Utekaji-nyara—Je, Kuna Utatuzi?
“VISA vya utekaji-nyara vimefikia kiwango kisichoweza kuvumiliwa na taifa zima, na jamii nzima lazima ipambane na uovu huo,” ndivyo alivyosema kwa mkazo waziri mkuu wa Chechnya alipokuwa akiahidi kukomesha pigo hilo katika jamhuri yake iliyoko Urusi iliyokumbwa na visa vya utekaji-nyara.
Kukomesha utekaji-nyara? Mradi huo ni wenye kusifika, lakini swali ni, Jinsi gani?
Jitihada Zinazofanywa
Wenye mamlaka wa Kolombia wameteua maajenti wa siri 2,000, waendesha mashtaka wa umma 24, na hata mratibu wa pekee wa kikundi cha kupambana na utekaji-nyara. Katika Rio de Janeiro, Brazili, maandamano ya hadharani yaliyokuwa yakipinga visa vingi vya utekaji-nyara jijini yalivutia takriban waandamanaji 100,000. Katika Brazili na Kolombia, vikundi vyenye hadhi ya kijeshi vimelipiza kisasi kwa kuteka nyara jamaa za watekaji-nyara. Na Wafilipino fulani wameamua kuchukua sheria mikononi—wamewachoma watekaji-nyara!
Wenye mamlaka wa Guatemala walianzisha adhabu ya kifo kwa watekaji-nyara, naye rais akatuma jeshi ili kuzuia kuenea kwa utekaji-nyara. Katika Italia serikali ilianzisha hatua madhubuti za kuzuia utekaji-nyara, kwa kuharamisha malipo ya fidia na kutwaa fedha na mali ili kuzuia watu wa jamaa wasilipe. Wenye mamlaka wa Italia wanajisifu kwamba hatua hizo zimechangia kupungua kwa visa vya utekaji-nyara. Hata hivyo, wahakiki wanadokeza kwamba kama tokeo, familia hujaribu kusuluhisha kesi kwa siri na kwamba jambo hilo hupunguza idadi rasmi ya visa vya utekaji-nyara. Washauri wa kibinafsi wa usalama wanakadiria kwamba idadi ya visa vya utekaji-nyara katika Italia kwa kweli vimeongezeka maradufu tangu miaka ya 1980.
Madokezo Mengi—Utatuzi Usiotosha
Kwa familia nyingi ambazo watu wao wametekwa nyara, kuna utatuzi mmoja tu unaowezekana—kutoa dhamana kwa ajili ya wapendwa wao haraka iwezekanavyo. Lakini wataalamu wanaonya kwamba ikiwa kiasi cha fidia ni cha juu na kinalipwa haraka sana, huenda watekaji-nyara wakaona familia hiyo kuwa rahisi kushambuliwa na hurudi mara ya pili. Au wanaweza kuomba fidia ya pili kabla ya kumwachilia mhasiriwa.
Familia fulani zimelipa fidia ya kiasi kikubwa na kugundua kwamba mhasiriwa alikuwa amekufa tayari. Kwa hiyo wataalamu wanasema kwamba mtu hapaswi kamwe kulipa fidia au kuanza majadiliano kabla hajapata uthibitisho kwamba mhasiriwa yuko hai. Uthibitisho huo ungeweza kuwa kwa kuuliza swali ambalo linaweza kujibiwa na mhasiriwa peke yake. Familia fulani huomba picha ya mhasiriwa akiwa amebeba gazeti la hivi karibuni.
Vipi shughuli za uokoaji? Mara nyingi zinahusisha hatari kubwa. “Asilimia sabini na tisa ya mateka wote huuawa wakati wa majaribio ya uokoaji katika Amerika ya Latini,” asema Brian Jenkins, mtaalamu wa utekaji-nyara. Hata hivyo, nyakati fulani, uokoaji hufaulu.
Haishangazi kwamba utatuzi mwingi hukazia kuzuia utekaji-nyara. Si wenye mamlaka wa serikali peke yao wanaohusika katika majaribio ya kuzuia utekaji-nyara. Magazeti hufunza watu namna wanavyoweza kuepuka kutekwa nyara, jinsi ya kuruka kutoka kwenye gari lililo mwendoni, na jinsi ya kutumia werevu na kuwashinda watekaji-nyara. Vituo vya kujifunzia judo na karate hutoa mafunzo ya kujilinda dhidi ya kutekwa nyara. Makampuni yanauza transmita ndogo sana za dola 15,000 za Marekani zinazoweza kuingizwa ndani ya meno ya watoto ili kusaidia polisi kuwasaka watoto endapo wanatekwa nyara. Kwa wale walio na fedha za kutosha, watengenezaji-magari hutengeneza magari “yasiyoweza kutekwa nyara” yenye vifaa vinavyotoa gesi ya kutoa machozi, matundu ya kurushia risasi, madirisha yasiyopenya risasi, magurudumu yasiyoweza kutobolewa, na vifaa vinavyotoa utando wa mafuta.
Baadhi ya watu matajiri huona utatuzi unapatikana kwa kuwa na walinzi wa kibinafsi. Hata hivyo, kuhusu hali ilivyo huko Mexico, mtaalamu wa usalama Francisco Gomez Lerma asema: ‘Walinzi wa kibinafsi hawasaidii kwa sababu huvutia watekaji-nyara.’
Tatizo la utekaji-nyara ni tata sana na mizizi yake imepenya ndani kabisa hivi kwamba hakuna jambo ambalo mwanadamu anaweza kufanya la kutosha ili kulikomesha. Basi, je, hakuna utatuzi halisi?
Kuna Utatuzi
Gazeti hili limetaja tena na tena utatuzi pekee wa matatizo hayo yote yanayokabili wanadamu. Utatuzi huo ni ule ambao Mwana wa Mungu, Yesu Kristo, alitaja alipowafundisha wanafunzi wake wasali: “Acha ufalme wako uje. Mapenzi yako na yatendeke, kama ilivyo katika mbingu, pia juu ya dunia.”—Mathayo 6:10.
Kwa wazi, tunahitaji serikali ya ulimwengu yenye uadilifu ili kusimamia mambo ya watu wa namna mbalimbali duniani—naam, Ufalme wa Mungu ambao Yesu alisema juu yake. Kwa kuwa wanadamu wameshindwa kusimamisha serikali ya namna hiyo, ni hekima kwetu kumtegemea Muumba wetu, Yehova Mungu. Neno lake Biblia lasema kwamba alikusudia kufanya jambo hilihili.—Zaburi 83:18.
Nabii Danieli alirekodi kusudi la Yehova, alipoandika: “Katika siku za wafalme hao Mungu wa mbinguni atausimamisha ufalme ambao hautaangamizwa milele. . . . utavunja falme hizi zote vipande vipande na kuziharibu, nao utasimama milele na milele.” (Danieli 2:44) Biblia inaeleza jinsi serikali hii ya Mungu itakavyochukua hatua ili kukomesha uhalifu wote, kutia ndani utekaji-nyara.
Elimu Inayofaa Ni Muhimu
Bila shaka utakubali kwamba kukazia kanuni zinazofaa ndani ya watu ni muhimu ili kutatua tatizo la utekaji-nyara. Kwa mfano, fikiria wanadamu wangekuwaje ikiwa wote wangetii onyo hili la upole katika Biblia: “Acheni namna yenu ya maisha iwe bila upendo wa fedha, huku nyinyi mkiridhika na vitu vilivyopo.” (Waebrania 13:5) “Nyinyi watu msiwe mkiwiwa na yeyote hata jambo moja, ila kupendana.”—Waroma 13:8.
Unaweza kupata mwono wa jinsi ambavyo maisha yangekuwa kwa kuchunguza programu ya elimu inayofanywa na Mashahidi wa Yehova katika nchi zaidi ya 230 duniani kote. Programu hiyo imeathiri watu wengi kwa njia ifaayo ambao zamani walikuwa wenye pupa au wahalifu hatari. Mtekaji-nyara mmoja wa hapo awali alisema hivi: “Baada ya muda niling’amua kwamba ili kumpendeza Mungu nilihitaji kuvua utu wangu wa kale na kuvaa utu mpya—ulio mpole na unaofanana na ule wa Kristo Yesu.”
Lakini, hata programu nzuri ya elimu haitawabadili wahalifu wote, labda hata si wengi wao. Ni nini kitakachowapata wale wanaokataa kubadilika?
Kuondolewa kwa Wakosaji
Wakosaji wa kukusudia hawataruhusiwa wawe raia wa Ufalme wa Mungu. Biblia husema: “Je, hamjui kwamba watu wasio waadilifu hawatarithi ufalme wa Mungu? Msiongozwe vibaya. Wala waasherati, . . . wala watu wenye pupa, . . . wala wanyang’anyi hawataurithi ufalme wa Mungu.” (1 Wakorintho 6:9, 10) “Wanyofu watakaa katika nchi . . . Bali waovu watatengwa na nchi.”—Mithali 2:21, 22.
Kulingana na Sheria ya Mungu katika nyakati za kale, mtekaji-nyara asiyetubu alipaswa kuuawa. (Kumbukumbu la Torati 24:7) Watu wenye pupa, kama vile watekaji-nyara, hawatakuwa na fungu lolote katika Ufalme wa Mungu. Wahalifu wa leo waweza kukwepa hukumu ya kibinadamu, lakini hawataweza kukwepa hukumu ya Mungu. Wakosaji wowote watalazimika kubadili njia zao ikiwa wataishi chini ya utawala wa uadilifu wa Ufalme wa Yehova.
Bila shaka, ikiwa hali zinazochangia uhalifu zitabaki, ndivyo itakavyokuwa na uhalifu. Hata hivyo, Ufalme wa Mungu hautaruhusu jambo hilo litukie, kwa kuwa Biblia inaahidi: “Ufalme . . . utavunja falme hizi zote vipande vipande,” kutia ndani watu wote wanaofanya mabaya. Unabii huo wa Biblia waendelea kusema kwamba Ufalme wa Mungu utasimama milele na milele. (Danieli 2:44) Ebu wazia mabadiliko yatakayotukia!
Ulimwengu Mpya wa Uadilifu
Fikiria unabii mwingine wa Biblia. Ni ule unaoeleza juu ya wakati ujao kwa maneno haya yenye kupendeza: “Nao watajenga nyumba na kukaa ndani yake; watapanda mizabibu, na kula matunda yake. Hawatajenga, akakaa mtu mwingine ndani yake; hawatapanda, akala mtu mwingine; maana kama siku za mti ndivyo zitakavyokuwa siku za watu wangu, na wateule wangu wataifurahia kazi ya mikono yao muda wa siku nyingi.”—Isaya 65:21, 22.
Ufalme wa Mungu utabadili sayari nzima. Wote walio hai watafurahia uhai kwa ukamili, wakisitawisha uwezo wao wa kiasili kwa kushiriki kazi inayoridhisha na tafrija yenye kujenga. Hali ulimwenguni pote zitakuwa kwamba hakuna mtu atakayefikiria kamwe kumteka nyara jirani yake. Kutakuwa na usalama kamili. (Mika 4:4) Hivyo, Ufalme wa Mungu utakuwa umekomesha kabisa utekaji-nyara hivi kwamba hakuna mtu atakayeufikiria tena.—Isaya 65:17.
[Picha katika ukurasa wa 10]
“Hapana mtu atakayewatia hofu.”—Mika 4:4