Utekaji-nyara—Sababu Zake za Msingi
UTEKAJI-NYARA umekuwa pigo la kisasa. Lakini ndivyo ilivyo na ubakaji, wizi, kusumbua watoto kingono, na hata maangamizi ya jamii nzima-nzima. Kwa nini maisha yamekuwa hatari sana hivi kwamba mara nyingi watu wanaogopa kujasiria kutoka nje ya nyumba zao usiku?
Sababu za msingi za kuenea kwa uhalifu, kutia ndani utekaji-nyara, zinahusiana na dosari zilizotia mizizi ndani ya jamii ya kibinadamu. Je, uling’amua kwamba yapata miaka 2,000 iliyopita, Biblia ilikuwa imetabiri nyakati hizi hatari? Tafadhali chunguza yaliyotabiriwa kwenye 2 Timotheo 3:2-5.
“Watu watakuwa wenye kujipenda wenyewe, wapenda-fedha, wenye kujitanguliza, wenye kiburi, wakufuru, wasiotii wazazi, wasio na shukrani, wasio waaminifu-washikamanifu, wasio na shauku ya kiasili, wasiotaka upatano wowote, wachongezi, wasio na hali ya kujidhibiti, wakali, wasio na upendo wa wema, wasaliti, wenye vichwa vigumu, wenye kututumuka kwa kiburi, wenye kuzipenda raha badala ya kuwa wapenda-Mungu, wakiwa na namna ya ujitoaji-kimungu lakini wakithibitika kuwa si kweli kwa nguvu ya hiyo.”
Labda unakubali kwamba maneno hayo yaliyorekodiwa muda mrefu uliopita yanafafanua kwa njia nzuri sana hali ya mambo leo. Katika muda wetu wa maisha dosari zimetokea katika jamii ya kibinadamu kwa kiwango kikubwa kweli kweli. Jambo muhimu ni kwamba ufafanuzi ulio juu wa hali yenye kusikitisha ya mwenendo wa kibinadamu unatangulizwa katika Biblia kwa maneno: “Katika siku za mwisho nyakati za hatari zilizo ngumu kushughulika nazo zitakuwa hapa.” (2 Timotheo 3:1) Acheni tufikirie dosari kuu tatu za jamii ambazo zimechangia kuenea kwa utekaji-nyara.
Matatizo ya Kutekeleza Sheria
“Kwa sababu hukumu juu ya tendo baya haitekelezwi upesi, mioyo ya wanadamu huthibitishwa ndani yao ili kutenda mabaya.”—Mhubiri 8:11.
Vikosi vingi vya polisi havina vifaa vya kukabiliana na kuenea kwa uhalifu. Kwa hiyo katika nchi nyingi, utekaji-nyara umekuwa uhalifu ambao huleta pesa. Mnamo mwaka wa 1996, ni asilimia 2 tu ya watekaji-nyara wa Kolombia walioshtakiwa. Katika Mexico, angalau dola milioni 200 za Marekani zililipwa zikiwa fedha ya fidia mnamo mwaka wa 1997. Watekaji-nyara fulani katika Filipino wamekubali malipo ya fidia yafanywe kwa hundi.
Kwa kuongezea, ufisadi miongoni mwa idara za kutekeleza sheria nyakati nyingine huzuia jitihada za kukabili uhalifu kwa njia yenye matokeo. Viongozi wa vikosi bora vya kukabiliana na utekaji-nyara katika Mexico, Kolombia, na katika zile zilizokuwa jamhuri za Sovieti wamelaumiwa kuwa watekaji-nyara. Katika gazeti Asiaweek, rais wa Bunge la Filipino, Blas Ople, asema kwamba tarakimu rasmi zaonyesha kuwa asilimia 52 ya visa vya utekaji-nyara katika Filipino huhusisha polisi wanaofanya kazi au waliostaafu au wanajeshi. Mtekaji-nyara sugu wa Mexico alisemekana kuwa alizingirwa na “ulinzi rasmi uliowezekana kwa kuwahonga maofisa na waendesha mashtaka wa manispaa, jimbo na serikali.”
Umaskini na Ukosefu wa Haki wa Kijamii
“Kisha nikarudi na kuona madhalimu yote yanayotendeka chini ya jua; na tazama, machozi yao waliodhulumiwa, ambao walikuwa hawana mfariji; na upande wa wale waliowadhulumu kulikuwa na uwezo.”—Mhubiri 4:1.
Watu wengi leo wako katika hali za kiuchumi na za kijamii zilizozorota, na mara nyingi wao ndio huhusika na utekaji-nyara. Kwa hiyo, katika ulimwengu ambamo pengo kati ya matajiri na maskini linazidi kupanuka na ambamo mara nyingi ni vigumu sana kupata fedha kwa njia ya haki, kishawishi cha utekaji-nyara kitazidi kuwepo. Maadamu kuna uonevu, utekaji-nyara utakuwa njia ya kulipiza kisasi na kuelekeza uangalifu kwa hali inayoonwa kuwa isiyovumilika.
Pupa na Ukosefu wa Upendo
“Kupenda fedha ni mzizi wa mambo mabaya ya namna zote.” (1 Timotheo 6:10) “Kwa sababu ya kuongezeka kwa uasi-sheria upendo wa idadi iliyo kubwa zaidi utapoa.”—Mathayo 24:12.
Katika historia yote kupenda fedha kumefanya watu watende mambo ya kuchukiza sana. Na labda hakuna uhalifu mwingine ambao hutokeza faida za kifedha sawa na utekaji-nyara kwa kusababisha wanadamu wapatwe na maumivu makali, kihoro, na kukata tumaini. Kwa wengi ni pupa—kupenda fedha—ndiko huwachochea wamtendee kinyama mtu wasiyemjua na kumtesa na kuiletea familia yake masaibu kwa majuma kadhaa, miezi, na nyakati nyingine miaka kadhaa.
Kwa wazi, kuna kasoro kubwa sana katika jamii inayokazia fedha na kupuuza maadili ya kibinadamu. Bila shaka, hali hiyo hutokeza hali zinazoendeleza kila aina ya uhalifu, kutia ndani utekaji-nyara.
Je, hilo lamaanisha kwamba tuko katika zile zinazoitwa na Biblia “siku za mwisho”? Ikiwa ndivyo, jambo hilo litamaanisha nini kwa dunia na kwetu sisi? Je, kuna utatuzi kwa matatizo mabaya sana yanayokabili jamii ya kibinadamu, kutia ndani utekaji-nyara?
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 8]
Si Jambo Jipya
Sheria ya Kimusa ilitoa adhabu ya kifo kwa watekaji-nyara huko nyuma katika karne ya 15 K.W.K. (Kumbukumbu la Torati 24:7) Julius Caesar alitekwa nyara ili kupata fidia katika karne ya kwanza K.W.K., ndivyo na Richard wa Kwanza, mfalme wa Uingereza mwenye Moyo Kama wa Simba, katika karne ya 12 W.K. Fidia kubwa zaidi iliyowahi kulipwa ilikuwa tani 24 za dhahabu na fedha ambazo Wainka walimpa mshindi Mhispania Francisco Pizzaro ili aachilie chifu wao mtekwa Atahuallpa katika mwaka wa 1533. Hata hivyo washindi hao walimnyonga hadi akafa.
[Picha katika ukurasa wa 9]
Licha ya polisi kuwa na vifaa, visa vya utekaji-nyara vimeenea sana