Kuutazama Ulimwengu
Kuwasaidia Viziwi Katika Afrika
Gazeti “UNAD NEWS lapongeza upendezi usio na ubinafsi na jitihada za Mashahidi wa Yehova za kujifunza lugha ya ishara,” likasema jarida la Shirika la Kitaifa la Viziwi la Uganda (UNAD). Jarida hilo liliripoti kwamba kikundi cha Mashahidi wasio viziwi katika Kampala, Uganda, kimeanza kujifunza lugha ya ishara kikiwa na mradi wa kuwasaidia kiroho watu wenye matatizo ya kusikia katika nchi hiyo. Ripoti hiyo iliongezea kwamba wakalimani wawili wenye kutokeza “ni mapainia wa kawaida au [wahudumu] wa wakati wote katika mojawapo ya dini zenye kukua zaidi na kustahiwa zaidi duniani, dini inayojulikana sana kwa kushikamana kabisa na mafundisho ya kibiblia.”
Nawa Mikono Yako!
Shirika la Marekani la Mikrobiolojia hivi majuzi lilidhamini utafiti wa kujua ni watu wangapi hunawa mikono baada ya kwenda choo cha umma, laripoti The New York Times. Yaonekana kwamba karibu kila mtu anajua kwamba anapaswa kunawa mikono. Katika uchunguzi uliofanywa kupitia simu kwa watu wazima 1,004, asilimia 94 walidai wao hunawa mikono baada ya kwenda choo cha umma. Lakini kweli wanafanya hivyo? Watafiti waliochunguza vyoo katika majiji matano makubwa ya Marekani walipata kwamba kati ya watu 6,333, ni asilimia 61 tu ya wanaume na asilimia 74 ya wanawake ndio walionawa mikono baada ya kwenda choo. Mikono michafu hueneza maradhi kwa urahisi, na mtu mmoja tu anayeshughulikia vyakula kwa mikono michafu aweza kufanya makumi ya watu kuwa wagonjwa. Tatizo hilo laweza kuchangiwa kwa sehemu na ukosefu wa mwelekezo wa wazazi. “Mara nyingi leo akina mama hawaambii watoto wao wanawe mikono,” akasema Dakt. Gail Cassell. “Shule haziambii watoto wanawe mikono baada ya kutoka choo. Tunahitaji kukumbushwa kwamba hilo ni jambo muhimu.”
Ucheke, Ukaishi Muda Mrefu?
Kwa muda mrefu imeaminiwa kwamba kucheka ni tiba nzuri. Miaka kumi ambayo imepita wanasayansi kwenye Chuo Kikuu cha New York waliamua kugundua ni kwa nini kucheka ni tiba nzuri. Hivi majuzi wao walifunua ugunduzi wao kwamba kucheka husaidia kuchochea kuachiliwa kwa homoni zenye nguvu ambazo huupa nishati mfumo wa kinga wa mtu. Kikundi kimoja cha homoni, kiitwacho cytokines, kimepatikana kuendeleza utendaji wa chembe nyeupe za damu, ambazo huhitajiwa kukinza maambukizo ya virusi na bakteria na ambazo huharibu chembe ziwezazo kusababisha kansa. Hizo ni baadhi tu ya “kemikali ambazo viwango vyazo huongezeka kwa kucheka,” lasema The Sunday Times la London. Uhusiano uliopo baina ya kucheka na cytokines umefanya watafiti wengine waziite homoni zenye furaha. Hivyo, gazeti hilo lataja kucheka kuwa “njia ya kuishi muda mrefu.”
Kanisa Katoliki Limo Katika “Wakati wa Matatizo”
Hati iliyotolewa na kikundi fulani kilichotia ndani maaskofu saba yafafanua Kanisa Katoliki kuwa katika “wakati wa matatizo,” laripoti Star-Telegram, la Arlington, Texas. Hati hiyo “inaomba kanisa lisuluhishe migawanyiko yalo,” lasema gazeti hilo la habari. Mahoji yaonyesha kwamba wengi wa Wakatoliki milioni 60 katika Marekani hawakubaliani na mafundisho ya kanisa kama vile makasisi kutofunga ndoa na kutawazwa kwa wanawake. Katika mkutano wa kutoa taarifa ya hati hiyo kwa vyombo vya habari, kadinali Joseph Bernardin ambaye amekufa alitaja hangaiko lake kuhusu “mgawanyiko unaozidi kukua kanisani na, nyakati nyingine, uchoyo mwingi” ambao huhitilafiana na utume wa kanisa. “Tokeo ni kwamba, muungano wa kanisa unatishwa,” akasema. “Washiriki waaminifu wa kanisa wamechoka na ushahidi wetu kwa serikali, jumuiya na utamaduni umedhoofishwa.”
Maendeleo kwa Kuchunguza Nyuma
Kabla ya transista, kulikuwa na chubu ombwe. Sasa watafiti wanachunguza nyuma. “Tunachunguza tena chubu ombwe za miaka 1940,” asema mwanafizikia Griff L. Bilbro, wa Chuo Kikuu cha Jimbo la North Carolina. “Lakini sasa tunatumia kwa faida vifaa vipya na zana za ubuni wa kompyuta za kukadiria uwezo wa chubu ombwe kwa marudio ya juu sana, ili zitumiwe katika rada na simu za kuchukulika.” Tofauti moja kati ya chubu za zamani na mpya ni saizi. Chubu mpya ni ndogo sana nazo zatofautiana sana zikikaribia kutoshana na kichwa cha mshale wa kiberiti. Hizo hutengenezwa kwa “kufunika elektrodi kwa almasi, kisha kuondoa hewa yote kutoka ndani,” lasema gazeti Science News. “Tofauti kubwa kati ya chubu ombwe mpya za almasi na balbu kubwa za kioo za miaka 50 iliyopita ni joto. Chubu za zamani zilihitajika kuwaka nyekundu ili kuweza kupitisha mikondo ya elektroni. Chubu mpya hutokeza mkondo kwa halijoto ya nyumba.” Mbali na kudumu zaidi kuliko vipitisha-umeme vilivyo hafifu na chipu za kompyuta, hizo chubu mpya pia hufanya bora zaidi kwa viwango vya juu vya joto, volteji, na mnururisho.
Dolfini Waokoaji
Mtu mmoja aliyekuwa akiogelea katika Bahari Nyekundu huenda aliokolewa na kikundi cha dolfini, laripoti Journal of Commerce. Mark Richardson, wa Uingereza, alikuwa akiogelea katika pwani ya Misri aliposhambuliwa na papa. Baada ya kuumwa upande mmoja wa mwili na mkono, alizingirwa na dolfini watatu wenye pua kama chupa “wakipigapiga mapezi yao na mikia ili kuogopesha papa huyo.” Kisha dolfini hao “wakaendelea kumzingira Bw. Richardson mpaka marafiki wake wakamsaidia.” Kulingana na Journal, “tabia hiyo ya dolfini ni ya kawaida wakati dolfini wa kike wanapolinda watoto wao.”
Komunyo “Iliyopakiwa Tayari”
Mfanyabiashara mmoja wa Marekani, Jim Johnson, anatokeza sakramenti ambazo tayari zimepakiwa na zenye kutumika mara moja katika Komunyo ya ibada za kanisa, laripoti Christianity Today. Vikombe vidogo vya plastiki vyenye rangi ya zambarau vinavyotoshana na kufanana na kiwekeo cha mtindi wa kahawa, vina kiasi kidogo cha maji ya zabibu au divai. Vikombe hivyo pia vina mkate mdogo mwembamba usiotiwa chachu uliofungiwa ndani ya vibandiko viwili. Kulingana na Johnson, bidhaa hiyo ina mafaa kwa vile inatengenezwa kwa haraka na haihitaji usafishaji mwingi baadaye, gharama, na ni safi kiafya. Zaidi ya makanisa 4,000 tayari yameanza kutumia bidhaa hiyo mpya, ingawa malalamiko fulani yamezushwa kuhusu kuona Komunyo kuwa “biashara kubwa.” Johnson ajibu: “Yesu aliandaa chakula chepesi cha kwanza alipolisha umati wa watu.”
Njiwa Wenye Kusafiri kwa Ukawaida
Kwa muda mrefu njiwa katika London wameonekana wakipanda magari-moshi ya chini ya ardhi pamoja na watu, laripoti gazeti New Scientist. Kwa kuongezea, watu fulani hudai kwamba ndege hao hata hujua stesheni wanayopaswa kushuka. Baada ya kuombwa na gazeti hilo, wasomaji kadhaa waliandika wakisema mambo waliyojionea kuhusiana na ndege hao. Kwa mfano, mtu mmoja aliandika: “Katika kipindi cha 1974-1976, mara nyingi nilikutana na njiwa mmoja mwenye rangi ya nyekundu hafifu-hafifu akipanda gari-moshi la chini ya ardhi katika Paddington na kushuka kwenye stesheni iliyofuata.” Mtu mwingine aliona jambo kama hilo nyuma katika 1965. Inaonekana kwamba njiwa wamekuwa wakikwepa kulipa nauli katika mfumo wa reli ya chini ya ardhi ya London kwa miaka ipatayo 30!
Jimbo Moja la Australia Lahalalisha Mauaji ya Huruma
Mtu mmoja katika Mkoa wa Kaskazini wa Australia amekuwa mtu wa kwanza kufa chini ya sheria mpya ya jimbo hilo inayoruhusu mtu kujiua kwa kusaidiwa na daktari, laripoti The New York Times. Mtu huyo alikuwa katika miaka ya 60 naye alikuwa akiugua kansa ya tezi-shahawa ambayo ilionwa kwamba ingemwua. “Hii ndiyo mara ya kwanza kabisa ambapo mtu amemaliza uhai wake kisheria,” akasema Dakt. Philip Nitschke, tabibu aliyempa dawa hizo za barbiturates zilizomwua. “Mtu huyo alikuwa ameunganishwa kwa mashine ambayo ilimruhusu kuanzisha mwendo wa kifo chake mwenyewe kwa kubonyeza kibonyezo kilichokuwa kwenye kompyuta ndogo kando ya kitanda,” akaeleza Nitschke. Hata hivyo, sheria hiyo mpya inapata upinzani mkali. Bunge la kitaifa sasa linafikiria kutunga sheria itakayoharamisha sheria hiyo, na sheria hiyo inabishaniwa mahakamani na baadhi ya madaktari na makanisa.
Makanisa Yamegeuzwa
Kulingana na gazeti la habari la Uholanzi Het Overijssels Dagblad, majengo yapatayo 300 ya kanisa katika Uholanzi yamegeuzwa kuwa maduka, nyumba za kuishi, majumba ya wonyesho, na majengo ya ofisi. Kwa sababu hudhurio la kanisa katika Uholanzi limepunguka kwa karibu asilimia 50 kwa kulinganisha na miaka 15 ambayo imepita, makanisa mengi hufurahi kupata mtu aliye tayari kuwaondolea mzigo wa kudumisha majengo hayo. Baadhi ya majengo ya kanisa yameuzwa kwa kiasi kidogo sana cha fedha kama guilda moja (karibu senti 60, za Marekani)! Lakini kugeuza jengo lililokuwa kanisa kuwa la kibiashara kunatokeza uchungu mwingi wa kihisia moyo, hasa miongoni mwa wazee-wazee. Mtu mmoja mwenye mamlaka alisema: “Wamehudhuria hapo kwa miaka mingi. Walibatizwa na kufunga ndoa hapo, na sasa wanaona watu wakifanya mambo ya kawaida sana hapo . . . , hata wakilaani.”