Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g97 11/8 kur. 3-5
  • Kelele—Kisumbufu cha Kisasa

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Kelele—Kisumbufu cha Kisasa
  • Amkeni!—1997
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Si Tatizo Jipya
  • Kichafuzi cha Kisasa Kilichoenea Sana
  • Kelele—Yale Uwezayo Kufanya Kuihusu
    Amkeni!—1997
  • Je, Kutakuwako Amani na Utulivu Wakati Wowote?
    Amkeni!—1997
  • Kutoka kwa Wasomaji Wetu
    Amkeni!—1998
  • Kuutazama Ulimwengu
    Amkeni!—2005
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1997
g97 11/8 kur. 3-5

Kelele—Kisumbufu cha Kisasa

NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA UINGEREZA

“Ni mojawapo ya visababishi vikubwa vya mkazo maishani.”—Makis Tsapogas, mshauri wa Shirika la Afya Ulimwenguni.

“Kichafuzi kilichoenea kote katika Amerika.”—The Boston Sunday Globe, Marekani.

“Kichafuzi kibaya zaidi cha wakati wetu.”—Daily Express, London, Uingereza.

HUWEZI kuiona, kuinusa, kuionja, au kuigusa. KELELE, chanzo cha madhara ya maisha ya mjini ya kisasa, yachafuza pia sehemu za mashambani.

Mwanaviumbe mmoja Mmarekani ambaye alitumia miaka 16 akirekodi sauti za asili ameipata kazi yake ikizidi kuwa ngumu. Katika mwaka wa 1984 alichunguza sehemu 21 katika jimbo la Washington, Marekani, ambazo hazikuwa na kelele kwa vipindi vya dakika 15 au zaidi. Miaka mitano baadaye, ni sehemu tatu tu zilizobaki.

Kwa wakazi wengi wa dunia, ni vigumu sana kupata sehemu tatu zisizo na kelele. Katika Japani, ripoti ya nchi yote ya 1991 ilitaarifu kuwa kelele ilitokeza malalamiko mengi zaidi kuliko aina nyingine yoyote ya uchafuzi. Kwa kweli, The Times la London kwa kufaa lafafanua kelele kama “pigo kubwa zaidi ya maisha ya wakati huu.” Kutoka mbweko wa mbwa wenye kuudhi na wenye kudumu hadi mlio wa kinanda cha jirani au mlio wenye kudumu wa king’ora cha gari au redio, kelele imekuwa kawaida. Lakini uchafuzi wa kelele si jambo jipya. Ina historia ndefu.

Si Tatizo Jipya

Ili kupunguza msongamano wa magari, Julius Caesar alipiga marufuku magari yasiwemo katikati ya mji wa Roma wakati wa mchana. Kwa kusikitisha yeye na Waroma wenzake, amri hiyo ilitokeza uchafuzi mwingi wa kelele usiku, “magurudumu ya mbao na chuma yakikimbia kwenye barabara za mawe.” (The City in History, cha Lewis Mumford) Zaidi ya karne moja baadaye, mshairi Juvenal alilalamika kwamba kelele iliwasababishia Waroma ukosefu wa usingizi wenye kudumu milele.

Kufikia karne ya 16, mji mkuu wa Uingereza, London, ulikuwa umekuwa mji mkuu wenye kelele nyingi. “Jambo la kwanza ambalo lazima liwe liliwavutia wageni wengi,” aandika Alison Plowden, mwandishi wa Elizabethan England, “ni ile kelele: vitu vinavyogongana na mipigo ya nyundo kutoka katika karakana elfu moja, mvumo na sauti nyembamba za magurudumu ya magari ya kukokotwa, mlio wa ng’ombe wakipelekwa sokoni, mchanganyiko wa sauti za wafanya-biashara wakitangaza bidhaa zao barabarani.”

Karne ya 18 ilikuwa mwanzo wa mvuvumko wa kiviwanda. Sasa athari za kelele ya mitambo ikaonekana wazi kwani wafanyakazi wa viwandani walipatwa na uharibifu wa uwezo wao wa kusikia. Lakini hata wakazi wa mjini ambao hawakuishi karibu na viwanda walilalamika kuhusu ongezeko la usumbufu. Mwanahistoria Thomas Carlyle alikimbilia “chumba ambacho hakikufikiwa na kelele za barabarani” kwenye dari ya nyumba yake huko London ili kuepuka kuwika kwa jogoo, piano za majirani, na shughuli zilizokuwa katika barabara iliyokuwa hapo karibu. Gazeti The Times laripoti: “Haikusaidia.” Kwa nini? “Sasa alisumbuliwa zaidi na kelele nyinginezo mpya, kutia ndani honi za mashua na ving’ora vya garimoshi”!

Kichafuzi cha Kisasa Kilichoenea Sana

Leo wanaoteta dhidi ya kelele hulenga viwanja vya ndege huku mashirika ya ndege yaendeleapo kukataa majaribio ya kutunga sheria dhidi ya uchukuzi wa kelele. Wakati kiwanja cha ndege cha Manchester katika Uingereza kilipoanza kutoza faini za lazima kila wakati ile ndege aina ya Concorde yenye mwendo wa kasi kushinda sauti ilipoondoka uwanjani, je, hili lilifanikiwa? La. Rubani mmoja wa Concorde alikiri kwamba ndege hiyo ilikuwa na kelele lakini ikiwa wangeondoka kiwanjani wakiwa na mafuta kidogo ili kupunguza kiwango cha kelele, haingefika Toronto au New York bila kutua mahali.

Ni tatizo pia kuzuia kelele ya magari barabarani. Kwa kielelezo, katika Ujerumani, uchunguzi wafunua kwamba aina hii ya uchafuzi husumbua asilimia 64 ya idadi ya watu huko. Na ni tatizo linaloendelea kukua, yaripotiwa kuwa umeongezeka kufikia kuwa mara elfu moja kuliko wakati wa kabla ya watu waanze kutumia magari. Ripoti moja kutoka Ugiriki yataarifu kuwa “Athens ni mmoja kati ya miji yenye kelele zaidi katika Ulaya na kelele hiyo ni mbaya sana hivi kwamba inaharibu afya ya watu wa Athens.” Vivyo hivyo, Shirika la Mazingira la Japani huona mwelekeo unaozidi kuzorota wa kelele ya barabarani na kusema kuwa huo husababishwa na utumizi wenye kuendelea kuongezeka wa magari. Gari likiwa katika mwendo wa polepole injini yake ndiyo kiini hasa cha kelele, lakini ikipita kiwango cha kilometa 60 kwa saa moja, magurudumu ndiyo hutokeza kelele zaidi.

Kisababishi kikubwa zaidi cha malalamiko kuhusu kelele katika Uingereza ni kelele za nyumbani. Katika 1996, Taasisi ya Britain’s Chartered Institute of Environmental Health iliona ongezeko la asilimia 10 katika malalamiko kuhusu majirani wenye kelele. Msemaji mmoja mwanamke wa taasisi hiyo alieleza hivi: “Ni vigumu kueleza. Kisababishi kimoja huenda kikawa kwamba msongo wanaoupata watu katika mahali pao pa kazi unawaongoza kutaka amani zaidi na utulivu nyumbani.” Thuluthi mbili za malalamiko hayo yote yaliyotoka Uingereza katika 1994 yalihusu muziki wa usiku sana na injini zenye kelele, ving’ora, na honi za magari. Lakini namna gani kuhusu ile asilimia ipatayo 70 ya wahasiriwa wa uchafuzi wa kelele ambao hawalalamiki kwa kuhofia kulipizwa kisasi? Kwa kweli tatizo hili limeenea sana.

Likiwa tokeo la usumbufu wa kelele wenye kuenea sana, mashirika yenye lengo la kulinda mazingira yasisitiza kuwe na sheria ili kumaliza uchafuzi wa kelele. Kwa kielelezo, katika Marekani, jumuiya fulani zimekubali kutumia kanuni za kwao ili kupunguza utumizi wa mashine za umeme za kusawazishia ardhi. Katika Uingereza Sheria mpya Dhidi ya Kelele huwalenga majirani wenye kelele na imekubali faini za papo hapo zitozwe wenye kuvunja sheria hizo kati ya saa tano usiku na saa moja asubuhi. Wenye mamlaka za huko hata wana uwezo wa kutwaa kinanda chenye kelele. Na bado, kelele yaendelea.

Uchafuzi wa kelele ukiwa tatizo lenye kuongezeka kweli, huenda ukajiuliza jambo uwezalo kufanya ukiwa mhasiriwa. Lakini, pia, waweza kuepukaje kufanya kelele? Je, kutakuwako amani na utulivu wa kudumu wakati wowote? Soma makala zifuatazo ili upate majibu.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki