Mtunza-Bustani Stadi
CHUNGU mkata-jani wa Amerika Kusini huwashangaza wanabiolojia kwa mbinu zake za hali ya juu za kutunza bustani. Ili kuandaa chakula, mdudu huyu mdogo sana hukata jani vipande vidogo-vidogo naye hukusanya takataka kutoka kwenye sakafu ya msitu na kuvipeleka katika kiota chake kilichoko chini ya ardhi. Kisha chungu huyo husaga vipande hivyo kuwa mseto ili kuwa mbolea katika bustani yake ya kuvu. Ili kupata matokeo bora, mkata-jani huyu ajua kisilika jinsi ya kutunza kuvu wake katika halijoto yenye kufaa na kiwango kifaacho cha unyevuanga. Ili kutayarisha maeneo mapya, atahamisha vipande kutoka kwenye mimea iliyokuwapo tayari hadi kwenye shamba jipya. Chungu mkata-jani amemudu hata ustadi wa kupogoa ili kupunguza ukuzi wa kuvu. Watafiti wa Wales wamegundua kwamba mtunza-bustani huyu stadi hurekebisha juhudi zake kulingana na mahitaji ya chakula ya kiota, hivyo akihifadhi wakati na nishati.
Utunzaji wa bustani huhusisha kazi ngumu, na chungu mkata-jani ni mwenye kushangaza katika jambo hili. Si ajabu kwamba Biblia husema: “Ewe mvivu, mwendee chungu, zitafakari njia zake ukapate hekima. Kwa maana yeye hana akida, wala msimamizi, wala mkuu, lakini hujiwekea akiba ya chakula wakati wa jua; hukusanya chakula chake wakati wa mavuno.” (Mithali 6:6-8) Kwa kweli, silika ya chungu mkata-jani yathibitisha hekima ya Muumba wake, Yehova Mungu.—Mithali 30:24, 25.