Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g97 11/8 kur. 12-17
  • Mtu Aliyeufungua Ulimwengu

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Mtu Aliyeufungua Ulimwengu
  • Amkeni!—1997
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Kutoka Kuwa Mhudumu wa Nyumba ya Mfalme Hadi Kuwa Baharia Jasiri
  • Je, Mfalme wa Hispania Atasikiliza?
  • “Utimizo Mkubwa Zaidi wa Baharini Katika Historia”
  • Masaibu Katika Pasifiki
  • Msiba—Ndoto Yaporomoka
  • Msiba Wakumba Safari ya Kurudi Nyumbani
  • Jina la Magellan Ladumu
  • Kutoka kwa Wasomaji Wetu
    Amkeni!—1998
  • Safari ya Baharini Yenye Kutokeza ya Vasco da Gama
    Amkeni!—1999
  • Kuvuka Mstari
    Amkeni!—2001
  • Amri Zilizogawa Mabara
    Amkeni!—2015
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1997
g97 11/8 kur. 12-17

Mtu Aliyeufungua Ulimwengu

NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA AUSTRALIA

WANADAMU walipoenda kwenye mwezi kwa mara ya kwanza, wao walipanga kwa usahihi wa kihisabati walikokuwa wakienda na jinsi ambavyo wangefika huko. Nao waliweza kuwasiliana na nyumbani. Lakini merikebu ndogo tano za mbao za Ferdinand Magellana—nyingi zake zikiwa na urefu wa karibu meta 21, zikitoshana na nusu-trela za kisasa kwa urefu—zilipoondoka Hispania mnamo 1519, zilielekea kusikojulikana. Zikawa pweke kabisa.

Zikiwa miongoni mwa matimizo ya baharini yenye ujasiri na moyo mkuu zaidi ya yote, safari za Magellan ni uthibitisho wenye kudumu wa hiyo Enzi Kubwa ya Uvumbuzi—enzi ya moyo mkuu na hofu, msisimuko na msiba, Mungu na Mali. Basi ebu turudi nyuma hadi karibu mwaka wa 1480, wakati Ferdinand Magellan alipozaliwa kaskazini mwa Ureno, na kumtazama huyu mtu mwenye kutokeza aliyeufungua ulimwengu na pia tutazame safari zake za kihistoria.

Kutoka Kuwa Mhudumu wa Nyumba ya Mfalme Hadi Kuwa Baharia Jasiri

Familia ya akina Magellan ni ya ukoo bora, basi kama ilivyo desturi, Ferdinand aitwa akiwa angali kijana kuwa mhudumu katika nyumba ya mfalme. Hapo, mbali na kupata elimu, yeye ajifunza moja kwa moja matimizo ya watu kama Christopher Columbus, ambaye amerudi punde tu kutoka nchi za Amerika baada ya kutafuta njia ya magharibi baharini ya kufikia Visiwa vya Vikolezo (Indonesia) vilivyo mashuhuri. Upesi Ferdinand mchanga aanza kufikiria siku ambayo yeye pia ataweza kuabiri na kuhisi usoni pake rasharasha za bahari ambazo hazijavumbuliwa.

Kwa kusikitisha, mnamo 1495 mfadhili wake Mfalme John auawa, na Dyuki Manuel, ambaye azingatia sana kupata mali lakini si uvumbuzi, aanza kutawala. Kwa sababu fulani, Manuel hampendi Ferdinand mwenye umri wa miaka 15 na kwa miaka mingi apuuza maombi yake ya kutaka kuabiri. Lakini Vasco da Gama arudipo kutoka India, akiwa amejaza shehena za vikolezo, Manuel aanza kufikiria njia ya kupata mali nyingi. Hatimaye, mnamo 1505, yeye ampa Magellan ruhusa ya kuabiri. Magellan aondoka kwenda Afrika Mashariki na India katika kundi la merikebu za vita za Ureno ili kusaidia kuwanyang’anya wafanya-biashara Waarabu udhibiti wa biashara ya vikolezo. Baadaye, yeye aabiri kuelekea mashariki zaidi kwenda Malacca katika safari nyingine ya kijeshi.

Katika fujo fulani nchini Moroko mnamo 1513, Magellan ajeruhiwa vibaya kwenye goti. Tokeo ni kwamba yeye achechemea maishani mwake mwote. Aomba Manuel aongeze malipo yake ya uzeeni. Lakini uhasama wa Manuel haupunguzwi kamwe na matimizo, dhabihu, na bidii ya karibuni ya Magellan. Yeye amwacha aende akaishi kama maskini.

Katika hali hii yenye kusikitisha zaidi maishani mwa Magellan, yeye atembelewa na rafiki wa zamani, nahodha mashuhuri João de Lisboa. Hao wawili wajadili njia za kufikia Visiwa vya Vikolezo kwa kuelekea kusini-magharibi, kupitia el paso—mlango-bahari uliosemekana kwamba ulivuka katikati ya Amerika Kusini—na kisha kuvuka bahari ambayo Balboa alivumbua majuzi alipovuka shingo ya nchi ya Panama. Hao waamini kwamba upande ule mwingine wa bahari hiyo kuna Visiwa vya Vikolezo.

Sasa Magellan atamani sana kufanya kile ambacho Columbus alishindwa kufanya—kupata ile njia ya magharibi ya kuelekea Mashariki, ambayo yeye aamini ni fupi kuliko njia ya mashariki. Lakini yeye ahitaji udhamini wa kifedha. Kwa hiyo, akiwa bado anasononeka juu ya hasira ya kisasi ya Manuel, yeye afanya jambo ambalo Columbus mwenyewe alifanya miaka kadhaa mapema—yeye atafuta udhamini wa mfalme wa Hispania.

Je, Mfalme wa Hispania Atasikiliza?

Ramani zikiwa zimefunguliwa wazi, Magellan atokeza hoja zake kwa mfalme mchanga wa Hispania, Charles wa Kwanza, ambaye anapendezwa sana na njia ya magharibi ya Magellan ya kuelekea Visiwa vya Vikolezo, kwa sababu hiyo ingeepusha kuvuka njia za merikebu za Ureno. Isitoshe, Magellan amwambia kwamba Visiwa vya Vikolezo huenda hata vikawa katika eneo la Hispania, wala si la Ureno!—Ona sanduku “Mkataba wa Tordesillas.”

Charles asadikishwa. Yeye ampa Magellan merikebu tano nzee azirekebishe kwa ajili ya safari hiyo, amfanya awe nahodha-mkuu wa merikebu hizo, na amwahidi kumgawia faida za vikolezo atakavyoleta nyumbani. Magellan aanza kazi mara moja. Lakini kwa sababu Mfalme Manuel ajaribu kwa ujanja kuvuruga mradi huo, inachukua zaidi ya mwaka mmoja kabla ya merikebu hizo kuwa tayari hatimaye kwa safari hiyo ya kihistoria.

“Utimizo Mkubwa Zaidi wa Baharini Katika Historia”

Septemba 20, 1519, merikebu San Antonio, Concepción, Victoria, na Santiago—zikifuatana kwa ukubwa—zafuata merikebu, Trinidad, ya Magellan yenye kuongoza, merikebu ya pili kwa ukubwa zaidi, ziabiripo kuelekea Amerika Kusini. Desemba 13, wao wafika Brazili, na wakiukabili Pão de Açúcar, au Mlima Sugarloaf wenye fahari, wao waingia ghuba yenye kuvutia ya Rio de Janeiro ili wafanye marekebisho na kupata maandalizi. Kisha wao waendelea kusini na kuingia katika eneo ambalo sasa ni Argentina, wakiwa macho wakati wote kuona el paso, ule mlango-bahari wenye kujificha wa kuingia bahari nyingine. Kwa wakati huo, siku zawa baridi zaidi na vilima vya barafu vyatokea. Hatimaye, siku ya Machi 31, 1520, Magellan aamua kupitisha kipindi cha baridi kali katika bandari ya San Julián.

Safari hiyo sasa imekuwa ndefu mara sita zaidi ya safari ya kwanza ya Columbus ya kuvuka Atlantiki—na bado mlango-bahari hauonekani! Motisha imekuwa chini sana kama baridi ya San Julián, na wanaume hao, kutia ndani baadhi ya manahodha na maofisa, wanatamani sana kurudi nyumbani. Basi haishangazi kwamba maasi yatokea. Lakini kupitia hatua ya mara moja ya kukata maneno kwa upande wa Magellan, maasi hayo yazimwa, na viongozi wawili wa maasi wauawa.

Kuwapo kwa merikebu za kigeni katika bandari bila shaka kwazusha udadisi wa wenyeji wakakamavu na wenye miili mikubwa. Wakijiona kama mbilikimo wakiwa kando ya majitu hao, wageni hao waliita bara hilo Patagonia—kutokana na neno la Kihispania limaanishalo “miguu mikubwa”—jina ambalo limedumu hadi leo. Wao pia waona ‘mbwa-mwitu wa baharini wanaotoshana na ndama, na vilevile bata bukini wa rangi nyeupe na nyeusi waogeleao chini ya maji, walao samaki, na wenye midomo kama kunguru.’ Ndiyo, umekisia kweli—sili na ngwini!

Latitudo za ncha za dunia hupatwa na dhoruba za ghafula zenye nguvu sana, na kabla ya majira ya baridi kali kwisha, merikebu hizo zapata hasara ya kwanza—ile merikebu ndogo Santiago yavunjwa vipande-vipande. Lakini, kwa uzuri mabaharia hao waokolewa kutoka kwenye mvunjiko huo. Baadaye, merikebu nne zilizobaki, zikiwa zimepigwa-pigwa kama nondo na dhoruba zenye barafu, zaelekea kusini katika maji yaliyo baridi hata zaidi—hadi Oktoba 21. Kupitia marasharasha na mvua ya barafu, macho yote yamekodolewa yakitazama mlango uelekeao magharibi. El paso? Ndiyo! Hatimaye, wao wageuka na kuingia katika mlango-bahari ambao baadaye waitwa Mlango-Bahari wa Magellan! Lakini, hata pindi hiyo ya ushindi yakuwa na matatizo. Merikebu San Antonio ikatoweka kimakusudi katika vijia vingi na visiwa vingi vya huo mlango-bahari na kurudi Hispania.

Merikebu tatu zilizosalia, zikiwa zimezingirwa kwa milima yenye miinuko mikali na vilele vyenye theluji, zatapatapa kwa ushupavu kuvuka huo mlango-bahari ulio mgumu. Kwa upande wa kusini wao waona mioto mingi sana, labda kutoka katika kambi za Wahindi, na basi wao waita bara hilo Tierra del Fuego, “Bara la Moto.”

Masaibu Katika Pasifiki

Baada ya majuma matano yenye kuumiza sana, wao waanza safari katika bahari tulivu sana hivi kwamba Magellan aiita Pasifiki. Watu hao wasali, waimba nyimbo za kidini, na kufurahia ushindi wao kwa kulipua mizinga yao. Lakini furaha yao ni ya punde tu. Ole mkubwa kuliko hali yoyote waliyopata kukabili unawangoja, kwa sababu hii si ile bahari ndogo waliyotazamia—yaendelea na kuendelea bila mwisho, na watu hao wapatwa na njaa zaidi, wadhoofika zaidi na kuwa wagonjwa zaidi.

Antonio Pigafetta, Mwitalia mkakamavu, aandika matukio. Yeye aandika: “Jumatano, tarehe ishirini na nane ya Novemba, 1520, sisi . . . tuliingia katika bahari ya Pasifiki, ambako tulidumu kwa miezi mitatu na siku ishirini bila kutwaa maandalizi . . . Tulikula tu biskuti za zamani ambazo zilikuwa zimesagika zilizojaa mabuu, na zenye uvundo kutokana na mavi ya panya waliokunyia biskuti hizo . . . , na tuliyanywa maji ambayo yalikuwa yamegeuka rangi ya kimanjano na yenye uvundo. Pia tulikula ngozi ya ng’ombe . . . , mavumbi ya mbao, na panya ambao walitugharimu shilingi tano kwa kila mmoja, isitoshe hawakupatikana kwa wingi.” Hivyo, pepo mpya za msimu zijazapo matanga yao na wapitapo maji mangavu, watu hao walala chini wakidhoofika kwa ugonjwa wa kiseyeye. Kumi na tisa wafa kufikia wakati wafikapo Visiwa vya Mariana, Machi 6, 1521.

Lakini kwa sababu ya uhasama wa wakaazi wa visiwa hivyo, wao wafaulu kupata chakula kidogo tu kizuri kabla ya kuendelea na safari. Hatimaye, Machi 16, wao waona Filipino. Hatimaye, watu wote wala vizuri, wapumzika, na kupata nafuu na nguvu tena.

Msiba—Ndoto Yaporomoka

Akiwa mtu wa kidini sana, huko Magellan abadilisha dini ya wenyeji wengi na watawala wao kuwa Wakatoliki. Lakini bidii yake pia yamharibia. Yeye ahusika na mzozo wa baina ya makabila ya huko na, akiwa na watu 60 pekee, ashambulia wenyeji wapatao 1,500, akiamini kwamba nyuta, gobori, na Mungu atamhakikishia ushindi. Badala ya hivyo, yeye na watu wake kadhaa wauawa. Magellan ana umri upatao miaka 41. Pigafetta aliye mwaminifu-mshikamanifu aomboleza: ‘Wao walimwua kioo chetu, taa yetu, faraja letu, na kiongozi wetu wa kweli.’ Siku kadhaa baadaye, maofisa wapatao 27 waliokuwa wametazama tu tukio hilo kwa usalama wa merikebu zao wauawa na machifu ambao awali walikuwa wenye urafiki.

Magellan alipokufa, alikufa katika mazingira aliyoyafahamu. Kidogo tu upande wa kusini kulikuwa na Visiwa vya Vikolezo na upande wa magharibi, Malacca, ambako alikuwa amepigana vita mnamo 1511. Ikiwa, kama vile wanahistoria fulani wafikirivyo, aliabiri kwenda Filipino baada ya vita ya Malacca, basi kwa kweli alifaulu kuzunguka tufe—lakini bila shaka si katika safari moja. Alikuwa amefika Filipino kutoka upande wa mashariki na vilevile upande wa magharibi.

Msiba Wakumba Safari ya Kurudi Nyumbani

Kwa vile sasa ni wanaume wachache tu wabakio, haiwezekani kuendesha merikebu tatu, basi wao wazamisha Concepción na kuabiri na merikebu mbili zilizokuwa zimebaki hadi mahali walipotaka kwenda, Visiwa vya Vikolezo. Kisha, baada ya kujaza shehena za vikolezo, merikebu hizo mbili zatengana. Lakini mabaharia wa ile merikebu Trinidad yenye kutapatapa wakamatwa na Wareno na kutiwa gerezani.

Lakini ile Victoria, ikiwa chini ya Juan Sebastián de Elcano ambaye zamani alikuwa mwasi, yatoroka. Wakiepuka bandari zote ila moja, wao wajihatarisha katika njia hiyo ya Ureno kuzunguka Rasi ya Good Hope. Lakini kutotua ili kupata vyakula kwatokeza msiba mbaya sana. Hatimaye wafikapo Hispania Septemba 6, 1522—miaka mitatu tangu watoke huko—ni watu 18 tu walio wagonjwa na kudhoofika wanaookoka. Na bado, bila shaka wao ni watu wa kwanza duniani kuzunguka dunia. Na De Elcano anakuwa shujaa. Kwa kushangaza, tani 26 za vikolezo vilivyofika kwa merikebu Victoria zalipia safari hiyo yote!

Jina la Magellan Ladumu

Kwa miaka mingi Magellan anyimwa umaarufu wake katika historia. Wakipotoshwa na ripoti za manahodha walioasi, Wahispania waharibu sifa yake, wakisema alikuwa mtu mkali asiyeweza kutekeleza mambo. Wareno wamwita mhaini. Kwa kusikitisha, kitabu chake cha matukio kilipotea alipokufa, labda kiliharibiwa na wale ambao kingewafunua. Lakini kwa sababu ya Pigafetta asiyeshindika—mmoja wa wale watu 18 waliozunguka dunia—na karibu watu wengine 5 wa safari hiyo, angalau tuna rekodi fulani ya safari hiyo yenye msiba na isiyo ya kawaida.

Baada ya muda, historia ilirekebisha uamuzi wake, na leo jina Magellan laheshimiwa ifaavyo. Kuna mlango-bahari wenye jina lake na vilevile Mawingu ya Magellan—zile galaksi mbili hafifu-hafifu zilizofafanuliwa kwa mara ya kwanza na mabaharia wake—na kichunguza-anga cha Magellan. Na, bila shaka, jina la bahari kubwa kuliko zote—Pasifiki—latokana na Magellan.

Kwa kweli, “hakuna safari yenye umaana sana kama hiyo iliyopata kufanywa hadi wakati Apollo 11 ilipotua kwenye Mwezi miaka 447 baadaye,” aandika Richard Humble, katika The Voyage of Magellan. Kwa nini safari hiyo ilikuwa yenye umaana sana? Kwanza, ilithibitisha kwamba nchi za Amerika hazikuwa sehemu ya Asia wala hazikuwa karibu nayo, kama Columbus alivyokuwa amefikiri. Pili, mwishoni mwa safari hiyo, hitilafiano ya siku moja ilionyesha uhitaji wa kuweka mstari wa tarehe wa kimataifa. Na, hatimaye, kama vile mwandikaji wa sayansi Isaac Asimov alivyosema, ilionyesha kwamba dunia ni duara. Ndiyo, katika habari ya kwamba dunia ni duara, Magellan alithibitisha kwa njia halisi yale ambayo Biblia yenyewe ilikuwa imekuwa ikisema kwa miaka 2,250. (Isaya 40:22; linganisha Ayubu 26:7.) Hakuna shaka kwamba mtu huyo aliye wa kidini sana ambaye aliufungua ulimwengu angefurahia hilo.

[Maelezo ya Chini]

a Jina lake la Kireno lilikuwa Fernão de Magalhães.

[Sanduku katika ukurasa wa 14]

Mkataba wa Tordesillas

Ulimwengu mkubwa ukifunguka mbele yao, Ureno na Hispania zilikubaliana kufuata mkataba wa kugawana biashara na haki za kutawala mabara mapya. Basi, chini ya mwelekezo wa Mapapa Aleksanda wa Sita na Julius wa Pili, wao walichora mstari wa kuwaziwa kupitia eneo ambalo leo ni Brazili. Mabara ambayo yangevumbuliwa mashariki ya mstari huo yangekuwa ya Ureno; na yaliyosalia yangekuwa ya Hispania. Magellan alimpendekezea Mfalme Manuel wa Ureno isivyo hekima kwamba mstari huu ukipitia ncha za dunia hadi upande ule mwingine wa tufe, Visiwa vya Vikolezo huenda vikaangukia himaya ya Hispania. Mawazo hayo yenye kufuatia haki, yakitegemea wazo la kawaida kwamba Bahari ya Pasifiki ni ndogo sana, ilifanya akaripiwe vikali. Kumbe, Magellan alijithibitisha kuwa alikosea. Hata hivyo, itikadi yake ilimpa sababu zaidi ya kutafuta ufadhili wa mfalme wa Hispania.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 15]

Masaibu ya Baharia wa Awali

Hasa katika safari ndefu zaidi za uvumbuzi—ambazo mara nyingi zilidumu kwa miaka mingi—maisha ya baharia wa hali ya chini haikuwa ya raha. Hapa pana madokezo tu ya hali ya baharia:

• Sehemu za kulala zenye kufinyana sana na ukosefu wa faragha

• Mara nyingi kuna adhabu za kikatili ikitegemea nahodha

• Kiseyeye na kifo kutokana na ukosefu wa vitamini C

• Kifo kutokana na mvunjiko wa merikebu, njaa, kiu, kuhatarishwa, na wenyeji

• Kuhara damu au homa ya matumbo kutokana na maji machafu na yenye uvundo

• Kuugua kutokana na vyakula vilivyooza na kuambukizwa

• Homa ya panya, kutokana na kuumwa na panya wenye njaa

• Homa ya chawa, kutokana na chawa wengi katika miili michafu na mavazi machafu

• Katika visa vingi, uwezekano wa kurudi nyumbani ukiwa hai ulikuwa nusu-nusu

[Hisani]

Century Magazine

[Ramani/Picha katika ukurasa wa 16, 17]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

Safari ya Magellan, 1519-22

⇦••• Njia □ Mwanzo na mwisho

Mlango-Bahari wa Magellan

Magellan aliuawa katika Ufilipino

Mkondo wa mwisho alioabiri Juan Sebastián de Elcano

[Hisani]

Magellan: Giraudon/Art Resource, NY; ramani ya ulimwengu: Mountain High Maps® Copyright © 1995 Digital Wisdom, Inc.; astrolabe: Kwa hisani ya Adler Planetarium

[Picha katika ukurasa wa 16]

Ferdinand Magellan

[Picha katika ukurasa wa 16]

“Victoria,” merikebu ya kwanza iliyozunguka tufe. Kati ya merikebu zake tano, hiyo ilikuwa ya nne kwa ukubwa nayo ilibeba watu 45. Merikebu hiyo ilikuwa na urefu wa karibu meta 21

[Picha katika ukurasa wa 17]

Vyombo vya kuabiri: Shisha ilipima wakati, na astrolabu ilipima latitudo ya merikebu

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki