Linda Uwezo Wako wa Kusikia!
UCHUNGUZI mmoja wa majuzi wa vijana 400 katika Ufaransa ulifunua kwamba 1 kati ya kila 5 ana tatizo la kusikia. Uchunguzi kama huo uliofanywa mwongo mmoja uliopita ulionyesha kwamba ni kijana 1 tu kati ya kila vijana 10 aliyekuwa na matatizo ya kusikia. Likichukua hatua dhidi ya ongezeko hilo la ghafula la tatizo la kusikia miongoni mwa vijana, mapema mwaka huu Bunge la Kitaifa la Ufaransa lilipiga kura kupunguza kiasi cha sauti za stirio kufikia desibeli 100.
Sauti za juu zinazotoka kwenye hedifoni za stirio ndizo visababishi vikubwa vya matatizo ya kusikia. Mpasuaji wa sikio Jean-Pierre Cave asema kwamba kiasi cha sauti kipitacho desibeli 100 chaweza kuharibu kabisa sikio baada ya muda wa saa chache. Inachukua dakika chache tu kwa madhara hayo kutokea ikiwa sauti ni zaidi ya desibeli 115. Duka la FNAC, ambalo ndilo duka mashuhuri zaidi la kuuza vifaa vya elektroni katika Ufaransa, lasema kwamba nyingi za stirio ambazo linauza hutokeza sauti inayozidi desibeli 100. Stirio nyinginezo za kibinafsi zaweza kutoa desibeli 126, hiyo ikiwa ina nguvu mara 400 kuliko za desibeli 100!
Maonyesho ya roki huenda yanadhuru vijana wengi hata zaidi kuliko stirio, kulingana na mtaalamu wa sikio Mfaransa Christian Meyer-Bisch. Hakika, wahudhuriaji wa kawaida wa maonyesho ya muziki wa roki wana tatizo kubwa la kusikia kwa kulinganisha na vijana wenye afya wenye umri wa miaka 18. Si ajabu kwamba mbunge mdogo wa Bunge la Kitaifa la Ufaransa Jean-François Mattei alionya: “Tunatokeza kizazi cha viziwi.”
Basi ili kulinda uwezo wako wa kusikia, jihadhari na kiasi cha juu cha sauti!