Utekaji-nyara—Shughuli ya Tufeni Pote
KATIKA mwongo uliopita, kumekuwa na ongezeko kubwa sana katika visa vya utekaji-nyara ulimwenguni pote. Ripoti moja yasema kwamba kati ya 1968 na 1982, takriban mateka elfu moja walichukuliwa katika nchi 73. Lakini katika mwisho-mwisho wa miaka ya 1990, watu wanaokadiriwa kuwa 20,000 hadi 30,000 walitekwa nyara kila mwaka.
Utekaji-nyara ni uhalifu ambao unazidi kupendwa na wahalifu tufeni pote, huku watekaji-nyara wakiwa tayari kuteka kiumbe chochote kilicho hai. Katika pindi moja mtoto mchanga mwenye umri wa siku moja tu alitekwa nyara. Katika Guatemala mwanamke mwenye umri wa miaka 84 akiwa katika kiti cha magurudumu alitekwa nyara na kuzuiliwa kwa miezi miwili. Katika Rio de Janeiro, wahalifu wa mitaani wananyakua watu moja kwa moja barabarani, nyakati nyingine wakidai fidia ya kiasi kidogo kama dola 100 za Marekani.
Hata wanyama hawako salama. Miaka kadhaa iliyopita wahalifu shupavu huko Thailand waliteka nyara tembo mwenye uzito wa tani sita anayetumiwa kufanya kazi na kudai fidia ya dola 1,500. Magenge ya uhalifu katika Mexico yanasemekana kwamba yanawatia moyo washiriki wake wachanga wajizoeze kuteka nyara wanyama vipenzi na wanyama wa kufugwa kabla ya kuwateka nyara wanadamu.
Zamani, watekaji-nyara walilenga hasa matajiri, lakini mambo yamebadilika. Ripoti moja kutoka kwa shirika la habari la Reuters yasema: “Utekaji-nyara unatukia kila siku katika Guatemala, ambako watu hukumbuka kwa upendo nyakati nzuri zilizopita ambapo waasi wa mrengo wa kushoto walilenga tu idadi ndogo ya matajiri. Sasa matajiri na maskini, wadogo kwa wakubwa, wanaweza kushambuliwa na magenge ya watekaji-nyara.”
Visa vinavyojulikana na umma huelekezewa uangalifu mkubwa sana na vyombo vya habari, lakini kwa kiwango kikubwa visa vingi vya utekaji-nyara husuluhishwa bila kutangazwa. Kwa hakika, kwa sababu kadhaa, nchi “hazijishughulishi sana kutangaza tatizo la utekaji-nyara.” Makala ifuatayo itazungumzia sababu kadhaa kati ya hizo.
[Ramani katika ukurasa wa 3]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
MEXICO
Kukiwa na watu 2,000 wanaotekwa nyara kwa mwaka mmoja, utekaji-nyara umeitwa “biashara ndogo iliyopangwa.”
UINGEREZA
Bima ya utekaji-nyara katika kampuni ya Lloyd ya London imeongezeka kwa asilimia 50 kila mwaka tangu 1990.
URUSI
Katika eneo la Caucasus pekee lililo kusini mwa Urusi, idadi ya waliotekwa nyara iliongezeka kutoka 272 mwaka wa 1996 hadi 1,500 mwaka wa 1998.
FILIPINO
Kulingana na gazeti “Asiaweek,” “labda Filipino ndicho kituo cha utekaji-nyara cha Asia.” Kuna zaidi ya magenge 40 yaliyopangwa ya utekaji-nyara huko.
BRAZILI
Katika mwaka mmoja watekaji-nyara hapo waliripoti kuwa walipata kiasi kikubwa sana cha fedha ya fidia cha dola bilioni 1.2 za Marekani.
KOLOMBIA
Katika miaka ya karibuni maelfu ya watu wametekwa nyara kila mwaka. Katika Mei 1999, waasi waliteka nyara wakazi mia moja wa parokia wakati wa Misa.
[Hisani]
Mountain High Maps® Copyright © 1997 Digital Wisdom, Inc.