Kuutazama Ulimwengu
Utekaji wa Watu Katika Amerika ya Latini
Utekaji wa watu umekuwa biashara kubwa katika Amerika ya Latini, kulingana na gazeti la habari la Argentina Ámbito Financiero. Katika 1995 visa vipatavyo 6,000 viliripotiwa huko. Uchunguzi wa majuzi ulifunua kwamba kwa mbali Kolombia ilikuwa na visa vingi zaidi, visa 1,060 vya utekaji wa watu katika 1995, ikifuatwa na Mexico, Brazili, na Peru, kila nchi ikiwa na mamia ya visa hivyo kwa kipindi kilekile cha wakati. Kila mwaka, watekaji wa Kolombia hulipwa karibu dola milioni 300 za kukomboa watu waliotekwa. Katika Brazili fedha zinazolipwa watekaji ziliongezeka mara tatu katika 1995, zikifikia jumla ya dola bilioni moja. Huenda wenye kutekwa ni matajiri na watu mashuhuri au ni watalii wa kawaida au wake wa nyumbani katika familia zenye mapato ya chini. Katika visa fulani watekaji hukubali kupokea malipo polepole. Wakiogopa utekaji mwingine, pindi kwa pindi wahasiriwa huendelea kulipa polepole hata baada ya mtekwa kuachiliwa.
Kutazamia Mazuri Kwaweza Kuleta Afya Nzuri
Uchunguzi wa majuzi uliofanywa Finland ulithibitisha tena ile itikadi ya kwamba kutazamia mabaya kwaweza kuongeza uwezekano wa kupatwa na magonjwa ya kiakili na kimwili, huku kutazamia mazuri kukiweza kuleta afya nzuri. Karibu wanaume 2,500 wenye umri wa kati ya miaka 42 na 60 walichunguzwa kwa kipindi cha kati ya miaka 4 hadi 10. Kulingana na gazeti Science News, wanasayansi waliripoti kwamba wanaume “waliokata tamaa kwa kiasi cha kawaida hadi kukata tamaa zaidi walikufa . . . kwa kiwango cha mara mbili au tatu kuliko wale ambao hawakuwa wamekata tamaa; hao wenye kukata tamaa vilevile walishikwa na kansa na mishiko ya moyo mara nyingi zaidi.”
Watoto Wanene Kupita Kiasi
Kulingana na gazeti la habari The Weekend Australian, Dakt. Philip Harvey, mwanalishe wa umma, hivi majuzi alitangaza kwamba “watoto wa Australia wanazidi kunenepa nao wananenepa kwa kasi sana.” Hangaiko lake lategemea uchunguzi mmoja wa majuzi ulioonyesha kwamba idadi ya watoto wanene kupita kiasi katika Australia imeongezeka maradufu katika miaka kumi ambayo imepita. Karibu asilimia 10 ya watoto wenye umri wa kati ya miaka 9 na 15 wahitaji kutibiwa kwa sababu ya unene wao. Dakt. Harvey aamini kwamba asilimia ya watoto wanene kupita kiasi yaweza kuongezeka maradufu tena katika miaka kumi ijayo. Kama ilivyo kwa watu wazima, kukosa kufanya mazoezi ni kisababishi kikuu cha unene kupita kiasi miongoni mwa watoto, lasema gazeti hilo la habari, na kisababishi kingine ni mlo wenye mafuta mengi.
Hewa Chafu
Hazina ya Ulimwengu ya Wanyama wa Pori (WWF) imekata kauli kwamba Roma linachafuliwa kwa benzeni, ambayo ni kichafuzi kinachotokezwa na magari na ambacho hufikiriwa kuwa huleta kansa. Watafiti wa WWF waliwapa wajitoleaji wachanga 400 wenye umri wa kati ya miaka 8 na 18 zana za kutambua benzeni. Uchunguzi huo ulionyesha kwamba katika Roma “hewa ya kyubiki moja ya meta ina wastani wa mikrogramu 23.3 za benzeni,” ambayo inazidi sana kiwango halali cha mikrogramu 15 kwa kila kyubiki ya meta. Kwa kutegemea uchunguzi huu, wanasayansi walieleza kwamba kupumua hewa chafu kwa siku moja tu katika Roma kunalingana na kuvuta sigareti 13, laripoti gazeti la habari la Italia la La Repubblica.
Kuenea kwa Ugonjwa wa Utando wa Ubongo Katika Afrika Magharibi
Zaidi ya watu 100,000 wamekuwa wagonjwa na zaidi ya watu 10,000 wamekufa katika mojawapo ya mweneo mkubwa zaidi ya maradhi ya kuambukiza katika Afrika Magharibi katika historia ya majuzi, laripoti International Herald Tribune. Utando wa ubongo unaosababishwa na bakteria umekumba zaidi sehemu kavu na yenye vumbi ambayo iko kusini tu ya Jangwa la Sahara, ambako magonjwa ya mfumo wa upumuaji ni ya kawaida. Maradhi hayo husababisha mchochota katika utando wa ubongo na uti wa mgongo. Huenezwa kupitia hewa—kohozi au chafya yaweza kuyapitisha kwa mwingine. Maradhi hayo yaweza kuzuiwa kwa chanjo nayo yaweza kutibiwa, hasa katika hatua za mapema, kwa dawa za viuavijasumu. “Mweneo wa utando wa ubongo wa 1996 kwa wazi ndio mbaya zaidi uliopata kuonekana katika sehemu ya Afrika iliyo kusini ya Sahara,” akasema msemaji mmoja wa shirika la Doctors Without Borders. “Idadi ya wanaokufa inaendelea kupanda tu,” akaongezea.
Hakuna Marufuku juu ya Mabomu ya Kutegwa Chini ya Ardhi
Baada ya miaka miwili ya mazungumzo katika Geneva, Uswisi, wajadili wa kimataifa walishindwa kukubaliana juu ya kupiga marufuku mabomu ya kutegwa ardhini duniani kote. Ingawa waliamua kuharamisha aina fulani za mabomu hayo na kuweka vizuizi kwa mengineyo, marufuku kamili kwa mabomu hayo yote ya kutegwa ardhini hayatafikiriwa mpaka wakati wa mkutano wa kuyajadili ambao umepangwa kufanywa mwaka wa 2001. Kulingana na kadirio moja, katika miaka hiyo mitano, mabomu hayo ya kutegwa ardhini yaelekea yataua watu wengine 50,000 na kulemaza 80,000—hasa raia. Uhariri mmoja katika The Washington Post uliomboleza juu ya uamuzi huo, ukisema: “Mataifa yenye kiasi kingi cha mabomu hayo kwa uovu huvutiwa sana na silaha hizo, bila kufikiria madhara makatili yenye kuendelea ambayo mabomu hayo hutokeza kwa raia baada ya pambano ambalo yalikusudiwa yatumike kwisha.” Kulingana na makadirio yaliyofanywa na Umoja wa Mataifa, kwa sasa kuna mabomu yapatayo milioni 100 ambayo yamezikwa katika nchi 68.
Ukuzi wa Haraka wa Majiji
Watu wengi zaidi na zaidi wanahamia majijini, charipoti kichapo cha Umoja wa Mataifa The State of World Population 1996. Katika miaka kumi ijayo, wakazi wa majiji ya ulimwengu watakuwa bilioni 3.3, hiyo ni karibu nusu ya idadi ya watu wa ulimwenguni pote inayokadiriwa kwamba itakuwa bilioni 6.59. Katika 1950, majiji 83 yalikuwa na watu zaidi ya milioni moja kila moja. Leo, kuna majiji zaidi ya 280, hesabu ambayo inatarajiwa kuongezeka maradufu kufikia mwaka 2015. Katika 1950, ni New York City pekee lililokuwa na zaidi ya wakazi milioni 10; leo, kuna majiji 14 kama hayo, na ni Tokyo linaloongoza likiwa na watu milioni 26.5.
“Asili Inajua Zaidi”
“Asili inajua zaidi baada ya mimwagiko ya mafuta,” laripoti gazeti New Scientist. Wahifadhi walihofu kwamba kungetokea msiba wa kimazingira katika 1978 wakati meli kubwa ya mafuta Amoco Cadiz ilipovunjika pwani ya Brittany, kaskazini mwa Ufaransa. Wenye mamlaka wa sehemu hiyo walitumia miezi sita kuondoa maelfu ya tani ya matope na udongo wa bwawa uliochafuliwa kwa mafuta katika eneo moja. Sehemu nyingine iliyochafuliwa sana ilibaki bila kusafishwa. Sasa kulinganishwa kwa sehemu hizo mbili kwafunua kwamba vikundi vya kusafisha viliondoa matope mengi na udongo mwingi wa bwawa hivi kwamba kufikia asilimia 39 za mimea ya mabwawa zimeshindwa kukua tena. Hata hivyo, katika lile eneo ambalo halikuguswa, mawimbi ya bahari yamesafisha udongo vizuri sana hivi kwamba sasa kuna ukuzi wa asilimia 21 zaidi ya mimea kuliko wakati wa kabla ya mmwagiko wa mafuta. Bwawa hilo lilirudia hali yalo, na hakuna dalili za uchafuzi wa mafuta ambazo zimeonekana hapo kwa miaka kadhaa.
Kuendesha Vibaya Pikipiki za Maji
Boti za watu binafsi, ambazo kwa kawaida huitwa pikipiki za maji, zinazidi kupendwa katika Marekani. Boti hizi ndogo hufikia mwendo wa kilometa 100 kwa saa nazo huweza kubadili-badili mwendo haraka kama pikipiki. Jambo lenye kuhangaisha zaidi ni ongezeko la aksidenti mbaya, nyakati nyingine zikisababisha vifo, ambazo huzipata hizi boti. Kulingana na The Wall Street Journal, inakadiriwa kwamba “kufikia asilimia 60 ya aksidenti husababishwa na watu wanaozikodi.” Ingawa waendeshaji wengi huvalia vesti za kuokoa uhai kwa kufuata sheria, wengi hawana uzoefu wa utaratibu wa kuendesha boti nao huziendesha vibaya. Mlinzi mmoja wa Pwani alieleza kwamba “mwendeshaji anaporushwa akienda mwendo wa kilometa 80 kwa saa, kugonga maji ni kama kugonga jengo.”
Imepatikana—Mashua Yenye Miaka 2,000
Upungufu mkubwa zaidi wa maji katika Bahari ya Galilaya katika 1986 ulifunua mashua iliyotumiwa tangu wakati wa Yesu. Tangu wakati huo, mashua hiyo imekuwa ikiloweshwa katika dawa fulani ya kuhifadhi ili isiharibike upesi. Sasa, National Geographic laripoti, imeondolewa kutoka kwenye dawa hiyo ya kuhifadhi na sasa imewekwa maonyeshoni karibu na mji wa Magdala. “Ina urefu wa karibu meta 8, ilitumia jarife, na huenda ilikuwa na wapiga makasia wanne na mshika usukani mmoja,” aeleza Shelley Wachsmann, aliyeongoza kazi ya uchimbuzi. Yeye aliongezea hivi: “Angalau mbao za aina saba zilitumiwa, kutia ndani vipande kutoka kwenye mashua nyinginezo. Ama miti ilikuwa nadra kupatikana ama mwenyewe alikuwa maskini sana.”
Kuhakikisha Ukuzi wa Kawaida
Ukuzi wa mtoto huathiriwa na mambo mengi mbali na urithi tu, yasema ripoti moja katika Jornal do Brasil. “Lishe nzuri ndiyo uhakikisho mkubwa kwamba kutakuwa na ukuzi ufaao,” lasema gazeti hilo, likiongeza kwamba lishe mbaya ni kawaida sana hata miongoni mwa familia zenye mapato ya kadiri. “Kisababishi kingine kikuu cha ukuzi ni kufanya mazoezi kwa ukawaida,” asema profesa wa endokrinolojia Amélio Godoy Matos. “Lazima ihakikishwe kwamba kuna usingizi wa kutosha wa muda wa saa nyingi kwa sababu homoni ya ukuzi hutolewa tu mtoto anapolala,” yeye alisema. Matatizo ya kihisia moyo vilevile yaweza kupunguza ukuzi wa mtoto. Kulingana na mtaalamu wa endokrinolojia Walmir Coutinho, “kutazama televisheni kwa muda wa saa nyingi bila kukoma, hasa sinema zenye jeuri, hudhuru usingizi wa mtoto nayo yaweza kuharibu ukuzi wake mzuri.”