Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g96 11/8 kur. 22-25
  • Picha ya Mtu—Jinsi ya Kuipiga Vizuri

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Picha ya Mtu—Jinsi ya Kuipiga Vizuri
  • Amkeni!—1996
  • Habari Zinazolingana
  • Jinsi Upigaji-Picha Ulivyoanza
    Amkeni!—2006
  • Kuboresha Ustadi Wetu Katika Huduma​—Kuhubiri Katika Maeneo Yenye Ulinzi Mkali
    Daftari la Mkutano wa Huduma na Maisha Yetu ya Kikristo—2020
  • Je, “Ukristo” Wenye Kubadilika-Badilika-Unakubaliwa na Mungu?
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2000
  • Je, umepata kuona mmweko wa kijani?
    Amkeni!—1996
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1996
g96 11/8 kur. 22-25

Picha ya Mtu—Jinsi ya Kuipiga Vizuri

Ni vitu vichache vinavyothaminiwa kuliko picha za marafiki na washiriki wa familia. Kwa vyovyote, picha nzuri ya mtu ni zaidi ya kuwa picha tu; ni picha ambayo imekusudiwa kunasa utu kamili wa mtu!

Tatizo ni kwamba picha za kitaalamu huelekea kuwa ghali—zisiweze kugharimiwa na baadhi yetu. Na unapojaribu kupiga picha ya mtu, upesi unagundua kwamba kuna mengi zaidi yanayohusika kuliko tu kulenga kamera na kupiga. Hii ni kwa sababu picha nzuri ya mtu haitii ndani mwenye kupigwa picha peke yake bali pia inahusisha nuru, mandhari-nyuma, mahali alipo, mkao, mambo yaonyeshwayo na uso, na rangi.

Hata hivyo, ukiwa na kamera na uko tayari kujifunza mbinu chache za msingi, unaweza kupiga picha nzuri za watu. Kwa njia gani? Ili kujibu, tutauliza maswali fulani ya mtaalamu wa kupiga picha ambaye ana uzoefu wa kazi hiyo kwa zaidi ya miaka kumi.

• Kwanza kabisa, ni njia gani iliyo bora zaidi ya kufanya mtu atabasamu unapompiga picha? Hakikisha kwamba mtu huyo yuko katika hali ya kupigwa picha! Kwa kielelezo, tuseme unataka kupiga picha ya msichana mdogo. Ikiwa amechoka au ana njaa, itakuwa vigumu kumpiga picha vizuri. Isitoshe, uchovu utatokeza mkazo kwenye uso wake na macho yake, jambo ambalo litaharibu picha. Basi mtie moyo alale kidogo na kula chakula chepesi kabla ya kuanza kumpiga picha.

Pia inasaidia kuongea na mtu huyo. Uwe mwenye furaha na mchangamfu. Mtulize kwa kuzungumza naye, lakini usijaribu kumfanya aangue kicheko. Kufanya hivyo hufanya macho yajifunge kidogo na hilo huleta damu kwenye uso. Jaribu kupiga picha maonyesho mbalimbali ya uso. Kadiri upigavyo picha nyingi, ndivyo uongezekavyo uwezekano wako wa kupata sura nzuri zaidi ambayo mtu huyo huonyesha.

• Vipi kuhusu mavazi na mapambo? Katika picha za vikundi, ni vizuri rangi zipatane. Kwa kielelezo, ikiwa unapiga picha familia, dokeza kwamba wavalie mavazi yenye rangi zinazopatana. Au labda wote wavalie mavazi ya rangi moja. Lakini, kumbuka kwamba watu wanene huonekana vizuri zaidi katika mavazi ya rangi nyeusi-nyeusi na kwamba watu wembamba huonekana vizuri zaidi kwa mavazi ya rangi nyangavu.

Ni lazima pia utoe uangalifu kwa mambo madogo-madogo: Je, mavazi yamenyooka, yakiwa na mikunjo michache tu? Je, tai imenyooka? Je, nywele ni nadhifu? Huenda macho yako yasione nywele zilizoenda kombo, lakini picha itaonyesha! Ikiwa mwenye kupigwa picha ni mwanamke, je, amejipaka virembeshi kwa njia ifaayo?

• Namna gani watu ambao huvaa miwani? Kwa sababu ya mng’ao, hilo laweza kuwa tatizo. Kwanza tazama kupitia tundu la kutazamia kuona ikiwa kuna mng’ao usiotakikana. Ikiwa hivyo, mfanye yule anayepigwa picha ageuze kichwa polepole mpaka mng’ao huo uondoke katikati ya macho au upotee. Nyakati nyingine, kumfanya huyo mtu arudishe kidevu chini kutasaidia—lakini uwe mwangalifu usitokeze videvu viwili!

• Je, haidhuru ni nini kipo katika mandhari-nyuma? Ni jambo muhimu kabisa! Mandhari-nyuma iliyojaa nyaya za umeme, barabara, au magari itaharibu tu picha yako. Basi tafuta mandhari-nyuma ambayo yaweza kuboresha au kufanya yule unayempiga picha apendeze zaidi, kama vile mti, kichaka chenye kuchanua maua, ua wa mbao, au hata kando ya ghala ya zamani.

• Namna gani ikiwa unapiga picha ndani ya nyumba? Unaweza kujaribu kumketisha huyo unayempiga picha kwenye kiti au sofa mbele ya ukuta wenye rangi nyangavu au mbele ya mmea wa ndani ya nyumba. Inapendeza hasa kuonyesha mtu akiwa kazini au akiwa anajihusisha na hobi yake au utendaji wake apendao zaidi, kukiwa na benchi ya kazi, dawati, au vifaa vya kushona katika mandhari-nyuma.

• Namna gani ikiwa huwezi kupata mandhari-nyuma yenye kuvutia? Jaribu kufanya mandhari-nyuma isiwe wazi kwenye picha. Hiyo hufaulu zaidi katika picha za nje ambazo unaweza kumweka yule unayempiga picha umbali fulani kutoka kwenye mandhari-nyuma. Unafanya hivyo kwa kurekebisha f-stop, au ukubwa wa shimo la lenzi. Nambari ya chini ya f-stop, kama vile f5.6, itafanya mtu unayempiga picha aonekana vizuri lakini mandhari-nyuma isionekane vizuri.—Ona picha 1.

• Je, kuna madokezo yoyote juu ya mfanyizo? Kwanza kabisa, husaidia kuweka kamera yako kwenye kiweko chenye miguu mitatu; kisha unaweza kukazia akili zaidi mfanyizo wa picha. Kwa kawaida, picha huwa za mwili wote, robo-tatu (tokea kiuno kuelekea juu), au za juu (kichwa na mabega au kichwa pekee). (Ona picha 2.) Lenzi yoyote kati ya milimeta 105 na milimeta 150 itafaa sana picha za watu. Ikiwa huwezi kurekebisha au kubadili lenzi ya kamera yako, jaribu kusonga karibu na mwenye kupigwa picha au kurudi nyuma mpaka upate picha unayotaka. Na kwa kutaja tu, ni jambo la akili kupiga picha kwa njia ya kuacha nafasi fulani juu ya kichwa, kandokando, na chini ya miguu. Kwa kufanya hivyo unaepuka kukata kichwa, miguu, au mwili ikiwa utataka picha hiyo ipanuliwe. Waona, kadiri unavyopanua, ndivyo na picha iwezavyo kupotea wakati wa kupanuliwa, kwa kutegemea ukubwa wa fremu ya picha.

Mwongozo mmoja wenye mafaa ni kile kiitwacho sheria ya thuluthi. Huo wahusisha kutia mwenye kupigwa picha thuluthi moja kutoka juu, chini, au kandokando ya picha. (Ona picha 3.) Hata hivyo, nyakati nyingine kuweka macho katikati ya picha hufaulu.

• Namna gani kumwekea mwenye kupigwa picha kikao? Mfanye mwenye kupigwa picha aangalie kamera akiwa ametulia, ama akiwa ameketi, amesimama, ama akiwa ameegama, lakini akiwa amegeuka kidogo upande. Uso ukionekana ukiwa mviringo zaidi, mfanye huyo ageuze kichwa au mwili kidogo ili sehemu nusu ya uso pekee iwe kwenye nuru. Ile sehemu nyingine ambayo imesitiriwa yapaswa kuwa karibu zaidi na kamera. Hilo litafanya uso kuwa mwembamba zaidi. Kwa upande mwingine, ukitaka uso uonekane umenenepa, mfanye mtu huyo ageuze kichwa au mwili mpaka uso wote uwe katika nuru.

Toa uangalifu wa pekee kwa mikono. Hiyo inapaswa kuonekana imetulia nayo yapaswa kuwa katika hali ya kawaida ya mwenye kupigwa picha, kama vile ikiwa imetulia kwa wanana kwenye shavu au kando ya uso. Ikiwa mtu huyo amesimama, epuka lile kosa lililo kawaida sana la kuacha mikono ining’inie kando ikielekea chini. Ni afadhali kufanya mikono ishike kitu au ipumzike kwa njia ya kawaida.

• Je, kuna madokezo yoyote ya kupiga picha wenzi wa ndoa? Jaribu kuwafanya wageuze vichwa vyao kidogo kuelekeana. Mara nyingi ni afadhali zaidi kuepuka kuwa na wote kwenye urefu mmoja. Unaweza kuwaweka pamoja ili macho ya mtu mmoja yalingane na pua ya mwingine.—Ona picha 4.

• Ebu tuongee juu ya nuru. Ni wakati gani ulio bora wakati wa mchana wa kupiga picha nje? Alasiri ikielekea jioni. Mara nyingi hewa imetulia, na rangi ya nuru ni changamfu zaidi. Jaribu kuweka rafiki yako ili nuru ya jua iangaze upande mmoja wa uso wake, huku kukiwa na nuru kidogo tu ya kuangaza sehemu nyingine ya uso ambao umesitiriwa. Hilo litamzuia mtu huyo asijaribu kufunga macho. Ukitaka kupiga picha ya uso, sogeza kamera yako kwenye upande wa uso ambao umesitiriwa. Na uhakikishe kwamba umesitiri lenzi ya kamera yako kutokana na jua.

• Namna gani nuru ikiwa kali mno? Jaribu kumweka rafiki yako katika hali ambayo jua liko nyuma yake.

• Je, kufanya hivyo hakutasitiri uso wake? Ndiyo, lakini unaweza kutumia nuru ya kamera yako ili kuangaza sehemu zenye kusitiriwa. Kamera nyingine hufanya hivyo peke yazo. Suluhisho jingine ni kuwa na rafiki awe msaidizi wako. Huyo anaweza kubeba kiakisi au kadibodi kubwa nyeupe na kuelekeza baadhi ya nuru ya jua kwenye uso wa mwenye kupigwa picha.

• Namna gani nuru ya ndani ya nyumba? Unaweza kutumia nuru ya kawaida kwa kumweka mwenye kupigwa picha kando ya dirisha. Kitambaa chembamba chaweza kupunguza nuru ya jua. Ikihitajika unaweza kutumia kimweko cha kamera au kiakisi cha kadibodi ili kuangaza maeneo katika sura ambayo yanaonekana kuwa giza-giza mno.—Ona picha 5.

• Namna gani ikiwa hakuna nuru ya kutosha? Katika hali kama hizo utalazimika kutumia kimweko cha kamera yako. Jaribu kumweka mwenye kupigwa picha katika eneo ambalo lina ukuta mweupe. Geuza kidogo kimweko chako ili nuru idunde kutoka ukuta wa kando. Nuru ikiwa inatoka upande wako, utadhibiti zaidi jinsi unavyotaka uso uangazwe.

Ni kweli kwamba ili kupata matokeo mazuri ni lazima ujaribu na kukosea. Lakini kanuni za msingi za kupiga picha ya mtu ni sahili. Kwa kupanga vizuri na kutoa uangalifu kwa mambo madogo-madogo, unaweza, hata ukitumia kamera sahili zaidi, kupiga picha nzuri ya mtu—picha ambayo wewe na wapendwa wako mtafurahia kwa miaka mingi ijayo!

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki