Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g97 3/8 kur. 28-29
  • Kuutazama Ulimwengu

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Kuutazama Ulimwengu
  • Amkeni!—1997
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Dawa za Kuandikiwa Zatumiwa Vibaya
  • Wahasiriwa Wasio na Hatia Katika Rwanda
  • Matatizo ya Nyayo
  • Uraibu wa Kununua Vitu
  • “Kikundi Kikubwa cha Watazamaji wa Televisheni Wachanga Sana”
  • Wanawake na Ujiuaji-Kimakusudi
  • “Kitovu cha Tufeni Pote” cha UKIMWI
  • Majeraha ya Michezo
  • Jihadhari na E. Coli O157:H7
  • Kuutazama Ulimwengu
    Amkeni!—1995
  • Magonjwa ya Kuambukiza Katika Karne ya 20
    Amkeni!—1997
  • UKIMWI—Matokeo Yenye Msiba Mkubwa kwa Watoto
    Amkeni!—1992
  • Kuutazama Ulimwengu
    Amkeni!—1996
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1997
g97 3/8 kur. 28-29

Kuutazama Ulimwengu

Dawa za Kuandikiwa Zatumiwa Vibaya

Katika jimbo la Victoria, Australia, gazeti la habari la Melbourne Herald Sun laripoti kwamba “Waaustralia wanatumia dola bilioni 3 kwa mwaka kununua dawa na wanaendelea kuwa waraibu wa dawa za kuandikiwa za kuondoa maumivu.” Waziri wa afya wa Victoria alionya kwamba “utumizi mbaya wa dawa za kuandikiwa unakuwa tatizo bila ya sisi kujua na waweza kuwa hatari kwa afya na mtindo-maisha kama dawa za kulevya zisizo halali.” Yeye pia alionyesha hangaiko kuhusu ripoti kwamba watu wengi zaidi sasa ‘wanawaendea madaktari tofauti-tofauti’ ili kupata kuandikiwa dawa kadhaa. Tembe fulani huhifadhiwa, kisha hupondwa-pondwa na hudungwa kwa sindano katika mkondo wa damu. Kulingana na uchunguzi mmoja, asilimia ya watu watumiao dawa za kuondoa maumivu kando na utumizi halali wa kitiba iliongezeka kutoka asilimia 3 katika 1993 hadi asilimia 12 katika 1995.

Wahasiriwa Wasio na Hatia Katika Rwanda

Wakati wa machinjo ya hivi majuzi katika Rwanda, mamia ya maelfu ya wanawake walibakwa na wengine hata kuwekwa wakiwa watumwa wa ngono. Katika visa vingi wabakaji hao walikuwa wanaume walewale ambao waliwaua kikatili waume na watu wa ukoo wa wanawake hao. Asilimia 35 hivi ya wahasiriwa wa ubakaji walipata mimba. Wanawake fulani walichagua kutoa mimba au kuua vitoto kuwa njia ya kutatua tatizo lao; wengine waliwaacha watoto au kuwapa wakaasilishwe. Na bado “kwa makadirio ya kiasi, kuna watoto wasiotakwa 2,000 hadi 5,000 katika Rwanda ambao mama zao walibakwa wakati wa vita hivyo vya wenyewe kwa wenyewe,” laripoti The New York Times. Idadi kubwa ya wajane na watoto wao imekuja kuwa watu wasiotakwa na jamii zao. Times lataja kwamba “wanawake wengi waliona ikiwa vigumu kupata waume wapya au kuanza maisha mapya.” Akina mama wengine huona watoto wao kuwa kikumbusha cha daima cha aibu na kifo chenye jeuri cha wapendwa wao. Kwa sababu ya kumbukumbu hizi, akina mama fulani wanaona ikiwa vigumu kuonyesha watoto wao upendo.

Matatizo ya Nyayo

Kulingana na makadirio yaliyofanywa na Utumishi wa Afya wa Shirika la Serikali la Matabibu katika Ujerumani, nusu ya wananchi wa nchi hiyo wanatatizwa na nyayo zao. “Watu wengi hupuuza kutunza nyayo zao au kutenda nyayo zao vibaya kwa kuvaa viatu vinavyobana sana au viwezavyo kuharibu afya yao,” laripoti gazeti la habari Nassauische Neue Presse. Kuvaa kwa ukawaida viatu vyenye kisigino kirefu au kisichotoshea vizuri kwaweza kutokeza maumivu magotini, nyongani, au mgongoni. Maradhi yasababishwayo na kuvu, kama vile athlete’s foot na mycosis, pia yanaenea sana. Hatua ya kuzuia ambayo inadokezwa na Shirika la Serikali la Matabibu ni “kutakatisha sabuni yote na kukausha kwa uangalifu katikati ya vidole.”

Uraibu wa Kununua Vitu

Katika Ireland kununua vitu kutokana na ushurutisho “sasa kunatambuliwa kuwa uraibu na kunajiunga na alkoholi, dawa za kulevya, uchezaji kamari na matatizo ya kula kukiwa tamaa mbaya sana isiyotulizika ya kihisia-moyo na kiakili ambayo yahitaji msaada wa kitaalamu,” lasema The Irish Times. Wahasiriwa wa tamaa hii isiyotulizika waweza kutumia fedha nyingi mno kununua vitu ambavyo hawahitaji. Ripoti hiyo yaeleza: “Kipindi kifupi cha raha ya kujasiria kununua nguo huchochea michozo ya dopamine na serotonin mwilini, ambayo hutokeza hisia ya kuwa na hali-njema.” Kwa mnunuzi mwenye ushurutisho, kama kwa mraibu wa dawa za kulevya, raha hizo huwa vigumu zaidi na zaidi kuzipata.

“Kikundi Kikubwa cha Watazamaji wa Televisheni Wachanga Sana”

Uchunguzi wa familia 21,000 katika Italia umefunua kwamba watoto wengi sana wa Kiitalia ni wenye kutegemea televisheni. Gazeti la habari La Repubblica lilitaja kwamba “kikundi kikubwa cha watazamaji wa televisheni wachanga sana” kinazoea kutumia kiteua-stesheni ya televisheni kwa umbali tangu mwaka wa kwanza wa uhai. Zaidi ya watoto milioni nne wa Kiitalia kati ya umri wa miaka mitatu na kumi hutazama televisheni, wakiwa wamenaswa kabisa kwa zaidi ya muda wa saa mbili na nusu kwa siku. Wataalamu wa akili wanahangaika juu ya uhakika wa kwamba watoto wengi wenye umri mchanga kama miezi sita hadi nane tayari ni watazamaji wa televisheni wenye hamu sana.

Wanawake na Ujiuaji-Kimakusudi

“Kuna visa vya ujiuaji-kimakusudi 4,500 katika Uingereza kila mwaka: wanaume watano kwa kila mwanamke mmoja,” laripoti The Times la London. Lakini idadi ya ujiuaji-kimakusudi wa wanawake wachanga kati ya umri wa miaka 15 hadi 24 umeongezeka sana katika miaka minne ambayo imepita. Profesa mmoja katika Chuo Kikuu cha Southampton alieleza moja ya visababishi viwezekanavyo: “Wanawake wachanga wanataka kufanya vyema kazini mwao na bado wachukue madaraka ya kutunza familia. Akina mama wachanga wa daraja la katikati wanaajiri mayaya ili waweze kuchukua daraka la kazi zao. Kisha baadaye wanahuzunika na kuhisi hatia. Miili yao inawaambia wawe akina mama na akili zao zawaambia waende kuleta riziki.” Profesa huyo aamini kwamba mkusanyo wa mikazo yote hii na misongo huenda ukaongoza kwenye ujiuaji zaidi.

“Kitovu cha Tufeni Pote” cha UKIMWI

India ni kama “gari-moshi la moja kwa moja linaloteremka mbio kuelekea msiba” na yawa kwa haraka sana “kitovu cha tufeni pote cha moja ya tauni mbaya zaidi iliyopata kuwafikia wanadamu,” wasema uchunguzi mpya uliofanywa na Chuo Kikuu cha Thames Valley, katika London. Vivyohivyo, Dakt. Peter Piot, mkuu wa programu ya UKIMWI ya Umoja wa Mataifa, aliuambia mkutano wa kimataifa wa 11 wa UKIMWI kwamba India kwa ghafula ilizuka ikiwa taifa lililo na idadi kubwa sana ya watu walioambukizwa na kirusi cha UKIMWI—zaidi ya watu milioni 3 kati ya idadi yayo ya watu milioni 950. Kulingana na gazeti la habari Indian Express, uchunguzi mmoja ulikadiria kwamba makahaba huendewa kwa ukawaida na asilimia 10 ya zaidi ya wanaume milioni 223 katika India walio watendaji kingono. Makahaba ambao wanafanya kazi katika maeneo makubwa ya mijini na wanapatikana kwamba wameambukizwa, kwa kawaida hurudishwa nyumbani kwao vijijini ambapo kwa sababu ya ukosefu wa ufahamu wa ugonjwa huo pamoja na vifaa vya kitiba vya hali ya chini kuliko vile vya majijini maradhi hayo yanaenea kwa haraka sana. Inakadiriwa kwamba kufikia mwaka 2000, India itakuwa na watu milioni tano hadi nane walioambukizwa kirusi cha HIV na angalau visa milioni moja vya UKIMWI uliokolea kabisa.

Majeraha ya Michezo

• “Uendeshaji wa baiskeli za kupanda milimani unaongezeka haraka sana, na waendeshaji wanaishia hospitalini,” laripoti Vancouver Sun la Kanada. Kati ya 1987 na 1994, gazeti hilo laripoti, idadi ya watu wanaoendesha baiskeli za kupanda milimani katika Marekani imeongezeka kwa asilimia 512, kutoka milioni 1.5 hadi milioni 9.2. Waanzaji wenye bidii kupita kiasi ambao huendesha kupita kiwango cha uwezo wao katika barabara na vijia vya ndanindani sana hurushwa kutoka baiskeli zao na kupata si tu mikato na mikwaruzo bali pia majeraha mabaya visiginoni, viwikoni, mabegani, na kwenye mitulinga. Majeraha fulani, ingawa si ya kuhatarisha uhai, yaweza kuwa na matokeo mabaya ya muda mrefu. Dakt. Rui Avelar, ambaye anashughulikia hasa matibabu ya majeraha ya michezo, aamini kwamba kuvunjika kwa kimoja cha vifupa vinane vya kiwiko kwaweza kukosa kuonekana katika eksi-rei. Yeye atahadharisha: “Ukianguka huku mkono wako umenyooka, wapaswa kuchukua hali hiyo kwa uzito.” Mtu aweza kupatwa na yabisi ya gegedu na vifundo vya mfupa na madhara ya kudumu.

• “Katika Ujerumani, kati ya aksidenti za michezo milioni 1.2 na milioni 1.5 hutukia kila mwaka,” laripoti Süddeutsche Zeitung. Wafanyakazi wa kitiba kwenye Chuo Kikuu cha Bochum wamechanganua majeraha 85,000 ya utendaji wa kitafrija na michezo katika jitihada ya kukusanya habari sahihi, ya kina kuyahusu. Wachezaji wa kandanda walipata karibu asilimia 50 ya majeraha yote. Hata hivyo, walipofikiria washiriki katika michezo tofauti-tofauti, watafiti walipata kwamba kandanda, handiboli, na mpira wa vikapu yote ina kiwango kilekile cha majeraha. Moja hivi kati ya aksidenti tatu za michezo hupata kisigino, ikifuatiwa na 1 kati ya 5 kwenye goti.

Jihadhari na E. Coli O157:H7

“Kutokea kwa usumishaji wa chakula usababishwao na aina mbaya ya bakteria E. coli . . . kumeongezeka ulimwenguni pote,” laonya The New York Times. “Idadi ya bakteria ambazo zaweza kubeba sumu inaongezeka, sawa na idadi ya maambukizo na vifo ulimwenguni pote.” Aina ya kibakteria, O157:H7, ilitambuliwa kuwa tatizo kwa mara ya kwanza katika 1982. Hata hivyo, tangu wakati huo imechukua jeni mpya na kufanyiza sumu iitwayo Shiga, ambayo husababisha ugonjwa wa kuhara damu aina ya Shigella. Kusipotibiwa mara moja, kuhara huko kwaweza kutokeza kuvuja damu, kuharibika kwa figo, na kifo. Katika 1993, katika Marekani kaskazini-magharibi, watu 4 walikufa na 700 kuwa wagonjwa baada ya kula hamburgers ambazo hazikuwa zimeiva vizuri katika mikahawa kadhaa iliyo chini ya usimamizi mmoja. Katika miaka ya hivi majuzi mweneo wa maradhi pia umetokea katika Afrika, Australia, Japani, na Ulaya. Katika Marekani pekee, E. coli O157:H7 ndiyo huenda husababisha magonjwa 20,000 kila mwaka na vifo kuanzia 250 hadi 500. “Wateja wanaweza kuepuka kuambukizwa kwa kuhakikisha kwamba wanapika nyama, hasa nyama za kusagwa, ili halijoto ndani ya nyama ifikie digrii 45 Selsiasi, ambayo ni ujoto wa kutosha kuondoa rangi nyekundu-nyeupe,” lasema Times.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki