Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g94 3/8 kur. 28-29
  • Kuutazama Ulimwengu

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Kuutazama Ulimwengu
  • Amkeni!—1994
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Waombaombaji Katika Mavazi ya Kondoo
  • Wadhulumiwa Wengine Zaidi Washtaki Kanisa
  • Nani Mwenye Watoto Wengi Zaidi?
  • Uwasiliano wa Mzazi Kabla ya Kuzaliwa
  • UKIMWI Katika Côte d’Ivoire
  • Makanisa Katika Hangari Yashiriki Lawama
  • Vifo Wakati wa Ujauzito
  • Kuharibika kwa Desibeli
  • Kuzuia Kujiua
  • Jiji la Kibiblia Lafukuliwa
  • Linda Uwezo Wako wa Kusikia!
    Amkeni!—1997
  • UKIMWI—Matokeo Yenye Msiba Mkubwa kwa Watoto
    Amkeni!—1992
  • Watoto—Ni Faida au Ni Hasara?
    Amkeni!—1993
  • Kusaidia Wale Walio na UKIMWI
    Amkeni!—1994
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1994
g94 3/8 kur. 28-29

Kuutazama Ulimwengu

Waombaombaji Katika Mavazi ya Kondoo

Katika China, kuomba-omba kunakuwa njia ya kutajirika kwa wadanganyifu stadi wasiojali, laripoti Worker’s Daily. Waomba-ombaji watoto wakiona mtu wamdhaniaye ana sura ya huruma, wao “huanza kulia machozi na kusema ‘mjomba, shangazi—njaa yaniuma.’ Mtu huyo mwenye uwezo wa kuchanga huwa hana namna ila kutoa,” lasema gazeti hilo la Kichina. Akina mama hufinya watoto wao kuwalilisha kisha hudai kwamba “watoto wao ni wagonjwa na hawana fedha za kuona madaktari.” Gazeti hilo lasema, walio wazee-wazee hupiga magoti, “hufanya shikamoo ya kunyenyekea sana, na kushurutisha kuchangiwa.” Kuhoji waomba-ombaji 25,000 kwa kipindi cha zaidi ya miaka mitatu kulifunua kwamba ni asilimia 8.5 tu kati yao wasiokuwa na mtu wa kutegemea na ni asilimia 18.5 tu ya wale walioonekana kuwa wasiojiweza ambao kwa kweli walikuwa hivyo, akasema ofisa Mchina.

Wadhulumiwa Wengine Zaidi Washtaki Kanisa

Wadhulumiwa waliotumiwa vibaya kingono katika taasisi za kidini za Australia ziendeshwazo na “mabradha” Wakatoliki wanaungana pamoja kuchukua ile ambayo kichapo The Canberra Times chaeleza kuwa ni moja ya hatua kubwa zaidi za kundi la watu katika historia ya kisheria katika Australia. Ombi la kuruhusu maandishi rasmi zaidi ya 250 yaandikishwe kutaka ridhaa liliwasilishwa mahakamani hivi majuzi na shirika linalowakilisha watu waliotendwa vibaya wakiwa watoto. Yasemekana waliendelea kutendwa vibaya kuanzia miaka ya 1940 hadi ya 1980, na washtakiwa wakuu waliotajwa katika maandishi rasmi ni kutia na dayosisi kuu kadhaa za Kikatoliki. Bradha mmoja Mmaria tayari ameshtakiwa ngono ya kutumia nguvu. Mwanasheria anayewakilisha mdhulumiwa katika kesi hiyo alisema hivi: “Tunachoona ni dalili ndogo tu. Kuna matendo chungu nzima ambayo yaelekea yatatukia miaka michache ijayo. Taasisi zote za kidini zingehitaji kuhangaika.”

Nani Mwenye Watoto Wengi Zaidi?

Ni taifa jipi lenye kiasi cha juu zaidi cha uzazi ulimwenguni? Kulingana na Umoja wa Mataifa, katika nafasi ya kwanza ipo Rwanda, ambako wanawake wenye umri wa kuzaa watoto huzaa wastani wa watoto 8.5 kila mmoja. Kisha kuna Malawi ikiwa na watoto 7.6, Côte d’Ivoire ikiwa na 7.4, na Uganda ikiwa na 7.3. Wastani wa ulimwengu ni watoto 3.3, hali kwa nchi zilizositawi ni 1.9. Kwa kushangaza, taifa lenye kiasi cha chini zaidi cha uzazi ulimwenguni, ambalo lina watoto 1.3 tu kwa kila mwanamke mwenye umri wa kuzaa, ni Italia iliyokuwa ikizaa sana. Zile siku ilipokuwa kawaida ya familia ya Kiitalia kuwa na watoto watatu, wanne, au zaidi zimekwisha. Kwa wazi, zile nyakati ambazo Waitalia walifuata maagizo ya Kanisa Katoliki kuhusu kudhibiti uzazi na kuzuia-mimba zimepita.

Uwasiliano wa Mzazi Kabla ya Kuzaliwa

Kwa nini kusema na mtoto mchanga ambaye angali katika tumbo la uzazi la mama yake? Katika gazeti la Brazili Veja, daktari Mswisi wa magonjwa ya akili ya watoto Bertrand Cramer asema hivi: “Maongezi ya aina hiyo huwaruhusu wazazi, hasa mama, kuwa na uwasiliano wa kwanza na mtoto kabla ya kuzaliwa.” Ingawa bado haijulikani kabisa ni jinsi gani mtoto mchanga hufasiri maongezi ya jinsi hiyo, “uhakika mmoja tu uliopo ni kwamba tayari kumbukumbu huwa likifanya kazi, jambo ambalo si la kawaida,” kulingana na Cramer. Zaidi ya hilo, baada ya kuzaa, kwa kuwa mtoto mchanga hutazama kwa makini hali za usoni za wazazi, Dakt. Cramer asema kwamba “matukio madogo yote maishani huwa tayari ni ya maana kubwa sana katika zile siku za kwanza.” Hata hivyo, yeye atahadharisha hivi: “Badala ya kuhangaikia mno kuwa na watoto wakamilifu, wazazi wapaswa kuepuka kuwa na uhusiano hafifu pamoja na watoto wao, jambo ambalo huenda likawafanya wawe watu wazima wenye akili zisizo timamu, wenye kushuka moyo. Yatosha kutamani kuwa na watoto timamu—wala si mabingwa wawezao kushinda zawadi ya Nobeli.”

UKIMWI Katika Côte d’Ivoire

Kati ya wakaaji karibu milioni 13 wa Côte d’Ivoire, Afrika Magharibi, angalau 1 kati ya watu wazima 10 ameambukizwa virusi ya UKIMWI, hiyo ikifanya hilo liwe moja la majimbo yaliyoathiriwa vibaya zaidi ulimwenguni. Madaktari wasema kwamba tayari UKIMWI ndio namba moja kwa kusababisha kifo miongoni mwa vijana wakubwa katika Abidjan, jiji kuu la taifa, na kwamba kipuku hicho kimefika karibu kila sehemu ya nchi. Serikali ya Ufaransa imesema kwamba itatoa msaada mkubwa zaidi wa kifedha kupambana na kipuku cha UKIMWI katika Côte d’Ivoire. Hata hivyo, madaktari Wafaransa na mawaziri wa serikali wasema kwamba shughuli ya kimataifa ya kutengeneza madawa haijasaidia sana nchi zinazositawi katika pambano lazo dhidi ya UKIMWI. Gazeti la Kifaransa Le Monde laandika kwamba miongozo inayowaamulia watengeneza-madawa bei za kuyauza imeinua sana bei za madawa yahitajiwayo kupambana na virusi kutibu wenye UKIMWI zikakaribia kutoweza kupatikana na watu wengi katika Afrika.

Makanisa Katika Hangari Yashiriki Lawama

Karibu Wayahudi nusu-milioni wasemwa waliuawa kimakusudi katika Hangari wakati wa Vita ya Ulimwengu 2. Makanisa ya Jumuiya ya Wakristo yaliitikiaje katika kipindi hicho cha kuogofya? Ripoti iliyotayarishwa na wasomi wa kidini wa imani za Kilutheri, Kibaptisti, na Katoliki ya Roma yafunua kwamba makanisa hayo “yasikitika kwamba hayakutenda kwa uthabiti zaidi kuwalinda raia-wenzao Wayahudi katika nchi yao.” Kwa nini makanisa yalikosa sana nia ya kupinga mnyanyaso huo? Msimamo huo wa kusita ulisemwa kuwa “tokeo la pokeo ambalo makanisa yamekuwa nalo la kupinga dini ya Kiyahudi, na pia uhusiano wayo wa karibu na wenye mamlaka tangu zamani za kale,” lasema Süddeutsche Zeitung.

Vifo Wakati wa Ujauzito

“Kuzaa ni kimoja cha visababishi vikuu vya kifo miongoni mwa wanawake wenye umri wa kuzaa katika nchi zinazositawi,” yataarifu 1992 Report iliyotolewa na Hazina ya Umoja wa Mataifa ya Kusaidia Watu.[1] Kila siku wakati wa 1992, wastani wa wanawake 1,359 katika ulimwengu unaositawi walikufa kutokana na matatizo yaliyohusiana na ujauzito au kuzaa. Tofauti na hivyo, yasema ripoti hiyo, mwaka huo huo, vifo vilivyohusiana na ujauzito katika nchi zilizositawi viliua watu 11 kwa siku.[2] Ingawa hatari ya mwanamke kufa wakati wa ujauzito katika nchi fulani zilizositawi hutofautiana kuanzia 1 kati ya 6,000 hadi 1 kati ya 9,000, hatari katika nchi zenye usitawi wa chini zaidi ni 1 kati ya 20. [3][4] Tarakimu hizo, yasema UNFPA, zafunua “tofauti kubwa sana kati ya ulimwengu unaositawi na ule uliositawi.”

Kuharibika kwa Desibeli

Mmoja kati ya vijana 4 Ufaransa wasikilizao muziki katika visikizo vya kichwani vya stirio ya kibinafsi huenda sasa akaharibika uwezo wa kusikia, laripoti gazeti la Paris Le Point. Muziki wa desibeli nyingi ndio wa kulaumiwa. Zaidi ya theluthi mbili za vijana Ufaransa wana stirio za kibinafsi. Nyingi za stirio hizo huingiza kuanzia desibeli 100 hadi 110 za sauti ya nishati ya juu moja kwa moja ndani ya kijia cha sikio. Ili kuepuka uharibifu wa daima wa uwezo wa kusikia, madaktari wasema kwamba kusikiliza kusiendelee kwa muda uzidio dakika 40 kwa kiwango cha desibeli 100, na dakika tano tu kwa kiwango cha desibeli 110! Hata hivyo, vijana wengi wakiri kwamba wakati wao wa kusikiliza kwa kutumia visikizo vya kichwani huzidi saa tano kwa siku. Kwa kufikiria hesabu ya vijana wanaoendelea kupoteza uwezo wa kusikia mapema mno, Shirika la Afya Ulimwenguni limependekeza kuwekwe kiwango kisichozidi desibeli 90 za mtoko wa sauti kwa stirio za kibinafsi.

Kuzuia Kujiua

Kitovu kipya cha kuzuia visa vya kujiua na vya kujaribu kujiua kimeanzishwa kwenye Hospitali ya Karolinska katika Stockholm, Swedeni. Mkuu wa kitovu, Profesa Msaidizi Danuta Wasserman, asema katika gazeti la kila siku la Swedeni Dagens Nyheter kwamba kimoja cha visababishi vingi vya visa vya kujiua na vya kujaribu kujiua ni ukosefu wa uhakika ambao watu mmoja-mmoja watakao kujiua huwa nao ndani yao wenyewe na katika watu wengine. Kwa hiyo mwanamke huyo adokeza kwamba uwasiliano wa karibu zaidi pamoja na wengine na hisiamwenzi nyingi zaidi zitapunguza visa vya kujiua. “Katika Swedeni kuna elekeo lenye kusitawi la kutojali sana wengine na kuishi kwa kujifaidi binafsi tu,” asema mwanamke huyo. Yeye adokeza kwamba mawazo ya kujiua yakiendelea, mtu apaswa “aepuke kujifanya hana tatizo na kujitenga peke yake” na apaswa “kusema na mtu fulani.” Machunguzi ya muda mrefu kuhusu wale ambao wamejaribu kujiua yaonyesha kwamba asilimia 90 kati yao huja hatimaye kuwa na maisha ya kawaida baada ya ile shida kumalizika.

Jiji la Kibiblia Lafukuliwa

Le Figaro, gazeti la Kifaransa, laripoti kwamba kikoa cha waakiolojia Wajapani kimefukua magofu ya moja la majiji matano ya kale ya Kibiblia liitwalo Afeki. Kwa muda wa miaka wasomi wamejaribu bila mafanikio kuhusianisha mahali lilipokuwa jiji hilo la kale na kijiji cha ki-siku-hizi cha Afriki, au Fiki, kilometa tano mashariki mwa Bahari ya Galilaya. Hata hivyo, mwakiolojia Hiroshi Kanaseki aamini kwamba uvumbuzi wa sehemu moja ya ukuta wa kale huko ʽEn Gev, ulio kwenye ufuo wa Bahari ya Galilaya, wathibitisha kwamba kwa kweli hapo ndipo lilipokuwa jiji hili hususa la Kibiblia la Afeki. Limetajwa katika Biblia kwenye 1 Wafalme 20:26 kuwa mahali ambapo Mfalme Mshamu Ben-hadadi 2 alishindwa na majeshi ya Israeli yakiongozwa na Mfalme Ahabu.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki