Kuishi na Kasoro ya Kujifunza
Sehemu ya siku aipendayo sana David mwenye umri wa miaka sita ni wakati wa hadithi. Yeye hupenda kusomewa na mama yake, naye hana tatizo kukumbuka anachosikia. Lakini David ana tatizo. Hawezi kujisomea mwenyewe. Kwa hakika, kazi yoyote inayohitaji uwezo wa kuona humfadhaisha.
Sarah yuko katika mwaka wake wa tatu shuleni, hata hivyo mwandiko wake ni wa kizembe sana isivyo kawaida. Herufi zake hufanyizwa isivyofaa, nyinginezo huandikwa kuelekea nyuma. Jambo linaloongeza hangaiko la wazazi wake ni uhakika wa kwamba Sarah hutatizika hata kuandika jina lake mwenyewe.
Josh, tineja mchanga, hufanya vizuri katika kila somo shuleni isipokuwa hisabati. Wazo la thamani za tarakimu humfadhaisha kabisa. Kutazama tarakimu tu humfanya Josh akasirike, na anapoketi kufanya mgawo wake wa masomo ya nyumbani wa hisabati, hali yake ya moyoni huzorota kwa haraka.
NI KASORO gani waliyo nayo David, Sarah, na Josh? Je, wao ni wavivu tu, wenye shingo ngumu, labda wenye akili ifanyayo kazi polepole? Sivyo hata kidogo. Kila mmoja wa watoto hawa ana akili ya kawaida ya kiwango kilichopita wastani. Hata hivyo, kila mmoja wao huzuiwa na kasoro fulani ya kujifunza. David ana dyslexia, neno litumiwalo kwa idadi kadhaa za matatizo ya kusoma. Tatizo la Sarah baya sana la kushindwa kuandika huitwa dysgraphia. Na kutoweza kwa Josh kufahamu mawazo ya hisabati huitwa dyscalculia. Hizi ni kasoro tatu tu za kujifunza. Kuna nyinginezo nyingi, na wataalamu fulani hukadiria kwamba zote huathiri angalau asilimia 10 ya watoto huko Marekani.
Kufafanua Kasoro za Kujifunza
Ni kweli, nyakati fulani vijana wengi huona kujifunza kuwa jambo gumu. Ingawa hivyo, kwa kawaida, hilo haliashirii kasoro ya kujifunza. Badala ya hivyo, huonyesha tu kwamba watoto wote wana uwezo na udhaifu tofauti-tofauti wa kujifunza. Wengine wana uwezo wenye nguvu wa kusikia; wanaweza kufahamu habari vizuri sana kwa kusikiliza. Wengine hukazia fikira sana upande wa kuona; wanajifunza vyema zaidi kwa kusoma. Hata hivyo, shuleni wanafunzi huwekwa pamoja darasani na wote wanatarajiwa kujifunza haidhuru ni njia gani ya kufundisha yatumiwa. Kwa sababu hiyo, ni jambo lisiloepukika kwamba wengine watakuwa na matatizo ya kujifunza.
Hata hivyo, kulingana na wataalamu fulani, kuna tofauti kati ya matatizo ya kujifunza yaliyo sahili na kasoro za kujifunza. Inaelezwa kwamba matatizo ya kujifunza yaweza kutatuliwa kwa subira na jitihada. Kinyume na hilo, kasoro za kujifunza husemekana kuwa zenye kina zaidi. “Ubongo wa mtoto aliye na kasoro ya kujifunza huelekea kutambua, kuchakata, au kukumbuka aina fulani za kazi ya kiakili katika namna iliyo na kasoro,” waandika Madakt. Paul na Esther Wender.a
Hata hivyo, kasoro ya kujifunza si lazima imaanishe kwamba mtoto ni mlemavu kiakili. Ili kueleza hili, akina Wender hufanya ulinganifu na viziwi wa namna za sauti, watu ambao hawawezi kutofautisha namna za sauti ya muziki. “Viziwi wa namna za sauti hawajaharibika ubongo na hawana kasoro yoyote na kusikia kwao,” waandika akina Wender. “Hakuna mtu awezaye kudokeza kwamba uziwi wa namna za sauti unasababishwa na uvivu, ufundishaji wa hali ya chini, au kichocheo cha hali ya chini.” Na ndivyo ilivyo na wale walio na kasoro za kujifunza, wao wasema. Mara nyingi tatizo, hukazia sehemu moja ya kujifunza.
Hili hueleza kwa nini watoto wengi walio na kasoro za kujifunza huwa na akili ipitayo kiwango cha wastani; kwa hakika wengine wana akili sana. Ni hali hii iliyo kinyume ambayo huwatahadharisha madaktari juu ya uwezekano wa kuwapo kwa kasoro ya kujifunza. Kitabu Why Is My Child Having Trouble at School? hueleza: “Mtoto mwenye kasoro ya kujifunza hufanya kazi miaka miwili au zaidi chini ya kiwango kitarajiwacho kwa umri wake na uwezo wake wa akili uliopimwa.” Yaani, tatizo si tu kwamba mtoto huyo ana tatizo kuwa katika kiwango sawa na marika wake. Badala ya hivyo, matokeo yake hayatoshani na uwezo wake mwenyewe unaotarajiwa.
Kuandaa Msaada Uhitajiwao
Athari za kihisia-moyo za kasoro ya kujifunza mara nyingi huongezea tatizo hilo. Watoto wenye kasoro za kujifunza wasipofanya vyema shuleni, wao huonwa na walimu na marika, labda hata familia zao kuwa walioshindwa. Kwa kuhuzunisha, watoto wengi kama hao husitawisha kujiona vibaya ambako kwaweza kuendelea kadiri wanavyokua. Hilo ni hangaiko halali, kwa kuwa kasoro za kujifunza kwa kawaida hazitoweki.b “Kasoro za kujifunza ni kasoro za muda wote wa maisha,” aandika Dakt. Larry B. Silver. “Kasoro zilezile ambazo huzuia kusoma, kuandika, na kufanya hisabati pia zitazuia michezo na utendaji mwingineo, maisha ya familia, na kupatana na marafiki.”
Kwa hiyo, ni muhimu kwamba watoto walio na kasoro za kujifunza wapate utegemezo wa kimzazi. “Watoto wajuao kwamba wazazi wao huwaunga mkono kwa nguvu wana msingi wa kusitawisha hisi ya kufaa na kujiheshimu,” chasema kitabu Parenting a Child With a Learning Disability.
Lakini ili kuwa waungaji-mkono, ni lazima wazazi kwanza wachunguze hisia zao wenyewe. Wazazi fulani huhisi kuwa wana hatia, kana kwamba wanapaswa kulaumiwa kwa kadiri fulani kwa sababu ya hali ya mtoto wao. Wengine hupatwa na wasiwasi, wakihisi kushindwa na magumu yaliyo mbele yao. Maitikio yote hayo hayasaidii. Hufanya wazazi washindwe kuchukua hatua yoyote na kumzuia mtoto kupata msaada ahitajio.
Kwa hiyo ikiwa mtaalamu mwenye ustadi aamua kwamba mtoto wako ana kasoro ya kujifunza, usikate tumaini. Kumbuka kwamba watoto walio na kasoro za kujifunza wanahitaji tu utegemezo wa ziada katika ustadi hususa wa kujifunza. Chukua wakati wa kufahamu programu yoyote ambayo huenda yapatikana katika eneo lenu kwa watoto walio na kasoro za kujifunza. Shule nyingi zina vifaa vizuri vya kushughulikia hali kama hizo kuliko zilivyokuwa miaka mingi iliyopita.
Wataalamu hukazia kwamba wapaswa kumsifu mtoto wako kwa chochote anachotimiza, hata kiwe kidogo kadiri gani. Uwe mkarimu wa kutoa pongezi. Kwa wakati huohuo, usipuuze nidhamu. Watoto wahitaji muundo, na ndivyo ilivyo hasa na wale walio na kasoro ya kujifunza. Acha mtoto wako ajue unachotarajia, na ushikamane na viwango ulivyoweka.
Hatimaye, jifunze kuona hali yako kwa njia halisi. Kitabu Parenting a Child With a Learning Disability hutolea hali hiyo kielezi hivi: “Wazia unakwenda kwenye mkahawa wako uupendao sana na kuitisha kipande cha nyama ya ndama. Mhudumiaji anapoweka sahani mbele yako, wagundua kwamba ni sehemu ya mbavu za kondoo. Vyote ni vyakula vitamu, lakini ulikuwa ukitarajia nyama ya ndama. Wazazi wengi wahitaji kubadili kufikiri kwao. Huenda hukuwa ukitarajia nyama ya kondoo, lakini wagundua kwamba ina ladha nzuri sana. Ndivyo ilivyo unapolea watoto walio na mahitaji ya kipekee.”
[Maelezo ya Chini]
a Uchunguzi fulani hudokeza kwamba kasoro za kujifunza huenda zikawa na sehemu ya tabia ya urithi au kwamba visababishi vya kimazingira, kama vile kusumishwa na madini ya risasi au dawa au alkoholi wakati wa ujauzito, huenda vikachangia. Hata hivyo, kisababishi au visababishi hususa havijulikani.
b Katika visa fulani, watoto hudhihirisha kasoro ya kujifunza ya muda kwa sababu ukuzi wao katika sehemu fulani unachelewa. Baada ya muda, watoto hao hukua na dalili hizo hutoweka.