Kelele—Yale Uwezayo Kufanya Kuihusu
MWISHONI mwa siku yenye kuchosha, wapata usingizi mzito. Kwa ghafula, waamshwa na kelele za mbwa wanaobweka katika ujirani. Wajipindua kitandani na kutumaini kuwa kelele hiyo yenye kusumbua itaisha upesi. Lakini yaendelea. Tena na tena mbwa waendelea kubweka. Ukiwa umekasirika, na kuvunjika moyo kutokana na kukosa usingizi, na sasa ukiwa macho kabisa, wawaza jinsi majirani wako wawezavyo kuchukuliana na kelele hizo.
Watu hutofautiana sana katika jinsi wanavyovumilia kelele. Wafanyakazi wa viwanja vya ndege ambao huishi karibu na barabara ya ndege hawasumbuliwi sana na kelele za ndege kama wale ambao kazi yao haihusiani na ndege. Mke wa nyumbani ambaye hutumia kisaga-chakula kinachotumia umeme huvumilia kelele hiyo vema zaidi kuliko mtu aliye katika chumba kingine anayejaribu kusoma kitabu ama kutazama televisheni.
Uchafuzi wa Kelele Ni Nini?
Nchi hutofautiana katika njia ambayo hizo hufafanua uchafuzi wa kelele. Katika Mexico, kelele ni “sauti yoyote isiyopendeza ambayo inasumbua au ni yenye madhara kwa watu.” Katika New Zealand kelele hufikiriwa kuwa imezidi ikiwa “ni ya namna inayovuruga amani, faraja na starehe ya mtu yeyote kupita kiasi.”
Wanasayansi wawili mashuhuri, Alexander Graham Bell, mvumbuzi wa simu, na Heinrich Hertz, mwanafizikia Mjerumani, wanahusianishwa kwa ukaribu na upimaji wa sauti. Kipimo cha Bel, au zijulikanazo sana kama decibel (sehemu moja ya kumi ya bel), hupima ukubwa wa sauti, ilhali hezi hupima kidatu, au marudio, ya sauti. Kelele inapopimwa, kwa jumla ripoti hurejezea kiwango cha decibel ya sauti.a
Lakini ni nani aamuaye ni kiasi gani cha usumbufu ambacho sauti husababisha? Wewe, mwenye kuisikia! “Likiwa kama kitu cha kukadiria sauti yenye kusumbua, sikio la binadamu labaki likiwa kigunduzi bora zaidi,” laonelea gazeti The Independent la London.
Matokeo ya Kelele
Kwa kuwa sikio ndilo “kigunduzi bora zaidi” cha kelele, bila shaka ndicho kiungo kielekeacho kuumizwa zaidi na kelele. Madhara kwa chembe za neva zilizo nyetivu za sikio lako la ndani yaweza kutokeza uziwi kabisa. Ni kweli kwamba watu hutofautiana katika kuitikia sauti kubwa. Lakini kuwapo mahali penye sauti zinazozidi decibel 80 hadi 90 kwa kurudia-rudia kwaweza kutokeza uziwi polepole. Kwa kweli, kadiri viwango vya kelele vilivyo juu, ndivyo uwavyo na wakati mchache zaidi ulio salama wa kuwa katika mazingira hayo kabla hujapatwa na madhara ya kusikia.
Gazeti New Scientist huripoti kuwa vinanda vingi vya kibinafsi vinavyouzwa huko Ufaransa vyaweza kutoa kufikia decibel 113. Likitaja uchunguzi mmoja, gazeti hilo lilionelea kwamba “muziki wa roki ukichezwa kwa sauti ya juu zaidi kwa muda wa saa moja katika mashini za kuchezea diski songamano za kibinafsi mara nyingi zilipita decibel 100 na kufikia vilele vya karibu decibel 127.” Tokeo lililo baya hata zaidi ni la kelele inayofanyizwa katika maonyesho ya muziki ambapo wachezaji na wahudhuriaji wako pamoja. Mchunguzi mmoja alipata watu wakiwa wamerundamana karibu na vikuza-sauti vilivyokuwa vimerundikwa kimoja juu ya kingine wakiwa katika hali ya kuzubaa. “Nilikuwa sioni vizuri, mwili wangu ukivuma kwa mdundo mzito wa besi,” asimulia, “na kelele hiyo ilifanya masikio yangu yaniume.”
Kelele yaweza kuwa na matokeo gani kwako? Mamlaka moja yataarifu: “Kelele za daima za kiasi hadi viwango vya juu husababisha mkazo, uchovu, na kuudhika.” “Kuteswa-teswa na kelele hakumfanyi mtu awe bila furaha tu, bali kwaweza kumfanya mtu awe mnyong’onyevu kimwili na kihisia-moyo,” aonelea Profesa Gerald Fleischer, wa Chuo Kikuu cha Giessen, Ujerumani. Kulingana na Profesa Makis Tsapogas, wakati kelele inapokuwa chanzo kikuu cha mkazo, yaweza kusababisha mshuko wa moyo na pia magonjwa mengine ya viungo.
Kukaa mahali palipo na kelele kwa muda mrefu kwaweza kuathiri utu wako. Wakati watafiti wa serikali ya Uingereza walipowauliza wahasiriwa wa kelele walivyohisi kuhusu wale waliosababisha uchafuzi wa kelele, wahasiriwa hao walisema kuwa walihisi chuki, kulipiza kisasi, na hata kuwaua kimakusudi. Kwa upande ule mwingine, wanaofanya kelele mara nyingi huwa wenye kuchokozeka wanapokuwa shabaha ya malalamiko ya kurudia-rudia. “Kelele hupunguzia watu tabia ya kufikiria wengine kuliko wao wenyewe na hutokeza uchokozi na uhasama,” adai mfanya-kampeni mmoja dhidi ya kelele.
Wengi ambao wameteseka kutokana na uchafuzi wa kelele wanatambua kuwa wanapoteza polepole uwezo wao wa kukinza usumbufu. Wao wana maoni kama ya mwanamke mmoja ambaye majirani wake wenye kelele walikuwa wakicheza muziki kwa sauti ya juu kila wakati: “Unapolazimishwa kusikiliza jambo usilotaka kusikiza, hilo lakufanya uwe mnyong’onyevu. . . . Hata wakati kelele ilipoisha, tulikuwa tukiingojea ianze tena.”
Basi, je, hakuna njia yoyote ya kukabiliana na uchafuzi wa kelele?
Lile Uwezalo Kufanya
Kelele ikiwa imeenea sana hivyo, watu wengi kwa kawaida hawatambui wanapowasumbua wengine. Ikiwa wangejua, wengine bila shaka wangeacha kufanya huo utendaji wenye kuudhi. Ni kwa sababu hii kwamba kumwendea jirani mwenye kelele kwa njia yenye urafiki kwaweza kusaidia. Mtu mmoja alikasirika kwa sababu ya malalamiko rasmi ya majirani wake kuwa alikuwa mwenye kelele. Alisema: “Nilifikiri kuwa wangekuja kwangu moja kwa moja kuniona ikiwa walikasirishwa na kelele hiyo.” Mama aliyeandaa karamu kwa ajili ya watoto fulani wachanga alishangaa alipokabiliwa na ofisa mmoja akichunguza lalamiko kuhusu kelele hiyo. “Ingekuwa bora kama waliolalamika wangeubisha mlango wangu na kuniambia ikiwa hawakufurahi,” yeye akaonelea. Basi, haishangazi kuwa ofisa mmoja Mwingereza wa afya ya kimazingira alishangaa kugundua kwamba asilimia 80 ya wale wanaolalamika kuhusu kelele ya nyumbani hawajawahi kuwaomba majirani wao wapunguze kelele.
Kujizuia kwa watu kuzungumza na majirani wao wenye kelele huonyesha ukosefu wa staha kati yao. ‘Nikitaka kucheza muziki wangu, naweza. Ni haki yangu!’ ndilo jibu watarajialo kupata na mara nyingi ndilo wapatalo. Wanaogopa kuwa pendekezo la fadhili la kupunguza sauti laweza kuongoza kwenye makabiliano ikiwa jirani mwenye kelele aona lalamiko lao kuwa lisilofaa. Ni wonyesho mbaya kama nini wa jumuiya ya wakati wa sasa! Ni kama tu taarifa ya Biblia kwamba katika hizi “nyakati za hatari zilizo ngumu kushughulika nazo,” watu kwa ujumla watakuwa ‘wenye kujipenda wenyewe, wenye kiburi, wakali, na wenye vichwa vigumu’!—2 Timotheo 3:1-4.
Yategemea sana jinsi mhasiriwa anavyomwendea. Gazeti Woman’s Weekly lilitoa hali ifuatayo ya jinsi ya kutatua hali yenye uvutano baada ya lalamiko lenye uchokozi kukosa kufaulu: “Kwa njia yenye uchangamfu na yenye kueleweka waweza kusema, ‘Nasikitika—nilikasirika sana lakini mimi huwa mchovu sana ninapokosa kulala’ labda ndilo tu lihitajiwalo ili kupatana tena na [majirani wenye kujitetea].” Huenda ikawa watasogeza vyombo vyao vya sauti kutoka kwenye ukuta unaowaunganisha na labda kupunguza sauti kwa njia fulani.
Kwa uhalisi, ni kwenye manufaa kudumisha mahusiano mazuri na majirani wako. Mamlaka za serikali za mahali fulani hutoa huduma za upatanisho ili kuwapatanisha majirani wanaopingana. Kwa kufikiria hisia zenye uhasama ambazo malalamishi rasmi husababisha, kuita ofisa wa kutekeleza sheria kwapaswa kuonwa kuwa “jambo la mwisho kabisa mengine yote yakishindwa.”
Ikiwa watazamia kuhamia makao mapya, utaona likiwa jambo la hekima kuchunguza vyanzo viwezekanavyo vya usumbufu wa kelele kabla ya kutamatisha kandarasi. Mawakala wa uuzaji wa nyumba wapendekeza kwamba utembelee mahali unapotarajia kuishi katika saa tofauti za siku ili uchunguze kelele. Waweza kuwauliza majirani maoni yao. Ukikabiliwa na matatizo baada ya kuhamia makao yako mapya, jaribu kuyatatua kwa njia yenye ujirani. Kwenda mahakamani kwa kawaida huchochea uhasama.
Lakini namna gani ikiwa waishi katika ujirani wenye kelele na huna namna ya kuhamia kwingine? Je, utateseka bila mwisho? Si lazima.
Jinsi ya Kupata Ulinzi Dhidi ya Kelele
Tazama uone ni nini uwezalo kufanya ili kuikinga nyumba yako dhidi ya kelele ya nje. Chunguza kuta na sakafu uone ikiwa kuna mashimo yoyote yawezayo kuzibwa. Angalia hasa mahali palipo na soketi za stima. Je, ziko salama?
Mara nyingi kelele huingia nyumbani kupitia milango na madirisha. Kuweka tabaka ya pili ya kioo kwenye madirisha kwaweza kusaidia kupunguza kelele. Hata kwa kuongeza sponji nyembamba kwenye fremu ya mlango wako kutahakikisha kuwa mlango wako watoshea sawasawa. Labda kujenga ukumbi na kuweka mlango wa pili kutailinda sebule yako dhidi ya kelele yenye kusumbua ya magari.
Ijapokuwa kelele ya magari inazidi kuongezeka sana, wenye kutengeneza magari kila wakati wanatokeza vifaa na njia mpya za kupunguza viwango vya sauti ndani ya gari lako. Kutumia magurudumu yasiyo na kelele sana kwenye gari lako pia kwasaidia. Katika nchi nyingi majaribio ambayo yamefanyiwa aina tofauti za uso wa barabara yametokeza vitu kama “barabara kimya,” ambapo vifaa fulani vigumu kama kokoto huachwa bila kufunikwa na basi kuna msuguano wa mara kwa mara tu. Imeripotiwa kuwa kwa kutumia barabara kama hiyo hupunguza kiasi cha kelele kwa decibel mbili katika magari mepesi na decibel moja katika magari mazito. Ijapokuwa hili laweza kuonekana kuwa dogo sana, kupungua kwa decibel tatu kwa wastani ni sawa na kupunguza kelele ya magari kwa nusu!
Wajenzi wa barabara sasa wanabuni barabara kuu zilizofichwa kwa kingo za mchanga, kwa njia hiyo kunakuwa na matokeo katika kupunguza kelele. Hata mahali ambapo hakuna nafasi ya kufanya hivyo, nyua zilizojengwa kwa njia maalumu, kama ule ulio mashariki ya London uliotengenezwa kwa kufuma machipukizi ya miti willow na mimea idumuyo kuwa ya kijani kibichi, huwazuia wakazi walio karibu na barabara kuu dhidi ya kelele isiyotakiwa.
Kusitiri sauti zenye kukengeusha fikira na kile kiitwacho kelele nyeupe—kwa kielelezo, umeme au mpitisho wa hewa—kwaweza kuwa kwenye manufaa katika mazingira fulani, kama vile maofisi.b Katika Japani piano zisizo na kelele sasa zauzwa madukani. Badala ya kuupiga uzi, nyundo hufanya mzunguko wa umeme utoe sauti kwenye earphone za mwenye kuicheza.
Tayari wanasayansi wametumia muda wa saa nyingi wakichunguza kutokezwa kwa kile kiitwacho kidhibiti-kelele. Kwa msingi, hili lahusisha kutumia chanzo kingine cha sauti ili kutoa mitikiso ambayo huondoa athari za kelele. Bila shaka, hili lahusisha vifaa zaidi na gharama zaidi na kwa kweli haliondoi kiini cha tatizo. “Hadi watu waanzapo kuiona kelele kama takataka,” laonelea U.S.News & World Report, “vidhibiti-kelele vyaweza kuwa njia pekee ya kupata utulivu wa muda.” Labda hivyo, lakini je, kukaa kimya ndilo suluhisho la uchafuzi wa kelele?
Je, kuna matumaini yoyote ya kuwa na amani na utulivu katika nyumba yako na katika ujirani wako? Makala yetu ifuatayo yatoa tumaini halisi.
[Maelezo ya Chini]
a Viwango vya kelele kwa jumla hujulikana kwa kutumia meta ambayo hupima sauti katika decibel. Kwa kuwa sikio husikia marudio fulani kwa uwazi zaidi kuliko mengine, meta hiyo imeundwa iitikie kwa njia hiyohiyo.
b Kama vile nuru nyeupe ni mchanganyiko wa marudio yote katika spektra ya nuru, kelele nyeupe ni sauti inayotia ndani marudio yote katika kiwango cha kusikika, karibu katika viwango sawa vya ukubwa wa sauti.
[Sanduku katika ukurasa wa 6]
Jinsi Uwezavyo Kuepuka Kuwa Jirani Mwenye Kelele
● Wafikirie majirani wako unapofanya jambo lenye kelele, na uwajulishe mapema.
● Shirikiana unapoombwa na jirani upunguze kelele.
● Tambua ya kwamba furaha yako haipaswi kumletea jirani yako msononeko.
● Kumbuka kwamba kelele na mitikiso hupitishwa kwa urahisi kupitia kumbi na sakafu.
● Weka vitu vya nyumbani vyenye kelele juu ya vitu vyororo.
● Hakikisha kuwa mtu aweza kuitwa kushughulikia ving’ora vya nyumba na gari viliavyo kiaksidenti.
● Usifanye kazi zenye kelele au kutumia mashine zenye kelele usiku sana.
● Usicheze muziki kwa sauti itakayowaudhi majirani wako.
● Usiwaache mbwa wakiwa peke yao kwa vipindi virefu.
● Usiwaruhusu watoto kurukaruka kwenye sakafu na hivyo kuwasumbua watu wanaoishi chini.
● Usipige honi, kugongesha milango, au kungurumisha injini ya gari usiku.
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 7]
Kelele na Wewe
“Kelele ndiyo hatari iliyoenea sana ya kiviwanda katika Uingereza leo,” lataarifu gazeti The Times, “na uziwi ndilo tokeo lake la kawaida.” Uchunguzi fulani wa afya na utendaji huonyesha kuwa kelele iliyozidi decibel 85 yaweza kukidhuru kijusu. Uwezo wa mtoto mchanga wa kusikia waharibika, na mtoto mchanga aweza kuwa na mvurugo wa kihomoni na pia kasoro za kuzaliwa.
Kuwa mahali penye kelele ya juu huifinya mishipa ya damu na kupunguza mzunguko wa damu katika viungo vyako. Likiwa tokeo, mwili wako waitikia kwa kutoa homoni ambazo huzidisha msongo wa damu na kuongeza mpigo wa moyo, wakati mwingine hilo likileta mpigo wako wa moyo wa kasi au hata ugonjwa wa angina.
Kelele inapovuruga utaratibu wako, matatizo mengine yaweza kutokea. Usingizi usiotosha waweza kuathiri utendaji wako wa wakati wa mchana. Huenda kelele isibadili mwendo wako wa kazi kwa ujumla, lakini yaweza kuhusika katika idadi ya makosa unayofanya.
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 9]
Kinga Ukiwa Kazini
Ikiwa waona kelele ikiwa tatizo kazini, fikiria kuvaa kitu fulani cha kukinga masikio.* Tumia earmuffs ambazo hutoshea kuzunguka kichwa chako kama hedifoni na kwa jumla ni zenye matokeo mahali ambapo viwango vya sauti viko juu. Uzuri wake ni kwamba waweza bado kusikia mazungumzo na ishara za maonyo za mashini, isipokuwa zaweza kufanya iwe vigumu kwako kutambua sauti yatoka wapi. Nazo earplugs zapaswa kuwa na ukubwa unaotoshea masikio yako vizuri na hazifai ikiwa una ugonjwa wa sikio au mwasho katika mfereji wa sikio.
Utunzaji mzuri wa mashine waweza kupunguza mitikiso. Kuwekelea vifaa juu ya mpira kutasaidia kupunguza uchafuzi wa kelele, na pia kuiweka mashine ya kelele mahali pengine.
*Sheria katika nchi nyingi huwataka waajiri wahakikishe kuwa wafanyakazi wao wanavaa kinga inayofaa kwa ajili ya uwezo wao wa kusikia.
[Picha katika ukurasa wa 8]
Waweza kujikingaje dhidi ya kelele inayosababishwa na vyombo vya kusafiria?