Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g99 12/22 kur. 4-7
  • Utekaji-nyara—Tisho la Kujifaidi Kifedha

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Utekaji-nyara—Tisho la Kujifaidi Kifedha
  • Amkeni!—1999
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Kukabiliana na Vurugu Hiyo
  • Matokeo Zaidi
  • Washauri wa Usalama Wapata Faida Kubwa
  • Sababu Zinazochangia Ongezeko Hilo
  • Nia Haiwi Ile Ile Sikuzote
  • Utekaji-nyara—Je, Kuna Utatuzi?
    Amkeni!—1999
  • Utekaji-nyara—Shughuli ya Tufeni Pote
    Amkeni!—1999
  • Utekaji-nyara—Sababu Zake za Msingi
    Amkeni!—1999
  • Je, Wahitaji Bima?
    Amkeni!—2001
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1999
g99 12/22 kur. 4-7

Utekaji-nyara—Tisho la Kujifaidi Kifedha

“UTEKAJI-NYARA si kama uhalifu wa mali. Ni kitendo cha hila, ukatili na cha kutojali kikundi cha msingi zaidi cha kibinadamu, familia,” asema Mark Bles, katika kitabu chake The Kidnap Business. Utekaji-nyara husababisha msukosuko wa kihisia-moyo kwa washiriki wa familia. Kila dakika ipitayo na kila saa ipitayo, wanahisi wakiwa na tumaini, na mara wanakata tamaa wanapopambana na hisia za moyoni za hatia, chuki, na kutojiweza. Hali hiyo yenye kuogofya yaweza kuendelea kwa siku, majuma, miezi kadhaa au, nyakati nyingine hata miaka kadhaa.

Katika utafutaji usiokoma wa fedha, watekaji-nyara hutumia hisia za familia ili kujifaidi. Kikundi cha watekaji-nyara kilimlazimisha mtekwa mmoja aandike mambo yafuatayo katika barua iliyochapishwa kwa ajili ya waandishi wa habari: “Nawaomba Waandishi wa Habari wachapishe habari hii kila mahali ili nisiporudi kosa litakuwa la watekaji-nyara lakini pia litakuwa la familia yangu ambayo inathibitika kuwa inapenda fedha zaidi kuliko mimi.” Watekaji-nyara wa Italia hudai kwa nguvu fedha za fidia kwa kukata sehemu za mwili na kuzipeleka kwa jamaa au kwenye vituo vya televisheni. Mtekaji-nyara wa Mexico hata aliwatesa wahasiriwa wake alipokuwa akijadiliana na familia zao kwa simu.

Kwa upande mwingine, watekaji-nyara fulani hujaribu kupata upendeleo wa wahasiriwa wao. Kwa mfano, katika Filipino mwanabiashara aliyetekwa nyara aliwekwa kwenye hoteli ya anasa huko Manila, ambako watekaji wake walimpa kileo na kumtumbuiza na makahaba hadi fidia ilipolipwa. Hata hivyo, wahasiriwa wengi hufungiwa huku mahitaji yao ya kimwili au ya usafi wa kiafya yakipuuzwa. Wengi hutendwa kikatili. Kwa vyovyote vile, sikuzote lazima mhasiriwa apatwe na hofu ya kutaka kujua ni nini kitakachompata.

Kukabiliana na Vurugu Hiyo

Hata baada ya wahasiriwa kuachiliwa, huenda wakawa na makovu ya kihisia-moyo yatakayoendelea kwa muda. Muuguzi mmoja Msweden aliyetekwa nyara huko Somalia alitoa maoni haya: “Kuna jambo moja lililo la maana zaidi kuliko kitu kingine chochote. Lazima uongee na marafiki na jamaa zako na utafute msaada wa kitaalamu ikiwa unauhitaji.”

Wanatiba wamebuni njia ya kusaidia wahasiriwa wa namna hiyo. Katika vipindi kadhaa vichache wahasiriwa huchanganua mambo yaliyowapata kwa msaada wa kitaalamu kabla ya kukutana na familia zao na kurudia maisha ya kawaida. “Tiba inayotolewa muda mfupi baada ya tukio hilo hupunguza hatari ya madhara ya kudumu,” asema Rigmor Gillberg, mtaalamu wa tiba ya kupambana na matatizo wa shirika la Msalaba Mwekundu.

Matokeo Zaidi

Si wahasiriwa na familia zao peke yao wanaoathiriwa na utekaji-nyara. Hofu ya kutekwa nyara inaweza kukomesha utalii na kupunguza vitega-uchumi; pia husababisha hali ya kutohisi usalama katika jamii. Katika miezi michache tu mwaka wa 1997, makampuni sita ya kimataifa yaliondoka Filipino kwa sababu ya tisho la utekaji-nyara. Mwanamke mmoja Mfilipino anayefanya kazi katika shirika linaloitwa Citizen Against Crime alisema hivi kwa mkazo: “Tunaishi katika hali yenye kutia hofu.”

Makala moja katika The Arizona Republic yasema: “Miongoni mwa mameneja wa Mexico, hofu ya kutekwa nyara inakaribia kuwa isiyozuilika, kukiwa na sababu zifaazo.” Gazeti la Brazili Veja laripoti kwamba watekaji-nyara na wanyang’anyi wamechukua mahali pa madubwana katika ndoto zenye kuogofya za watoto wa Brazili. Huko Taiwan, somo la kuzuia utekaji-nyara hufundishwa shuleni, na huko Marekani, kamera za usalama zimewekwa katika shule za watoto wadogo ili kuzuia utekaji-nyara.

Washauri wa Usalama Wapata Faida Kubwa

Ongezeko la utekaji-nyara na masuala nyeti yanayohusiana nao yamesababisha kuongezeka haraka kwa mapato ya makampuni ya usalama. Katika jiji la Brazili la Rio de Janeiro, kuna makampuni kama hayo zaidi ya 500, yenye mapato ya dola bilioni 1.8 za Marekani.

Idadi inayoongezeka ya makampuni ya kimataifa ya usalama hufundisha kujizuia na utekaji-nyara, huchapisha ripoti kuhusu maeneo hatari, na hujadili fidia. Yanashauri familia na makampuni, yakiwafundisha mbinu za watekaji-nyara na kuwasaidia wakabiliane kisaikolojia. Makampuni mengine hata hujaribu kuwakamata watekaji-nyara na kupata pesa za fidia baada ya mateka kuachiliwa. Hata hivyo, huduma zao hulipiwa.

Licha ya jitihada hizo, visa vya utekaji-nyara vinaongezeka katika nchi nyingi. Akitoa maoni kuhusu jinsi hali ilivyo katika Amerika ya Latini, Richard Johnson, makamu msimamizi wa Seitlin & Company, asema: “Tunaweza kutarajia kwamba visa vya utekaji-nyara vitaongezeka.”

Sababu Zinazochangia Ongezeko Hilo

Wataalamu wanadokeza sababu kadhaa za ongezeko hilo la hivi karibuni. Moja ni kwamba hali ya kiuchumi imezorota katika maeneo fulani. Mfanyakazi mmoja wa huduma za kuandaa misaada katika mji wa Nal’chik, Urusi, alisema: “Njia bora ya kupata fedha ni kupitia utekaji-nyara ulio mashuhuri.” Katika zile zilizokuwa jamhuri za Sovieti, visa vya utekaji-nyara vinasemekana kuwa vinaandaa fedha kwa ajili ya majeshi ya kibinafsi ya mababe wa kivita wa sehemu hizo.

Watu wengi wanafunga safari za kibiashara au za utalii kuliko wakati mwingine uliopita, hivyo wakitokeza fursa mpya kwa watekaji-nyara wanaotafuta mawindo. Idadi ya wageni waliotekwa nyara imeongezeka maradufu katika muda wa miaka mitano. Kati ya mwaka wa 1991 na 1997, watalii walitekwa nyara katika nchi 26.

Watekaji-nyara hao wote hutoka wapi? Mapambano kadhaa ya kijeshi yanakwisha, yakifanya askari-jeshi wa zamani wakose kazi na fedha. Watu hao wana stadi zote za msingi zinazohitajika ili kufanya biashara hii yenye faida.

Vivyo hivyo, hatua kali za kinidhamu dhidi ya wizi wa benki na ulanguzi wa dawa za kulevya zimesababisha wahalifu wageukie utekaji-nyara ukiwa njia badala ya kujipatia mapato. Mike Ackerman, mtaalamu wa utekaji-nyara, alieleza hivi: “Tunapofanya uhalifu kwa ajili ya mali uwe jambo gumu zaidi katika jamii zote, tunazidisha uhalifu dhidi ya watu.” Kutangaza hadharani malipo ya juu ya fidia kungeweza pia kuchochea watu wawezao kuwa watekaji-nyara.

Nia Haiwi Ile Ile Sikuzote

Watekaji-nyara wengi hutaka fedha, fedha peke yake. Madai ya fidia hutofautiana kutoka kiasi kidogo cha dola hadi fidia iliyovunja rekodi ya dola milioni 60 za Marekani zilizolipwa kwa ajili ya mfanya biashara tajiri wa Hong Kong ambaye hakuwahi kuachiliwa licha ya malipo hayo kutolewa.

Kwa upande mwingine, watekaji-nyara fulani wametumia wahasiriwa wao ili wapate kutangazwa hadharani, wapate chakula, dawa, redio, magari na vilevile shule mpya, barabara, na hospitali. Meneja mmoja aliyetekwa nyara huko Asia aliachiliwa baada ya watekaji-nyara kupewa yunifomu za mpira wa kikapu na mipira. Vikundi fulani pia huteka nyara ili kutisha na kuogofya watega-uchumi wa kigeni na watalii, vikiwa na kusudi la kukomesha kutumiwa vibaya kwa ardhi na mali asili.

Kwa hiyo kuna nia nyingi, njia nyingi za kutumiwa, na watu wengi wawezao kuwa watekaji-nyara au wahasiriwa. Je, utatuzi unapatikana kwa wingi? Ni nini baadhi ya utatuzi, na je, unaweza kutatua tatizo hilo? Kabla ya kujibu maswali hayo, acheni tuchunguze sababu nyingine kuu na za msingi za ongezeko katika biashara ya utekaji-nyara.

[Sanduku katika ukurasa wa 5]

Endapo Watekwa Nyara

Wale ambao wamechunguza habari hiyo wanatoa madokezo yafuatayo kwa watu ambao huenda watekwe nyara.

• Uwe mwenye ushirikiano; epuka tabia ya kuwa mkaidi. Mateka wanaoonyesha uadui mara nyingi hutendwa kikatili, na wanakabili hatari kubwa zaidi ya kuuawa au kutengwa na wengine ili kuadhibiwa.

• Usihofu. Kumbuka kwamba wahasiriwa wengi huokoka utekaji-nyara.

• Buni njia fulani ya kuhesabia wakati.

• Jaribu kuwa na utaratibu fulani wa kila siku.

• Fanya mazoezi, hata ingawa huenda usiwe na fursa za kutosha za kusonga huku na huko.

• Uwe mwelekevu; jaribu kukumbuka mambo, sauti, na harufu. Fahamu mambo fulani kuhusu watu wanaokuteka nyara.

• Piga gumzo ikiwezekana na jaribu kuanzisha mawasiliano. Ikiwa watekaji-nyara wanatambua sifa zako, hawataelekea kukudhuru au kukuua.

• Wajulishe mahitaji yako kwa njia ya upole.

• Usijaribu kamwe kujadili fidia yako.

• Ukijikuta katikati ya jaribio la uokoaji, jilaze chini na kusubiri kwa utulivu tu mambo yanapoendelea.

[Sanduku katika ukurasa wa 6]

Bima ya Utekaji-Nyara—Suala Linalobishaniwa

Bima ni biashara inayokua haraka ambayo inahusiana na kuongezeka kwa visa vya utekaji-nyara. Kampuni ya bima ya Lloyd ya London imekuwa na ongezeko la asilimia 50 kila mwaka katika bima ya utekaji-nyara katika miaka ya 1990. Makampuni mengi yanazidi kutoa bima hiyo. Bima hiyo hushughulikia msaada wa mtu anayejadili utekaji-nyara, malipo ya fidia, na nyakati nyingine jitihada za wataalamu za kupata tena fidia hiyo. Hata hivyo, suala la bima linabishaniwa sana.

Wapinzani wa bima ya utekaji-nyara hudai kwamba inafanya uhalifu huo uwe shughuli ya kibiashara na kwamba si jambo la kiadili kujifaidi kutokana utekaji-nyara. Pia wanasema kwamba mtu aliyekatiwa bima aweza kupuuza usalama wake mwenyewe na kwamba bima hiyo itafanya iwe rahisi kwa mtekaji-nyara kutwaa pesa kwa nguvu, hivyo kuendeleza uhalifu huo. Wengine hata wanahofu kwamba kuwepo kwa bima kutawatia watu moyo wapange kutekwa nyara ili wapate pesa za bima. Bima ya utekaji-nyara ni haramu katika Italia, Kolombia, na Ujerumani.

Watetezi wa bima ya utekaji-nyara wanasema kwamba kama ilivyo na makampuni mengine ya bima, jambo hilo hufanya wengi walipie hasara ya watu wachache. Wanasababu kwamba bima hutokeza usalama wa kiasi fulani, kwa kuwa huwezesha familia na makampuni yaliyokatiwa bima yalipie huduma za wataalamu, wanaoweza kufanya hali isiwe mbaya zaidi, kujadili fidia ya kiasi kidogo, na kufanya iwe rahisi zaidi kuwashika watekaji-nyara.

[Sanduku katika ukurasa wa 7]

Tabia Isiyo ya Kawaida ya Stockholm

Kutekwa nyara kwa Patty Hearst, mnamo mwaka wa 1974, aliyekuwa binti ya bilionea wa kampuni ya magazeti Randolph A. Hearst, kulichukua mwelekeo mpya alipoamua kujiunga na watekaji wake na kushiriki uhalifu wa kutumia silaha pamoja na kikundi hicho. Katika kisa kingine mcheza kandanda Mhispania aliyekuwa ametekwa nyara aliwasamehe watekaji wake na kuwatakia mema.

Mapema katika miaka ya 1970, tukio hilo liliitwa Tabia Isiyo ya Kawaida ya Stockholm, baada ya tukio lenye kupendeza la utekaji-nyara mwaka wa 1973 kwenye benki moja huko Stockholm, Sweden. Kwenye pindi hiyo baadhi ya mateka hao walianzisha urafiki wa pekee pamoja na watekaji wao. Urafiki wa namna hiyo umekuwa ulinzi kwa mateka, kama ielezwavyo na kitabu Criminal Behavior: “Kadiri mhasiriwa na mtekaji wanavyojuana, ndivyo hupendana zaidi. Tukio hilo laonyesha kwamba baada ya muda fulani huenda mkosaji asimdhuru mateka.”

Mhasiriwa mmoja Mwingereza huko Chechnya aliyebakwa alisema hivi: “Naamini kwamba mlinzi huyo alipofahamu sisi ni watu wa aina gani alitambua kwamba ilikuwa kosa kunibaka. Aliacha kunibaka na akaomba radhi.”

[Picha katika ukurasa wa 4]

Utekaji-nyara ni mojawapo ya jambo linalovuruga zaidi kihisia-moyo na lenye kujaribu zaidi washiriki wa familia

[Picha katika ukurasa wa 5]

Wahasiriwa wanahitaji faraja

[Picha katika ukurasa wa 7]

Wahasiriwa wengi hufungiwa huku mahitaji yao ya kimwili au ya usafi wa kiafya yakipuuzwa

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki