Kutoka kwa Wasomaji Wetu
Watoto na Vita Nilisoma mfululizo wa makala “Mambo Ambayo Vita Huwafanyia Watoto” kwa huzuni nyingi. (Oktoba 22, 1997) Mimi pia nilikuwa mtoto wa vita. Wakati wa Vita ya Ulimwengu ya Pili, nilitumia miaka minne na nusu katika kambi za mateso za Japani za Ngawi na Bandung. Nikiwa na umri wa miaka kumi, nilitenganishwa na familia yangu na kufanya kazi ngumu siku saba kwa juma katika jua la kitropiki—bila chakula cha kutosha na kuugua beriberi na ugonjwa wa kuhara damu. Na bado niliyojionea si kitu yakilinganishwa na ukatili usioelezeka unaofanywa kwa mamilioni ya watoto leo. Na tusivunjike moyo kamwe kwamba Yehova ameruhusu wakati kwa watu ulimwenguni pote, kutia ndani watoto wa vita, wapate kujua ahadi zake zenye kufariji!
R. B., Marekani
Chungu cha Mafuta Nilikuwa nikihuzunika sana na kujisikitikia. Mwaka mmoja uliopita mume wangu aliamua kwamba hataki mke Mkristo, kwa hiyo akanifukuza pamoja na mwana wangu kutoka katika nyumba nzuri aliyokuwa amesema kwamba ameninunulia. Nikaingiwa na umaskini. Maisha yangu yakawa bila tumaini, nikamwomba Yehova anisaidie. Nilipata somo kutoka kwenye makala “Somo Kutokana na Chungu cha Mafuta.” (Oktoba 22, 1997) Ilinikumbusha kuridhika na riziki na mavazi na kutanguliza masilahi ya Ufalme.
K. P., Marekani
Matatizo ya Ndugu Makala “Vijana Huuliza . . . Kwa Nini Ndugu Yangu Anapata Uangalifu Wote?” (Oktoba 22, 1997) ilikuja wakati barabara tulipoihitaji. Ilitusaidia kung’amua kwamba kutendewa kwa njia tofauti-tofauti si lazima kuwe ni kudhulumiwa. Sasa twaona kwamba wazazi wetu wana sababu nzuri za kuwapa ndugu zetu uangalifu wa ziada. Kwa kweli twakubaliana na makala hiyo.
B. K., H. K., na G. U. O., Nigeria
Uchafuzi wa Kelele Nimefanya kazi katika kiwanda kikubwa kwa miaka kadhaa, tukiwa huko mimi pamoja na baadhi ya wafanyakazi wenzangu tumesumbuka kutokana na madhara ya kelele. Nilichukua toleo la Novemba 8, 1997 kazini (“Kelele—Kichafuzi Chetu Kibaya Zaidi?”), na wasimamizi wa kiwanda wamechukua tahadhari zifaazo ili kulinda afya ya wafanyakazi wote.
R. P., Italia
Kwa miaka kadhaa nimesumbuliwa na kelele za jirani yangu. Hufanya biashara mpaka wakati wa usiku sana. Nyakati nyingine nimekasirika sana. Lakini nilitiwa moyo kujua kwamba kuna ndugu na dada Wakristo ambao pia husumbuliwa na kelele lakini ambao hukabiliana nayo kwa kujidhibiti.
T. O., Japani
Nina jirani ambaye hunisumbua kwa kupiga simu alfajiri. Makala hizi zimenipa madokezo mazuri juu ya jinsi ya kushughulika na jambo hili kwa njia ya Kikristo ya amani.
J. R., Uingereza
Magellan Nilithamini na kufurahia kikweli ile makala kuhusu Ferdinand Magellan iliyokuwa na kichwa “Mtu Aliyeufungua Ulimwengu.” (Novemba 8, 1997) Makala hiyo ilipotokea, tulikuwa tukijifunza juu yake katika darasa letu la tano. Nilijifunza mengi kumhusu katika makala hiyo kuliko nilivyojifunza katika kitabu cha historia. Nilimpa mwalimu wangu makala yangu ya kibinafsi ya gazeti hilo, na aliifurahia! Siku chache baadaye, nilirudishiwa gazeti hilo, likiwa na barua fupi ya kunishukuru tena.
B. V., Marekani
Ilistaajabisha kuwazia jinsi mwanamume mjasiri Ferdinand Magellan, alivyoshinda uhasama na magumu mbalimbali ili kupata mojawapo mafanikio makubwa zaidi katika historia. Asanteni kwa kuandika habari yenye kuvutia.
M. E., Italia