapo penye msukosuko. . . . Nilipokuwa nikitazama, aliruka chini, akifumba mabawa yake ili ajitose wima. Aliteremka kwa meta mia moja kisha mabawa yakafunuka kidogo sana, hilo likimrusha kuelekea juu ili kufikia kimo ambacho alikuwa amepoteza wakati wa kuruka chini. . . . Alijisawazisha kwa kubiringika nusu, kisha akapuruka juu zaidi [na] kurudia mruko wa chini tena na tena, akipita mbio sana kwa kutazamisha kuingia kwenye sakafu ya bonde na kupanda juu tena katika wonyesho uliodumishwa wenye kufurahisha.”
Akiwa na upana wa mabawa wa meta 2.5 na mkia wenye umbo la kabari, haiwezekani kukosa kumtofautisha mfalme huyo mwenye madaha na nguvu na ndege mwingine yeyote katika anga za Australia. Kucha zake zaweza kubana kwa kani ya tani tatu! Hata hivyo, kwa kipindi fulani cha wakati, njia “ifaayo” tu ambayo watu walimwona tai mwenye mkia wenye umbo la kabari ilikuwa kupitia mtutu wa bunduki wakati walipomwinda. Sawa na binamu yake furukombe wa Marekani, ambaye alipigwa risasi bila huruma ili kulinda samaki aina ya salmoni na biashara za manyoya, tai huyu wa Australia alinyanyaswa kwa kuua kondoo mara kwa mara. “Ni ndege wengine wachache wawindaji ulimwenguni,” chasema kitabu Birds of Prey, “ambao wamenyanyaswa vibaya sana kama vile Tai mwenye mkia wenye umbo la Kabari . . . Kwa karibu miaka 100 alionwa kuwa mwindaji . . . , na fedha zililipwa kwa wale walioonyesha uthibitisho kwamba walimuua.”
Hata hivyo, baada ya miaka mingi, mashtaka hayo yaliondolewa. Mlo wake mkuu ulithibitika kuwa sungura wa mwituni na pindi kwa pindi wanyama wenyeji, kutia ndani walabi walio na karibu uzito mara mbili wa uzito wa ndege huyo. Ufunuo huo, hatimaye, ulimpa tai huyo urafiki pamoja na mwanadamu na vilevile ulinzi wa kisheria.
Ndiyo, ndege ni sehemu tata sana na yenye kuvutia kama nini ya ikolojia iliyo tata ya dunia! Huenda tukajifunza hilo hatimaye, lakini hekima huja kuchelewa mno—baada ya pupa na kutojua mambo kusababisha madhara. Lakini inafariji kama nini kujua kwamba tukikaza uangalifu, hata sasa, masikio yetu yaweza kufurahia, milio kama ya maji kooni, mlio mwembamba mkali, mbinja, mlio kama wa bata bukini, mlio wa filimbi, mlio kama wa bata, na kilio cha ghafula kikali katika anga, misitu, na mabwawa ya sayari hii yenye kuvutia!
[Picha katika ukurasa wa 16]
Kasowari
Brolga
[Hisani]
Kushoto na chini: Australian Tourist Commission (ATC); juu katikati na kulia: Billabong Sanctuary, Townsville, Australia
[Picha katika ukurasa wa 17]
Tai
Emu
Jabiru
[Hisani]
Makinda ya tai na kichwa cha emu: Graham Robertson/NSW National Parks and Wildlife Service, Australia; tai mwenye kuruka: NSW National Parks and Wildlife Service, Australia; emu na mtoto na jabiru: Australian Tourist Commission (ATC)
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 15]
Kushoto: Graham Robertson/NSW National Parks and Wildlife Service, Australia; kulia: Australian Tourist Commission (ATC); juu: Billabong Sanctuary, Townsville, Australia